Kikosi cha Yanga cha mwaka 1994. Kutoka kushoto waliosimama ni Salum Kabunda 'Ninja', Constantine Kimanda, Steven Casmir Nemes, Kenneth Pius Mkapa, Selemani Mkati. Waliochuchumaa kutoka kushoto ni Nico Bambaga 'Machine', Sekilojo Chambua, Edibily Lunyamila, James Tungaraza 'Boli Zozo', na Said Mwamba 'Kizota'.
Na Daniel
Mbega
YOUNG
Africans, ambayo mwaka 1993 iliteswa sana na wapinzani wake wa jadi, Simba,
baada ya kutamba misimu miwili ya nyuma, hatimaye Jumamosi Februari 26, 1994
iliingia kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwakabili ‘wanyama hao wakali’
wa Msimbazi, ambao mwaka huo walikuwa wameongeza makucha yao kwa kuwasajili
wachezaji mahiri na wauaji wa mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara, Yanga.
Katika mchezo huo wa raundi ya nne ya Ligi Daraja la Kwanza ya Tanzania Bara, Young Africans waliingia uwanjani wakiwa wanadharauliwa kutokana na ubutu wa fowadi yao tokeo ligi hiyo ianze na kutokana na jinsi walivyoonyesha mchezo hafifu dhidi ya Moroka Swallows ya Afrika Kusini katika mechi ya Kombe la CAF kwenye uwanja huohuo Jumamosi ya Februari 19.
Katika mchezo huo wa raundi ya nne ya Ligi Daraja la Kwanza ya Tanzania Bara, Young Africans waliingia uwanjani wakiwa wanadharauliwa kutokana na ubutu wa fowadi yao tokeo ligi hiyo ianze na kutokana na jinsi walivyoonyesha mchezo hafifu dhidi ya Moroka Swallows ya Afrika Kusini katika mechi ya Kombe la CAF kwenye uwanja huohuo Jumamosi ya Februari 19.
Licha ya
kuwa na wachezaji kama Edward Chumila na Dua Said, ambao walikuwa wauaji
wakubwa wa Young Africans, siku hiyo pia Nteze John Lungu aliongezeka katika
safu ya wachezaji wa Simba waliokuwa na usongo na timu ya Jangwani, kwani
makeke yake yalikuwa yanaeleweka wakati alipokuwa na Pamba ya Mwanza. Kwa
upande mwingine, Young Africans kwa wakati huo haikuwa na mchezaji yeyote
aliyekuwa na asili ya kuitisha Simba, hasa baada ya Said Mwamba kuumia na
kulikuwa na hati hati ya kutocheza siku hiyo.
Mchezo
huo ndio uliotarajiwa kudhihirisha mengi katika msimu huo wa ligi na hasa
ulikuwa mtihani wa mambo kadhaa kwa timu zote mbili.
*Mchezo
huo ulikuwa mtihani mkubwa zaidi kwa uongozi mpya wa Young Africans chini ya
Mwenyekiti Dk. Jabir Katundu.
*Mchezo
huo ulikuwa mtihani mkubwa kwa makocha wa kigeni, Tambwe Leya wa Zaire
aliyekuwa akiifundisha Young Africans na Dragan Popadic wa Yugoslavia aliyekuwa
akiinoa Simba.
*Mchezo
huo ulikuwa mtihani mkubwa kwa wachezaji wapya wa timu zote mbili ili
kudhihirisha kama usajili uliofanyika ni wa maana. Uwezo wa walinzi Constantine
Kimanda na Ngandou Kazadi Ramadhani kutoka Burundi ulitarajiwa kuthibitishwa
katika ngome ya Yanga, pia akina Philemon ‘Fumo’ Felician, Sekilojo Chambua,
James Tungaraza, Nteze John, Masoud Shaaban, Dua na mdogowe Samora Said na
wengineo, nao walikuwa wakiangaliwa wangefanya nini siku hiyo.
*Pia
mchezo huo ulikuwa unaangaliwa kama ungeweza kusababisha migogoro mingine
kwenye klabu hizo, ambazo kila mara zilikuwa zikiparaganyika baada ya mchezo
kama huo.
Fowadi ya
Young Africans, ambayo msimu huo ilikuwa inaelezwa kuwa butu, hatimaye siku
hiyo ya Jumamosi Februari 26, 1994 iligeuka kuwa kali na kuwakata vibaya
wapinzani wake wa jadi, Simba kwa kuicharaza magoli 2-0. Safu hiyo ya
ushambuliaji ilionekana kuwa kali tangu mchezo huo ulipoanza, ambapo
washambuliaji kama James Tungaraza, Sekilojo Chambua, Edibily Lunyamila,
Mohammed Hussein walifanya kazi nzuri huku wakisaidiwa na mabeki walioongozwa
na Warundi Constantine Kimanda na Ngandou Ramadhani.
Magoli
yote mawili ya Yanga yalipatikana katika kipindi cha pili baada ya timu zote
kukosa nafasi nzuri za kufunga katika kipindi cha kwanza, hasa Yanga, ambayo
washambuliaji wake walitaka kuonekana butu kweli kabla ya kubadilika katika
kipindi cha pili.
Mohammed
Hussein alifunga goli lake la kwanza kutokana na juhudi zake za kuuwahi mpira
baada ya George Masatu aliyelala chini kuuparaza kwa mkono. Lakini goli la pili
ndilo lililokuwa la kiufundi zaidi, ambalo lilikaribiana na goli ambalo
lilifungwa na Boli Zozo wa Stella Abidjan ya Ivory Coast dhidi ya Simba katika
fainali ya Kombe la CAF mjini Dar es Salaam mwaka 1993, ambalo nalo lilikuwa la
pili katika kipindi cha pili.
James
Tungaraza, ambaye alifunga goli hilo, alipokea pasi kutoka kwa Sekilojo Chambua
na kuanza kuwahesabu mabeki wa Simba mmoja baada ya mwingine hadi alipomuona
Mohammed Mwameja alikokuwa ameelekea na kuujaza mpira upande mwingine wa nyavu,
tena huko ndiko Boli Zozo alikoukwamisha.
Goli hilo
liliwafanya mashabiki kulipuka kwa hoi hoi wakilitamka jina la Boli Zozo...Boli
Zozo!!
Washambuliaji
wa Simba, Nteze John, Madaraka Selemani, Edward Chumila (na baadaye Abdul
Ramadhani Mashine) na Juma Amir, hawakuonekana walichokifanya na hata mabeki wa
Simba, wakiongozwa na George Magere Masatu na Godwin Aswile walizidiwa maarifa
na kumfanya kipa wao Mwameja mwenye majivuno mengi kuelemewa na mashambulizi ya
Yanga.
YANGA: Stephen Nemes, Ngandou Ramadhan, Kenneth
Mkapa, Method Mogella, Constantine Kimanda, Nico Bambaga, Sanifu Lazaro/Fumo
Felician, Sekilojo Chambua, James Tungaraza, Mohammed Hussein, Edibilly
Lunyamila/Alli Yusuf ‘Tigana’. Kocha: Tambwe Leya (Zaire)/Nzoysabah Tauzany
(Burundi).
SIMBA: Mohammed Mwameja, Kasongo Athumani, Mustafa
Hoza/Thomas Kipese, Godwin Aswile, George Masatu, Iddi Selemani, Athumani
China, Edward Chumila/Abdul Mashine, Juma Amir, Nteze John. Kocha: Dragan
Popadic (Yugoslavia)/Abdallah Kibadeni.
Waamuzi
wasaidizi walikuwa Joseph Kimoho wa Morogoro na Leslie Liunda wa Dar es Salaam,
wakati mgeni rasmi alikuwa Augustine Lyatonga Mrema, Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment