*Baadhi wanauita mti mtakatifu, wengine wanasema wa mashetani
Na DANIEL MBEGA
TANGU utotoni tulizowea kuambiwa kwamba mti wa mbuyu ni wa
mashetani na tusithubutu hata siku moja kukaa karibu pindi mvua inaponyesha kwa
sababu radi linaweza kuupiga na kuugawanya katikati. Hata hivyo, bado
tuliendelea kukwea na kuchuma matunda yake nyakati za kiangazi.
Tuliambiwa kwamba wachawi hupendelea kuweka maskani yao kwenye miti hiyo ya mibuyu, ambayo ni miongoni mwa miti mikubwa na inayoweza kukua na kumea katika maeneo yenye ukame, kama Dodoma na Singida kwa hapa Tanzania.
Tuliambiwa kwamba wachawi hupendelea kuweka maskani yao kwenye miti hiyo ya mibuyu, ambayo ni miongoni mwa miti mikubwa na inayoweza kukua na kumea katika maeneo yenye ukame, kama Dodoma na Singida kwa hapa Tanzania.
Lakini ukiachilia mbali mbuyu, pia wazee wetu walikuwa
wakitukataza tusipendelee kucheza kwenye miti ya mikuyu, ambayo inatajwa kwamba
ndiyo ‘malkia wa miti yote’. Sababu kubwa waliyotuambia ni kwamba miti hiyo ni
ya miungu na ndiyo maana inapendelea kuota sehemu zilizotulia kwenye mapito ya
maji huku ikiwa inaongoza kwa kuwa miti pekee yenye mizizi mingi.
“Ninyi hamuoni, hata nyakati za kiangazi mti unaonekana
umependeza, tofauti na ule mbuyu. Ule mbuyu ni mti wa mashetani, lakini huu ni
mti wa miungu. Msije mkathubutu hata siku moja kuukata ama kuuchezea, miungu
ikikasirika mtapata shida,” nakumbuka mzee mmoja alipata kutuambia wakati
tukiwa wadogo, zaidi ya miaka thelathini iliyopita.
Kweli hatukuwa tukiikata miti hiyo, lakini daima
tulipendelea kucheza chini ya vivuli vyake na kukwea kuchuma matunda yake
mazuri kuyatazama, matamu kuyala, lakini yakiwa yamejaa wadudu wengi ambao
unalazimika kuwaondoa kabla ya kuyala.
Huo ndio mkuyu, mti ambao ni wa ajabu ambao si wengi
wanaoufahamu kutokana na kutoota kila mahali kama ilivyo miti mingine. Tena
basi si mti wa kupandwa, bali hujiotea wenyewe, hasa katika maeneo ya
kitropiki, ingawa baadhi ya jamii yake inaweza kuota kwenye maeneo ya joto.
Tunaambiwa kwamba mti mashuhuri wa mkuyu (Ficus carica)
asili yake ni Asia na Mashariki ya Kati lakini umefanikiwa kumea hata katika
maeneo mengine, ukiwa unazaa matunda matamu sana, ambayo kama unaweza
kuhudumiwa kama yalivyo matunda mengine, huwezi kukuta wadudu ndani ya matunda
yake yenye majimaji mengi.
Wataalamu wa mambo ya kale wanasema kwamba mti huu wa mkuyu
unaweza kuwa mmoja kati ya mimea iliyowahi kutunzwa na binadamu (katika sehemu
nyingine mikuyu inatunzwa, hasa kwa watu wenye maeneo makubwa, kwa sababu miti
hii huchukua maeneo makubwa sana kutokana na mfumo wao wa mizizi kuwa yenye
kutambaa). Mkuyu unatajwa ndani ya Biblia, wakati Adam na Eva wanapotumia
majani yake kujistiri baada ya kuona wako uchi ndani ya Bustani ya Eden.
Ukristo siyo dini pekee ambayo imeupa mkuyu nafasi kubwa
kama unavyotajwa pia katika Injili. Jamii nyingine ya mkuyu au mtini wa Kiasia,
Ficus religiosa, unachukuliwa kama mti mtakatifu na Wahindu, Wajaini, na
Mabuddha. Inasemekana Buddha Mkuu, Siddhartha Gautama, alipata ufunuo wakati
alipokuwa ameketi chini ya mti mtakatifu wa mkuyu, ambao pia unajulikana kama
bo au pipal. Waislamu pia wanaichukulia miti mingine ya jamii ya mkuyu kama
mitakatifu.
Kwa hakika, kati ya miti yote duniani, mikuyu (Ficus) ndiyo
miti pekee ambayo ukuaji wake umetandwa na utata utata na hata uchavushaji wake
ni wa ajabu. Jaribu kufikiria mti ukiwa umejaa mizizi inayofanana na nyoka,
ikiwa imejiviringisha na kuchomoza kwenye shina ama matawi ya mti mkubwa na
kutanda kila sehemu na hata kuinyonga miti mingine ya jirani yake.
