Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 31 March 2014

HUYU NDIYE ABUNUASI!


Ndugu zangu,
Tembea uone, na hasa unapoona mazingira ya asili. Kwa bahati nzuri sisi wengine tulizaliwa porini, maana siyo vijijini, kwa sababu wakati huo hata Vijiji vya Ujamaa vilikuwa havijaanza bado. Huku mjini nilikuja wakati nasoma - muda wote ni Bush, kuchunga ng'ombe na kukutana na hayawani aina kwa aina.
Kwa maana hiyo nimebahatika kuyasawiri mandhari ya asili kabisa ambayo babu zetu walirithishwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Kufukuzana na mbwa mwitu, mbeha na fisi ilikuwa ni sehemu ya maisha yangu enzi hizo miaka ya 1970. Miungurumo ya simba ilikuwa kama vinubi nyakati za usiku, wakati mwingine walikuja mpaka nyuma ya boma wakivizia ng'ombe wetu.
Wapo wanyama wengi tuliokuwa tukiwaona, walikuwa kama jirani zetu, wengine kama tuliwinda, basi ilikuwa ni kwa ajili ya kitoweo tu, vinginevyo tulipishana nao mwituni bila shida.
Lakini wengi kati ya wanyama hao ni mnyama aitwaye Abunuasi ambaye kwa Kiingereza anaitwa Springhare au Rodent. Mnyama huyu, ambaye kwa jina la kisayansi anajulikana kama Pedetes capensis ambaye anapatikana zaidi Afrika, hasa Kusini na Mashariki mwa bara hilo. Anatokea kwenye jenasi ya Pedetes, familia ya Pedetidae, kundi dogo la Anomaluromorpha na Oda ya Rodentia.
Kwa sasa wanyama hawa, ambao wanafahamika zaidi kama East African springhare, au kwa jina la kitaalamu Pedetes surdaster, wametoweka na ni nadra sana kukutana nao. Mnyama huyo huonekana zaidi nyakati za usiku na ni nadra sana kumuona. 
Lakini baada ya miaka zaidi ya 30 tangu nimuone kwa mara ya mwisho, hatimaye niliweza kumuona Desemba 6, 2013 usiku, pale katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ya pili kwa ukubwa nchini Tanzania na ndicho kitovu cha utalii na pato la taifa katika sekta hiyo. Pengine nilikuwa na bahati ya mtende kuota jangwani.
Wanyama hawa wana kawaida ya kulala mchana kwenye mashimo. Wanakula majani, mizizi na mbogamboga, na mara moja moja hula wadudu.
Utamtambua Abunuasi kutokana na mwendo wake, kwani anapenda kurukaruka kwa kutumia miguu yake ya nyuma. Yaani yuko kama Kangaroo, ingawa yeye ni mdogo sana.
Kwa kweli nimefurahi sana mwenzenu, maana nakumbuka mara ya mwisho kumuona ilikuwa takriban miaka 33 iliyopita wakati nikiwa nachunga ng'ombe wa familia enzi hizo.
Nitaendelea kuwapa dondoo mbalimba za yale ninayoyaona.

Ndugu yenu,
Daniel Mbega

AFC YADAIWA KUPANGA MATOKEO KUTWAA UBINGWA WA MKOA ARUSHA


Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha


Washindi wa pili wa mkoa wa Arusha timu ya Mana FC wamepinga uhalali wa ubingwa wa soka mkoani Arusha walioupata timu ya AFC wakituhumu mchezo mchafu wa upangaji wa matokeo katika mchezo wa mwisho uliozikutanisha timu ya AFC na Laibon ya  Longido.
Katika mchezo huo AFC ilishinda kwa magoli 9-1 na kuizidi Mana FC kwa tofauti ya magoli baada ya AFC kufikisha magoli 16 dhidi ya magoli 9 ya Mana wakati timu hizo zikiwa zimelingana kwa pointi, hivyo AFC kuwa mabingwa kwa kuizidi Mana kwa tofauti ya mabao 4 kwani AFC imefungwa mabao 3 na Mana ilikuwa haijafungwa hata bao moja.
Meneja wa mana FC Abraham Magumira alisema ukiangalia ushindani uliokuwepo katika Ligi ya Mkoa pamoja na uimara wa timu zote zilizoshiriki hatua ya sita bora ya ligi hiyo ni vigumu mno kwa timu kushinda mabao zaidi ya matano kwani katika michezo yote iliyotangulia hakuna timu iliyofungwa zaidi ya magoli matatu.
Magumira aliongeza kuwa kabla ya mchezo huo walishatoa malalamiko kwa uongozi wa chama cha soka mkoani Arusha juu ya tetesi za AFC kupanga matokeo kwani tayari Mana FC walikua wanaongoza kwa pointi 11.
Alisema kuwa AFC walikuwa wanauwezo wa kufikisha pointi hizo ila mana walikuwa wanawazidi AFC kwa tofauti ya magoli 3 zaidi ya kufunga hivyo AFC walitakiwa kuifunga laiboni zaidi ya mabao 4-0 ili waipiku Mana FC.
Aliongeza kuwa hilo lilijitokeza katika mchezo huo wa mwisho kwani hali ya mchezo ilionyesha waziwazi kuwa laibon walikuja kwa ajili ya kufungwa na mwisho wa siku AFC walishinda 9-1.
Akizungumzia juu ya ubora wa timu Magumira alisema Mana FC imekua na matokeo bora kwani imeshinda michezo mitatu na kutoka sare miwili na haijafungwa hata goli moja tofauti na AFC iliyofungwa magoli matatu na kulazimika kupanga matokeo katika mchezo wa mwisho.
“Timu ya Laiboni haikuwa timu dhaifu kiasi hichi hadi kufungwa magoli tisa kwani katika michezo iliyotangulia ilitoka sare mara mbili na hata michezo iliyopoteza ilifungwa kwa tabu," alisema Magumira.
“Sisi ndio mabingwa halali wa hilo kombe na  na AFC ni mabingwa wa kupangwa na hata kombe walilopewa ni kama wametushikia tu na kama wataendelea na tabia hiyo hawatafika mbali katika mashindano ngazi ya kanda na taifa na kama wanabisha subiri tutaona huko mbeleni,” alitamba meneje huyo wa Mana FC.
Alipoulizwa kuhusu shutuma za upangaji huo wa matokeo Katibu wa Chama cha Soka mkoani Arusha (ARFA) Adam Brown alisema hakuna ushahidi wowote juu ya hilo na kama ni idadi kubwa ya magoli waliyopata AFC ni jambo la kawaida kwenye mchezo wa kandanda kwa vile hakuna idadi rasmi ya magoli inayotakiwa timu kufunga ili ionekane imepanga au kutokupanga matokeo. 
“Kuna timu zinaweza kupanga matokeo hata ya ushindi mdogo wa goli moja ila kinachotakiwa ni ushahidi, hatuna ushahidi wa upangaji wa matokeo na ushindi wa AFC ni wa halali kwani magoli yalikuwa hayana utata na mchezo ulikuwa wa kawaida, kama wana ushahidi watuletee tutaufanyia kazi,” alimalizia Adam Brown.

TANAPA YAKANUSHA 'KUUZWA' KWA HIFADHI YA KATAVI

Katika gazeti la Jamhuri Toleo Namba 129 Machi 25-31, 2014 kulikuwa na habari iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari “Nyalandu ‘auza’ Hifadhi” ambapo maelezo ya habari hiyo yaliitaja Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuwa inatarajiwa kukabidhiwa kwa wawekezaji kutoka nchini Afrika Kusini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu.

Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi pamoja na Hifadhi nyingine 15 nchi nzima linapenda kukanusha habari hiyo iliyoandikwa kwa lengo la kupotosha umma kama ifuatavyo.

Mosi, hakuna mpango wala uamuzi wowote uliopo au uliokwisha kufanywa wa kuingia Mkataba wa Uendeshaji wa aina yoyote ile baina ya Shirika la Hifadhi za Taifa naMwekezaji yeyote kutoka nchini Afrika ya Kusini ikiwa ni pamoja na African Parks Network waliotajwa katika habari husika.

Pili, Sheria inayosimamia uanzishwaji wa maeneo ya Hifadhi za Taifa ikiwemo Katavi imelipa dhamana hii pekee shirika kusimamia maeneo haya kwa niaba ya Watanzania na ni kinyume cha sheria kukabidhi kwa wawekezaji kwa ajili ya usimamizi kama ilivyobainishwa katika habari hiyo.

Tatu, Shirika la Hifadhi za Taifa bado linao uwezo thabiti wa kusimamia uendeshaji wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi ili kuhakikisha rasilimali za wanyama na mimea zinaendelea kutunzwa kwa miaka mingi ijayo kama ambavyo imekuwa ikifanya tangu kuanzishwa kwa hifadhi hiyo mwaka 1974.

Aidha, kama ambavyo shirika limekuwa likipanga katika mipango yake ya maendeleo mwaka hadi mwaka, katika mwaka mpya wa fedha ujao shirika limepanga kuongeza idadi ya watalii katika Hifadhi za Kusini ikiwemo Katavi Saadani, Mikumi na Ruaha. Mkakati huu utahusisha kuongeza ubora wa utoaji huduma ikiwa ni pamoja na malazi ili kukuza utalii wa ndani. Shirika litafungua ofisi Jijini Dar es Salaam na kuimarisha ofisi za Mwanza na Iringa ili watalii wapate taarifa za Hifadhi na kuweza kufanya ‘bookings’ kwa urahisi. Aidha, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa masoko ya nje, Shirika sasa litaanzisha ‘Road shows’ mbalimbali kwa soko la ndani na nchi za jirani. Vilevile, Shirika litaongeza kujitangaza kupitia Mitandao ya Jamii, TV, majarida na tovuti ya Shirika itaboreshwa katika kuarifu wadau masuala mbalimbali yanayojiri kwenye Hifadhi zetu.

Tayari Shirika limeanzisha Kurugenzi mpya ya Utalii na Masoko kwa ajili ya kutekeleza mkakati huu wa kuzifanya hifadhi za ukanda wa kusini kuvutia watalii wengi zaidi.

Imetolewa  na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
30.03.2014

WARIOBA AMSHUKIA PROFESA SHIVJI


Jaji Joseph Sinde Warioba
Dar es Salaam. Mjadala wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.
Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo ambalo sasa analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya Profesa Shivji kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la Vijana lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano Baada ya Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Profesa Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi kuzingatia mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika pande hizo mbili za Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa viongozi halina budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa Zanzibar, Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.
Katika majumuisho yake, Profesa Shivji, ambaye aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa kuangalia sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba walikuwa na nia njema.
Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa kusema “the road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba alisema Profesa Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa Zanzibar na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.
“Shivji ni msomi na mimi najua anaelewa matumizi ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili nyumbani kwake jana jioni.
“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi.”
Jaji warioba alisema Shivji ndiye amekuwa chanzo cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake. Alisema waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa Zanzibar.
“Shivji alikuwa anasema Tanganyika imejificha kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi isijifiche,” alisema Jaji Warioba.
“Na Shivji amechochea hilo… wote wale waliokuwa wanamnukuu walikuwa wanatoa hayo kwenye maandishi yake na kwamba mpaka leo hii kuna watu wa Zanzibar wanaamini Muungano huu si halali kisheria kutokana na Shivji ambaye alisema Baraza la Mapinduzi halikuridhia articles (ibara) za Muungano.”
Alipoulizwa jana usiku kuhusu tuhuma hizo za uchochezi na chanzo cha hisia za utaifa wa Uzanzibari na Utanganyika, Profesa Shivji alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hajamsikia Jaji Warioba akizungumzia hilo.
“Hey, amezungumza lini?” alihoji. “Siwezi kujibu kwa kuwa sijamsikiliza mwenyewe.”
Lakini Jaji Warioba alisema watu walitumia msingi huo kudai utaifa wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Shivji amesababisha hisia za utaifa na kwamba haya yanayoendelea sasa yanatokana uchochezi huo.
“Hata kabla ya sisi kuanza mchakato huu, Shivji alikwenda Zanzibar akazungumza na Baraza la Wawakilishi na akawaambia issue kwa Zanzibar ni self determination (kujitambua), Sasa leo anaona kama hatari ni Tanganyika, lakini yeye ndio amechochea nationalism (utaifa),” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu takwimu, Jaji Warioba alisema maraya kwanza Profesa Shivji alizungumzia takwimu za Zanzibar kuhusu muundo wa Muungano akisema kuwa waliozungumzia suala hilo walikuwa 47,000, huku watu 27,000 wakitoka Tanzania Bara na 19,000 kutoka Zanzibar.
 “Safari hii ametaja zile za Tanzania Bara na kusema hiyo ni figure (namba) ndogo sana ukilinganisha na watu 300,000 waliotoa maoni,” alisema Warioba.
Alisema Tume ilitumia takwimu zinatokana na watu waliozungumzia suala ambalo wameliwekea asilimia na si kwa ujumla na ndio maana anaona Profesa Shivji anataka kupotosha kwa makusudi.
Warioba alimuelezea Profesa Shivji kuwa sasa ameamua kueneza propaganda za serikali mbili kwa kuponda Rasimu ya Katiba ambayo inaonyesha kuwa muundo wa serikali tatu ndio unaoifaa Tanzani kwa sasa.
Aidha, Warioba alisema msimamo wa Profesa Shivji ni kwamba Zanzibar haikukosea kubadilisha Katiba mwaka 2010.
“ Nimeshangazwa na Shivji kusema kwamba kitendo cha Zanzibar kubadili Katiba yao kuwa ‘Zanzibar ni Nchi’ halikuwa jambo la ajabu,” alisema Warioba.
Alisema Shivji ni msomi ambaye anafahamu kitendo cha kubadilisha Katiba kilikuwa na madhara makubwa katika muundo wa Muungano.
“Nadhani mnakumbuka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipoulizwa Bungeni kama Zanzibar ni nchi au siyo nchi, alijibu kuwa Zanzibar siyo nchi, vurugu zake mnakumbuka,” alisema.
Alisema lakini msomi kama Shivji haoni kama suala hilo la ‘Zanzibar ni nchi’ lina madhara makubwa katika mstakabali wa taifa letu.
Jaji Warioba alisema kama serikali tatu hazitakiwi, basi kinachotakiwa kufanywa ni kwa Zanzibar kubadili Katiba yake ili iseme kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, vinginevyo haiwezekani.
“Maana kama ni kusahihisha, ni lazima kwanza Katiba ya Zanzibar itumie maneno yale yale yaliyo kwenye Katiba ya Muungano. Yaani Zanzibar iwe sehemu ya nchi. Zanzibar wakubali hilo,” alisema.
“Zanzibar wakubali Rais wa Muungano ana madaraka nchi nzima maana mabadiliko ya 2010 yamemuondolea Rais wa Jamhuri ya Muungano madaraka yake.”
Akitoa mfano wa mbunge wa Simanjiro,Christopher Ole Sendeka, Jaji Warioba alisema amekuwa akidai takwimu hazionyeshi uhalisia wa maoni ya wananchi.
“Kwa mfano, Jimbo la Simanjiro linakuwa na watu 100,000 lakini waliojiandikisha kupiga kura ni watu 20,000 na waliopiga kura ni watu 15,000. Hii ina maana ushindi wake utakuwa katika watu waliopiga kura na siyo idadi ya watu wa Simanjiro,” alisema Warioba.

PROFESA ISSA SHIVJI ACHAMBUA KATIBA YA ZANZIBAR NA KUHOJI 'SASA TUNAZO NCHI MBILI’?

Profesa Issa Shivji

UCHAMBUZI WA MABADILIKO YA 10 YA KATIBA YA ZANZIBAR YA MWAKA 1984: JE, ‘SASA TUNAZO NCHI MBILI’?


Na Issa Shivji


UTANGULIZINimefurahi kwa sababu huu ni mkusanyiko wa wanazuoni na wasomi wenzangu ambao tumekusanyika kujadili jambo muhimu sana juu ya hatma ya nchi yetu. 

Sisemi hivyo kwa sababu huu ni mkusanyiko wa vijana; kwangu mimi ujana na uzee hautegemei umri bali unategemea fikra na mawazo. Kama wewe una fikra za kimaendeleo na ukombozi, basi wewe ni kijana bila kujali umri wako. Na kama umechagua kujiunga na matabaka ya wanyonyaji na wakandamizaji na kusambaza mtazamo wao basi, kwangu, wewe umezeeka hata kama una umri wa miaka 25!

Kwangu mimi nafasi hii niliyopewa ni kujadili mambo mazito na kuelimishana. Kwa hivyo, mhadhara wangu utakuwa wa kuchochea mawazo na fikra mbadala.

Maana ya mawazo mbadala kwangu ni mawazo ambayo huwezi kuyakuta kwenye magazeti, kusikia yakisemwa na wasemaji wa kisiasa au kuyakuta kwenye uchambuzi wa wasomi wa mambo ya utawala.

Nchi yetu (na hata bara letu la Afrika, ingawa leo nitazungumzia zaidi nchi yetu) inapitia kwenye kipindi kigumu, kiasi kwamba tuna wasiwasi kwamba nchi hii ya Tanzania itabaki kuwa nchi au itasambaratika. Na mchakato wa Katiba Mpya unadhihirisha hali hiyo na ugumu wa kipindi hiki.

Mjadala unaoendelea juu ya Katiba Mpya umejikita, karibu asilimia mia moja, kwenye suala la muungano, hususan muundo wake. Na hili suala haliepukiki kwa sababu mambo yote mengine katika Rasimu yanategemea sana muundo wa muungano.

Haraka haraka nitoe mifano miwili tu: Ukitaka kujadili malengo makuu ya taifa (Sura ya Pili ya Rasimu), awali ya yote hunabudi ujibu swali: Taifa lipi? Taifa la Tanganyika au la Zanzibar au la Tanzania? Na hili Taifa la Tanzania liko wapi, na lina nafasi gani, katika rasimu?

Mfano wa pili: Ukitaka kujadili maadili na miiko ya uongozi (Sura ya Tatu), inakubidi ujiulize: Viongozi wepi? Viongozi wa serikali ya muungano, au serikali ya Tanganyika au serikali ya Zanzibar. Ukisoma Rasimu kwa makini, utakuta viongozi wanaomaanishwa ni viongozi wa serikali ya muungano. Kama ni hivyo, maadili haya – mazuri tu – yanawagusa vipi wananchi wa Tanganyika na wananchi wa Zanzibar, wakati viongozi hao wa Muungano hawana mamlaka juu ya rasilimali zao, ardhi yao, huduma zao, ustawi wao na, kwa jumla, hali yao halisi. Mambo haya yote siyo mambo ya muungano na serikali ya muungano haina mamlaka nayo.

Katika mjadala unaoendelea kumekuwa na malumbano na mabishano kati ya wasemaji, wafuasi na wapigadebe wa ama serikali tatu au serikali mbili. Wachambuzi, kama wapo, ni wachache sana – na hata hao wachache hawasemi au hawasikiki. Rai yangu kwenu ni kwamba sisi kama wanazuoni tusijidandie kundi lolote kati ya makundi hayo matatu.

Jukumu na wajibu wetu ni tofauti kabisa. Wajibu wetu ni kuchambua hali halisi bila jazba; na kutokana na uchambuzi wetu kuonesha uzuri na ubaya wa mambo. Sisi wanazuoni nafasi yetu ni kuwa kioo cha jamii, kuonesha jamii uzuri na ubaya wake na kwa vipi na kwa njia gani uzuri unaweza kuimarishwa na ubaya kupunguzwa.

Na huu ndiyo mwongozo wangu katika kufanya uchambuzi wa mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar. Hoja nyingine juu ya muundo wa muungano, kwa kweli, sitazigusia sana kwa sababu niliwahi kutoa mhadhara juu ya Rasimu ya Kwanza, na Rasimu ya pili haijabadilika sana na vilevile mawazo yangu hayajabadilika sana.

Na pia, kwa sababu, hivi karibuni imetokea hoja mpya ambayo inarudiwarudiwa sana na wasemaji na wafuasi (pamoja na magazeti) wa serikali tatu. Kwa hivyo, nimeona ni vema nijikite kwenye hoja hiyo ya mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.
HOJA YA KUWA NA NCHI MBILI
Hoja ya mabadiliko ya 10 kuzaa nchi ya Zanzibar na kwa hivyo kuwepo kwa nchi mbili zenye serikali mbili hivi sasa imewekwa vizuri na kwa ufasaha katika Taarifa ya Mwisho ya Tume iliyotoka magazetini tarehe 26 Machi, 2014 (ang. Mwananchi ya tarehe hiyo, uk. 37). Kwa hivyo, nitatumia hoja kuu za Taarifa hii kufanya uchambuzi wangu. Hoja zenyewe ni hizi zifuatazo:

1. Zanzibar imetangaza kuwa Nchi
Katika mabadailiko ya 10 Zanzibar “imetamka kwamba ni Nchi tofauti na ilivyokuwa imetamka kwamba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano kabla ya Mabadiliko hayo.” Hii ni kinyume na Katiba ya Muungano.

2. Upunguzaji wa Mamlaka ya Bunge la Muungano
Katiba ya Zanzibar imeweka mipaka ya mamlaka ya Bunge la Muungano katika Ibara ya 132 “ambayo inaelekeza kwamba Sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kuanza kutumika Zanzibar ipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi na kupata ridhaa ya kutumika Zanzibar”. Hii pia ni kinyume na Katiba ya Muungano.
3. Upunguzaji wa Mamlaka ya Rais
Katiba ya Muungano imempa Rais wa jamhuri kuigawa Jamhuri katika maeneo ya kiutawala katika Mikoa na Wilaya. Mabadiliko ya 10 sasa yameweka mamlaka hayo ya kuligawa eneo la Zanzibar katika Mikoa na Wilaya mikononi mwa Rais wa Zanzibar. Kwa hivyo, marekebisho haya yamevunja Katiba ya Muungano.
4. Upunguzaji wa Mamlaka ya Mahakama ya Rufaa
“Katiba ya Muungano ya 1977 imetoa mamlaka ya kusikiliza rufaa nchi nzima. Lakini Zanzibar imezuia mahakama hiyo kusikiliza rufaa kutoka Mahakama za kadhi, kutafsiri Katiba ya Zanzibar na rufaa kuhusu mashauri ya haki za binadamu.” Hii pia ni uvunjaji wa Katiba ya Muungano.

Baada ya hoja hizo, Tume katika Taarifa yake inahitimisha kama ifuatavyo:

“Waasisi walituachia Bunge lenye madaraka nchi nzima. Sasa ni lazima lipate idhini ya Baraza la Wawakilishi.
Waasisi waliacha Rais akiwa na madaraka kamili. Madaraka hayo yamepunguzwa bila kufuata utaratibu wa Katiba.
Waasisi walituachia Mahakama ya Rufani yenye madaraka kamili. Madaraka haya yamepunguzwa.
Waasisi waliunganisha nchi mbili ikawa nchi moja. Sasa tunazo nchi mbili. … … … “.

“Tume iliona ni vigumu kwa Zanzibar kurudi kwa hiyari kwenye hali ya awali, yaani kurudisha mambo yote yaliyotolewa kwenye orodha ya Muungano, kurudisha madaraka ya rais na kufuta kipengere cha nchi mbili kwenye Katiba yake. Tume iliona kwamba pamoja na mambo haya kufanywa kinyume na Katiba ya Muungano hali ibaki hivyo hivyo. Lakini kwa kufanya hivyo basi malalamiko ya Tanzania Bara nayo yasipuuzwe. Hivyo Tume nayo ikapendekeza Serikali ya Tanganyika iundwe.”

Ndivyo, kwa hoja hizo, Tume inavyohalalisha pendekezo lake la Serikali tatu. Na bila shaka Tume iliona kwamba hoja hizo ni nzito sana kiasi kwamba ndio hoja pekee iliyozungumziwa na kutolewa ufafanuzi katika Taarifa yao ya mwisho.

Nitakachofanya sasa ni kuangalia hoja moja baada ya nyingine. Tuwe pamoja.
1. Zanzibar imetangaza kuwa Nchi
Kabla ya kuingia kwenye ibara yenyewe ya Mabadiliko ya 10, kwanza tuelewe dhana ya nchi, dola na serikali na jinsi ilivyotumika katika katiba zetu.

Nchi maana yake ni eneo la ardhi yenye mipaka ambayo inatambulika; na eneo hilo lina utambulisho wake.

Dola maana yake ni chombo au mamlaka ya utawala ambayo inatawala eneo maalum lenye mipaka yake. Yaani mipaka ya utawala wa dola ni mipaka ya jurisdiction au mamlaka yake. Vyombo vitatu, yaani chombo cha utendaji (ambacho huitwa serikali), chombo cha utungaji sheria (tunakiita Bunge) na chombo cha kutoa haki (ambacho tunakiita Mahakama) ndivyo kwa pamoja vinaunda dola. Mara nyingi sana katika lugha nyepesi tunachanganya dhana ya dola na serikali. Serikali ni chombo kimoja tu katika vyombo vitatu vinavyokamilisha dola. Ni muhimu sana kutofautisha serikali na dola.

Kwa mfano, huko Zanzibar kabla ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, CCM ndicho kilikuwa chama tawala. Kwa hivyo, tunasema ilikuwa serikali ya CCM, lakini dola ni ya Zanzibar. Kama, kwa mfano, CUF wangeshika madaraka, serikali ingekuwa serikali ya CUF, lakini dola ingebaki kuwa dola ya Zanzibar.

Sasa mara nyingi katika msamiati wa kawaida maneno serikali na dola yanachangaywa. Ili kujua tafsiri yake sahihi hatunabudi tuangalie maneno haya katika muktadha (context) wake.

Sasa tuangalie mabadiliko ya 10 yanasemaje: Nukuu ya ibara ya 1:

Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya watu wa zanzibar.

Neno linalotatiza hapa ni “nchi”. Lakini tujiulize, neno hili ‘nchi’ inamaanisha dhana ipi? Hoja yangu ni kwamba neno ‘nchi’ katika muktadha wa Katiba inamaanisha dhana ya DOLA na ndivyo limetumika katika Katiba ya Zanzibar pamoja na Katiba ya Muungano. Nitathibitisha:

1. Ang. 9(1) ya Katiba ya Zanzibar: “Zanzibar ni nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii”. Maneno hayo hayo yametumika katika Katiba ya Muungano: Ang. Ibara ya 8(1): “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii …”. Tafsiri yake rasmi ya kiingereza ni, nitanukuu tafsiri ya 1998: “The United Repiublic of Tanzania is a state which adheres to the principles of democracy and social justice ….”. Katika hili hakuna shaka kwamba neno NCHI limetumika kumaanisha dhana ya dola, ambayo ni sahihi kabisa.
Hata Katiba ya Mungano inatambua dola ya Zanzibar (pamoja na dola ya muungano). Ninukuu ibara ya 4:

4 (1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwi na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.

Na ibara ndogo (2) inaainisha vyombo hivyo: nukuu:

4 (2). Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni serikali ya Jamhuri ya muungano na serikali ya Mapinduzi ya zanzibar; vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Mahakama ya serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Sasa ukijumlisha vyombo viwili viwili unapata dola ya Muungano na dola ya Zanzibar.

Kwa hivyo, kama Katiba ya Zanzibar imetambua na kufafanua kwamba Zanzibar ni dola, kosa liko wapi? Kwanini, jambo hilo linakuzwa mpaka kudai kwamba Zanzibar imetangaza kuwa nchi?

2. Kama kweli mabadiliko ya 10 yaliitangaza Zanzibar kama Nchi kwa maana ya “country”, basi Zanzibar wangeuandikia Umoja wa Kimataifa (UN) kwamba kwa mujibu wa Katiba yao Zanzibar ni ‘sovereign republic’ yenye ‘international personality’. Hii haijafanyika. Katika ngazi ya kimataifa kuna ‘sovereign republic’ moja tu na ni Jamhuri ya Muungano. Bila shaka, kwa mambo ya ndani mamlaka yamegawanyika kati ya dola ya Muungano na dola ya Zanzibar (divided sovereignty). Na ndivyo inavyotokea katika muungano na shirikisho.

3. Kama kweli, Zanzibar ni nchi yenye madaraka kamili tangu 2010, kwa mujibu wa tafsiri ya Taarifa ya Tume, kwanini baadhi ya Wazanzibari wanadai mamlaka kamili wakati already wanayo tangu 2010?

4. Kama kweli, neno nchi maana yake siyo dola, basi, tujiulize Rasimu katika pendekezo lake la muundo wa serikali tatu limependekeza nchi tatu? Yaani Nchi ya Tanganyika, Nchi ya Zanzibar na Nchi ya Tanzania? Na hii nchi ya Tanzania ni ipi? Ni nchi hewa!

Ni wazi, na inathibitishwa na Rasimu yenyewe, kilichopendekezwa ni nchi moja yenye dola tatu: dola ya Muungano, dola ya Tanganyika na dola ya Zanzibar. Sasa ugumu wa kukubali Zanzibar kama dola uko wapi?

Ni kweli, kama Tume invyosema katika Taarifa yake, kwamba kabla ya mabadiliko haya, Katiba ya Zanzibar ilisema kwamba “Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Kwanini basi Wazanzibari waliona haja ya kutolea ufafanuzi 2010? Ninavyohisi mimi ni kwamba kwa kweli Wazanzibari walichoka na wanasiasa, wasomi na hata mahakama [ang. Hukumu ya Mahakama ya Rufaa iliyoandikwa na Jaji Ramadhani katika kesi ya S. M. Z. v. Machano Khamis Ali & 17 Others,] kutokutambua Zanzibar kama dola. Kipigo cha mwisho kilikuwa mwaka 2008 wakati Mhe. Waziri Mkuu aliposema kwamba Zanzibar siyo Nchi. Kauli hii ya Waziri Mkuu ilileta mabishano na malumbano makali ambayo hatimaye yalitulizwa na Rais Kikwete katika hotuba yake Bungeni. Nionavyo mimi, hii ndiyo sababu iliyowafanya Wazanzibari waweke wazi kwamba Zanzibar ni nchi kwa maana ya dola.

2. Upunguzaji wa Mamlaka ya Bunge la Muungano

Hii inahusu Ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar. Kwanza, ibara hii haikuongezwa wakati wa mabadiliko ya 10. Imekuwa katika Katiba ya Zanzibar tangu 1984, wakati muasisi mmojawapo bado alikuwepo. Na rasimu ya katiba hii iliridhiwa na CCM. Nukuu ya ibara yenyewe ni hii:

132(1) Hakuna Sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka Sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

(2) Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika.

Ibara hii inaweka masharti matatu ili sheria iliyopitishwa na Bunge la Muungano itumike Zanzibar.
a) Iwe kwa ajili ya mambo ya Muungano. Hii haina ubishi kwa sababu ndivyo Ibara ya Katiba ya Muungano (ib. 64) inavyoelekeza.
b) Iwe imepitishwa kulingana na maelekezo ya vifungu vya Katiba ya Muungano. Hii pia haina ubishi.
c) Ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi. Kinachozungumzwa hapa na sheria hiyo kuwa tabled katika Baraza la Wawakilishi kwa taarifa.

Hii haina madhara yoyote. Ni kawaida kabisa kwa nyaraka mbalimbali (kwa mfano sheria ndogondogo zinazopitishwa na serikali za mitaa au Taarifa za Mashirika ya Umma) hupelekwa mbele ya Bunge kwa taarifa. Lakini hii haina maana kwamba Bunge linaidhinisha au linaridhia nyaraka hizo.

Kwa bahati mbaya, Taarifa ya Tume imeongeza sharti lingine jipya la kupata idhini ya Baraza la Wawakilishi ambalo halimo kabisa katika ib. ya 132.

Ili kuthibitisha hoja yake kwamba sheria kama hizo zinahitaji idhini ya Baraza la Wawakilishi, Tume inanukuu mifano miwili. Moja ni Sheria ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Commission for Human Rights and Good Governance Act) na nyingine ni ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority Act) ambazo zilirudishwa na zilitakiwa ziridhiwe na Baraza la Wawakilishi. Lakini hii ilikuwa ni sahihi kabisa kwa sababu sheria zote hizo mbili hazikuwa juu ya mambo ya Muungano – haki za binadamu au uvuvi siyo mambo ya Muungano.

Ukweli ni kwamba ni Bunge la Muungano ndilo lilivuka mipaka ya mamlaka yake kwa kupitisha sheria juu ya mambo yasiyo ya muungano na kutaka zitumike Zanzibar.

3. Upunguzaji wa Mamlaka ya Rais
Jambo hili linahusu madaraka ya rais kuigawa Jamhuri katika maeneo ya utawala, yaani Mikoa na Wilaya. Ni kweli kwamba ibara ya 2 ya Katiba ya Muungano imeweka mamlaka haya mikononi mwa Rais wa Jamhuri lakini anapogawa Zanzibar katika mikoa na wilaya anatakiwa kushauriana na rais wa Zanzibar. Ni kweli pia kwamba, mabadiliko ya 10 yameweka mamlaka haya mikonini mwa Rais wa Zanzibar.

Labda tuchambue jambo hili kwa kina kabla hatujafikia hitimisho.
1. Mambo ya utawala wa mikoa na wilaya, kwa jumla serikali za mitaa, sio jambo la Muungano. Kwa hivyo, ni kosa kutoa mamlaka haya kwa Rais wa Jamhuri. Kwa hivyo, kama kuna kosa, basi ni kosa la Katiba ya Muungano na sio Katiba ya Zanzibar.

2. Katiba ya Zanzibar ya 1979 (ambayo ilikuwa katiba ya kwanza ya Zanzibar baada ya mapinduzi) katika ibara yake ya 2(2) inasema, nainukuu:

Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar aweza kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu au kukubaliwa na Chama cha Mapinduzi.

Rasimu ya Katiba ya 1979 iliidhinishwa na Kamati Kuu ya CCM.

Kwa hivyo, kilichofanyika na mabadiliko ya 10 ni kurudisha mamlaka haya mikononi mwa Rais wa Zanzibar ambayo ni sahihi. Kwa hivyo, kama kuna Katiba inayotakiwa kurekebishwa, basi ni Katiba ya Muungano na sio Katiba ya Zanzibar.
4. Upunguzaji wa Mamlaka ya Mahakama ya Rufaa
Ni kweli kwamba Mahakama ya Rufaa ni jambo la Muungano, ingawa uamuzi wa kuongezwa kwake katika orodha ya mambo ya Muungano una utatanishi. Ni kweli pia kwamba Katiba ya Zanzibar imeweka mipaka ya mamlaka yake, kwa mfano, kesi kutoka Mahakama za Kadhi, kesi kuhusu tafsiri ya Katiba ya Zanzibar na kesi kuhusu haki za binadamu haziwezi kwenda Mahakama ya Rufaa. Kwa hivyo, kuna mgongano kati ya Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Muungano. Hata hivyo, Mahakama zetu, pamoja na Mahakama ya Rufaa yenyewe, wamekwepa kutolea maamuzi jambo hili, wamewaachia wanansiasa kufanya marekebisho.

Mgongano huo ungeepukika, pale ambapo Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashiriki ilipovunjika, kama kungekuwa na mashauriano zaidi na Wazanzibari jinsi ya kuunda Mahakama ya Rufaa ya Muungano na mamlaka yake. Hata hivyo, kwangu mie jambo hilo sio kubwa na wala halipaswi kukuzwa. Linarekebishika bila shida. Na mgongano huo haujawahi kuhatarisha uhai wa Muungano.

Mwisho, ningependa kutoa tahadhari. Hoja za Tume zinajaribu moja kwa moja kulaumu Wazanzibari kwamba ni wakosaji kwa kuvunja Katiba. Hio sio sahihi. Ningependa kutoa mfano moja ambao uzito wake unapita hoja hizo zote. Na mfano huu utadhihirisha kwamba kuna kasoro kubwa mno katika Katiba ya Muungano.

Ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano inasema kwamba Mamlaka ya Kutunga sheria juu ya mambo ya Muungano yamo mikononi mwa Bunge la Muungano na mamlaka ya kutunga sheria za Zanzibar juu ya mambo yasiyo ya muungano ni ya Baraza la Wawakilishi. Hii ni sawa kabisa na inaendana na mfumo wa “serikali mbili”, au kwa usahihi zaidi, dola mbili, zilizowekwa na Hati ya Muungano mnamo mwaka 1964 na katika Katiba ya Muungano wa 1977.

Lakini ibara ndogo ya 64(4) inasema: [nitanukuu maneno yanayohusika]
Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote haitatumika Tanzania Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo –
(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vivile Tanzania Zanzibar ….; au
(b) ……
(c) Sheria hiyo iwe inahusu Mambo ya Muungano, … .
Maana ya ibara hii ni kwamba Bunge la Muungano linaweza kutunga sheria juu ya mambo yoyote yale hata kama sio mambo ya Muungano na yatatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ilimradi imesema tu kwamba yatatumika Bara na Zanzibar. Hii, kwa kweli, inamaanisha kwamba Bunge la Muungano limepokonya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi na kwa hivyo kuvuruga kabisa muundo wa dola mbili. Ibara hii iliwekwa katika mabadiliko ya Katiba ya Muungano ya 1984 baada ya machafuko ya hali ya hewa wakati Mheshimiwa Warioba akiwa Waziri wa Sheria. [Ilitakiwa kuwekwa neno ‘na’ badala ya ‘au’.] Mbaya zaidi, ibara hii imetumika kupitisha zaidi ya shertia 40 juu ya mambo yasiyo ya muungano na kutumika Zanzibar mpaka Wazanzibari wakaamka na kupinga sheria zile mbili ambazo tumekwisha zizungumzia.

Ibara hii moja kwa moja inaathiri muundo uliowekwa na Hati ya Muungano. Kwa hivyo, tunapolaumu Wazanzibari kuvunja katiba lazima pia tuangalie upande mwingine wa sarafu. Na tukifanya hivyo ndio tutaweza kusawazisha mambo haya yote katika Katiba mpya, badala ya kuyatumia kuhalalisha muundo wa serikali tatu ambao ni wazi kabisa kwamba utavunja muungano.
***
Sasa nije kwenye hitimisho la Tume. Kama nilivyoonesha, hoja tatu kati ya nne za kudhihirisha hoja kuu ya Tume sio sahihi. Na hoja ya Mahakama ya Rufaa ni dogo. Kwa vyovyote vile, hoja hii ya mwisho haituruhusu kabisa kuhitimisha kwa kusema kwamba waasisi waliunganisha nchi mbili ikawa moja na sasa tunazo nchi mbili zenye serikali mbili. Kutokana na uchambuzi wangu ambao ninawasilisha kwenu hitimisho langu ni kwamba waasisi walidhamiria nchi moja yenye dola mbili na mpaka sasa tuna nchi moja yenye dola mbili. Ni kweli muundo tuliyonao una matatizo lakini haya yanaweza kutatuliwa bila kuhatarisha uhai wa muungano.

Hoja ya Tume kwamba kwa kuwa ni vigumu kwa “Zanzibar kurudi kwa hiyari kwenye hali ya awali” na ndio maana wamependekeza Serikali ya Tanganyika haina mashiko na inagongana. Kwanza, kama nilivyoeleza kwamba sio sahihi kusema kwamba Zanzibar imetangaza kuwa nchi huru kwa maana ya nchi. Pili, hata kama hii ingekuwa kweli, au kuna migongano kati ya Katiba hizi mbili, basi ilikuwa ni lengo la mchakato wa Katiba Mpya kusawazisha na kuondoa migongano hii. Isitoshe, pendekezo lenyewe la Tume halitambuwi Zanzibar kuwa nchi na Tanganyika kuwa nchi, bali linaweka dola tatu katika nchi moja badala ya dola mbili katika nchi moja kama ilivyo chini ya Katiba ya 1977. Na hatunabudi, sisi ambao tunadai kuwa wataalam wa sheria za Katiba kuwaeleza wanachi wote kwamba ikiwa Katiba Mpya (ya aina yoyote ile) itapita kwa kura ya maoni ya wananchi wa pande zote mbili, basi sheria na katiba ya sasa ya Zanzibar hazinabudi zirekebishwe au hata kuandikwa upya ili kuendana na Katiba Mpya ya Muungano. Kwa kuwa itakuwa ni mara ya kwanza kwa katiba ya Muungano kupitishwa kwa kura ya maoni, hakuna yeyote, pamoja na wanasiasa wa pande zote mbili, wa kung’ang’ania katiba yao ya sasa. Kisheria na kikatiba, Hati ya Muungano pamoja na Katiba ya Zanzibar ya 1984 hazitakuwa na nguvu za kisheria; zitakuwa, kama tunavyosema, superceded. Muungano utakuwa umewekwa kwenye misingi imara ya kikatiba ambayo chimbuko lake ni wananchi wenyewe wa pande zote mbili.
HITIMISHO
Katika kuhitimisha mada yangu juu ya hoja hizi zinazojikita kwenye mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, ningependa kutoa tahadhari.

1. Bila kukusudia, hoja hii kama ilivyoandikwa katika Taarifa ya mwisho ya Tume inaweza ikawa na hatari. Hii ni kwa sababu, moja, inaamsha na kushawishi hisia za Utanganyika, na, pili, kufanya watu wa Tanzania Bara wawachukie wenzao wa Zanzibar. Kwa hivyo, inahatarisha muungano badala ya kuuimarisha. Na muungano wowote hauwezi kudumu, au kudumu kwa amani, kama hauna mizizi katika watu na hisia zao.

Mimi binafsi sina shaka kwamba wazee wa Tume hawakuwa na nia hii. Naamini kabisa kwamba wazee hawa walikuwa na nia njema tu. Lakini kama usemi wa kizungu unavyosema: The road to hell is paved with good intentions kwa maana kwamba ‘Njia ya jehanam imetandikwa na nia njema.’

2. Juu ya hilo la Utanganyika, ningependa kuongeza maneno machache hasa kwa faida ya vijana wetu. Nimeshangaa kidogo kwamba hata mzee na mwanazuoni mwenzangu ametumia msamiati wa ‘Utaifa wa Tanganyika’ bila kudadisi kihistoria ‘Utaifa wa Tanganyika’.

Kwa muhtasari tu, kabla ya vita vya kwanza, hatukuwa na Tanganyika. Tulikuwa na German East Africa ambayo eneo lake lilijumuisha Burundi, Rwanda na eneo hilo la ‘Tanganyika’ chini ya himaya ya ubeberu wa Wajerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika vita, Rwanda na Burundi ziligawiwa kwa Ubelgiji na Tanganyika kwa Uingereza. Waingereza ndio wakaunda neno hili ‘Tanganyika’ na iliitwa ‘Tanganyika Territory’, yaani, ni bustani ya wakoloni, sio taifa.

Mababu zetu waliopigania uhuru walijikita kwenye dhana ya Utaifa wa Kiafrika, kama alivyoeleza vizuri tu Profesa Mpangala. Vyama vya wananchi, kutoka TAA (Tanganyika African Association) mpaka TANU (Tanganyika African National Union), viliweka msisitizo kwenye ‘African’, Uafrika wao. Iliwabidi kuweka neno Tanganyika kwa sababu tu ndio lilikuwa eneo la utawala wa wakoloni.

Tulipopata uhuru mnamo Desemba 1961, hatukuwa taifa kwa sababu mkuu wa nchi bado alikuwa Malkia. Mwezi wa Novemba 1962 ndio tukawa Jamhuri ya Tanganyika wakati Mwalimu alipochaguliwa kuwa Rais. Na Mwalimu tangu mwanzo alisistiza kwamba sisi hatukuwa na taifa bali ni mkusanyiko wa makabila na ilikuwa jukumu la serikali huru kujenga utaifa (nation-building). Lakini Mwalimu hakupata muda wa kutosha kujenga utaifa wa Tanganyika kwa sababu mwezi wa Aprili 1964, yaani baada ya miezi 14 tu, tukaungana na Zanzibar kuwa Tanzania. Na kwa takriban nusu karne tumekuwa tunajenga Utaifa wa Tanzania. Sasa hii dhana ya Utaifa wa Tanganyika, au Utanganyika, unatoka wapi? Na mantiki na historia yake ni ipi?

Ningependa kujua hapa tulipo ni vijana wangapi kati yenu mlizaliwa kama Watanganyika. Nyosheni mikono. Nyinyi wote mlizaliwa mkiwa Watanzania, utaifa wenu ni Utanzania, Utambulisho wenu ni Utanzania, mnajitambua kama Watanzania na mnatambuliwa na wengine kama Watanzania.

Ukweli ni kwamba mking’ang’ania Utanganyika wenu ambao wala hamjui, mtakuwa mnavunja taifa na ndio maslahi na matakwa ya mabeberu na wanasiasa wachache wenye uchu wa madaraka. Na Utanganyika wenu hautadumu kwa sababu mtaanza kudai sasa Jamhuri ya Makonde na Jamhuri ya Sukuma! Mtakuwa vipande vipande. Hivi sio vitisho; kuna mifano hai mbele yetu. Somalia imesabaratika, Libya pia, Sudan, Afrika ya Kati, na nchi nyingine nje ya Afrika – Afghanistan, Pakistan, Syria, Iraq bila kutaja nchi za Ulaya.

3. Kuna suala la Utaifa wa Zanzibar. Ukweli wa kihistoria ni kwamba Wazanzibari angalau wanaweza kuzungumzia utambulisho wao kwa sababu Zanzibar ina umri wa zaidi ya karne mbili. Na katika muungano wetu utambulisho wao ulipewa kipaumbele kuondoa hisia za kumezwa na kupoteza utambulisho wao kutokana na hali halisi ya watu wachache, nchi ndogo n.k. Na Zanzibar kupewa special dispensation sio jambo geni hata kidogo. Popote pale kunakokuwa na muungano wa nchi ambazo hazilingani kutakuwa na special dispensation.

Mie sina shaka kwamba kama tungefanikiwa kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki mara baada ya uhuru, Zanzibar ingeomba na ingepewa special dispensation. Ushahidi upo.

4. Mwisho, narudia tu nilichosema katika mhadhara wangu niliotoa juu ya Rasimu ya Kwanza. Rasimu hii ina matatizo mengi. Kwa kweli Muungano hauwezi kudumu ikiwa Rasimu hii itapitishwa na Bunge Maalum kama ilivyo. Shirikisho lolote lile ambalo lina serikali ya shirikisho dhaifu, bila vyanzo vya uhakika vya mapato, bila udhibiti madhubuti wa rasilimali, bila kuwa na mamlaka juu ya sera za uchumi, fedha, forodha na masoko ya nje, na bila kuwa na mamlaka juu ya ukusanyaji wa kodi, hauwezi kujiendesha.

5. Pamoja na hayo, mimi sisemi kwamba muundo wa serikali au dola mbili tulionao hauna matatizo. Unayo. Lakini tusiangalie muungano kwa jicho la idadi ya serikali. Tuuangalie kwa mtazamo wa demokrasia. Na tukifanya hivyo tunaweza kubuni muundo ambao utakidhi mahitaji yetu bila kuhatarisha uhai wa muungano.

6. Mie mwenyewe nimewahi kupendekeza mfumo mbadala lakini sina muda wa kutosha kuelezea mfumo huo. Hata hivyo, nikipata nafasi nyingine mwafaka nitajaribu kufanya hivyo.

7. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.


CHANZO: WANABIDII

TAARIFA YA MSAJILI KUHUSU MWENENDO WA KAMPENI CHALINZE


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MWENENDO WA KAMPENI KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA JIMBO LA CHALINZE

1.0 UTANGULIZI

Ndugu zangu wanahabari, awali ya yote nawashukuru sana kwa kuitikia wito wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Natambua mna majukumu mengi ya kuhabarisha umma, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba na uchaguzi huu mdogo wa Chalinze.

Kwanza nianze kwa kuvipongeza vyama vyote vya siasa ambavyo vimeweka wagombea katika uchaguzi huu. Hivi sasa hapa nchini kuna vyama vya siasa ishirini na moja (21) vyenye usajili wa kudumu na ambavyo kisheria 
vinastahili kushiriki chaguzi zote, lakini vyama vya siasa vilivyofanikiwa kuweka wagombea ni vitano (5) tu, AFP, CCM, CHADEMA, CUF na NRA. Pongezi hizi nazitoa kwa kutambua kuwa, kushiriki uchaguzi ni gharama.

2.0 MAJUKUMU YA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KATIKA UCHAGUZI

Kabla ya kuwaeleza madhumuni ya kuwaita, naomba kwanza nitumie nafasi hii kuwaeleza majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika uchaguzi, kwani kuna wadau ambao bado hawaelewi kwa nini Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ipo katika jimbo la Chalinze na Ofisi hii inafanya nini katika uchaguzi huu.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba 7 ya mwaka 2010 katika chaguzi zote ikiwamo chaguzi ndogo za wabunge na madiwani.

Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inafuatilia na kutoa adhabu kwa vyama vya siasa vinavyojihusisha na vitendo vifuatavyo:-

a)Chama ambacho wanachama na/au mashabiki wake wanajihusisha na vitendo vya fujo, vurugu na uvunjifu wa amani wa aina yoyote ile;

b)Chama ambacho viongozi na/au wanachama wake wanatumia maneno ya matusi, kashfa na uchochezi; na

c)Chama ambacho kinatumia na/au mgombea wake anatumia mali za Serikali katika kampeni na uchaguzi.

Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kuweka sawa uwanja wa ushindani katika siasa, kwa kufuatilia na kupendekeza/kutoa adhabu kwa chama cha siasa na/au mgombea anayejihusisha na masuala yafuatayo.

a)Kutumia fedha nyingi zaidi ya kiwango kilichowekwa na Sheria katika jimbo husika. Katika jimbo la Chalinze sheria inasema mgombea asitumie zaidi ya shilingi milioni hamsini;

b)Uwazi katika matumizi ya pesa katika kampeni ambapo kila chama, mgombea na taasisi za kiraia zinazoshiriki katika kampeni, zinatakiwa kutoa taarifa ya fedha zitakazotumia katika kampeni na uchaguzi na baada ya uchaguzi kuisha, kutoa taarifa ya fedha zilizotumia katika uchaguzi.

c)Chama cha siasa au mgombea kushawishi kupigiwa kura au kushawishi wananchi kuacha kumpigia kura mgombea mwingine kwa kutoa vitu vya thamani kama pesa, chakula, pombe au ahadi za kupewa cheo au kazi.

d)Matumizi ya mali za Serikali katika kampeni;

e)Vyombo vya habari vya Serikali vinavyopendelea upande mmoja katika kampeni.

Aidha, jukumu lingine la muhimu sana ni kutoa elimu kwa wananchi, vyama vya siasa na wagombea, kuhusu wajibu wao na makatazo yaliyomo katika Sheria tajwa hapo juu.

3.0 MADHUMUNI YA KUONGEA NA WANAHABARI

Ndugu wanahabari, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeona sasa ni wakati muafaka wa kufanya tasmini ya kampeni zinavyofanyika katika jimbo la Chalinze, kwani tumeshavuka nusu ya muda wa kampeni na umebaki muda wa wiki moja tu, ambao kwa maneno ya mitaani naweza kusema ni muda wa lala salama.

Hivyo, tumewaita katika mkutano huu kwa madhumuni yafuatayo:

a)Kuwafahamisha wananchi kupitia kwenu kazi zilizofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tangu kampeni za uchaguzi mdogo wa Chalinze zianze mpaka sasa;

b)Kuwafahamisha wananchi tathimini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu mwenendo wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Chalinze; na

c)Dhumuni jingine la kuwaita ni kuwaeleza shughuli iliyopo mbele yetu mapaka siku ya uchaguzi.

4.0 KAZI ZILIZOFANYWA MPAKA SASA

Ndugu wanahabari; Kazi kubwa zilizofanywa na maafisa wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tangu kampeni za uchaguzi wa Chalinze zianze ni zifuatazo:-

a)Kutoa elimu kwa umma kwa wananchi, vyama vya siasa na wagombea kuhusu wajibu wao na makatazo yaliyomo katika Sheria ya Vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi;

b)Kuonana na wadau wa uchaguzi kupata maoni na malalamiko kuhusu kampeni; na

c)Kufuatilia taarifa na malalamiko ya uvunjifu wa Sheria tajwa hapo juu, ili kujua ukweli na kuwaasa wahusika wajirekebishe, wasipojirekebisha kuchukua hatua za stahiki.

Mpaka sasa tumeonana na wagombea vyama vinne, CUF, CCM, CHADEMA na NRA, bado mgombea mmoja wa AFP ambaye tunaendela kuwasiliana naye.

5.0 TATHMINI YA KAMPENI KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA CHALINZE

Ndugu wanahabari, mpaka sasa kampeni zinaendalea vizuri, ila kuna malalamiko na vitendo vichache vya uvunjifu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambavyo kimsingi malalamiko mengi na vitendo vingine vinahitaji uchunguzi wa kina.

Baadhi ya vyama vya siasa vimealalamikia vitendo vya kuingiliwa na wafuasi au wanachama wa chama kingine katika mikutano yao ya kampeni, mabango yao kuchanwa, bendera kushushwa, viongozi, wanachama na wafuasi wao kupigwa na ununuzi wa shahada za mpiga kura. Aidha, kumekuwa na matumizi ya maneno ya kashfa na dhihaka katika majukwaa ya kampeni.

Kimsingi, ikiondoa matumizi ya maneno za kashfa na dhihaka jukwaani, ambayo yanasikika kwa watu waliopo na muongeaji anaonekana na vitendo vya wanachama na mashabiki wa chama kuingilia mkutano wa kampeni wa chama kingine, vitendo vingine vinahitaji uchunguzi wa kina wa taasisi husika, ili kujua wahusika na mazingira ambayo kitendo husika kimetokea, kwa lengo la kuchukua hatua stahiki.

Kwa upande wake, Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa inaendelea kufuatilia malalamiko iliyopata kutoka kwa vyama vya siasa na wagombea, ili kupata undani wake na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuchukua hatua stahiki. Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ipo makini na ufuatiliaji wa masuala ya vyama vya siasa kuvunja Sheria inazozisimamia hasa wakati wa uchaguzi. Ila haiwezi kuchukua hatua stahiki kwa chama husika bila kuwa na ushahidi wa kutosha kuwa, chama hicho kimehusika na kitendo hicho cha uvunjifu wa sheria.

Ndugu waandishi wa habari, natumia nafasi hii pia kusisitiza kuwa, ahadi aliyoitoa Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francisi S.K. Mutungi, kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatafuta mwarobaini wa vurugu katika kampeni, haikuwa utani wala ahadi hewa. Kwani uzoefu tunaoupata katika chaguzi hizi ndogo unatusaidia katika kutengeneza mwarobaini huo.

6.0 WITO WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KWA VYAMA VYA SIASA NA WAGOMBEA

Ndugu zangu wanahabari, kwa kuzingatia mwenendo wa kampeni na ukweli kuwa, kampeni huwa kubwa na pilika nyingi wiki ya mwisho kuelekea siku ya uchaguzi, naomba nitumie nafasi hii kuviasa vyama vya siasa na wagombea wote katika uchaguzi huu mdogo wa Chalinze ifuatavyo:-

a)Kuepuka kutumia maneno ya matusi, kashfa na mambo yanayofanana na hayo, badala yake wanadi sera zao, kwani licha ya kuwa maneno ya matusi na kashfa ni kinyume na sheria na maadili, lakini wananchi wanahitaji kulikiliza sera si matusi na kashfa;

b)Kuepuka vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani, kwani licha ya kuwa vinaleta madhara kwa watu na mali zao, lakini pia vinawaogopesha wananchi kushiriki kampeni na hata kwenda kupiga kura;

c)Kutochukua hatua za kisheria mkononi, badala yake wakiona au kusikia mtu kavunja sheria watoe taarifa katika vyombo husika;

d)Kutojihusisha na vitendo vya uchokozi mfano kuingilia mikutano ya kampeni ya chama kingine;

e)Kutojihusisha na vitendo vyovyote vya rushwa, mfano kununua au kuuza shahada ya mpiga kura;

f)Kutoa taarifa kwa vyombo husika ili zifanyiwe kazi, badala ya kutoa tu kwa wanahabari na kulalamika;

g)Kuepuka propaganda ambazo zinawatia hofu wananchi na wapiga kura.

Aidha, Waandishi wa habari waepuke kutoa taarifa bila kuzifanyia uchunguzi ikiwamo kupata maoni ya upande wa pili, kwani kufanya hivyo kunaweza kuwapa hofu wananchi wa nchi nzima na wapiga kura ikiwa taarifa iliyotolewa ni ya kuogofya wakati si ya kweli.

7.0 KAZI ZILIZO MBELE YETU

Siku za kampeni zilizobaki, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imejipanga kuendelea kutekeleza majukumu yake niliyoyataja hapo juu, isipokuwa siku ya uchaguzi tarehe 06 Aprili, 2014, Ofisi imejipanga kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufuatilia chama cha siasa na wagombea wanaofanya mambo yalikatazwa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ikiwamo kubeba wapiga kura katika vyombo vya usafiri kuwapeleka au kuwatoa katika vituo vya kupiga kura.

8.0 FAIDA YA UWEPO WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KATIKA CHAGUZI MBALIMBALI

Ndugu waandishi wa habari; naomba nitumie nafasi hii pia kuwaeleza faida za uwepo wa Ofisi ya Msajili ya Vyama vya Siasa katika chaguzi mbalimbali hasa chaguzi ndogo.

Uwepo wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika chaguzi mbalimbali unasaidia uchaguzi kufanyika vizuri, kwa amani na utulivu na wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kwa namna zifuatazo:-

a)Kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Ofisi vya Msajili wa Vyama vya Siasa inasaidia kuweka uwanja sawa wa ushindani katika uchaguzi kwa kuepusha matumizi makubwa ya fedha katika kampeni, kuweka uwazi katika matumizi ya fedha na rasilimali nyingine katika kampeni na kuepusha matumizi ya mali za Serikali katika kampeni.

b)Kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Ofisi vya Msajili wa Vyama vya Siasa inasaidia kuepusha vitendo vya vurugu, matusi na uchochezi kwa kuchukua hatua stahiki kwa chama kinachohusika kwa mujibu wa Sheria.

Aidha, kitendo cha maafisa wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwepo tu katika kampeni, kinawatia hofu wanasiasa na vyama vya siasa vyenye lengo la kuvunja sheria, kwani wanaelewa fika kuwa, Ofisi ya Msajili ipo na inafuatilia. Hivyo, uwepo wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kampeni za uchaguzi hupunguza sana vitendo vya uvunjifu wa sheria nilizozitaja hapo juu.

9.0 MWISHO

Namalizia kwa kutoa wito kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huu kuelewa kuwa, vinawajibu wa kisheria wa kuwaasa na kuwadhibiti wanachama na wagombea wao kuheshimu na kufuata Sheria zote zinazohusika. Hivyo, kila chama kitekeleze wajibu wake, ili uchaguzi huu unafanyike kwa amani na utulivu. Nawaomba pia wanachi wa Chalinze waendelee kuhudhuria mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa bila hofu na woga. Aidha, washawishike kwa hoja na sio rushwa. Watoe taarifa kwa vyombo husika pale wanapoona mtu yeyote anajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa Sheria na wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.

Asanteni kwa kunisikiliza na ninawatakia kazi njema katika kazi yenu ya kuwahabarisha wananchi kuhusu kampeni za uchaguzi wa Chalinze.

Sisty L. Nyahoza
Kny: MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
30 Machi, 2014

Sunday 30 March 2014

WALEMAVU WA VICOBA WATAPELIWA


Na Oliver Motto, Iringa


KAMA inavyofahamika hali ngumu ya maisha sasa inatoa funzo kwa kila wananchi kuona umuhimu wa kutafuta namna ya kuhifadhi fedha, iwe katika taasisi za kifedha, vikundi vya mitaani (upatu) na hata katika vikundi rasmi vya Benki za Wananchi wa Vijijini -VICOBA.
Asilimia kubwa ya wananchi wa mjini na vijijini wamehamasika kujiunga katika vikundi vya aina hiyo, huku baadhi yao wakikopeshana fedha kwa riba nafuu ili kusaidiana katika changamoto mbalimbali za kimaisha, iwe kusomesha watoto au kumudu mahitaji mbalimbali ya maisha.
Mwamko huo wananchi pia unatokana na serikali  kuwahimiza wananchi kujiunga katika vikundi mbalimbali vya akiba na mikopo, ili wananchi waweze kukopesheka kwa fedha kutoka serikalini na hata kutoka katika asasi mbalimbali, baada ya wananchi kutambulika kupitia katika vikundi vyao.
Jambo hilo ni jema na lenye tija katika maisha haya ya sasa ambayo yanahitaji akili ya ziada, na pia nisema mpango huo unahitaji pongezi kwani umelenga moja kwa moja kumkwamua mwananchi kutoka katika hali ya umasikini wa kipato na hivyo kuwa na uchumi wa kuendesha maisha yake naya familia yake pia.
Lakini kuna msema wa waswahili uliosema "Kwenye wengi kuna mengi" Msemo huo unakamilika kutokana na hivi karibuni kuzuka utata katika VICOBA, ambapo wanachama wa vikundi hivyo wamelalamikia kutapeliwa fedha zaidi ya shilingi Milioni 200  na kiongozi mmoja wa ngazi ya Taifa.
Hatua hiyo imewekwa hadharani katika uzinduzi wa Kikundi cha Vicoba cha Nyerere kilichopo katika eneo la Kibwabwa Kata ya Ruaha Manispaa ya Iringa, na kuwa ubadhirifu huo umefanywa kwa kikundi cha wanachama wa Vicoba Wenye Ulemavu Ilala jijini Dar es Salaam.
Wakilalamikia hali hiyo wanachama hao wamesema licha ya kuhimizwa kujiunga katika vikundi ili kupata mikopo ya fedha, kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia fulsa hiyo kujinufaisha hatua ambayo inatishia kuwasambaratisha.
Wamesema kuna kila sababu wanavicoba wote nchini kuungana katika kudai haki zao pindi   wenzao wanapokumbana na changamoto hizo za kifedha ili kuimarisha umoja wao kwa kuwa tabia hiyo inachangia kuwarudisha nyuma wanavicoba.
George Kalenga mwanachama wa kicoba cha Nyerere amesema baada ya kupata taarifa ya dhuruma ya fedha za misaada ya walemavu wamejikuta wakikata tamaa, ambapo amewataka viongozi wote wapenda haki wa serikali kuchukua hatua dhidi ya tabia ya kiongozi huyo.
Fatuma Mkini naye amesema dhuruma kwa kiongozi mkubwa wa aina hiyo ni jambo la aibu mbele ya jamii, na hasa wadhfa alionao kiongozi huyo ambaye haendani na matukio ambayo amekuwa akiyafanya, na hasa kwa hilo la dhuruma kwa watu wenye ulemavu, ambapo ameiomba serikali kulifuatilia suala hilo ili kiongozi huyo arejesxhe fedha hizo kwa wahusika.
Fatuma amesema kulinyamazia suala hilo ni kudumaza uchumi na kukuza pato la wananchi, kwa kuwa wao wamejiunga katika vikundi hivyo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi, huku shinikizo kubwa likitoka kwa serikali.
Spedito Sanga amesema viongozi wa aina hiyo wanatakiwa kupigiwa kelele ili tabia hiyo isikike kwa wananchi, kwa kuwa kulinyamazia kimya jambo hilo ni njia ya kulifanya likue na hivyo tatizo hilo kuwakumba wananchi walio wengi.
Tisiana amesema kiongozi huyo wa ngazi ya juu awali alifanya utapeli wa aina hiyo kwa waratibu wa mikoa yote Tanzania, ambapo aliwahadaa waratibu akiwemo nayeye kuchangia fedha ili kuanzisha hisa.
"Ukweli baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wanatutesa sana, sasa kama hili linawavunja moyo wanachama, kwani ametia doa hasa ukiangalia kundi ambalo amelifanyia ubadhirifu ni kundi la walemavu, kiongozi mkubwa kabisa anawarubuni wanachama wakaweke pesa kwenye akaunti yake,".
Amesema waratibu kupitia mpango wa uwahamasishaji wa kujiunga na vicoba kwa kundi la  walemavu, lakini kupitia hili dosari hiyo hata wanachama wengine hawana imani na viongozi na hivyo kazi hiyo kuifanya kwa ugumu zaidi tofauti na awali.
Amesema sasa anataka kuwafikisha Mahakamani wote watakaofika mkoani kwake na kuwavuruga wanachama wa vicoba, kwani hali hiyo imelenga kurudisha nyuma uchumi wa wananchi tofauti na malengo ya uanzishwaji wa vikundi hivyo.
"Hili siwezi kulifumbia macho, kwani hii tabia sasa inaota mizizi, kiongozi huyu amekuwa akituvuruga sana, kwani kuna wakati tulipewa fedha shilingi milioni miamoja na mkurugenzi wa IPP Regnand Mengi, fedha hiyo aling'ang'ania iingizwe kwenye akaunti yake, lakini mpaka leo hii hatujui zipo wapi na zinafanya nini, nitaongea hili mpaka dakika ya mwisho," Alisema.
Amesema kundi la walemavu baada ya kupata taarifa ya utapeli huo wameingia woga kujiunga katika vikundi, huku wengi wao wakitangaza kujiondoa katika umoja huo kwa kuhofia adha hiyo.
Tisiana ameitaka serikali kuingilia kati suala hilo ili kurejesha imani kwa wanachama, kwa madai kuwa kulifumbia macho tatizo hili litaondoa imani pia kwa serikali ambayo nayo imekuwa ikiwahimiza wananchi kujiunga na vicoba.
Nyerere VICOBA wamesema baadhi ya viongozi  wao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kwa manufaa yao,  kwa kusanya fedha  za misaada ya vikundi kupitia Akaunti zao binafsi, jambo ambalo linawakatisha tamaa na kamwe hawatakubaliana nalo.
Mapema mwaka 2013 baadhi ya wanachama wa  vikundi vitatu vya VICOBA katika Wilaya ya Kilolo mkoni Iringa walilalamikia kutapeliwa zaidi ya shilingi milioni 30, baada ya kuibuka kwa mtu mmoja na kuwachangisha fedha kwa madai kuwa anataka kuwasaidia na kuongeza hisa zao.

KINANA AICHAMBUA RASIMU YA WARIOBA


KATIBU Mkuu wa CCM, Kanali Abdulrahman Omar Kinana
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameikosoa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akidai imeshindwa kuwasilisha kwa usahihi maoni yaliyotolewa na wananchi.
Alisema Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba iliwasilisha maoni yaliyokuwa yakiunga mkono mlengo wake badala ya maoni halisi yaliyotolewa na Mabaraza ya Katiba.
Madai hayo mapya ya Kinana yamekuja wakati tayari Tume hiyo imevunjwa rasmi na Rais, kwa mujibu wa sheria.
“Kulikuwa na utaratibu wa kupata maoni kutoka kwenye mabaraza na kuna kata zilihojiwa, tume haijatuambia kwa sababu gani hawakuyasema wanayoyataka wao,” alisema Kinana.
Alisena kuwa kulikuwa na mabaraza 171, lakini Tume pia ilishindwa kutoa takwimu za watu wangapi walikuwa wakiunga muundo wa muungano wa serikali mbili au tatu katika mabaraza hayo.
“Majaji walisema masilahi ya nchi yapo kwenye serikali mbili na wakuu wa mikoa hali kadhalika, lakini mbona Tume hawakusema hayo?” alihoji Kinana.
Katibu Mkuu huyo alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam jana, kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hotuba aliyoitoa katika Bunge Maalumu la Katiba hivi karibuni.
Alisema chama chake kinaunga mkono mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini lazima wahakikishe katiba hiyo ni ya wananchi.
Hii ni mara ya pili kwa viongozi wa juu wa chama hicho kukosoa takwimu za Tume, mara ya kwanza Rais Kikwete alitilia shaka takwimu zilizomo katika ripoti ya Tume hiyo wakati akitoa hotuba yake bungeni.
Kinana alisema pamoja na kuhoji weledi wa Tume ya Warioba pia alitetea hoja ya wingi wa wajumbe wa CCM katika Bunge Maalumu la Katiba.
“Kuna watu kila siku wanalia eti wao wapo wachache na sisi tupo wengi, hii ni lugha ya ajabu kweli kweli, usiku na mchana wanakutana kujadiliana na walipoona chama kimoja kimoja hakiwezi wakaanzisha Ukawa.
“Hao wanaosema tunatumia wingi kupinga masilahi ya nchi, sasa ni masilahi gani yasiyowahusisha CCM?” alihoji Kinana huku akishangaliwa na wafuasi wa chama hicho.

WATU 12 WA FAMILIA MOJA WAFA AJALINI



Moshi. Mji wa Hedaru uliopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro, jana ulizizima kwa vilio na simanzi baada ya waombolezaji 12 wote ndugu, kufariki dunia kwa ajali ya barabarani.
Waombolezaji hao wanawake, walipewa lifti ya gari na Diwani wa Kata ya Hedaru, Gerard Mgwena (CCM), kwa ajili ya kuwapeleka msibani eneo la Majengo ambako mtu mmoja alifariki kwa kusombwa na maji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Robert Boaz alithibitisha ajali hiyo akisema ilitokea juzi saa 2:00 usiku na kwamba ilikuwa mbaya zaidi tangu kuanza kwa mwaka 2014.
“Ni ajali iliyohusisha magari matatu kwa wakati mmoja…; watu 11 walifariki pale pale na mwingine alifariki dunia leo (jana), asubuhi Hospitali ya Rufaa ya KCMC,”alisema Boaz.
Hata hivyo, alisema hakuwa na nafasi nzuri ya kufafanua kwa undani ajali hiyo kwa vile alikuwa nje ya Mkoa wa Kilimanjaro na kuelekeza atafutwe Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa (RTO), JosephMwakabonga.
Akizungumza kwa niaba ya RPC, Mwakabonga alisema, lori aina ya Mitsubish Fusso lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar liligonga kwa nyuma gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up.
Alisema kuwa baada ya kuligonga gari hilo lililowabeba waombolezaji hao, nalo lilisukumwa na kwenda kuligonga lori aina ya Scania lililokuwa na tela lake.
Lori hilo aina ya Scania lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Moshi likiendeshwa na dereva wake, Gabriel David. Madareva wawili wa Toyota Pick-Up na Toyota Fusso wote hawajulikani waliko.
Taarifa zilizopatikana baadaye, zilisema dereva wa Fusso alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC, wakati Kigogo wa CCM aliyekuwa amewabeba waombolezaji akilazwa hospitali moja jijini Arusha.
Mwakabonga aliwataja waliofariki kuwa ni Stella John(45), Salma Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52), Rehema George (29) na Sophia Mbike (51).
Wengine ni Ritha Kalani (55), Mama Kalani Stephano (55), Kolina Mmatha(55), Bahati Daud(25) na Farida Kiondo mwenye umri wa miaka 25.
Majeruhi mmoja, Maria John (33) ambaye ni miongoni mwa watu 10 waliojeruhiwa, alifariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikolazwa kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, watu hao walipata ajali hatua 10 kutoka katika eneo ambalo ndugu yao aliosombwa na maji na kufa, ambapo maiti yake iliokotwa eneo hilo.
Alex Shirima mmoja wa mashuhuda alisimulia kuwa gari la diwani lilikwama kweye topekatikati ya Barabara ya Moshi Dar es Salaam.
Alisema, kabla ya kushuka kuangalia namna ya kulinasua gari lake, likatokea lori gari aina yaFuso kwa nyuma ambalo liliigonga gari lake iwani na kulisukuma mita kadhaa mbele ambako lilikutana uso kwa uso na lori lingine aina ya Scania lililokuwa likitokea Dar es Salaam.
Alisimulia kuwa kutokana na ukubwa wa ajali hiyo, eneo hilo lilitapakaa viungo vya binadamu na damu.
Shirima ambaye ni dereva aliyefika katika eneo hilo dakika mbili baada ya ajali kutokea, alisema eneo hilo ni hatari kwa madereva kwa kuwa mvua zikinyesha, barabara hujaa maji na matope.
Hali ilivyo kijijini
Mmoja wa watoto ambaye mama yake mzazi amefariki katika ajali hiyo, Sebali Mkwizu alisema kuwa kijiji chao kimekumbwa na ukimya na majonzi, huku wakishindwa kuamini kilichotokea.
Alisema kuwa ajali hiyo imechukua maisha ya ndugu zake wanane na kati ya hao, saba walikuwa wakiishi kijijini hapo kwenye nyumba tofauti zinazofuatana.
“Nimepoteza mama yangu mzazi, mama mdogo, shemeji zangu watatu, mke wa ndugu yangu na watoto wawili. Hapa nyumba saba zina msiba,” alisema Mkwizu.
Alibainisha kwamba mazishi ya wanawake hao yanatarajiwa kufanyika leo katika eneo la pamoja kijijini hapo.

“Tumeambiwa watazikwa eneo moja, lakini bado hatujajua ni sehemu gani, hadi kesho (leo) ndiyo tutapata taarifa kamili,” alisema.