Mzee Kungubaya akiwa na gitaa la galatone enzi hizo. Picha kwa hisani ya Kijiwe cha Kitime.
Na Daniel Mbega
Wakati
umewadiwa
Wa
salamu za wagonjwa
Hospitalini
Leo
tunawapa pole x2
Ajuaye
Bwana Mungu
Kwa
mzima kuwa mfu
Mgonjwa
kuwa salama
Leo
tunawapa pole x2
Kipindi
chenu kinawapa pole
Wote
tunawapa pole
Mungu
awajalieni pole x2
Tunawapa
pole x2.
SWADAKTA kabisa. Hapana
shaka yoyote kwamba, mashairi haya si mageni masikioni mwa Watanzania walio
wengi, kwani ndiyo hufungua na kufunga kipindi cha saa nzima cha Ugua Pole,
kilichobeba jina la wimbo huo, kinachosikika Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD)
kila siku ya Jumapili kuanzia saa 4.02 asubuhi hadi saa 5.00.
Lakini pamoja na kufahamika kwa mashairi hayo hata kwa vijana wa kizazi cha leo, ni dhahiri kwamba si wengi wanaomfahamu mtunzi wa wimbo huo unaoendelea kutamba redioni mpaka leo.
Lakini pamoja na kufahamika kwa mashairi hayo hata kwa vijana wa kizazi cha leo, ni dhahiri kwamba si wengi wanaomfahamu mtunzi wa wimbo huo unaoendelea kutamba redioni mpaka leo.
Huyu si mwingine bali ni
Omar Kungubaya, mkongwe wa muziki aliyedumu katika fani hiyo kwa zaidi ya miaka
50.
Kwa wale vijana wa zamani,
yaani wa miaka ile ya '47, enzi ambazo nyimbo kama za 'Nina Mpenzi wangu Kibamba' zilikuwa zikitamba sana katika majukwaa
ya muziki, basi watakuwa na kumbukumbu tosha ya mwanamuziki huyo mkongwe,
ambaye hata hivyo, kama walivyo wengi wao, hakunufaika na lolote katika muziki.
Wapenzi wengi wa muziki wa
dansi walishafikiria kwamba huenda mzee huyu alikwisharejesha namba kwa Mungu
kutokana na ukimya wake wa muda mrefu katika majukwaa makubwa ya muziki,
tofauti na wakongwe wengine ambao wanaendelea kuimba katika bendi
zinazofufuliwa na kisha kuzikwa tena kutokana na kushindwa ushindani wa
kibiashara.
Sijui kwa sasa mahali
aliko, lakini nakumbuka nilikutana naye mwaka 2002 katika ukumbi wa Container
Bar, Maili Moja Kibaha na kufanya mazungumzo naye, wakati akiishi Kibamba. Kama
yu hai, basi wakati huu atakuwa na miaka 74.
Hata hivyo, staili aliyokuwa
akiitumia wakati nakutana naye ni tofauti na ile ya zamani ya kuwa na bendi,
kwani kila siku za wiki endi alikuwa anazunguka kwenye kumbi mbalimbali, baa na
hata vilabu vya pombe za kienyeji akiwa na 'bunduki' yake, yaani gitaa aina ya galatone akiwaburudisha wateja waliokaa
kwenye meza kwa ajili ya kustarehe.
Kwa upande wao, wateja nao
huamua kumtuza chochote, lakini ilimuwia vigumu kuweza kuwashawishi ili
wampatie fedha kutokana na nyimbo anazoimba.
Hali hiyo ilimfanya mwanamuziki
huyo mkongwe awe akizunguka mpaka kwenye vilabu vya uchochoroni, hususan huko
Kibaha-Maili Moja, ambako nilikutana naye.
Kwa ujumla, staili hiyo,
inayojulikana zaidi kama 'Chuna Buzi', haikuwa ikimnufaishi chochote zaidi ya
kumuwezesha kupata angalau senti kidogo kwa ajili ya mkate wake wa kila siku
tofauti kabisa na mchango wake alioutoa katika jamii.
ALITOKA
WAPI?
Mzee Kungubaya ni matunda
mengine ya hazina isiyokwisha kutoka mkoa wa Morogoro, ambao umejaa vipaji vya kila
aina. Alizaliwa mwaka 1939 katika Kijiji cha Mgaza Vigolegole, Morogoro, ambapo
alipata elimu yake ya msingi (darasa la nane) Msamvu Middle School mwaka 1955.
Alishindwa kuendelea na
masomo ya darasa la tisa kutokana na wazazi wake kushindwa kumlipia karo.
Historia yake kimuziki
inaanzia mwaka huo wa 1955 akiwa shuleni Msamvu, ambapo wakati huo alikuwa na
umri wa miaka 16 tu, na aliweza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa bendi ya shule na
mara baada ya kumaliza shule akajiunga rasmi na bendi ya Cuban Marimba
iliyokuwa chini ya Salim Abdallah Yazidu 'Say'.
Itakumbukwa kwamba, bendi
hiyo iliyokuwa na maskani yake Nunge Welfare (sasa eneo hilo linajulikana kama
Mji Mpya), Morogoro ilikuwa tishio kwa bendi nyingi za Dar es Salaam na ndiyo
iliyoibua vipaji vya wanamuziki wengi. Kwa sasa bendi hiyo imetoweka katika
ulimwengu wa muziki.
Katika mahojiano maalum,
Mzee Kungubaya alimtaja Kibwana Katashingo, aliyekuwa dereva wa marehemu Salim
Abdallah na pia mpiga drum wa bendi hiyo, kwamba ndiye aliyekuwa mwalimu wake
wa kwanza katika muziki wakati alipojiunga na Cuban Marimba, ambapo yeye
Kungubaya alikuwa akipiga gitaa la galatone
lenye nyuzi sita.
Mwaka 1960 Kungubaya
alichanja mbuga na kuelekea Nairobi, Kenya kwa kile alichosema alikwenda
kujiendeleza kimuziki.
"Huko nilipokelewa na
wanamuziki wakongwe wakiwemo akina John Ondolo Chacha, John Mwale na David
Amunga, ambao wote walikuwa wakikung'uta magiaa ya galatone kwenye vilabu mbalimbali jijini humo.
"Hata hivyo, mwaka
uliofuata nilirejea Morogoro na kujiungan na bendi ya Kilosa Jazz iliyokuwa
ikiundwa na akina Yahya Abbas na marehemu Abel Baltazar. Nilidumu na bendi hiyo
hadi mwaka 1963," alieleza Kungubaya.
Alisema kwamba, aliamua
kurejea tena Cuban Marimba, ambapo viongozi wa bendi hiyo wakampeleka kwa Mzee
Mwaipungu aliyekuwa akiongoza bendi nyingine iliyokuwa tawi la Cuban Marimba,
lakini mwaka 1969 akaondoka.
Safari hii aliamua
kuyaweka kando masuala ya muziki na kuwa 'cashier' katika vituo vya kuuza
mafuta vya Capital Esso Services kilichopo Mtaa wa India na baadaye kituo cha
Agip Centre cha Mwembesongo. Hii ilikuwa mwaka 1970.
Alieleza kwamba, mwaka
1971 akaamua kurejea tena masuala ya muziki, ambapo mara hii alikuwa
akijitegemea mwenyewe. Kama ilivyo ilivyokuwa wakati nakutana naye, alikuwa
akipiga gitaa moja tu la galatone,
ambapo alihamia Dar es Salaam na kuanza kutumbuiza katika baa moja iliyokuwa
ikimilikiwa na Mama Hamm huko Tandale, Manzese.
Penzi, anasema, halina
mipaka na halichagui fukara wala tajiri. Kwanini? Anasema kwamba, bosi wake
huyo 'alimzimia' na kuanguka kwenye penzi.
"Hivyo nikaamua
kumuoa mama huyo, ambaye hadi anafariki mwaka 1995 hatukubahatika kupata mtoto.
Lakini mwaka 1974 tulinunua shamba kijijini Kwembe, na kuanzia hapo mpaka
anafariki tulikuwa kijijini na ndiko ninakoishi mpaka sasa," alibainisha.
Mzee Kungubaya alisema
kwamba, kabla mkewe huyo hajafariki alimpa ruksa ya kuoa mwanamke mwingine,
ameoa, na wamebahatika kupata watoto watatu, ingawa mmoja alifariki.
ANAFANYA
NINI SASA?
"Kama ujuavyo, hivi
sasa nimekuwa mwanakijiji. Shughuli zangu ni za kilimo ingawa kwa kweli sina
mtaji wa kutosha na mara nyingi natumia jembe la mkono," alisema.
Alisema ingawa yuko
kijijini, lakini muziki kwa vile uko kwenye damu yake hawezi kuuacha, ndiyo
sababu kila siku ya Ijumaa hadi Jumapili jioni alikuwa akionekana katika baa
mbalimbali huko Kibaha-Maili Moja, akiwatumbuiza watu kwa kutumia gitaa lake la
galatone alilolinunua miaka ya 1970.
Mara nyingi ungemkuta
akiimba nyimbo nyingi zilizopata kutamba miaka ya 1960 hadi 1970, hususan nyimbo
kama Mtoto si Nguo na Ndugu sikilizeni navunja vunja vikombe
zilizoimbwa na Heorge Mukabi wa Kenya, na Wanawake
wa Tanzania na Maneno madogo madogo
kwa mabibi na mabwana zilizoimbwa na marehemu Salim Abdallah kule Cuban
Marimba.
Wakati wa enzi zake alitunga
nyimbo nyingi sana, lakini alisema kwamba, katika miaka 47 akiwa kwenye jukwaa
la muziki hakunufaika na chochote zaidi ya kuishia kutumbuiza vilabuni!
Hata hivyo, aliitaka
serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuwajali wasanii wa zamani kwa kuwaenzi na
ikibidi iwekwe siku maalum ya kuwakumbuka wakongwe wa zamani na kazi zao.
Aidha, alisema kwa kuwa
Sheria ya Haki Miliki imekwisha pitishwa na serikali, basi ni vyema hata
wasanii wa zamani wafikiriwe kupewe chochote na Radio Tanzania kutokana na kazi
zao zilizohifadhiwa huko, ambazo sasa RTD (TBC Taifa) imekuwa ikiziuza.
Nipe maoni yako: brotherdanny5@gmail.com au 0715
070109
No comments:
Post a Comment