Picha kwa hisani ya jestina-george.com
SIMBA na Yanga zimetoka sare. Ni sare ambayo haikutegemewa
na mashabiki wa Yanga waliokuwa wanaamini timu yao ingeweza kupata ushindi wa
mabao mengi baada ya kuongoza kwa mabao 3-0 hadi timu zinakwenda mapumziko.
Lakini kitendo cha Simba kurudisha mabao yote matatu katika
kipindi cha pili, siyo tu kimedhihirisha kwamba ngome za timu zote ni mbovu na
kwamba timu zetu hazina utamaduni wa kulinda mabao yao, bali kimewakumbusha
wengi sare ya ajabu ya ‘funga-nirudishe’ kama ile ya mwaka 1996 mjini Arusha.
Yawezekana wengine wamesahahu mechi hiyo, ambayo ilikuwa ya
pili kwa timu hizo kukutana mjini Arusha. Ngoja niwamegee uhondo.
Wapenzi wa soka wa mikoa ya Singida, Dodoma, Mara,
Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dar es Salaam na nchi jirani ya Kenya walianza
kuwasili mjini Arusha kuanzia Novemba 7 kushuhudia pambano la soka la marudiano
la Ligi Kuu ya Muungano kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga, ambalo
lilipangwa kufanyika Jumamosi, Novemba 9, 1996 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid.
Timu hizo zilipambana baada ya miaka sita tangu
zilipopambana kwa mara ya kwanza mjini humo mwaka 1989 katika kuwania Kombe la
Bonanza lililoandaliwa na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) na
Yanga kunyakua ubingwa huo kwa ushindi wa goli 1-0 lililofungwa na Joseph
Machella.
Mashabiki hao waliwasili sambamba na timu hizo zilizoondoka
Jijini Dar es Salaam siku hiyo ya Alhamisi, Novemba 7 kwa mabasi kufuatia
msaada wa tiketi 30 ambazo kila moja ilipewa na Chama cha Soka Tanzania (FAT)
baada ya chama hicho kukosa shilingi milioni moja za kuipa kila timu kwa ajili
ya maandalizi. Simba iliwasili kwa basi la Super Star wakati Yanga ilikwenda
kwa basi la Tawfiq na kupelekwa na mfadhili wao wa mjini humo ‘kula maraha’
katika hoteli ya kitalii ya Sakina.
Pambano hilo, lilichezeshwa na mwamuzi Bakari Mtangi wa
Tanga aliyesaidiana na washika vibendera Aggrey Mnzavas wa Kilimanjaro na Sudi
Abdi wa Arusha. Kiingilio katika pambano hilo, ambalo mgeni rasmi alikuwa Jaji
wa Mahakama ya Kimataifa iliyokuwa inashughulikia mauaji ya Rwanda Leonnart
Aspegren, kilikuwa Shs. 5,200 kwa Jukwaa A, Shs. 2,200 mzunguko na Shs. 500 kwa
yosso.
Hata hivyo, bao lililofungwa na Dua Said dakika za majeruhi
siku hiyo liliiokoa Simba kuepuka janga la kuendelea kuwa mteja wa Yanga mwaka
huo na kuzifanya timu hizo zitoke sare ya magoli 4-4 katika pambano
lililopooza.
Hii ilikuwa mechi pekee ya sare ya magoli mengi kuliko zote
baina ya timu hizo. Mechi iliyokuwa na magoli mengi kuliko zote ilikuwa ya
mwaka 1992 Simba iliposhinda kwa penati 6-5 na mwaka 1966 Yanga ilipoifunga
Simba 5-4.
Simba ilikuwa inaongoza kwa
magoli matatu hadi dakika ya 60.
Iliwachukua vijana wa Mtaa wa Msimbazi dakika saba tu kuhesabu goli la kwanza
kupitia kwa Thomas Kipese kwa shuti kali la mpira wa adhabu lililokwenda moja
kwa moja wavuni. Adhabu hiyo ilitolewa na mwamuzi Bakari Mtangi wa Tanga baada
ya mlinzi Abdallah Msheli kumfanyia madhambi Ahmed Mwinyimkuu wa Simba katika
eneo la hatari.
Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya Yanga wazinduke na
kuliandama lango la Simba mfululizo katika dakika za 10,19 na 22, lakini
walikosa mabao ya wazi kabisa. Jitihada za timu hiyo kusawazisha zilizaa
matunda katika dakika ya 28 wakati Edibily Lunyamila alipoifungia bao kwa njia
ya penati. Lunyamila aliwasili mjini humo muda mfupi kabla ya pambano akitokea
Afrika Kusini kupitia Nairobi. Penati hiyo ilitolewa na mwamuzi Mtangi baada ya
Rajab Msoma wa Simba kuunawa mpira katika eneo la hatari katika jitihada za
kuokoa.
Dakika tatu baadaye kipa Baldwin Sisinawa wa Yanga ilimbidi
afanye kazi ya ziada kuokoa bao la wazi alipopangua kiki kali ya Bitta John na
kuwa kona ambayo haikuzaa matunda. Mwinyimkuu aliwarejeshea furaha mashabiki wa
Simba alipofunga bao la pili katika dakika ya 43 baada ya kuunganisha hewani
krosi ya Kipese aliyoituliza gotini kabla ya kufumua shuti kali lililojaa
wavuni. Hadi mapumziko Simba ilikuwa inaongoza kwa 2-1.
Kipindi cha pili Simba iliwatoa Hoza, Bitta na Mwinyimkuu
na kuwaingiza Marsha, Tigana na Dua, wakati Yanga iliwatoa Sylvatus Ibrahim na
Bushako na nafasi zao kuchukuliwa na Mgaza na Anwar. Mabadiliko hayo yalianza
kwa Simba kupata bao la tatu lililofungwa na Dua Said kwa kichwa katika dakika
ya 60 kufuatia krosi ya Mwanamtwa Kihwelu iliyomkuta Bitta (kabla hajatoka)
aliyemsogezea mfungaji ambaye aliukwamisha mpira wavuni.
Pamoja na magoli hayo, Yanga haikukata tamaa na juhudi zao
ziliwezesha kupata bao la ‘dezo’ katika dakika ya 64 wakati Hoza (kabla
hajatoka) alipojifunga mwenyewe wakati alipokuwa anamrejeshea kipa wake Issa
Manofu, ambaye alikuwa ametoka golini.
Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Kizota katika dakika ya
70 kwa kichwa baada ya kuunganisha wavuni mpira uliorushwa na Bakari Malima.
Katika dakika ya 75 Sanifu Lazaro aliifungia Yanga goli la nne kwa kichwa
lililoamsha mayowe mengi kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo. Sanifu alifunga bao
hilo kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Lunyamila aliyemlamba chenga Deo Mkuki
na kumimina krosi iliyomkuta mfungaji.
Wachezaji wa timu ya soka ya Yanga walilalamika kuwa,
walipunjwa mgao wao uliotokana na mapato ya mechi hiyo. Wachezaji hao walisema,
mbali ya kupunjwa mgao wao, walidanganywa pia na viongozi wao kuwa, klabu hiyo
ilipata shilingi milioni 4.0 kutokana na shilingi milioni 30.5 zilizopatikana
katika mechi hiyo. Kila mchezaji alipata Shs. 73,000, kiasi ambacho ni asilimia
40 ya shilingi milioni nne, kinyume na makubaliano kati yao na viongozi kwamba,
timu hiyo inapotoka sare wachezaji hustahili asilimia 50 ya mapato hayo.
Katika mchezo huo viongozi waliosimamia mapato huko Arusha walikuwa Mwenyekiti Jabir Katundu
na Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward Ngabona, ambaye ndiye aliyegawa fedha hizo kwa
wachezaji. Wakati kila mchezaji alipata Shs. 73,000, makocha wa timu hiyo,
Sunday Kayuni na Jella Mtagwa na daktari wa timu, Godfrey Kalimba, walipata
Shs. 109,000 kila mmoja.
Wachezaji hao walimshutumu Ngabona kwa kutoa taarifa kwenye
vyombo vya habari kuwa, kila mchezaji alipata Shs. 100,000 kutokana na mapato
ya mchezo huo wakati haikuwa kweli. Waliilaumu pia FAT kwa kuwapa mgao wa timu
hiyo viongozi wa klabu badala ya wachezaji kama walivyoomba kabla ya mchezo huo
kutokana na kutokuwa na imani nao baada ya kuwadhulumu zawadi ya ushindi wa
pili ya Shs. Milioni 2.5 ya Kombe la Hedex Afrika Mashariki na mechi
nyinginezo.
Walisema, kulaghaiwa kwao kulichangiwa sana na kuugua
ghafla kwa mjumbe wa Kamati ya Kudhibiti Mapato ya klabu hiyo, Majjid Suleiman,
mara baada ya mchezo huo, ambaye walisema alikuwa mstari wa mbele kutetea haki
na maslahi ya wachezaji wa timu hiyo. Majjid ndiye aliyesimamia mapato ya timu
hiyo ilipopambana na Simba kwenye mchezo wa awali wa Ligi Kuu ya Muungano na
pia zawadi ya Shs. Milioni 7.5 ilizopata kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Safari
Lager, ambapo kila mchezaji alipata Shs. 195,000.
SIMBA: Issa Manofu, Deo Mkuki, Alphonce Modest, Mustafa
Hoza/Hussein Marsha, Mathias Mulumba, Shaaban Ramadhan, Mtwa Kihwelu, Bitta
John/Ally Yussuf, Abdallah Mwinyimkuu/Dua Said, Rajab Msoma na Thomas Kipese.
YANGA: Baldwin Sisinawa, Sylvatus Ibrahim/Reuben Mgaza,
Kenneth Mkapa, Bakari Malima, Abdallah Msheli, Said Mwamba, Idelfonce Amlima,
Thabit Bushako/Anwar Awadh, Mohammed Hussein, Sanifu Lazaro na Edibily
Lunyamila.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment