Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 27 October 2013

RAIS WA USWISI AIFUNDA TANZANIA JINSI YA KUPATA FEDHA ZA KIFISADI


Katika mahojiano maalumu na timu ya waandishi wa Mwananchi na The Citizen jana, Graf alisema kuwa Serikali ya Tanzania inapaswa kusaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana taarifa za masuala ya usimamizi wa fedha na kodi ili kuweza kujua ni kina nani wameweka fedha nchini kwake na kunufaika na kodi.
Graf, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini, alisema kuwa hivi karibuni Serikali ya Uswisi ilisaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana taarifa kuhusu masuala ya fedha, ambao unajulikana kwa lugha ya Kiingereza kama `Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters’.
Alisema ikisaini mkataba huo ina maana itasaidiwa na Serikali ya Uswisi kupata fedha zilizofichwa na Watanzania.
“Serikali ya Tanzania inatakiwa kuweka mkakati wa kisheria utakaotengeneza mazingira ya kubadilishana taarifa za fedha na mataifa mengine. Kwa jambo hilo hata Serikali ya Uswisi inaweza kusaidia katika kupatikana kwa fedha zilizofichwa,” alisema Graf, ambaye anaongoza Serikali ya Uswisi kwani kwa kawaida Rais wa Bunge ndiye pia kiongozi wa taifa hilo.
Graf alisema kwa sasa itakuwa ngumu kwa Tanzania kupata fedha hizo kwani haijasaini mkataba wa kimataifa wa kubadilishana taarifa za fedha na mataifa mengine.
Alieleza pia katika miaka ya karibuni Serikali ya Uswisi imeandaa muswada wa sheria wa kubana fedha zilizopatikana kwa njia za kifisadi na kufichwa katika benki za Uswisi. Graf alisema sheria hiyo ikipita itaruhusu Serikali ya nchi hiyo kutaifisha fedha ambazo zimepatikana kwa njia haramu na kufichwa katika benki za huko.
Muswada huo unaoitwa kwa lugha ya Kiingereza `Freezing and Restitution of Assets of Politically Exposed Persons obtained by Unlawful Means Bill’ ulisomwa kwa mara ya kwanza kwenye Bunge la nchi hiyo mwezi Mei, mwaka huu.
Graf alisema faida nyingine ya Tanzania kusaini mkataba huo ni kuwa, itaweza kuwatoza kodi Watanzania hao walioweka fedha huko.
Alifafanua kuwa siyo fedha zote zinazowekwa kwenye benki za Uswisi kuwa ni haramu kwani kuna nyingine zimepatikana kihalali, lakini zinaweza kutozwa kodi.
“Tanzania inakosa kodi kutokana na fedha zilizohifadhiwa na Watanzania wenye akaunti kwenye benki za Uswisi,” aliongeza Graf, ambaye alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo Novemba 26, 2012 na kutakiwa kukaa madarakani kwa mwaka mmoja.
Graf alisema pia fedha za kodi zingeisaidia Tanzania kugharimia sekta mbalimbali za maendeleo.

Zito aitupia lawama SerikaliNaye Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, ambaye yuko nchini Uswisi akifuatilia masuala ya utoroshaji fedha na kufichwa kwenye benki za huko, alisema kuwa wakati shinikizo la dunia sasa limeelekea kumaliza tatizo la ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha kutoka nchi za Afrika, lakini Serikali ya Tanzania inasuasua juu ya kupambana na jambo hilo.
Zitto alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa moja ya njia ya Serikali za nchi maskini kupata taarifa za kampuni kubwa za kimataifa yanayokwepa kodi ni mfumo wa kupashana taarifa unaoitwa kwa lugha ya Kiingereza `automatic exchange of tax information’.
“Kutokana na shinikizo la nchi mbalimbali, hivi sasa nchi zinazoitwa `tax havens’ (nchi zinazohifadhi fedha kwa siri) fedha zimeanza kuweka sahihi makubaliano ya kutoa taarifa,” alisema Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Alisema kuwa Tanzania mpaka sasa haijaweka saini na Serikali haijatoa taarifa yoyote kwa umma juu ya sababu ya kutokufanya hivyo. “Ghana, Afrika Kusini na Nigeria nchi zinazotegemea sana rasilimali kama Tanzania zimeweka saini mkataba huu tayari,” aliongeza Zitto.Alisema asilimia 44 ya fedha za kigeni inazopata Serikali ya Tanzania zinatokana na mauzo ya madini nje. Kampuni za madini ndizo zinazoongoza kukwepa kodi.
Alisema Tanzania inapoteza jumla ya Dola 500 milioni (Sh783 milioni) na Dola 1.25 bilioni (Sh2 trilioni) kwa mwaka kutokana na kampuni kubwa za kimataifa kukwepa kodi.
“Hii ni sawa na kusema Tanzania inapoteza Dola2 milioni (Sh3.1 bilioni) kila siku kwa uporaji huu,” alisema Zitto.
Zitto alisema Serikali lazima ichukue hatua mara moja kuhakikisha Tanzania inaingia makubaliano ya kupashana taarifa za kikodi.

Jaji Werema agoma kujibuAlipoulizwa juu ya Tanzania kutokusaini mikataba ya kimataifa ya kubadilishana taarifa za utoroshaji fedha na mambo au kodi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema hawezi kujibu suala hilo.
“Muulize huyo aliyekwambia kuwa Tanzania haijasaini mikataba ya kubadilishana taarifa za utoroshaji fedha na masuala ya kodi. Naomba uniache nifanye kazi zangu,” alijibu Jaji Werema kwa mkato na kukata simu.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment