Mbunge wa Kyela ambaye ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe akizungumza na baadhi ya wananchi waliothirika na maji ya
mafuriko katika Kijiji cha Itope wilayani Kyela.
|
Kyela. Watu watatu wamefariki dunia na wengine
watatu hawajulikani walipo baada ya kukumbwa na mafuriko yaliyotokea katika
maeneo mbalimbali wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Mafuriko hayo pia yamesababisha shule 27 kufungwa zikiwamo 20 za
msingi na saba za sekondari kutokana na kuzingirwa na maji.
Mafuriko hayo pia yamezoa daraja la kamba linaloelea
(kiteputepu) katika Mto Kiwira, linalounganisha kata za Ndandalo na Ibungu na kusababisha
wananchi kukosa mahitaji mbalimbali, hivyo kulazimika kuomba boti.
Athari nyingine zilizotokana na mafuriko hayo ni kukatika kwa
mawasiliano katika barabara inayounganisha Kikusya - Kyela – Ipinda hadi Matema
na kufungwa kwa barabara ya kwenda Bandari ya Itungi katika Ziwa Nyasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mbunge wa Kyela ambaye
pia Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliyetembelea maeneo
yaliyoathirika na mafuriko hayo, wananchi walisema zimeleta madhara makubwa.
Mtendaji wa Kijiji cha Itope, Lutufyo Mwangamile alisema tangu
mvua hizo zilipoanza Aprili 14, mwaka huu nyumba nyingi zimeanguka na nyingine
kujaa maji.
“Katika kijiji changu, kaya 850 zimeathiriwa na mafuriko haya na
wananchi 250 wamekosa mahali pa kulala na wameomba hifadhi katika vijiji
jirani,” alisema Mwangamile.
“Kuna watu wasioona wanane ambao hawana uwezo, wanahitaji
kusaidiwa maana nyumba zao zimezingirwa na maji, hawana chakula na hakuna ndugu
wa kuwasaidia,” alisema.
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika, Dk
Mwakyembe alisema athari ni kubwa kwani mvua zilizonyesha ni za kihistoria
ambazo zimeathiri kata kumi na moja kati ya 20 za wilaya hiyo.
Kuhusu shule zilizofungwa, Dk Mwakyembe alisema Serikali
inaendelea na mchakato wa kuzisaidia ili wanafunzi waendelee na masomo.
“Mvua ya safari hii ni ya kihistoria, haijawahi kutokea na hata
madaraja ambayo yalikuwa yakiaminika kwa ajili ya mawasiliano yamesombwa na
maji,” alisema.
Dk Mwakyembe aliahidi kutoa msaada wa chakula na vyandarua na
kuwataka watendaji wa halmashauri ya wilaya kufanya tathmini mapema ili
kuhakikisha chakula kinawafikia waathirika mapema.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment