Dua Said
Na Daniel
Mbega
LIGI Kuu
ya Muungano iliyosadikiwa kuwa na msisimko wa kipekee msimu huo kwa vile
ilikuwa inawahusisha kikamilifu mamilionea wote watano waliokuwa wanafadhili
soka nchini Tanzania, ilianza rasmi Jumamosi Septemba 25, mwaka huo 1993 na
ilitarajiwa kupamba moto zaidi Jumapili katika kindumbwendumbwe cha aina yake
kwa kuzikutanisha Simba na Yanga.
Siku hiyo ya Jumamosi Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora ulianza ukurasa mpya wa kumbukumbu zake kwa mechi za Ligi Kuu ya Muungano kuchezewa kwenye nyasi zake. Abbas Gulamali, Murtaza Dewji, Azim Dewji, Mohammed Raza na Naushad Mohammed, wafanyabiashara wa Tanzania wenye asili ya Asia, ambao walikuwa wamebobea katika kutumia utajiri wao kuzifadhili timu kubwa nchini, walitarajiwa kuonyesha ubabe katika ligi hiyo na mwenzao Salim Kanji alikuwa anakabiliwa na upinzani mkali. Hivyo, ligi hiyo ilitazamiwa kutegemea zaidi mbinu za midani kuliko kiwango cha soka.
Siku hiyo ya Jumamosi Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora ulianza ukurasa mpya wa kumbukumbu zake kwa mechi za Ligi Kuu ya Muungano kuchezewa kwenye nyasi zake. Abbas Gulamali, Murtaza Dewji, Azim Dewji, Mohammed Raza na Naushad Mohammed, wafanyabiashara wa Tanzania wenye asili ya Asia, ambao walikuwa wamebobea katika kutumia utajiri wao kuzifadhili timu kubwa nchini, walitarajiwa kuonyesha ubabe katika ligi hiyo na mwenzao Salim Kanji alikuwa anakabiliwa na upinzani mkali. Hivyo, ligi hiyo ilitazamiwa kutegemea zaidi mbinu za midani kuliko kiwango cha soka.
Naushad
wa Malindi Jumamosi hiyo alikuwa anamkabili Kanji wa Milambo huko Tabora, na
huko Zanzibar, Shangani ya Raza ilikuwa inachuana na Mlandege kwenye Uwanja wa
Amaan. Septemba 26 ndiyo siku iliyokuwa inatazamiwa kuwa ngumu zaidi, kwani
timu za akina Gulamali na Dewji wawili zilikuwa zinachuana kwa hali ya upinzani
wa juu.
Baada ya
kila timu kumfunga mwenzake katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Simba
na Yanga katika mchezo wao huo zilitarajiwa kuanza upya. Azim Dewji alisononeka
sana mpaka akagombana na polisi wakati Saidi Mwamba ‘Kizota’ alipofunga magoli mawili
dhidi ya moja la Edward Chumila hapo Machi 27, lakini Julai 17 ikawa zamu ya
Gulamali kulia machozi wakati Dua Said alipoifungia Simba goli pekee la
ushindi.
Sasa
Jumapili hiyo Azim alitarajiwa kutingwa na Gulamali na Murtaza, mfadhili
aliyeweza kuinyanyua Pan African kutoka daraja la tatu hadi la kwanza na wakati
huo sasa alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Yanga na jukumu lake la kwanza lilikuwa
kwenye ligi hiyo. Pengine ni kwa sababu hiyo Azim alilazimika kuyafuta mapokezi
ambayo awali yalipangwa kuwa makubwa wakati timu ya Simba ilipowasili Jumamosi
ikitokea Algeria ambako ilifaulu kuingia nusu fainali ya Kombe la CAF kwa
kuitoa USM El-Harrach ya huko kwa jumla ya magoli 3-2.
Swali
kubwa lilikuwa, Je, Simba ingefanya kile kilichofanywa na Yanga Aprili 22 mwaka
1992? Ikitokea Cairo, Misri kwa shindano la ubingwa wa Afrika dhidi ya
Ismailia, Yanga iliwasili Jumamosi mchana na kesho yake ikawalaza Simba goli
1-0.
Simba na
Yanga ndizo zilizokuwa zoefu kwenye ligi hiyo mwaka huo zikifuatiwa na Malindi,
lakini zilizosalia zote zilikuwa ngeni na mikikimikiki hiyo. Yanga, waliokuwa
mabingwa wa Tanzania Bara kwa misimu miwili mfululizo na kushikilia ubingwa wa
Afrika Mashariki na Kati, mpaka wakati huo ndiyo iliyokuwa inaongoza kwa kutwaa
ubingwa wa Muungano mara nyingi zaidi, na mwaka 1992 ilivuliwa na Malindi.
Mpaka wakati huo, Simba haikuwa imetwaa ubingwa huo kwa miaka 12 mfululizo na
pengine kazi kubwa ilikuwa inamkabili mwenyekiti mpya Amir Ally ‘Bamchawi’,
kufuta doa hilo kwa klabu yake ambayo hadhi yake haikustahili kuukosa ubingwa
wa taifa kwa muda wote huo.
Mabingwa
watetezi wa ligi hiyo, Malindi, safari hiyo hawakutamba sana huko Zanzibar
mpaka wakavuliwa taji na timu ngeni kabisa, Shangani. Malindi walikuwa
washiriki wa mara kwa mara wa ligi hiyo tangu mwaka 1989 na huo waliokuwa
wakiutetea ulikuwa ubingwa wao wa pili nchini Tanzania. Mabingwa wapya wa
Zanzibar, Shangani, pamoja na Milambo na Mlandege, ni timu zilizokuwa
zinashiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo, hivyo uwezo wao katika
ligi hiyo ungeonekana wakati wa harakati zenyewe.
Waswahili
husema, ‘Usimlaumu dobi, weusi wa kaniki nd’o rangi yake’. Hivyo ndivyo
ilivyokuwa kwa timu ya mtaa wa Jangwani, Jijini Dar es Salaam, Young Africans
(Yanga), ambayo ilimfukuza kocha wake, Nzoysabah Tauzany raia wa Burundi, baada
ya kushindwa kwa mara ya pili mfululizo na watani wao wa jadi, Simba pia ya Dar
es Salaam.
Mwanzoni,
Yanga ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Daraja la Kwanza
Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Julai 17, ushindi ambao
uliendelezwa pia Jumapili hiyo Septemba 26 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu
ya Muungano, tena na mshambuliaji yule yule, Dua Said, na kuwaacha wapenzi,
mashabiki, wanachama na viongozi wa Yanga wakiwa hawaamini kilichotokea.
Ushindi
wa vijana hao wa Msimbazi dhidi ya Yanga ulikuwa dhahiri tangu walipoweza
kuhimili fujo za Waarabu huko Algeria wakati wa mchezo wa marudiano katika
Kombe la CAF. Hivyo, mashambulizi ya Yanga hayakuwa tishio kubwa kutokana na
ukweli kuwa, Simba ilikuwa tayari na hesabu za kuwazuia kwa jinsi watakavyo.
Kama
Yanga wangekuwa na mashambulizi ya kimahesabu wangeweza kujipatia mabao kwenye
mechi hiyo iliyokuwa ngumu kutabirika wakati wa mwanzo, lakini Malota Soma
‘Ball Juggler’, ambaye alifunga bao kwenye dakika ya nane lakini likakataliwa,
alionyesha dhahiri kuwa, wapinzani wao hao walikuwa na mwanya ambao ungeweza
kutumika kuweza kujipatia bao, na katika dakika ya 13 Simba iliweza kulipata
kupitia kwa Dua Said kutokana na shambulizi kali lililojengwa na Kassongo Athumani,
Ramadhan Lenny, Abdul Mashine na Edward Chumila.
Bao hilo
la Dua halikuleta mzozo wowote kutokana na ukweli kwamba, ni bao ambalo
limezoewa na kila Mtanzania, akiwemo mwamuzi wa mchezo huo, Mfaume Ally wa
Zanzibar, kinyume na lilivyokuwa bao la Malota.
Ngome ya Simba ilistahili sifa zote kutokana na kuweza kulinda lango kwa
kutumia akili zaidi badala ya kubutua mpira ovyo. George Masatu, Fikiri
Magosso, Kasongo Athumani na Deo Mkuki walifanya kila lifanywalo na ngome
katika kudhibiti wapinzani ambao mara nyingi walijikuta wakiingiwa na mchecheto
kiasi cha kupiga mipira nje na hata walipokuwa wakibakia na kipa Mohammed
Mwameja walishindwa kumalizia.
Kwa
kufukuzwa Tauzany, Yanga sasa ilikuwa chini ya Charles Boniface Mkwasa
aliyekuwa kocha msaidizi.
YANGA: Riffat Said, Selemani Mkati, Kenneth Mkapa,
Willy Mtendawema, Issa Athuman, Method Mogella (nahodha), Sanifu Lazaro,
Stephen Mussa, Said Mwamba, Mohammed Hussein, Edibilly Lunyamila.
SIMBA: Mohammed Mwameja, Kasongo Athumani, Deo Mkuki,
Fikiri Magoso, George Masatu, Hussein Marsha (nahodha)/Iddi Selemani, Edward
Chumila, Ramadhan Lenny, Abdul Mashine, Malota Soma, Dua Said.
Mwamuzi
katika mchezo huo alikuwa Mfaume Ally wa Zanzibar na mgeni rasmi alikuwa Balozi
wa Sweden Nchini, Thomas Palme.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment