Mwalimu Nyerere akiwa na mama yake mzazi, Bi Mgaya (kushoto) na mkewe Bi Maria Nyerere mwaka 1993.
Na Daniel Mbega
DEMOKRASIA ya sasa imepanuka kuliko ilivyokuwa miaka ya
nyuma, hasa kipindi cha ukoloni. Leo hii tunashuhudia hata vijana wa shule
wanaifahamu vyema siasa, huku uongozi ukishikwa na vijana wadogo, wengine
wakiwa hawajafikisha hata miaka 30.
Mwaka huu tunapomuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo chake, tumeona bora tuzungumze, na tulete hotuba yake, akielezea namna alivyoanza siasa miaka ile ya 1950, mara baada ya kurejea kutoka mamsomoni Scotland.
Mwaka huu tunapomuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo chake, tumeona bora tuzungumze, na tulete hotuba yake, akielezea namna alivyoanza siasa miaka ile ya 1950, mara baada ya kurejea kutoka mamsomoni Scotland.
Yeye anasema kwamba alianza akiwa ‘mdogo’ akiwa na miaka 30
hivi mwaka 1952 aliporejea, lakini kwa sasa ukitaja miaka hiyo huwezi amini
kama hukuwakuta waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hata
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakiwa wametopea kweli kwenye siasa.
Kwa miaka ile umri huo alikuwa bado mdogo, na hata yeye
mwenyewe anakiri kwamba alikuwa kijana mdogo.
Hata hivyo, Mwalimu aliamini kwamba wazee ndio nguzo ya
maendeleo ya nchi, kwani yeye mwenyewe asingeweza kufanikiwa kama si kulelewa
na wazee waliompa miongozo ya kutosha hadi akafikia mahali alipofikia.
Mwalimu aliyasema haya mbele ya Baraza la Wazee wa Dar es
Salaam wakati alipokuwa akiagana nao kabla ya kung’atuka mwaka 1985. Hebu
tuungane…
“MIMI nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa
Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli. Nilirudi kutoka masomoni,
Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka
thelathini na kidogo hivi.
Niliporudi nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu
(sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini nikiwa shuleni – Chuo Kikuu –
nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya siasa. Niliamua hivyo:
Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali inavyokwenda na kuzoeana na
wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.
Niliporejea nchini hapo Oktoba, nikaenda Butiama. Januari
nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi. Nikataka kujua habari za African
Association. Mzee Mwangosi anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African
Association. Aliisha niambia habari hizo tangu nikiwa Makerere – Chuo Kikuu –
nikiwa mwanafunzi.
Pale, mimi na wanafunzi wenzangu tulikuwa tumeanzisha chama
kinachoitwa Tanganyika African Welfare Association (TAWA) cha wanafunzi wa
Tanganyika; mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri
kidogo.
Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na siyo
Tanganyika nzima. Kwa hiyo nikawaandikia baadhi ya watu Tanganyika. Nikasema,
jamani ee, tumeanzisha chama, kwanini msianzishe huko matawi ya chama hicho?
Ndugu Mwangosi
akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo. Akaniandikia –
nikiwa Makerere – akasema: Wewe kwanini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo
chama. Kipo Chama cha TAA (Tanganyika African Association).
Kwa hiyo la
maana si kuanzisha matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la maana ni
kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African
Association.
Hivyo ndivyo
tulivyofanya. Kwa hiyo mimi nikawa katibu wa katawi la TAA hapo Makerere.
Niliporudi Tabora na kuanza kufundisha pale St. Mary’s (sasa inaitwa Milambo
Sekondari), nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa
Tabora. Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa
mjumbe kutoka Tabora.
Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association.
Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za
TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es
Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA? Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa
Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo.
Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye naye aliteleza-teleza
na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu.
Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi
Radio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa
Sykes.
Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi
mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka.
Tukafanya mkutano hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa rais
wao – wa TAA.
Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa
walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na
Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.
Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa
hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais
wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa
madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.
Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili
lilipendekezwa na kina Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani,
walipokuwa askari vitani huko Burma (Vita vya Pili).
Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es
Salaam, kwa mguu; kila Jumamosi. Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa
ninakuja mjini kukutana na wenzangu; kufanya mikutano.
Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana.
Tukawa na uhusiano mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes,
Abbas Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.
Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: Wazee na
ndugu zangu! Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU.
Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo! Vijana
walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.
Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru!
Unaweza ukakosa kazi; na wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi. Kina
Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.
Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga
mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.
Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu. Huko
wazee walinipokea na kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika
nzima. Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha
wazee, ndani ya nyumba ya mtu.
Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini?
Nikawaambia natafuta uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na
wanakumbuka, kabisa, wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano
wa makini kweli. Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani
kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza?
Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza
wanawadanganya, Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League
of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati
tutakapokuwa tayari, watuachie tukajitawale.
Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi. Vita vimekwisha (vya
Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organisation – UNO)
umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao. Wamepewa
dhamana tu.
Kwa hiyo nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu.
Tuwaseme tu! Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao;
wamesahau kabisa!
Wazee wakauliza: Eh, inawezekana? Nikasema inawezekana. Kazi
yetu ya kwanza ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo
lilikuwa la kwanza. Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala,
lakini hawakujua waanzie wapi.
Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana.
Kwa hiyo kwa wazee sikuwa na matatizo. Wao hawakuwa na kazi; hawakumwogopa
Mwingereza. Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.
Mzee John Rupia (marehemu) alikuwa mfanyabiashara na kaidi
(mkaidi) kidogo. Aliwahi kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara.
Akaambiwa akiendelea kushirikiana na kijana mwenda wazimu (Julius Nyerere),
atanyang’anywa leseni moja kwa moja. Rupia aliwajibu: Potelea mbali!
Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na
imani yao kwa vijana wakati huo.
Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama
hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto
haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.
Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (Dar es Salaam).
Akasema: Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku.
Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana
wao kuniombea dua. Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani.
Tukamaliza.
Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi
wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika zilikuwa za Kurani; sasa zikaja dua za
wazee – za jadi.
Walikuwa na
beberu la mbuzi. Wamechimba shimo. Wakaniambia
simama. Nikasimama. Beberu akachinjwa, huku anaambiwa, “Twining (Twainingi)
umekwisha!” (Edward Twining alikuwa gavana wakati huo). Ndipo nikaambiwa:
Tambuka! Nikavuka lile shimo. Hapo nikaambiwa na wazee: Basi nenda zako; tangu
leo Twining amekwisha!
Sasa mimi Mkristo; hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi
katika mambo haya (ya kutambika). Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee wangu
hao. Kwa hiyo nilitambuka pale na kuambiwa: Nenda nyumbani salama. Twining amekwisha!
Wazee wangu wengine wanakumbuka tulikuwa tunakwenda Bagamoyo.
Kwenye makaburi kule! Tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.
Baadhi yetu mtakumbuka safari moja jamaa wa Kenya, hawa kina
Tom Mboya (marehemu) walishitakiwa. Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi?
Tukasema tufunge. Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo. Tufunge! Tukafunga.
Hakuna kula. Na siku ya kufunga tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko.
Tukafanya mkutano hadi saa 12 jioni.
Baada ya mkutano tukaenda nyumbani kwa mzee Mohammed Ramia
(marehemu). Hapa ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: Sheikh, una
Aspro? Akajibu: Kwa nini unataka Aspro? Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma
kwelikweli. Akasema subiri.
Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri. Mzee
Ramia akaniuliza: Bado unataka Aspro? Nikajibu kichwa sasa hakiumi. Kumbe
ilikuwa njaa.
Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana
sana. Tulishirikiana sana na wazee. <Mwisho>.
No comments:
Post a Comment