Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot.com, Arusha
ZAIDI ya wakulima 500 kutoka katika Kanda ya Kaskazini wanatarajiwa
kupewa elimu ya rasilimali fedha na kuongeza ufahamu na uelewa juu ya huduma
mbalimbali za kifedha zitolewazo na benki.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wakulima wa
Mbogamboga, Matunda na Viungo (TAHA) Jacqueline Mkindi wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na maonesho ya kuunganisha kilimo biashara na
taasisi za kifedha yatakayofanyika April 25 na 26 mwaka huu katika viwanja vya
AVDRC Tengeru.
Alisema kuwa, kwa sasa asilimia kubwa ya taasisi za kifedha
zimekuwa zikiwakandamiza wakulima kwa kuwatoza riba kubwa kwenye mikopo hali
ambayo imekuwa ikiwasababishia wakulima hao kupoteza imani na mikopo kutoka
katika taasisi hizo.
Alidai kuwa hali hiyo imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa
wakulima hao,kwani wakati mwingine imewawia vigumu kushindwa kufikia malengo
yao waliyojiwekea kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha katika kuendesha
miradi yao midogomidogo.
"Kutokana na changamoto hiyo sasa tumeamua kuandaa maonesho
yatakayoweza kuwakutanisha taasisi za kifedha pamoja na wakulima ambapo hapo
taasisi hizo zitaweza kutambua mahitaji ya wakulima, na jinsi ya kuweza
kuwasaidia tofauti na hapo awali," alisema Jacqueline.
Pia alisema kuwa maonesho hayo yataenda sambasamba na
uwasilishwaji wa mada mbalimbali ikiwemo uaandaji bora wa mipango biashara,
umuhimu wa soko la hisa katika kuhakikisha upatikanaji wa mitaji wa muda mrefu
na matumizi bora ya mikopo katika biashara hususani za kilimo ili
walengwa waweze kujifunza zaidi juu ya mbinu bora za kufikia na kupata mitaji
kwa kufanya biashara.
Kwa upande wake mratibu wa mtandao wa Agri-Hub Tanzania Tom Ole
Sikar alisema kuwa maonesho hayo yanalenga kuwawezesha wakulima pamoja na
wamiliki wa biashara za kilimo kama vile wachuuzi,wauzaji wa pembejeo na
wasindikaji kutambua fursa mbalimbali za mitaji pamoja na usalama wa kifedha
zilizopo kwa biashara za kilimo.
Hata hivyo alisema kuwa wadau ambao wengi wao ni wakulima
wataweza kupata fursa ya kutambua njia bora za kuboresha biashara na utoaji wa
huduma kwa walengwa pamoja na kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wengine wa
kilimo waliofanikiwa kutembelea maonesho yaliyopita.
No comments:
Post a Comment