Wakazi wa kusini mwa Tanzania yaani mkoa wa Mtwara wametakiwa kukaa mkao wa kula burudani ya nguvu ya muziki itapigwa moja kwa moja jukwaani siku ya tarehe 2 ya mwezi wa Mei katika ukumbi wa Makonde Club.
Shoo hiyo ya kipekee na ya aina yake italetwa na si mwingine bali ni mkali wa muziki wa bongo flava nchini anayepasua anga ya Afrika ya Mashariki kwa sasa kupitia vibao vyake vitamu kama vile cha My Number One remix alichomshirikisha msanii Davido kutoka nchini Nigeria, Raisi wa wasafi ama Diamond Platinumz”Asali ya warembo”kama mashabiki wake wanavyomwita.
Mwanamuziki Diamond atafanya shoo laivu mkoani Mtwara chini ya udhamini mkubwa wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania akisindikizwa na kipenzi chake, Malkia wa Bongo Movie nchini, Wema Sepetu – ‘Beautiful Onyinye’ au Madame kama mashabiki wake wanavyopenda kumwita.
Msanii Diamond ambaye kwa sasa ndiyo mwenye mafanikio makubwa ya kimuziki nchini amekuwa ni kivutio kikubwa kwa mashabiki wa ndani na nje ya nchi kila mahali anapoalikwa kufanya shoo na hivyo kujizolea sifa lukuki na hata kuchaguliwa kuwania tuzo mbali mbali za muziki barani Afrika.
Akizungumzia juu ya shoo hiyo ya kukata na shoka kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa amebainisha kuwa tukio hili limeandaliwa ikiwa ni sehemu ya burudani kwa wateja wetu, kufurahi kwa pamoja na kuwashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutumia huduma zetu.
“Hakuna kitu ambacho tunajali na kukithamini kama wateja wetu, haijalishi wawe kona gani ya Tanzania, walipo popote tutawafikia. Vodacom imekuwepo nchini kwa zaidi ya miaka kumi sasa na kwa kipindi chote hicho watanzania wameonyesha kutuunga mkono na kutufanya tuwe mtandao unaaongoza kwa mawasiliano nchini.” Alisema Twissa.
Kwa kuongezea Twissa amewataka wakazi na mashabiki wote wa Diamond na muziki wa Bongo Flava kujitokeza kwa wingi kwani mbali na burudani kutakuwepo na huduma na bidhaa mbali mbali za Vodacom.
Katika kunogesha shoo hiyo kwa wakazi wa kusini Malkia wa Bongo Movie nchini, Wema Sepetu naye akasema haitokuwa poa kama asipomsindikiza asali wake wa moyo kwenda kujivinjari pande hizo na mashabiki wao. Kwa tafsiri nyingine mashabiki wa Mtwara wanabahati kubwa ya kutembelewa na mastaa wawili wakubwa kutoka tasnia mbili tofauti nchini.
“Hii shoo si ya kukosa kabisa kwani hakuna kiingilio bali ni uwepo wako tu na kujiandaa kwako kwa burudani ndio kinachohitajika. Tunawapenda sana wateja wetu wa Mtwara, hatuna uwezo wa kulipa kutokana na kuwa wateja wetu waaminifu siku zote lakini ninaamini kwa pamoja tunaweza kujumuika na kufurahia wakati tulionao. Naombeni mjitokeze kwa wingi, rafiki amlete rafiki yake ili tuwe pamoja siku hiyo.” Alimalizia Twissa.
CHANZO, MOBLOG
No comments:
Post a Comment