Japokuwa watu wengi wanaufahamu mti wa mkuyu ambao ni wa
kale (Ficus carica), aina mbalimbali za jamii ya mikuyu hustawi kwenye maeneo
ya kitropiki. Ukuaji wake na mifumo yake ya mizizi inaweza kufananishwa na miti
inayoonekana kwenye filamu za "Tarzan" au "Rambo". Kuna
jamii ya miti hii ambayo iliwahi kupandwa katika jimbo la Florida na kusini mwa
California nchini Marekani, na ukiangalia ndiyo miti ambayo imetumika katika filamu
hizo ambazo mara kadhaa wahusika wanatumia mizizi yake inayoning’inia kubembea huku
wakiwashambulia adui zao.
Miti hii ambayo iko katika kundi (genus) la Ficus, katika
familia ya Mulberry (Moraceae), ndiyo yenye jamii kubwa zaidi ikiwa na aina ya
miti 1,000. Miti inayoifuatia kwa kuwa na jamii nyingi ni ile ya jamii ya
mikungugu yenye miiba maarufu kama Acacia (ambayo ina jamii 800), Mikaratusi
ama Eucalyptus (500), na Cassia (500).
Pamoja na kuambiwa na wazee wetu kwamba miti hiyo ni ya
miungu, lakini pia nakumbuka kwamba mahali ambako miti hiyo iliota ama ilikuwa
ni vyanzo vya maji au sehemu iliyopitisha maji kama mto, au sehemu iliyokuwa na
uoto mzuri na ardhi yenye rutuba.
Kama iliota sehemu za nyikani, basi tuliamini kwamba ikiwa
utachimba kisima mahali hapo maji hayakuwa mbali sana, na ndivyo ilivyokuwa,
hasa kwa sisi ambao tulikuwa tukiishi katika maeneo kame kama yale ya mikoa ya
kati.
Hata hivyo, hivi sasa miti hii, ambayo tuliiheshimu kwa
kuona kwamba ni miti ya miungu, imeanza kutoweka baada ya wananchi kuamua
kuikata kwa matumizi mbalimbali. Ile hofu kwamba ikikatwa inaweza kuleta
madhara haiwasumbui wengi na wanaona kama vile zilikuwa hekaya tu za wazee
wetu.
Kitu kimoja ambacho hawakielewi ni kwamba, wazee wetu
walikuwa na maana kwamba, miti hiyo ilikuwa vyanzo vikubwa vya maji na dalili
nyema kwamba nchi ilikuwa na neema, hivyo kuikata kulimaanisha kwamba janga la
ukame lingeweza kuibuka.
Janga hilo sasa liko dhahiri kwa sababu baada ya kukatwa
kwa miti mingine yote kwenye misitu, na waheshimiwa hawa kuigeukia mikuyu, hivi
sasa maeneo mengi ni makavu na hata mvua imekuwa ikinyesha kwa bahati, kwa
sababu ile miti ambayo ilikuwa ikivuta mawingu ya mvua haipo tena.
Kwa hakika, kama wana mazingira wakifanya utafiti wa
kutosha, na kama kuna uwezekano wa kuipanda miti hii, basi inaweza kusaidia
kutunza mazingira na kuwa kivutio cha mvua katika maeneo mengi, hasa yenye
ukame.
Faida yake ni kubwa, kwamba pamoja na kuwa vyanzo vya maji
na vivutio vya mawingu ya mvua, lakini matunda yake ni chakula kizuri sana kwa
ndege, wanyama wa porini na hata binadamu.
Tunaambiwa kwamba matunda ya mkuyu yana viiniisho kama
wanga, hamirojo, sukari, mafuta na protini kibao, hivyo ni mazuri sana kuliwa.
Kwa sisi tuliowahi kuyala wakati wa utotoni tunaujua utamu wake, lakini linaweza
kuwa jambo geni kwa wale ambao hata mti wenyewe hawaujui.
Tunda la mkuyu linachukuliwa kama tunda, lakini kwa hakika
hilo ndilo kama ua la mkuyu. Linaweza kutajwa kama ni tunda bandia ama tunda
linalojipogolesha, ambapo ua na mbegu hukua pamoja na kufanya tunda.
Pengine uwezo huu wa kutoa maua ambayo ni matunda, tofauti
na miti mingine, ndiyo yaliyowafanya hata wazee wetu waone kwamba huu ulikuwa
ni mti wa miungu, tofauti na mbuyu ambao maua yake yanaonekana mpaka matunda
yanapokomaa.
Yote kwa yote, kinachotakiwa kufanyika kwa sasa kwa wizara
ya Maliasili na Utalii, kwa kushirikiana na Wizara inayohusika na Mazingira, ni
kuilinda miti kama hii ambayo kuwepo kwake kuna faida kubwa kwa mazingira yetu
na sisi wenyewe kwa ujumla. <Mwisho>.
No comments:
Post a Comment