Marijani Rajabu Marijani 'Dozzer'
Na Daniel MbegaAHLANI Wasaalani mabibi na mabwana ambao mnaperuzi ukurasa huu na blog hii ambamo
tunabarizi na kujikumbusha ile mikito ya zamani, miziki ya Bakulutu ambayo
mpaka leo bado ni keki kweli inapodundwa.
Siku moja nikiwa kwenye daladala, ule usafiri wetu akina
siye, nilikumbana na mkasa mmoja ambao hakika ndio uliozaa mada yangu ya leo.
Akina mama wawili, mtu na rafikiye, walikuwa wameketi siti moja wakizungumza
kwa masikitiko makubwa.
Awali sikuelewa kisa ni nini, lakini baada ya muda mmojawao akapigiwa simu na baada ya kuzungumza na mtu huyo huku akipewa maelekezo, akasema kwamba wako njiani wanakwenda.
Awali sikuelewa kisa ni nini, lakini baada ya muda mmojawao akapigiwa simu na baada ya kuzungumza na mtu huyo huku akipewa maelekezo, akasema kwamba wako njiani wanakwenda.
Alipokata simu mwenzake akamuuliza ni nani. Yule wa kwanza
akasema kwamba wamempata mtu wanayemsaka. Mwenzake akamshauri awaambie
waliompigia simu wampeleke huyo mtu polisi, lakini wakakubaliana kwamba haina
haja kwa sababu walikuwa wamekaribia kufika. Wakateremka pale Keko Maflati
karibu na uwanja wa taifa.
Hata hivyo, baada ya simu hiyo mmoja wao alikuwa akilaumu
kwamba mtoto huyo wa kike amekuwa msumbufu sana. Ametafutiwa shule lakini
badala ya kwenda huko akaamua kuzamia moja kwa moja anakokujua yeye.
“Akipelekwa polisi atasema tu alikokuwa na hao aliokuwa nao
siku zote hizi. Yaani ni balaa kweli sisi wanawake, mtu wakati mwingine unaweza
kusema bora uzae mwanamume hata akiwa jambazi atauawa huko potelea mbali kuliko
mtoto wa kike ambaye daima anakupa presha,” akasema yule wa kwanza, ambaye nahisi
ndiye mama mzazi wa binti huyo.
Hapo ndipo nilipoelewa kwamba kumbe walikuwa wakimsaka
binti yao ambaye alitoweka nyumbani kwao siku kadhaa kwa maelezo kwamba yuko
kwa rafiki zake anajisomea, kumbe siyo! Unaona mambo ya dunia haya ndugu
zanguni?
Ni kwa mantiki hiyo basi leo nimeamua kuwaletea kibao hiki
cha Rosa Nenda Shule, kibao
kilichotungwa na Jabali la Muziki Tanzania, Marijani Rajab Marijani ‘Dozzer’,
mwaka 1973 wakati huo akiwa na bendi ya Safari Trippers.
Matukio kama haya yametukuta wengi, tukiwa kama wazazi ama
wanajamii. Watoto wa kike wanaosoma wanaleta matatizo sana, ingawa siwezi
kuwatetea wale wa kiume nao kwani kila mmoja ana matatizo yake.
Na hapa lazima niseme kwamba, simuungi mkono yule mama
anayesema bora mtoto wa kiume. Jamani mtoto ni mtoto tu, awe wa kiume au wa
kike. Namna tabia yake itakavyokuwa ni malezi ayapatayo, ikiwa ni pamoja na
kuepuka makundi na zaidi kumuomba Mungu amtangulie na ampe mwenendo mwema!
Hata hivyo, watoto wa kike wana matatizo makubwa sana
kuliko wa kiume, hasa wanapoingia kwenye ule umri wa ujinga, yaani foolish age.
Vichuchu vikianza kuchomoza tu na sauti nayo kubadilika, mtoto wa naye huanza
kubadili tabia. Atachagua mavazi, vipodozi na hata mwendo ataubadilisha! Ndio
umri wa balekhe huo ambao humfanya ajione kama yeye ndiye anayejua kila kitu.
Na hapa ndipo ninaposema kwamba, wengi wetu tumeshuhudia
tabia za watoto hawa, wengine wakishindwa kumaliza masomo, na kama wanamaliza,
basi huwa ni mbinde kweli kweli.
Tabia zao wengine hata walimu wao huziona jinsi
zinavyobadilika na walimu wengine waungwana huwa wanapenda kuwasiliana na wazazi
wa binti husika, kama Marijani anavyosema;
“Habari
zako nimezipata kutoka kwa walimu wako, Kwamba siku nyingi zimepita na wewe
shule mbona huonekani, Unaniaga baba nakwenda shule, Na mapesa mengi kuniomba,
Kumbe muongo mkubwa ukitoka kumbe una njia zako...”
Hebu nielezni ndugu zangu, ni nani kati yetu ambaye
hajashuhudia mambo haya? Mimi mwenyewe nimeshuhudia watu wengine wakishindwa
kumaliza masomo na wale waliomaliza hufanya hivyo ili kutimiza wajibu.
Lakini hakuna mzazi ambaye hamtakii mema mwanawe, na ndiyo
maana hivi sasa wazazi wote wako radhi kujinyima na hata kufanya vibarua ili
kugharamia elimu ya watoto wao, kwa sababu ndio urithi wao.
Katu wasijidanganye kusema, “Aaah, baba yangu mimi tajiri, hata nisiposoma nitaishi tu!” Huu ni
ujinga tena upumbavu. Hivi unajua mali aliyonayo babayo aliipata vipi? Unajua
jinsi alivyosoma? Si walisema Waswahili kwamba nguo ya kuazima haistili maungo!
Tazama yule binti mwingine ninayemfahamu mimi ambaye baba
yake alikuwa tayari kuachilia ujenzi wa nyumba ya familia ili amsomeshe baada
ya kufaulu mtihani wa darasa la saba. Lakini alipokwenda shule akaingia kwenye
makundi, akaanza kujirusha. Mtihani wa kidato cha pili ulipokuja, akaanguka
vibaya sana, lakini nyumbani akadanganya kwamba amepasi. Siri ilipogundulika, akaamua
kuachana na shule!
Marijani anasema hivi, hata mimi na mzazi mwingine
anayewatakia maendeleo watoto tunasema hivi; “Ooo Rosa wewe nenda shule eeee, Ukimaliza faida utaiona eeee... Wacha
tamaa Rosa ee wacha tamaa mama ee, Tamaa yako Rosa ee itakuponyesha… Ipende
shule mama ee wacha uhuni mama ee.”
Labda nimalizie kwa kuwaasa hawa binti zetu kwamba,
wanaume, yaani sisi wanaume, ashakum si matusi, ni washenzi kweli kweli. Wengi
wao wanapenda kuwahadaa mabinti pale wanapoona wameanza kuchipukia. Wakishamaliza
haja zao, na pengine tayari watakuwa wamewatwisha mimba, au hata magonjwa ya
zinaa, haoo wanakimbia.
Utahangaika na mzigo wako peke yako na ndipo hapo huwa
napenda kutumia ule msemo wa wahenga na wahenguzi kwamba, Kijuto msuto kisicho
kito! Yaani Majuto ni mjukuu, upo hapo mama.
Hebu wadogo zangu ngoja niwaambie. Hayo mapenzi hayo
mnayoyakimbilia yalikuwepo, yapo na yataendelea kuwepo. Walikuwepo akina babu
na bibi, wameondoka wameyaacha. Sasa kwa nini msisubiri mkamaliza jambo moja na
kasha muende jingine?
Halafu maskini ya Mungu, mara nyingi zaidi ukimfuatilia
binti huyu utakuta huyo anayemzuzua ni mwanafunzi mwenzake ama muuza chips au
hata kondakta wa daladala. Kama huyu mwanafunzi, ambaye dira yake haijui kabisa
kwa sababu bado na yeye anahudumiwa na wazazi, halafu leo hii anakudanganya
kwamba lazima akuoe! Hivi kwa nini muwe na akili za kuku kupewa mtama kwenye
ungo na kisha kuumwaga na kuuchanganya na mchanga ndipo uudonoe?
Gonganisheni vichwa vyenu, halafu mtapata majibu sahihi,
vinginevyo nendeni shule kwa sababu faida ni yenu wenyewe. Mali ya urithi
ukiitegemea utakufa kibudu!
Wasalaaam!
Tazama mashairi ya wimbo wa Rosa:
Tazama mashairi ya wimbo wa Rosa:
[Wote]
Habari zako nimezipata kutoka kwa walimu wako
Kwamba siku nyingi zimepita na wewe Shule mbona huonekani
Unaniaga baba nakwenda Shule
Na mapesa mengi kuniomba
Kumbe muongo mkubwa ukitoka kumbe una njia zako
(repeat)
(Chorus)
[Wote]
Ooo Rosa wewe nenda shule eeee
Ukimaliza faida utaiona eeee......
Wacha tamaa Rosa ee wacha tamaa mama ee
Tamaa yako Rosa ee itakuponyesha
Ooo Rosa wewe nenda shule eeee
Ukimaliza faida utaiona eeee......
Ipende Shule mama ee wacha uhuni mama ee
Kwa majadiliano, hoja na ushauri gonga 0715 – 070109, au brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment