Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Vangimembe Lukuvi
Kama walivyo Watanzania wengine wazalendo, nami naitafakari kauli yenye utata ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambayo anadaiwa kuitoa kwenye Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma mapema mwezi huu akiwa anamwakilisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kama mgeni rasmi.
Tumeelezwa kwamba, akiwa kwenye kanisa hilo, Waziri Lukuvi aliwataka waumini kwa niaba ya Watanzania wapinge muundo wa Muungano wa serikali tatu ambazo zimependekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.
Waziri Lukuvi anadaiwa kuwasema kwamba, Watanzania waipuuze Rasimu ya Katiba kwa sababu kuruhusu serikali tatu ni kutaka Watanzania waingie vitani.
Alinukuliwa akisema: “Serikali tatu zikipita ni wazi kuwa hata makanisa yatafungwa kwani nchi haiwezi kuwa na amani tena, angalieni nchi ya Korea Kusini na Korea Kaskazini ambao waligawanyika na sasa ni maadui wakubwa wanaokaa mipakani wamenyoosheana bunduki,” alisema na kuongeza: “Waumini ndugu zangu wapendwa, kwa sasa tupo katika hali mbaya sana hapo bungeni, tunaomba mtuombee kuna watu ambao wanataka madaraka kwa nguvu na wameanza kutafuta jinsi ya kuvunja Muungano na kudai kuwapo kwa Serikali tatu, nawaomba sana wapuuzeni wale wote ambao wanataka serikali tatu.”
Lukuvi alisema pia kwamba Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu.
Hii ni kauli ya vitisho, mabavu na uchochezi ambayo ndugu zangu Watanzania hatuna budi kuipinga na kuikemea kwa nguvu zote.
Hata alipotakiwa kufafanua kauli yake, Lukuvi alisema alichokizungumza kanisani hapo ni mawazo yake binafsi ambayo yanafanana na Watanzania wengi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete. Akanukuliwa pia: “Unajua jeshi haliwezi kukaa na bunduki bila fedha. Hiyo Serikali ya tatu ambayo jeshi litakuwa chini yake haina vyanzo vya mapato vya kueleweka, sasa hao wanajeshi watalipwa nini? Wenye mitutu watakubali kuishi bila fedha?”
Ndugu zangu, kinachoonekana hapa ni wanasiasa ambao wana uchu wa madaraka na wanataka kutumia kila mbinu kuhakikisha wanawatisha Watanzania, hasa katika mchakato huu wa Katiba Mpya.
Wanasiasa hawa sasa wamevuka mipaka na wanalichokoza jeshi letu tukufu wakilisingizia ili kubariki matakwa yao. Uchochezi kama huu tusiukubali.
Tumeshuhudia kwa mataifa ya wenzetu ambayo amani imetoweka jinsi ambavyo wananchi wanalia kwa sababu ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Chanzo ya vurugu za huko kwa wenzetu ni tamaa ya madaraka na kauli tata za wanasiasa kama hawa, ambazo hakika zimewafanya ndugu kwa ndugu kuchukiana, watu wa familia moja kuhasimiana na maokeo yake ni umwagaji wa damu.
Kwa nini wanasiasa hawamuogopi Mungu jamani? Miaka yote ambayo wamekaa kwenye madaraka na kujilimbikizia fedha bado tu haitoshi mpaka waanze kuchochea machafuko? Huu ni uchochezi kwa sababu huwezi kuvihusisha vyombo vya usalama moja kwa moja katika masuala yenu wanasiasa na ambayo hata nafsi zenu zinawasuta kwamba mnapigania mbaki madarakani.
Jeshi letu limejengwa kwa uadilifu mkubwa, lina nidhamu ya hali ya juu, limejawa na uzalendo siyo kama hawa wanasiasa waliozisaliti amri 10 za TANU/CCM.
Tunatambua kwamba, hata katika mfumo huu wa sasa wa Muungano, wanajeshi wetu hawalipwi vizuri. Kama ingekuwa taasisi nyingine kama za waalimu, madaktari na wengineo, pengine nao wangekuwa wameandamana kudai nyongeza ya mishahara. Lakini huko hawawezi kufika kwa sababu ya uzaendo.
Wanajeshi wetu wanayaona mambo yote machafu yanayoendelea - wizi, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na kadhalika. Wanawajua hata wanasiasa waongo na wanafiki ambao wanasababisha mambo haya, lakini wametulia tu.
Tumeshuhudia jinsi viongozi wetu wakuu wa serikali walivyouziana mashirika ya umma, walivyotumia hila kuingia mikataba mibovu ambayo inaendelea kuwagharimu Watanzania mpaka sasa, jinsi wanavyoendelea kutumia kila njia kuhakikisha wanabaki madarakani.
Wale waliofikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa ubadhirifu mkubwa wa mali ya umma tumeshuhudia ama wakiachiwa au wakipewa adhabu zisizolingana na makosa waliyoyatenda. Haya nayo wanajeshi wetu wanayaona.
Ndugu zangu, mara ngapi tumeambiwa kwamba maofisa wakuu wa umma wanajihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya?
Mara ngapi wametajwa kwenye usafirishaji wa nyara za serikali kama pembe za ndovu pamoja na ujangili? Si majuzi tu wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili hata Wabunge walitajwa kuhusika? Nini kimechukuliwa dhidi ya wale wahusika wakuu zaidi ya kushuhudia 'vidagaa' tu ndivyo vikikamatwa?
Ndugu zangu, usifike wakati tukawachokonoa mpaka wakachoka. Hii ni hatari sana kwa amani yetu.
Wanasiasa wanaofanya hivi tuwakemee na tuwaambie hadharani kwamba wanachokifanya siyo sahihi. Wakichukia shauri yao.
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0656 331974
No comments:
Post a Comment