Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 13 April 2014

SITTA AKOROGA MAMBO BUNGENI

Mchungaji Peter Msigwa, akisoma taarifa ya wapinzani




LICHA ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kuruhusu uvunjwaji wa kanuni ili kuruhusu wenyeviti wa Kamati za Bunge kufafanua baadhi ya mambo wakati wa uwasilishaji wa taarifa zao, haikusaidia kupunguza mashambulizi ya wapinzani.
Kanuni ya 33 ya Bunge Maalumu kifungu cha (4) na (5) vinaweka bayana kwamba baada ya mwenyekiti wa kamati kuwasilisha taarifa ya kamati inayohusika, atamwita mmoja wa wajumbe wa kamati aliyeteuliwa na wajumbe walioandaa maoni ya wachache kutoa ufafanuzi wa maoni yao kwa muda usiozidi  dakika 30.
Sitta, jana aliamua kuvunja kanuni hiyo kuwabeba wajumbe wa CCM waliokuwa wakilaumu wapinzani kupewa fursa kubwa ya kushambulia walio wengi huku mwenyekiti wa walio wengi akibanwa asifafanue jambo.
Sitta alisema ruksa kwa mwenyekiti wa kamati kutoa ufafanuzi wa taarifa ya walio wengi badala ya kusoma kama kasuku.
Hata hivyo mbeleko hiyo ya Sitta ilishindwa kutumiwa kikamilifu na wenyeviti wa kamati namba tatu na namba nne waliojikita zaidi kwenye ufafanuzi wa taarifa za kamati huku wakilenga kuminya muda wa kuwasilisha taarifa ya watu wachache.
Mwenyekiti wa Kamati namba tatu, Dk. Francis Michael, alitumia mwanya huo kutoa ufafanuzi wa mambo ambayo hayakuwepo kwenye vitabu vya taarifa ya kamati yake vilivyogawiwa kwa wajumbe.
Kitendo hicho kilifanywa juzi na Mwenyekiti wa Kamati namba moja, Ummy Mwalimu, wakati akiwasilisha taarifa ya kamati yake.
Hatua ya Dk. Michael, kujikita zaidi kutoa ufafanuzi badala ya kusoma taarifa ya kamati yake kilisababisha wajumbe wachache kupiga kelele na kumzomea.
Wajumbe wachache walidai kuwa Dk. Michael, alikuwa akifanya hivyo ili kuminya muda wao kwa lengo la kuzuia maoni yao yasipate nafasi kama inavyotakiwa.
Dk. Michael, alitoa kioja baada ya kugoma kusoma maoni ya walio wachache kwa madai amechoka.
Kauli hiyo ilichafua hali ya hewa ndani ya Bunge na kuwafanya wajumbe wachache kusimama, kuzomea na kuimba; ‘CCM… CCM…. CCM….’
Mwenyekiti wa Bunge, Sitta, alimlazimisha Dk. Michael kusoma taarifa ya wajumbe walio wachache lakini katika mshangao alisoma vichwa vya habari vya taarifa hizo huku akidai watafafanua wenyewe.
Kitendo hicho kilimfanya Sitta kuwakemea wajumbe waache kuzivuruga kanuni walizozitunga huku akimlazimisha mwenyekiti huyo kusoma taarifa yote kama ilivyoandaliwa.
Dk. Michael, alikaidi agizo la Sitta, hali iliyowafanya wajumbe wachache kuinuka kwenye vitu huku wakimzomea na kumtaka aondoke kwenye eneo la kutolea hotuba.
Wachache hao walibainisha kuwa mwenyekiti huyo alishasema tangu awali hatakuwa tayari kuisoma taarifa yao.
Mvutano huo ulihitimishwa baada ya  kuchaguliwa kwa mjumbe mmoja wa walio wachache, Mchungaji Peter Msigwa, kusoma taarifa hiyo na kutoa ufafanuzi.
Katika  ufafanuzi wake,  Msigwa alisema jina la Tanzania halina uhalali kwa sababu halipo kwenye Sheria ya Muungano ya mwaka 1964.
Alisema katika sheria hiyo nchi iliyoungana inayotajwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar.
“Hati ya Muungano haipo ndiyo maana haitolewi, jambo hilo limezidisha utata wa uhalali wa Muungano,” alisema.
“Tunataka kusogea mbele lakini  hakuna taarifa sahihi kuhusu Muungano, watu wanafichwa mambo kuhusu Muungano ambao sasa umekuwa kama fumbo la imani huku kero za Muungano zikiendelea kuchipuka kama uyoga, hatuwezi kwenda huko bila kutatua matatizo yetu,” alisema.
Alibainisha kuwa kitendo cha Zanzibar kutunga katiba yao inayokinzana na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimevunja Muungano na kimeongeza kero zake.
CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment