Nelson Mandela akipiga kura mwaka 1994.
Wananchi wa Afrika Kusini wanasherehekea leo hii miaka 20 tangu
kufanyika uchaguzi uliozishirikisha jamii zote za nchi hiyo katika uchaguzi
uliomaliza utawala wa ubaguzi wa rangi.
Siku hiyo inaadhimishwa
kwa maandamano mitaani, hotuba, sala, matamasha ya muziki na gwaride la
kijeshi. Sherehe kuu itaongozwa na rais Jacob Zuma katika majengo ya Ikulu
mjini Pretoria yajulikanayo ka Union Buildings, ambako viongozi wa serikali za
ubaguzi walizitia saini sheria nyingi za kibaguzi ambazo rais wa kwanza mweusi
wa nchini hiyo marehemu Nelson Mandela alizipinga karibu wakati wote wa uhai
wake.
Siku hiyo ya uchaguzi wa
kwanza wa kidemokrasia, tarehe 27 Aprili, 1994 imefanywa siku ya mapumziko,
ikijulikana kama Siku ya Uhuru. Kwa raia wengi wa Afrika Kusini inaambatana na
kumbukumbu ya furaha, wakati ambapo kwa mara ya kwanza watu weusi, wahindi,
machotara na wazungu walichanganyika katika mistari mirefu mbele ya vituo vya
kupigia kura.
Matumaini sambamba na
kukata tama
Mshindi wa Tuzo ya Amani
ya Nobel askofu mstaafu Desmond Tutu amesema siku hiyo ilikuwa na mihemko ya
mapenzi, huku rais wa mwisho wa serikali ya kibaguzi, FW de Klerk ameielezea
kuwa siku ya fahari kuu kwa Afrika Kusini.
Hata hivyo, miaka 20
baadaye, msisimko huo umemalizika, na watu wanakitathmini kipindi hicho cha
utawala wa demokrasia kuwa chenye mchanganyiko wa mafanikio na kushindwa.
Miongoni mwa mambo
mengine, Afrika Kusini inajivunia katiba ambayo ni mojawapo ya bora kabisa
duniani, mahakam huru na kuwa nchi ambayo pengine inaongoza kiuchumi barani
Afrika. Lakini mafanikio hayo yametiwa doa na matumizi mabaya ya fedha za umma
na lawama za ufusadi zinanoelekezwa kwa viongozi wa chama Tawala-ANC.
Changamoto zinaongezeka
Askofu Desmond Tutu
ambaye anazingatiwa kuwa Nuru ya uadilifu nchini Afrika Kusini, ameelezea
miongo miwili iliyopita kama kipindi cha mafanikio makubwa, lakini anaapa kuwa
hatakiunga mkono chama cha ANC katika uchaguzi mkuu ujao.
Maadhimisho haya ya miaka
20 ya uhuru yanafanyika katika mwaka ambamo pia kuna uchaguzi mkuu, tarehe 7
Mei. ANC inatarajiwa kushinda uchaguzi huo wenye ushindani mkubwa, licha ya
shutuma ubadhirifu na kupanuka kwa pengo kati ya matajiri na maskini ambavyo
vilishuhudiwa chini ya utawala wake.
Kuendelea kupendwa kwa
chama cha ANC ni ushahidi kwamba wananchi wengi wa Afrika Kusini wanahisi hali
ni bora zaidi ikilinganishwa na wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi
ulioendeshwa na wazungu walio wachache nchini humo.
Mazingira bora ya maisha
Serikali imeamua
kuadhimisha miaka 20 ya uhuru chini ya kauli mbiu isemayo, ''Afrika
Kusini-mahali bora pa kuishi''.
Katika kipindi hicho,
uchumi umeongezeka mara tatu, na serikali imesema imejenga nyumba zipatazo
milioni 3.7, kwa watu ambao hapo nyuma hawakuwahi kuishi katika nyumba za
kisasa. Vile vile, watu milioni 15 katika ya milioni 51 wa nchi hiyo wanapokea
msaada wa serikali.
Raia wengi weusi sasa
wanao uhuru wa kuishi na kufanya kazi watakako katika nchi yao, na weusi ambao
wanahesabiwa katika daraja la kati wameongezeka sana.
Hata hivyo bado kupishana
kwa kipato kumewafanya maskini wengi kuandamana mitaani, wakilalamikia ukosefu
wa huduma za msingi kama vile maji safi, umeme na makazi.
Afrika Kusini bado ni miongoni mwa nchi zenye
pengo kubwa sana kati ya matajiri na maskini.
CHANZO,
DW.DE.COM/SWAHILI
No comments:
Post a Comment