Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 16 March 2014

UTALII WA NDANI: TEMBELEA HIFADHI ZETU UWAONE VIGONG’OTA


 Kigong'ota madoa-meupe mdogo.
 Kigong'ota madoa-meupe mkubwa.
 Kigong'ota mkia-dhahabu.
Kigong'ota paji-jekundu.

Na Daniel Mbega (Mhifadhi Asilia)
UKO kwenye mbuga ya wanyama – haijalishi kama ni Serengeti, Ngorongoro, Mikumi, Manyara au Selous - mazingira yote yametulia ukifurahia mandhari ya asili na upepo mwanana uliosheheni harufu nzuri.
Waweza kuwa peke yako, wawili au hata wengi, lakini pengine lengo lenu ni kuyasawiri mazingira hayo tuliyojaaliwa na Muumba wetu ambayo hatuyalipii hata ushuru ili yaendelee kushamiri zaidi ya kuhitaji matunzo ya asili kwa kuacha kuchoma moto misitu, kuwinda ovyo bila vibali (ujangili) na kadhalika.
Basi, katika pitapita yako, ukiamini kwamba hakuna mtu mwingine ndani ya msitu huo isipokuwa ninyi pekee, ghafla unasikia sauti ndani ya msitu, katika miti mikubwa, kama mtu anatoboa miti kwa tindo.
Unashtuka na kustaajabu. Kama una silaha utaikamata barabara na kuanza kunyata kuelekea kule ulikoisikia sauti hiyo. Unaweza kuhisi ni jangili anayewinda wanyama ama anakata miti.
Sauti hii inasikika na kukoma, kama vile mtu anayesikilizia, halafu inaendelea tena. Unapoufikia mti ambao unadhani umeisikia sauti hiyo, ghafla sauti inakoma. Hili linakufadhaisha na unajiandaa ili uweze kumkabili huyo aliye juu ya mti.
Unapoangaza vizuri juu ya mti baada ya sauti kuanza kusikika tena, mara unamwona ndege mmoja mdogo mwenye mdomo uliochongoka ambaye anaendelea kutoboa mti bila hofu yoyote.
Nguvu zote zinakuishia na unabaki kumkodolea macho ndege huyu ambaye ama anaweza kuwa wa kijivu, mwenye madoa meupe na mkia wa njano, huku mdomo wake ukiwa mwekundu.
Ndege huyu anaitwa kigong'ota, au kwa majina mengine gongonola, gogota, vigotagota au ving'ota na katika sehemu nyingine huko Tanganyika (vijijini zaidi), wanaitwa Nyamkonghona. Ni ndege wa nusu-familia ya Picinae katika familia ya Picidae, ambaye kwa Kiingereza anaitwa Woodpecker.
Vigong'ota vinatokea misituni na maeneo mengine yenye miti kila mahali pa dunia isipokuwa Madagaska, Australia, New Zealand na kanda za Aktiki na Antaktiki.
Spishi nyingi ni nyeusi mgongoni kwenye madoa na/au mabaka meupe au njano. Spishi nyingine zina rangi ya majani au kahawa. Miguu yao ina vidole viwili vikabilivyo mbele na viwili vikabilivyo nyuma.
Mkia una manyoya shupavu na kumsaidia ndege kutembea wima mashinani kwa miti. Ndege hawa wana domo lenye nguvu ambalo hutumia kugogota miti na kutafuta wadudu katika nyufa za miti.
Ulimi wao mrefu wa kunata na wenye nywele huwasaidia kuwatoa wadudu. Zaidi ya wadudu vigong'ota hula matunda na makokwa; spishi nyingine hula hata utomvu wa miti. Dume huchimba tundu katika mti na pengine jike humsaidia. Huyu huyataga mayai 2-6 ndani ya tundu.
Kigong’ota wapo wa aina nyingi kwa spishi za Afrika kama Kigong'ota Mkia-njano (Campethera abingoni), Kigong'ota Sharubu-jekundu (Campethera bennettii), Kigong'ota Madoa (Campethera cailliautii), Kigong'ota Masikio-kahawia (Campethera caroli), Kigong'ota Mgongo-kijani (Campethera maculosa), Kigong'ota wa Mombasa (Campethera mombassica), Kigong'ota Kisogo-chekundu (Campethera nivosa), Kigong'ota Kusi (Campethera notata), Kigong'ota Nubi (Campethera nubica), Kigong'ota Madoa-madogo (Campethera punctuligera), Kigong'ota Kipaku (Campethera scriptoricauda), Kigong'ota Miraba (Campethera tullbergi), na wengineo.
Ndege hawa wanapatikana katika mbuga na hifadhi zetu nyingi zilizosheheni na mojawapo ya utajiri wetu wa asili ambao tunastahili kujivunia.
Jamani ndugu zangu, utajiri huu ni wetu na tunapaswa tuusawiri. Mbunga za wanyama zipo kwa ajili yetu, twendeni tukatembelee na kujionea vivutio hivi adhimu. Tukienda sisi tutawajengea watoto wetu utamaduni wa kuthamini vyao, badala ya kuwawekea mikanda ya akina Jet Li, Aki na Ukwa na mingine ambayo haiwapi mafunzo yoyote ya maana.

* Mwenye maoni, au anayewajua ndege hawa kwa majina ya kienyeji, anitumie kupitia namba 0715 070109, au e-mail: brotherdanny5@gmail.com.

No comments:

Post a Comment