Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 29 October 2013

NHC YAJIZATITI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA MAKAZI


Meneja Huduma kwa Jamii toka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw.Muungano Saguya akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)kuhusu hatua zinazochukuliwa na Shirika hilo kutatua tatizo la makazi hapa nchini ikiwa ni pamoja na mkakati wa miaka 5 wa utakaohusisha ujenzi wa nyumba 15,000,wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Bw. Frank Mvungi.
 
Meneja Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Willium Genya akitoa wito wa wananchi kupitia waandishi wa habari(hawapo pichani) kujitokeza kununua nyumba hizi ili kwa pamoja kusaidiana kuondoa tatizo la makazi nchini,wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Meneja Huduma kwa Jamii toka Shirika hilo Bw.Muungano Saguya. Picha na Hassan Silayo-MAELEZO



SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CHAMA CHA MAPINDUZI YA MWAKA 2010

1.0 UTANGULIZI:
     Awali ya yote, ningependa kuwapa kwa muhtasari hali ya ujenzi wa nyumba ilivyokuwa tangu kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba la Taifa, kabla sijaelezea jinsi tuliweza kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ya Chama Tawala.
     Tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Rais wa kwanza wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alithamini vitu vitatu vinavyoleta utu na maendeleo ya binadamu. Vitu hivyo ni chakula, mavazi na malazi. Kutokana na imani ya Mwalimu kuwa makazi ni sehemu ya utu wa binadamu, alilianzisha Shirika la Nyumba la Taifa mwaka 1962 ili kuwajengea wananchi hususan wa kipato cha chini nyumba bora.
      Hadi kufikia mwaka 1975, likitumia ruzuku ya Serikali, mikopo kutoka Benki ya Nyumba (THB) iliyoanzishwa mwaka 1973 na misaada kutoka Serikali ya Shirikisho ya Jamhuri ya Ujerumani Magharibi (FRG), Shirika hili lilifanikiwa kujenga nyumba 14,462 nchini kote nyingi zikiwa zimejengwa wakati wa oporesheni ondoa makuti (slum clearance). Asilimia 90 ya nyumba hizi zilikuwa ni nyumba za gharama nafuu.
     Kufikia mwishoni mwa miaka ya 70 na mwanzoni mwa miaka ya 80,  Shirika hili lilishindwa kutekeleza kazi zake za ujenzi kutokana na hali ngumu iliyoikumba nchi yetu na dunia kwa ujumla.  Hali hiyo ilsasababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la Dunia na vita vya Kagera. Uwezo wa Serikali ukawa mdogo na hali ya makazi ikazidi kuwa mbaya huku idadi ya watu wanaokimbilia mijini kutafuta maisha bora nayo ikiongeza ukubwa wa tatizo la nyumba. Nayo kodi ya nyumba za NHC iliyokuwa ikichangia asilimia 80 ya mapato yake, ambayo ilikuwa ndogo kutokana na ruzuku iliyokuwa ikitolewa na Serikali, ikaendelea kuwa hivyohivyo kwa kuwa Sheria ya Zuio la Kodi Na. 17 ya mwaka 1984 ilizuia kupandisha kodi. Hata pale Shirika lilipotaka kurekebisha kodi zake ili liweze kujiendesha na kutengeneza nyumba zake, ilipata upinzani mkubwa kutoka kwa wapangaji wake waliosaidiwa sana na Sheria hiyo. Hali hii ililifanya Shirika kujenga tu nyumba 1,664 kutoka kipindi cha mwaka 1976 hadi 1990.
     Katika kuhakikisha kuwa sekta ya nyumba inaleta tija ya kiuchumi na kijamii hapa nchini, mwaka 1990 Serikali ililiunganisha Shirika hili na iliyokuwa Msajili wa Majumba ya Mwaka 1971. Pamoja na kuunganishwa kwa mashirika haya mawili yaliyokuwa yakifanya kazi zinazofanana, bado sheria mbalimbali na kukosekana kwa mikopo ya fedha za kujenga au kununua nyumba, kuliidumaza NHC na kufanikiwa kujenga nyumba 600 tu hadi kufikia mwaka 2010.
     Ili kuondoa kusuasua kwa sekta ya nyumba nchini, mwaka 2005 na 2008, Serikali ilijitahidi kubadilisha sheria mbalimbali zilizokwamisha uwekezaji katika sekta ya nyumba. Sheria hizo ni pamoja na sheria ya ardhi ya mwaka 1999, sheria iliyolianzisha Shirika la Nyumba la Taifa, sheria ya mikopo ya nyumba na sheria ya hati pacha katika majengo ya ghorofa.
     Aidha, mwaka 2010, Serikali iliazimia kuliunda upya Shirika hili kwa kulipatia uongozi mpya, ambao umetengeneza  Mpango Mkakati wa miaka mitano 2010/11-2014/15 ambao umejikita katika kuwezesha ujenzi wa nyumba 15,000 katika kipindi hicho, idadi ambayo haijawahi kutekelezwa kwa kipindi kifupi na Shirika hili tangu lianzishwe mwaka 1962. Lengo ni kuhakikisha kuwa kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine zikiwemo taasisi za fedha, NHC inashiriki kikamilifu kuondoa uhaba wa nyumba hapa nchini ambao kwa sasa unafikia nyumba milioni 3 na ukiongezeka kwa nyumba 200,000 kwa mwaka.
     Katika kutekeleza hilo, Shirika limeweka msukumo wa pekee katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu za kuwauzia wananchi wa kipato cha kati na chini. Katika kuongeza msukumo wa jambo hili, Serikali sasa inaliunga mkono sana Shirika na mwezi Juni mwaka 2012 Mjini Dodoma, Mheshimiwa Rais Dk. Jakaya Kikwete, aliunda Kamati ya Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania, kuangalia namna ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini. NHC katika Kamati hiyo ni Katibu na mratibu wa utekelezaji wa maagizo hayo ya Mheshimiwa Rais.

2.0 UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI:
Kutokana na mpango mkakati wa Shirika na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya ya CCM ya mwaka 2010, pamoja na maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika limeagizwa kufanya yafuatayo:-

Ibara ya (iii) ya Ilani ya Uchaguzi inalitaka Shirika kuhakikisha  kuwa jumla ya nyumba 15,000 (kwa wastani nyumba 3,000 kila mwaka) zinajengwa na kwa kushirikiana na sekta binafsi.

• Katika kutekeleza hilo, Shirika limekamilisha matayarisho ya miradi 65 yenye jumla ya nyumba za makazi 17,078 ambazo ni za gharama nafuu, kati na juu, zilizoanza kujengwa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Kiasi cha 70% ya nyumba zinazojengwa kitauzwa na 30% kitapangishwa. Hadi kufikia Septemba, 2013, ujenzi wa miradi saba (7) yenye jumla ya nyumba 657 ulikamilika; ujenzi wa miradi 14 yenye  jumla ya nyumba  980  ulikuwa unaendelea; na ule  wa miradi 30 yenye jumla ya nyumba 3,096 ulitarajiwa kuanza katika kipindi cha 2013/14.  Aidha, Shirika lilikamilisha miradi miwili (2) ya majengo ya biashara iliyoko Dar es Salaam na Kigoma na kuendelea na ujenzi wa miradi minne (4) iliyoko katika mikoa ya Morogoro, Musoma na Mbeya. Ujenzi wa miradi 12 mingine ya majengo ya biashara unatarajiwa kuanza katika mwaka 2013/14. Vile vile, Shirika kwa kushirikiana  na waendelezaji binafsi, lilikamilisha miradi 11 ya majengo ya biashara na makazi kwa njia ya ubia na liliendelea  na ujenzi wa miradi 20.

Katika kipindi hiki, tulikamilisha pia Miradi mitatu (3) yenye jumla ya nyumba za kuuza 84 iliyoanza katika maeneo ya Kibla – Arusha (nyumba 48), Haile Selasie – Arusha (nyumba 4) na Mbweni JKT – Dar es salaam (nyumba 34). Katika kipindi hiki shirika pia liliweza kukamilisha mradi wa jengo la biashara lenye ghorofa nne (4) lililoko mtaa wa Lumumba mjini Kigoma kwa gharama shilingi bilioni 2.53. Ujenzi wa jengo hili ulianza mnamo Januari, 2010 na kukamilika mwezi Machi, 2012


Ibara ya (viii) ya Ilani ya Uchaguzi inalielekeza Shirika la Nyumba la Taifa kuwa mwendelezaji ardhi mkubwa (Master Estate Developer) na kujenga nyumba nyingi kwa ajili ya kuuza au kupangisha kwa wananchi wote na hasa watu wa kipato cha kati na cha chini.
·        Katika kutekeleza hilo,  Shirika lilianza  kwa  kununua ardhi, kuipima na kupanga maeneo. Lengo la mkakati huu ni kuendeleza  maeneo kwa kujenga nyumba na majengo ya biashara na kuuza baadhi ya  viwanja kwa waendelezaji wengine. Hadi kufikia Septemba, 2013,  Shirika lilikuwa limekamilisha ununuzi wa ekari 1,210.58 na viwanja 457. Upimaji, upangaji na utayarishaji wa michoro ya majengo, nyumba na miundombinu kwa maeneo ya Usa River – Arusha (ekari 296), Burka – Arusha (ekari 573), Iyumbu – Dodoma (ekari 236) na Kibada/Uvumba – Dar es Salaam (ekari 202), ulikuwa unaendelea. Ili Shirika liweze kutekeleza jukumu la kuwa Mwendelezaji Mkuu kwa ufanisi, limeiomba Serikali ruksa ya kuwa Mamlaka ya kupanga matumizi ya ardhi (planning authority).
     Shirika hivi sasa limeanza kwa kasi kutekeleza ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika Halmashauri mbalimbali za Miji na Wilaya. nchini. Ili kufanikisha hilo, Shirika limekuwa katika hatua mbalimbali za ununuzi wa jumla ya ekari 18,421 kwenye Halmashauri za Wilaya mbalimbali nchini kwa ajili ya kujenga nyumba hizi za gharama nafuu Hadi hivi sasa nyumba zipatazo 2500 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri za Miji na Wilaya zikiwemo Kibada-Temeke, Mvomero, Mkinga, Lindi, Mkuzo- Ruvuma, Bombambili-Geita, Mlole-Kigoma, Ilembo-Katavi, Kongwa, Unyankumi-Singida na Mrara-Babati. Awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba hizi inafuata katika maeneo ya Sumbawanga, Mwongozo- DSM, Longido, Uyui, Manyara, Kibada awamu ya pili-DSM, Monduli, Buswelu-Mwanza, Chalinze, Kyerwa, Muleba, Iwambi-Mbeya, Mbarali na Masasi. Lengo la Shirika ni kuhakikisha kuwa kila Halmashauri ya Wilaya na Miji hapa nchini inafikiwa na mradi huu katika mwaka huu wa fedha.
     Ujenzi wa nyumba hizi utawapatia makazi bora wananchi wapatao 7285 na ajira za moja kwa moja zipatazo 7170. Aidha, kutakuwa na huduma za kijamii zenye eneo la mraba 58,300 zikijumuisha maduka, shule, hospitali, viwanja vya kuchezea watoto na vituo vingine mbalimbali. Gharama ya utekelezaji wa miradi hii ni shilingi bilioni 53.8. Gharama za kuweka miundombinu ya umeme, barabara na maji pekee ni bilioni 10.8.  Hivyo, ili kuzifanya nyumba zinazojengwa kuwa za gharama nafuu, ni muhimu taasisi zote zinazohusika na uwekaji wa miundombinu muhimu kama umeme, barabara na maji kutimiza wajibu wao katika maeneo yote yanayojengwa nyumba mpya. Aidha, Halmashauri za miji na Wilaya ni vema zikasaidia kulipatia Shirika ardhi isiyokuwa na masharti yoyote ya kuwezesha kujenga nyumba hizi. Hii ni pamoja na Mamlaka za Miji kuwawezesha kupata kwa haraka vibali vya ujenzi ili kufanya gharama za ujenzi zisiongezeke pindi wanapochelewa kuanza mradi husika.

• Katika kipindi hiki, Shirika limeshiriki kikamilifu katika kusaidia juhudi za Serikali za kuondoa umaskini nchini. Kwa kuzingatia umuhimu wa kundi la vijana katika mustakabali wa amani na utulivu wa Taifa letu, Shirika limetengeneza sera ya kuhudumia Jamii, iliyojikita zaidi katika kusaidia vikundi vya vijana ili waweze kutengeneza matofali yatakayotumika kujenga nyumba za gharama nafuu. Hivi karibuni Shirika hili liliingia makubalianao na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) ya kuwatumia vijana waliyohitimu VETA kutengeneza matofali katika kanda tano zenye miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu wakitumia mashine za kisasa za Hydraform. Mradi huu utasaidia kutengeneza matofaliyenye thamani ya shilingi bilioni 53 hadi kukamilika.
• Aidha, Shirika hili kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 1962, limeamua kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuondoa umaskini kwa kutoa mashine za kufyatulia tofali 640 kwa Halmashauri zote za Wilaya na Miji 160 zilizoko nchini mwetu. Mashine hizo zitatumiwa na vikundi vya vijana vitakavyoundwa na Halmashauri hizo, kila Halmashauri ikipewa msaada wa mashine nne (4) ambazo, kila mashine itakuwa ikihudumia vijana wapatao kumi.

Katika mpango huo unaogharimu shilingi milioni 650, zitapatikana ajira ya moja kwa moja kwa vijana wapatao 6,400 katika Halmashauri zote 160. Aidha, vijana hao wataweza kuzalisha ajira zaidi ya 200,000 kutokana na kazi za ujenzi zitakazofanywa na wananchi kwa kutumia matofali yatakayotengenezwa na vijana hao. Kadhalika, vikundi hivyo vya vijana vitaunda SACCOS zao na hivyo kupanua shughuli zao za kiuchumi. Pamoja na msaada wa mashine hizo, Shirika litatoa Shilingi laki tano (500,000/=) kwa kila Halmashauri kama kianzio cha vijana hao kununua vifaa muhimu vya kuwezesha kazi ya kufyatua matofali kuanza.

Ili kufanikisha mpango huo wenye maslahi makubwa kwa vijana, na nchi yetu, Shirika kwa kushirikiana na Wakala wa Utafiti wa Vifaa Bora vya Ujenzi (NHBRA) iliyo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na VETA litatoa mafunzo ya siku 21 kuanzia mwezi Desemba 2013 hadi Januari 2014 kwa wataalam wapatao 50, wawili kutoka kila Mkoa ambao baadae watatumika kutoa mafunzo kwa vijana katika Halmashauri za Wilaya na Miji kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2014.  Mafunzo hayo yanahusu namna ya kutumia mashine hayo na udongo unaofaa katika kutengenezea matofali.
3.0 MIKAKATI ILIYOWEZESHA UTEKELEZAJI WA ILANI
Katika kuwezesha utekelezaji wa Ilani hii mikakati ifuatayo ilitumika:-
• Kuwa na mpango mkakati wa miaka mitano 2010/11 hadi 2014/15 ambao umekuwa ni dira ya kuongeza ufanisi na kutekeleza mipango tuliyojiwekea
• Kuungwa mkono na Serikali katika kusukuma mbele ajenda ya nyumba.
• Utafutaji wa mtaji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba- Serikali kupitia Wizara ya fedha ililiruhusu Shirika kukopa kiasi cha shilingi bilioni 300 kutoka katika mashirika mbalimbali ya kifedha. Kutokana na kibali hiki, benki 15 za ndani na nje ya nchi zilikubali kukopesha Shirika kiasi cha shilingi bilioni 310. Hadi Juni 2012, Shirika liliiingia mikataba na benki tisa (9) zilizokubali kutoa kiasi cha shilingi bilioni 165.4 kwa ajili ya kuongeza hazina ya ardhi na miradi ya ujenzi wa nyumba.
• Sambamba na juhudi hizo, Shirika pia liliingia mikataba na benki (8) nchini kwa ajili ya kuwakopesha wanunuzi wa nyumba za Shirika. Benki hizi zimeanza kutoa mikopo kwa wanunuzi wa nyumba za Shirika na kuwezesha kasi ya ujenzi wa nyumba kuwa kubwa hivi sasa.
• Kuwa na mkakati wa kuzungusha fedha zinazopatikana kwa kuuza nyumba hata kabla ya ujenzi kukamilika (pre - sale) kuswezesha ujenzi wa nyumba bila kutegemea mikopo mikubwa ya taasisi za fedha.
• Kuwa na utaratibu wa kushirisha mapato ya Shirika na taasisi binafsi (revenue sharing model) utaratibu unaowezesha kuwekeza mtaji mkubwa kujenga majengo makubwa ya kisasa.
• Kujenga nidhamu ya kazi na uadilifu wa wafanyakazi wetu hali iliyofanya wadau mbalimbali kuliunga mkono Shirika. Kwa sasa malalamiko yaliyoelekezwa kwenye Shirika na wananchi mbalimbali yamepungua sana.
• Kudhibiti mapato ya Shirika kwa kuhakikisha kodi ya nyumba inalipwa na kila mpangaji na kwamba wote waliyonufaika na nyumba za Shirika kinyemela wamekatiwa mirija hiyo na mapato stahiki kuingia katika mapato ya Shirika.
• Kupungua kwa kesi zilizokuwa zikitishia uhai wa mapato ya Shirika. Kesi hizi zilifunguliwa na watu wajanjawajanja ambao walitumia udhaifu wa Watendaji wa Shirika kushinda kesi kirahisi hata kama hawakuwa na uhalali wa kesi hizo. Baada ya kuona kuwa Shirika liko imara katika kusimamia kesi zake, watu wengi waliolifungulia kesi Shirika wamefuta kesi hizo au kuzimaliza nje ya mahakama.
4.0 MWISHO:
Ndugu Wanahabari, kama mnavyofahamu, sekta ya nyumba ni sekta mtambuka katika maendeleo ya uchumi. Sekta ya nyumba husaidia kuleta maendeleo ya haraka ya sekta zinginena kutoa ajira. Taifa linalozingatia sekta ya nyumba huwezesha nchi yao kuwa na amani, kwani mtu mwenye makazi bora, huthamini uwepo wa amani. Hivyo, natoa wito kwa wadau mbalimbali kuithamini na kuisaidia sekta hii ili iweze kuleta tija kwa maisha ya watanzania wengi. Natoa rai kwa taasisi zingine kuona umuhimu wa kusaidia Shirika letu kuweza kujenga nyumba hususan za watu wa kipato cha chini na kati ili kwa pamoja tuweze kujenga jamii huru yenye amani na siha njema.

No comments:

Post a Comment