Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 18 April 2014

MECHI YA 77 SIMBA NA YANGA LIGI KUU TANGU 1965

Picha kwa hisani ya sw-ke.facebook.com

Na Daniel Mbega

“KITIMTIMU, mtakiona leo, nyumba ya shetani mwendawazimu kaingiaje!” Naam, hilo ni chagizo la wimbo maarufu wa mashabiki wa Yanga kila wanapoishangilia timu yao, hasa inapocheza na Simba.
Lakini chagizo hilo litakumbana na kibwagizo cha mashabiki wa Simba, maarufu kama Mchacho Group (ambao sasa wameongezewa sapoti na tawi la Mpira Fedha) watakaokuwa wakiimba “Amesimama kidedea, eeee kidedea!”
Timu hizo mbili zinapopambana katika mechi ya Jumamosi hii Aprili 19, kukunja jamvi la Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa msimu wa 2013/2014, kila mtu anatazama nini kitatokea, iwe uwanjani ama nje ya uwanja.
Mechi baina ya timu hizi mbili kongwe katiba katika historia ya kandanda nchini huwa zinatawaliwa na vituko vingi mno. Kuvunja nazi, kuoga maji ya maiti, kuruka ukuta, kuingia uwanjani kinyumenyume na mengine kama hayo hutajwa kwamba ni sehemu ya kuhanikiza ushindani.
Hata hivyo, kwa sasa hawawezi kuruka ukuta kama ilivyokuwa miaka ile ya zamani, wala hawawezi kuoga maji ya kuoshea maiti au kuvunja nazi hadharani, kwa sababu Sheria za Soka haziruhusu ushirikina na tayari timu hizo mbili zimekwishawahi kutozwa faini kwa vitendo hivyo.
Simba ikiwa inatokea Zanzibar, na Yanga ambayo ilikuwa Kawe jijini Dar es Salaam, zinapambana Jumamosi hii zikitaka kulinda heshima tu, kwa sababu ubingwa tayari umekwishachukuliwa na Azam FC iliyofikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.
Ushindi wa Azam wa mabao 2-1 nyumbani kwa Mbeya City Jumapili iliyopita uliifanya iweke rekodi mpya kwa kuwa timu ya nane katika historia ya soka nchini kunyakua ubingwa huo ambao umekuwa ukitwaliwa na Simba na Yanga pekee. Mara ya mwisho kwa timu nyingine kutwaa ubingwa (mbali ya Simba na Yanga) ilikuwa mwaka 2000 wakati Mtibwa Sugar ilipotwaa kwa mara ya pili mfululizo ubingwa huo wa Bara.
Lakini pia ushindi wa Azam ulivunja rekodi ya kutofungwa ya Mbeya City kwenye uwanja wake wa nyumbani katika msimu huu, huku Azam ikiendelea kushikilia rekodi yake nyingine ya kutopoteza hata mechi moja katika msimu huu. Sijui leo hii hali itakuwaje.
Yanga yenyewe imeshika nafasi ya pili kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha dhidi ya JKT Oljoro na sasa inahitaji vitu viwili tu – kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 msimu wa 2011/2012 pamoja na kulinda hadhi yake, huku Simba ikitaka kuendeleza ubabe kwa vijana hao wa Jangwani kwa kuwa hakuna itakachopoteza katika nafasi yake ya nne iliyoifikia.
Lakini kwa upande mwingine ushindi ni muhimu sana kwa Simba ikiwa inataka kulinda hadhi yake japo kwa kumaliza ikiwa ya nne, kwa sababu ikiwa itapoteza mchezo huo, basi inaweza kujikuta ikimaliza ikiwa ya sita msimu huu. Hii ni kwa sababu mpaka sasa ina pointi 37 wakati nyuma yake kuna timu mbili za Kagera Sugar na Ruvu Shooting ambazo zina pointi 35 kila moja.
Kagera Sugar inayoshika nafsi ya tano ikishinda ugenini kwa Coastal Union na Ruvu Shooting ikiwalazama maafande wa Rhino Rangers ambao tayari wamekwishashuka daraja, zinaweza kuipiku Simba kimzaha mzaha tu.
Kelele za: “Simba! Simba! Simba!” na zile za: “CCM! CCM! CCM!” zitasikika kwenye Uwanja wa Taifa, lakini zitahitaji kuangalia matokeo ya uwanjani yakoje, vinginevyo upande mmoja unaweza kuzizima.
Hapo hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama buradani nyingine ndani ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye jezi za kijani na manjano.
Mandhari haya ndiyo yaliyokuwepo Jumapili Oktoba 20, 2013 kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, wakati Simba na Yanga zilipoumana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014.
Wakati Yanga, ambayo ilikuwa inatetea ubingwa wake huku ilikiwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo, ilikuwa inatafuta ushindi ili kukwea kileleni lakini pia kulipa kisasi cha mabao 5-0 ilichokipata mwaka 2012 katika mchezo wa mwisho. Jambo hili lilionekana kuwa ni ndoto baada ya kushindwa kuyalinda mabao yake matatu iliyoyapata katika kipindi cha kwanza, hivyo kuifanya Simba isawazishe na kuleta matokeo ya ajabu ya sare ya 3-3.
Simba wao walikuwa na mambo mawili: Kwanza, walitaka kulipa kisasi cha kufungwa katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Mei 17, 2013, lakini pili, walikuwa wanatafuta ushindi ili kujiweka sawa zaidi na kutwaa ubingwa baada ya kukosa hata nafasi ya pili.
Kama wachezaji wa timu hizo watatulia na kutandaza soka, huku wakiacha ubabe na kufuatisha kelele za mashabiki jukwaani, hakika hii itakuwa burudani safi ya kufungia msimu.

Mechi zao
Hii itakuwa mechi ya 77 kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Katika kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekeza mechi hizi umekuwa mkubwa, bila kujali nani anawania kitu gani.
Hata hivyo, katika mechi 76 zilizopita, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala zaidi kwa kushinda mara 29, wakati Simba imeshinda mara 22. Timu hizo zimetoka sare mara 25 huku mabao 162 yakifungwa. Kati ya mabao hayo, Yanga imefunga 86 na Simba imefunga 75. Ikumbukwe kwamba, mechi hizi hazihusishi mechi za Ligi ya Muungano.

Idd Pazi, Kaseja kiboko
Makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ na Juma Kaseja wana rekodi ya pekee kwenye mechi za Simba na Yanga kutokana na ukweli kwamba ndio makipa pekee baina ya timu hizo kufunga bao. Pazi alifunga bao la kuongoza kwa penalti Jumamosi Machi 10, 1984 katika dakika ya 20 na akajitahidi kulinda lango la Simba hadi dakika ya 72 wakati Omar Hussein alipomzidi ujanja na kusawazisha. Matokeo yakawa 1-1.
Kaseja naye aliingia kwenye rekodi hiyo katika mechi ya Mei 6, 2012 ambayo Simba ilishinda 5-0 baada ya kufunga kwa penalty katika dakika ya 67, likiwa ni la nne kwa timu yake.
Mlinzi Suleiman Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’, ndiye pekee aliyewahi kujifunga wakati timu hizo mbili zilipomenyana kwenye Ligi. Sanga alijifunga katika harakati za kuokoa katika mechi ya Julai 19, 1977 wakati Yanga ilipokubali kipigo cha mabao 6-0, huku Abdallah Athumani ‘King Kibadeni’ akifunga hat trick (mabao matatu) peke yake na mengine mawili yakifungwa na Jumanne Hassan Masimenti.

Wafungaji wa mabao
Katika mechi 76 zilizopita na kuzaa mabao hayo 161, Omar Hussein ‘Keegan’ wa Yanga ndiye anayeongoza kwa ufungaji, akiwa amezifumania nyavu mara sita akifuatiwa na Abeid Mziba ‘Tekero’, Idd Moshi na Jerry Tegete wa Yanga pia, pamoja na Edward Cyril Chumila na Musa Hassan 'Mgosi' ambao wamefunga mabao manne kila mmoja.
Waliofunga mabao matatu kila mmoja ni Kitwana Manara ‘Popat’, Maulid Dilunga, Said Mwamba ‘Kizota’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ wa Yanga, pamoja na Abdallah Athumani ‘Kibadeni’.
Orodha hiyo inaonyesha waliofunga mabao mawili kwa upande wa Yanga ni Salehe Zimbwe, Juma Mkambi, Rashid Hanzuruni, Said Sued 'Scud', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji’, Issa Athumani, Idelfonce Amlima, Sekolojo Chambua, Ben Mwalala na Sunday Manara.
Kwa upande wa Simba ni Jumanne Hassan ‘Masimenti’, John Makelele 'Zig Zag’, Malota Soma ‘Ball Jugler’, Nicodemus Njohole, Dua Said, Steven Mapunda, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe, Athumani Machupa, Emmanuel Okwi.
Wachezaji waliopachika bao moja kwenye mechi hizo kwa upande wa Yanga ni Mawazo Shomvi, Abdulrahman Lukongo, Andrews Tematema, Emmanuel, Leonard Chitete, Gibson Sembuli, Charles Boniface, Edgar Fongo, Justin Mtekere, Thomas Kipese, Sanifu Lazaro, Ken Mkapa, James Tungaraza, Akida Makunda, Constantine Kimanda, Salvatory Edward, Kally Ongala, Pitchou Mwango Kongo, Aaron Nyanda, Said Maulid, Athumani Idd, Stephano Mwasika, Davies Mwape, Said Bahanuzi, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza.
Nyota wa Simba waliofunga bao moja kila mmoja ni Mustafa Choteka, Haji Lesso, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid 'Mchacho', Adam Sabu, Mohammed Bakari ‘Tall’, Abbas Dilunga, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwein Ally, Kihwelu Musa, Zamoyoni Mogella, Mohammed Bob Chopa, Sunday Juma, Mavumbi Omar, George Masatu, Athumani China, Mchunga Bakari, Abdallah Msamba, Athumani Machepe, Abuu Juma, Juma Amir, Joseph Kaniki, Athumani Machupa, Nurdin Msigwa, Emmanuel Gabriel, Moses Odhiambo, Ramadhan Chombo, Haruna Moshi, Uhuru Suleiman, Hilary Echesa, Idi Pazi, Patrick Mafisango, Juma Kaseja, Felix Sunzu, Amri Kiemba.

Kukimbiana
Mechi za Simba na Yanga hazikosi kuwa na vituko, lakini vinavyojulikana zaidi ni kule ‘kukimbiana’ uwanjani ama kwa kutopeleka kabisa timu uwanjani, au kwa kugomea mchezo.
Zifuatazo ni rekodi za timu hizo kukimbiana kwenye Ligi Kuu:
05/11/1966: Mchezo ulivunjika katika dakika ya 75 baada ya Yanga kugoma kumtoa mchezaji wao Awadh Gessani aliyeamriwa atoke nje baada ya kumchezea vibaya yule wa Sunderland. Sunderland wakapewa ushindi na baadaye kuwa bingwa wa taifa kwa mara ya pili. Kabla ya mchezo kuvunjika Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0. Nahodha wa Yanga, Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’, alifungiwa na FAT kutocheza mpira kwa miezi 12 na kwamba asipewe cheo cha unahodha, na Awadh Gessani akafungiwa kutocheza mechi tatu. Yanga ikatishia kujitoa kwenye ligi pamoja na African Sports, lakini baadaye timu hizo zikashauriwa kuendelea na ligi.
30/03/1968: Mchezo ulivunjika baada ya mchezaji wa Sunderland, Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’, kumpiga mwamuzi Jumanne Salum katika dakika ya 20. Wakati huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Kitwana Manara. Mchezo huo ukapangwa kurudiwa Juni Mosi, 1968 ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 5-0.
03/03/1969: Sunderland iligoma kabisa kutia mguu uwanjani, hivyo, FAT ikaipa Yanga ubingwa na kuitoza Sunderland faini ya shilingi 500, ambazo hata hivyo, hazikulipwa baada ya kulisuluhisha suala hilo.
18/06/1972: Sunderland iligoma kuingia uwanjani kwa kipindi cha pili kupambana na Yanga huku Yanga ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Leonard Chitete. Huu ulikuwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Taifa, ambapo Yanga ilipewa ushindi.
10/08/1985: Simba iligomea penati iliyotolewa na mwamuzi Bakari Bendera wa Tanga katika dakika ya 84 baada ya sentahafu wake Twalib Hilal kuunawa mpira katika eneo la hatari. FAT ikaipa Yanga ushindi na kuwa bingwa wa Tanzania Bara.
26/08/1992: Yanga ilikataa kutia timu uwanjani kucheza na Simba katika mchezo wa marudiano wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kwa kuwa tayari ilikwishatwaa ubingwa. Simba ikapewa ushindi na kisha FAT ikaipiga Yanga faini ya shilingi 250,000 ambazo zililipwa na Murtazar Dewji aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Pan African.
25/02/1996: Simba iligoma kupeleka timu uwanjani baada ya FAT kukataa ombi lao la kuahirisha mchezo huo kwa kuwa ilikuwa inajiandaa na mechi ya Kombe la Washindi dhidi ya Chapungu FC ya Zambia, ambayo hata hivyo, haikuja kabisa. Yanga ikapewa ushindi.

Msimamo kamili
Yanga 76 29 25 22 86 – 75
Simba 76 22 25 29 75 - 86

Ratiba kamili ya funga dimba
Jumamosi 19/04/2014
Young Africans vs Simba SC
Coastal Union vs Kagera Sugar
JKT Ruvu vs Azam
Rhino Rangers vs Ruvu Shooting
JKT Oljoro vs Mtibwa Sugar
Tanzania Prisons vs Ashanti United
Mbeya City vs Mgambo JKT

Msimamo ulivyo hadi sasa
Azam                         25        17        8          0          50        15        +35     59
Yanga                        25        16        7          2          60       18        +42     55
Mbeya City               25        12        10        3          32        20       +12      46
Simba                        25        9          10        6          40       26        +14      37
Kagera Sugar            25        8          11         6          22        20       +2       35
Ruvu Shooting         25        9          8          8          26        32        -6        35
Ruvu Stars               25        10        1          14        23        39        -16       31
Mtibwa Sugar          25        7          9          9          29        30       -1         30
Coastal Union          25        6          11         8          16        19        -3        29
JKT Mgambo           25        6          8          11         18        34        -16       26
Tanzania Prisons     25        5          10        10        24        32        -8        25
Ashanti United        25        6          7          12        20       38       -18      25
JKT Oljoro FC          25        3          9          13        18        36        -18      18       
Rhino Rangers         25        3          7          15        17        36        -19       16


Daniel Mbega ni mwandishi wa habari mwandamizi nchini ambaye pia amefanya utafiti kuhusiana na soka la Tanzania. Kumbukumbu hizi ni kutoka katika muswada wa kitabu chake cha ‘SIMBA VS YANGA: VUTA-NIKUVUTE’ ambacho kipo katika hatua za mwisho za uchapaji.

No comments:

Post a Comment