Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 18 March 2014

‘NIKIPATA LAKI MOJA TU NIMETOKA’


Nje ya nyumba yupo mtoto mdogo akiwa amelala juu ya kipande cha mkeka. Kwa kumtazama tu utajua anasumbuliwa na maradhi kadhaa kutokana na afya yake kudorora.
Ukimtazama kwa haraka haraka anaonekana kuwa na umri wa miaka minne labda,  la hasha! Ni mtoto wa miaka saba ambaye kama afya yake ingekuwa nzuri, kwa wakati huu alitakiwa kuwa darasani na wenzake.
Anaingia mwanamke akiwa na mzigo kichwani, anautua na kupokea ugeni uliofika kumtembelea. Ni mwanamke mkarimu anayejitambulisha kuwa bibi wa mtoto aliyelala hapo nje.
Anasema siyo huyu tu, anao wajukuu wengine wawili ambao ni wadogo zake yule aliyelala katika kipande cha mkeka, lakini kwa wakati huo wamekwenda kucheza.
Mwanamke huyu anajitambulisha kwa jina la Amina Rajab anasema, kwa miaka minne sasa amekuwa akiishi na wajukuu zake hao baada ya wazazi wao wote wawili kufariki. Amina anasema, kuachiwa wajukuu kwake sio tatizo isipokuwa wakiwa na maradhi kama hawa wajukuu  kwake.
Anasema wajukuu wawili kati ya hao watatu, kwa muda mrefu wamekuwa wakisumbuliwa na maradhi mbalimbali kama vile kukohoa na magonjwa ya ngozi.
“Kuachiwa wajukuu wakiwa na afya  nzuri siyo tatizo, ila wakiwa wanaumwa kama hawa wa kwangu ndiyo ugumu, kwani mguu mmoja, hospitalini, mwingine kutafuta sembe, sasa katika umri huu kwa kweli kwangu ni mtihani mkubwa,” anasema Amina.
Mwanamke huyo anasema amekuwa akipata ugumu wa kufuatilia afya za wajukuu zake, kwa kuwa mzigo wa kuwatafutia chakula una mwelemea.
“Mwanangu hapa unaponiona ninatoka sokoni Buguruni kununua ndizi na machungwa ya biashara, kila siku kiguu na njia kuwatafutia chakula, suala la kwenda hospitalini mara kwa mara linanishinda kwani nitawaua na njaa hawa watoto,” anasema Amina.
Anafafanua kuwa kwa mtaji wake wa Sh12,000, kila siku analazimika kwenda sokoni kwa kuwa huisha tofauti na angekuwa na mtaji mkubwa.
Kwa wengine Sh50,000 ni fedha  ya matumizi ya siku, pengine ni zaidi ya hiyo.  Lakini kwa Bibi Amina ni tofauti, yeye ndoto yake ni kupata mtaji mkubwa ambao ni kati ya Sh50,000 au Sh100,000.

Ndoto ya mama huyo ni kupata mtaji mkubwa wa angalau kuanzia Sh50,000 mpaka Sh100,000 na maisha yake yatabadilika, kwani ataweza kununua bidhaa nyingi na hivyo kutolazimika kwenda sokoni kila siku.
“Katika vitu vinavyoniumiza ni hii hali ya kuamkia sokoni kila siku, sina mtu wa kumuachia wajukuu zangu kwa hiyo ninaamka alfajiri kuwaandalia kifungua kinywa halafu ninakimbilia sokoni kufanya ununuzi,” anasema Amina.
Maisha yake yako vipi
Amina anaishi Tabata Kisiwani katika chumba kimoja anacholipia Sh 20,000 kwa mwezi. Anasema ingawa anatakiwa kulipa kodi yake kila baada ya miezi sita lakini mwenye nyumba amemruhusu kulipia kila baada ya miezi mitatu pale anapopata pesa.
Ni chumba kilichojazana vitu kutokana na kuwa kidogo. Usiku unapoingia wajukuu zake watatu hulala juu ya vitanda naye husogeza vyombo vilivyopo chini na kutandika mkeka hapo.
Anasema: “Ninashukuru wasamaria wema ambao mara kwa mara huniwezesha, nikidunduliza nalipia kodi hiyo miezi mitatu maisha yanaendelea.”
Huamka asubuhi kwaajili ya kuwaandalia kifungua kinywa wajukuu zake kisha huelekea sokoni kununua matunda ambayo huyauza kwaajili ya kupata faida inayomsaidia kuendesha maisha yake. Mchana hufanya shughuli za nyumbani kama kuwaogesha, kuwafulia na kuwaandalia chakula cha mchana na jioni.
Saa kumi na moja jioni hujongea barabarani ambako ndipo huuza ndizi na machungwa. Saa tatu usiku au saa nne hurudi nyumbani.
Matibabu ya wajukuu zake
Ingawa hazungumzii moja kwa moja maradhi yanayowasumbua wajukuu zake, Bibi Amina anasema anataka kuanza kufuatilia matibabu yao ili wapate nafuu na ikibidi waanze masomo.
“Wajukuu zangu wawili hali yao ni kama hivi, huyu unayemuona hapa amedhoofu sana kwasababu aliwahi kugongwa na gari, lakini nia yangu hasa ni kuangalia zaidi matibabu yao kwani wakiwa wazima wa afya na mimi nitaweza kufanya kazi zangu kwa ufanisi,” anasema Bibi Amina.
Anasema zaidi anataka kujua afya ya huyu aliyepo nyumbani akisema: “Huyu anakohoa sana, ninataka nikampime Kifua Kikuu ikibidi, kwani nimemaliza kila ina ya dawa na bado hakiponi.”

Amina anasema atafurahi iwapo atapata msaada wa mtaji mkubwa kwani kawa hatua hiyo ataweza kufuatilia afya za wajukuu zake ambazo zimekuwa zikitetereka kila kukicha.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment