Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 27 March 2014

BUNGE KUAHIRISHWA

Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)


NA WAANDISHI WETU

Hali  ya maelewano miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba imezidi kuwa mbaya kiasi kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anakusudia kuwasilisha maombi kwa Rais Jakaya Kikwete ili aliahirishe.

Pinda alisema hayo jana alipokutana na waandishi wa habari akisisitiza kuwa kwa hali ya mambo ilivyo, hakuna uwezekano wa kupiga hatua katika Bunge hilo.

Kwa maana hiyo, atamuomba Rais Jakaya Kikwete aliahirishe hadi baadaye ili pamoja na mambo mengine kuipa serikali fursa ya kuendelea na shughuli nyingine ikiwamo kuitisha Bunge la Bajeti.

Bunge Maalumu la Katiba lilipangiwa kutekeleza kazi ya kupendekeza Katiba mpya ya nchi ndani ya siku 70.

Matukio kadhaa ya kuviziana na kutuhumiana miongoni mwa makundi ya wajumbe hususani yanayotokana na vyama vya siasa ndiyo yaliyosababisha kusuasua kwa Bunge hilo.

Pinda alisema kuwa kwa jinsi anavyoona mwenendo wa Bunge hilo, haoni uwezekano wa shughuli za Bunge hilo kukamilika kwa muda uliopangwa, jambo ambalo anahisi linaweza kuathiri na shughuli nyingine.

Alisema kwa jinsi mchakato wa kutunga katiba unavyoendelea unaonekana wabunge wanahitaji muda wa kutosha ili waweze kufikia mwafaka

“Bunge hili limepangiwa siku 70 na mwanzoni tuliweka kipengele kuwa linaweza kuongezewa siku 20, lakini kwa kuwa kipengele hicho ulikiondoa na kusema Rais anaweza kuongeza muda kwa namna atakavyoona inahitajika, tukifika hadi Aprili mwishoni au mwanzoni mwa Mei tukaona bado shughuli ni kubwa mbele yetu, inabidi tuombe tukapumzike kisha turudi na kuendelea tukiwa huru zaidi,” alisema Pinda.

Waziri Mkuu alisema uamuzi huo unaweza kukubalika kwa sababu suala la Katiba ni zito linalohitaji wabunge kupata muda mwingi na wakutosha kujadili kwa kina Rasimu ya Katiba ili hatimaye wananchi waweze kupata Katiba iliyo bora.

Aidha, Waziri Pinda alisema kutokana na mwingiliano wa shughul za kiserikali mwaka huu, anafikiria pia kumuomba Rais ili akubali kusogeza mbele uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alisema atapendekeza kwa Rais uchaguzi huo ufanyike mapema mwakani kwa kuwa inawezekana miezi ya Oktoba au Septemba ambayo kwa kawaida uchaguzi huo hufanyika inaweza ikawa ni miezi yenye pilika pilika nyingi, ikiwemo Bunge Maalum la Katiba kama litaahilishwa kupisha Bunge la Bajeti.

Bunge Maalum la Katiba lilianza shughuli zake Februari 18 mwaka huu likitarajiwa kukaa siku 70, lakini mpaka sasa shughuli ya kujadili Rasimu ya Katiba bado haijaanza, hali ambayo inatia shaka kuwa huenda Bunge hilo lisimalize kazi kwa muda uliopangwa.

Hadi sasa shughuli zilizofanyika ni semina za kanuni, kupitisha kanuni, kuapa na kuunda kamati.

SITTA KIKUNDI KINAVURUGA
Wakati Pinda akieleza wasiwasi huo, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amesema ameanza kubaini dalili za kikundi cha watu wachache wanaotaka kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Aliwaambia waandishi wa habari jana jioni baada ya Bunge hilo kuahirishwa kufuatia malalamiko ya wajumbe kadhaa wa upinzani kwamba kuna mpango mchafu wa kuchakachua kanuni.

Alisema wapo wajumbe wachache ambao aliwaita kuwa wameamua kutumia vibaya Umoja wa Katiba wa Wananchi (Ukawa), kuvuruga mchakato huo.

“Kikundi cha wanasiasa wachache ambao wamedharimia kuvuruga mchakato mzima wa katiba hii, tuhuma nilizotupiwa leo (jana) hususani na Mheshimiwa Tundu Lissu ni uongo, uzushi na wala hazikunitendea haki hata kidogo,” alisema Sitta.

Awali Tundu Lissu alisimama kuomba mwongozo, baada ya Sitta kuruhusu wajumbe hao kuomba miongozo ambayo waliiomba asubuhi.

Akiomba mwongozo, Lissu alisema Kiti cha mwenyekiti kimeyumba katika kutetea kanuni za Bunge.

Alisema Machi 11, mwaka huu Bunge lilipitisha azimio la kutunga na kupitisha Kanuni za Bunge Maalumu ikiwemo suala la kura.

Alitoa mfano wa kanuni hizo ni 37 na 38 kuhusu upigaji kura, ambayo alidai kuwa kuna jedwali linaloonyesha kanuni hizo kubadilishwa.

Sitta alisema Bunge hilo limeahirishwa baada ya wajumbe kupinga uwasilishaji wa mapendekezo ya kanuni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho.

Alisema baadhi ya wajumbe waliamua kuchukua karatasi yenye mawasiliano ya Kamati ya Uongozi na Kamati ya Kanuni na kuyapeleka ndani ya ukumbi wakidai kuwa hizo ndizo zinazoletwa ndani ya ukumbi.

Alisema vurugu hizo ni kutaka kudhoofisha jitihada za Rais Kikwete za kuacha kumbukumbu ya kuacha Katiba Mpya wakati atakapotoka madarakani.

Alisema kama watu hao hawana nia ya kupata Katiba Mpya, waondoke na wawaache wale wanaotaka kufanyakazi hiyo, kuliko kupoteza fedha za Watanzania.

Alisema msimamo wa watu hao wachache ni kutotoka ndani ya Bunge mpaka kieleweke, lakini alisema Kamati ya Uongozi inafuatilia haitafumbia macho jambo hilo na serikali haitakaa kimya.

UWAKA WAMSHUTUMU SITTA
Ukawa umeonya kuwa iwapo Sitta, ataendelea kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM), itafika wakati uvumilivu utawashinda, na hivyo watalazimika kurudi kwa wananchi kwenda kuwaeleza namna kanuni za Bunge hilo zinavyokiukwa.

Onyo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alipozungumza na waandishi wa habari jana.

Alisema wamefikia maamuzi hayo katika kikao cha wajumbe wote wa vyama vya upinzani wanoauunda Umoja huo kutokana na Sitta kukiuka maazimio mbalimbali yaliyofikiwa ndani ya Bunge hilo.

Mbowe alisema wakati wa vikao vya kamati ya kanuni viliazimia kupitisha kanuni zote za Bunge hilo, isipokuwa za 37 na 38 zinazohusu upigaji wa kura, ambayo walikubaliana ziwekwe kiporo.

Hata hivyo, alisema nakala ya mapendekezo ya majadiliano haijagusia kanuni hizo mbili, badala yake, yamefumuliwa maeneo mengine, ambayo walikuwa wameyakubali na kuanzisha mjadala upya, jambo ambalo kamwe hawakubaliani nalo.

Alisema hatua hiyo ni mkakati wa makusudi uliofanywa na serikali kwa kumuagiza Sitta pamoja na sekretarieti ya Bunge hilo kuhakikisha wanabadili kanuni mbalimbali ili kutoa upndeleo kwa wabunge wa CCM, ambao ndiyo wengi kupitisha katiba hiyo kwa manufaa yao.

LISSU
Naye mjumbe wa Ukawa, Lissu alisema kanuni zilizokuwa zimebaki ni 37 na 38, lakini kamati ya kanuni imefumua maeneo mengine kwa kuanzisha mjadala wa kanuni upya.

Alitolea mfano suala la mamlaka ya Bunge kutengua kanuni, akisema yapo tu katika masuala ya nyongeza ya muda wa majadiliano nje ya muda wa majadiliano.

Alisema Bunge halina mamlaka ya kutengua kanuni, hivyo hilo sharti wanataka kuliondoa ili watengue kanuni yoyote ile, jambo ambalo alisema hawawezi kulikubali kwa kuwa suala hilo lishapitishwa.

Lissu alisema ukiondoa masharti hayo, wajumbe wengi pamoja na mwenyekiti  wanaweza kuchezea kanuni wanavyotaka.
Alisema katika hilo, kanuni wasiyoitaka wataitengua na kupitisha mambo yao.

Pia kanuni yoyote wanaweza kuiharibu, hali inayoonyesha hawapo tayari kuijadili wala kuipitisha rasimu ya katiba.

Alisema eneo la pili ni utaratibu wa kufanya maamuzi katika kamati na kueleza kuwa Sheria ya Mabadiliko Katiba inasema kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba ni lazima ipatikane theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar ili kulinda wajumbe wachache kutoka Zanzibar.

Lissu alisema sheria iliweka utaratibu huo, na Rais Kikwete alikwisha kusema, lakini wamekuja na mapendekezo mengine.

LIPUMBA
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hawatakuwa tayari kupitisha matakwa ya CCM katika rasimu ya katiba.

Alisema msimamo wao kwa sasa ni kuhakikisha wanaunda kwa pamoja katiba inayotokana na maoni ya wananchi na kama hawatafanikiwa hilo wataungana kwa pamoja kurudi kwa wananchi na kuwaeleza jinsi CCM inavyovuruga mchakato huo wa katiba mpya na  ili wafanye maamuzi.

MBATIA 
James Mbatia alisema watahakikisha wanafanya maamuzi kwa maslahi ya taifa katika katiba hiyo na endapo CCM wataendelea na upendeleo na kutaka kukiuka kanuni, watatoka nje ya Bunge kuwaeleza wananchi.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment