Na Daniel Mbega
HAWAFI kwa Ukimwi wala malaria,
lakini Simba madume wametoweka katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Matokeo
yake wameacha wajane na yatima.
Hifadhi nzima kwa sasa ina Simba
dume mmoja tu, wawili wengine walikimbia baada ya ‘kuzidiwa’ na utoaji wa
huduma kwa Simba majike kwenye hifadhi hiyo.
Naam. Hayo ndiyo matokeo ya ujangili, janga la kitaifa ambalo kwa hakika linatishia uwepo wa rasilimali za asili kwa faida ya wachache wanaotaka kuchuma mahali wasipopanda.
Naam. Hayo ndiyo matokeo ya ujangili, janga la kitaifa ambalo kwa hakika linatishia uwepo wa rasilimali za asili kwa faida ya wachache wanaotaka kuchuma mahali wasipopanda.
Meneja wa Program ya Ujirani
Mwema wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Ahmed Mbugi, aliwaeleza
wanahabari katika semina iliyofanyika mwaka huu mjini Iringa kwamba, kipindi
cha miaka mitatu tu (2008 hadi 2010), jumla ya Simba waliouawa kijangili kwenye
Hifadhi ya Tarangire ni 62, huku madume wakiwa ndio wengi.
“Mwaka 2008 waliuawa Simba 15,
mwaka 2009 Simba waliouawa walikuwa 30 na mwaka 2010 jumla ya Simba 17 waliuawa
kwenye hifadhi hiyo. Majangili wanawinda zaidi madume, matokeo yake hifadhi
nzima ikabaki na Simba madume watatu tu, lakini kwa sasa wawili wamekimbia
hifadhini kwa sababu ya kuzidiwa na utoaji wa huduma kwa majike, amebaki dume
mmoja,” anasema Mbugi.
Hali hiyo, anasema,
“…Imesababisha kuwepo kwa wajane na yatima wengi kwa wanyama hao, hali
inayotishia ongezeko lao kwa miaka ijayo kwani dume mmoja naye anaweza kuchoka
na hata kufa. Pengine hata wadogo waliopo sasa, watakapokua hawataweza
kuzaliana kwa vile wanyama hao hawawezi kujamiiana kutoka familia moja.”
Lakini mauaji hayo hayakuwapata
Simba tu, kwani katika kipindi hicho pia watu 58 waliuawa na wanyama hao
wakali, “…wengi wakiwa katika harakati ya kuwawinda Simba kwenye makazi yao,”
anaongeza Mbugi.
Hali inaonekana kuwa mbaya zaidi
katika Hifadhi ya Manyara kuhusu uwepo wa Tembo ambapo katika kipindi cha mwaka
2007 hadi 2009, jumla Tembo 104 waliuawa kijangili.
“Binadamu waliojeruhiwa na Tembo
katika kipindi hicho walikuwa 63,”
anasema na kuongeza kwamba wengi kati ya watu hao ni wale wanaofanya shughuli
zao katika ushoroba wa Tembo.
Mbugi anasema hali hiyo
imeifanya TANAPA kuongeza juhudi katika mpango wa ujirani mwema kwa kuwashirikisha
wanajamii wanaoishi pembezoni mwa hifadhi zote huku shirika likisaidia miradi
mbalimbali ya kijamii.
“Miradi hii wanaibua wananchi
wenyewe, hatuwezi kwenda kuwajengea vyoo wakati mahitaji yao ni zahanati. Kwa
kufanya hivi tunataka kujenga ushirikiano wa karibu na kuwaelimisha wanajamii
kwamba maliasili hizi ni za Watanzania wote,” anasema.
TANAPA, kupitia program hiyo,
inachangia asilimia 70 kwenye miradi yote ya kijamii, wakati asilimia 30 ni
nguvukazi za wananchi husika na Mbugi anasema, “…Katika kipindi cha miaka 10,
yaani kuanzia 2003/2004 – 2012/2013, shirika hilo limetoa jumla ya Shs.
13,848,784,463.19 kusaidia miradi 1,003 ya jamii.
Katika mwaka wa fedha 2003/2004,
TANAPA ilifadhili miradi 94 iliyogharimu Shs. 805,821,034.24; mwaka 2004/2005
jumla ya Shs. 618,502,682.95 zilitumika katika miradi 60; mwaka 2005/06 jumla
ya Shs. 865,860,778
zilitumika katika miradi 65; mwaka 2006/07 jumla ya Shs. 1,212,619,300
zilitumika katika miradi 90; mwaka 2007/08 walitumia Shs. 3,447,154,353 katika
miradi 141; na mwaka 2008/09 walitumia Shs. 1,736,751,235 katika miradi 87.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2009/10 walifadhili miradi 98 iliyogharimu
Shs. 2,320,893,785; mwaka 2010/11 walitumia Shs. 536,136,868 kugharamia miradi
33; mwaka 2011/12 walitumia Shs. 744,244,212 kugharamia miradi 26 na mwaka
2012/13 wametumia Shs. 1,560,800,212 katika miradi 36 ya jamii.
Fedha hizo, anasema, zinatokana
na asiliamia ya mapato yatokanayo na hifadhi hizo, “…hasa baada ya kutoa
gharama za bajeti ya idara husika.”
Ufadhili huo wa TANAPA, anasema
Mbugi, umesaidia kupunguza migogoro baina ya hifadhi na wananchi na pia
umepromoti uhifadhi wa mazingira huku mpango ukisaidia kuibua ajira kwa
kusaidia makundi mbalimbali ya jamii.
Mpango wa Ujirani Mwema, awali
ukijulikana zaidi kama Huduma za Uhifadhi kwa Jamii (CCS) ulianzishwa mwaka
1985 kufuatia mkutano uliofanyika Seronera ambao ulikuwa na madhumuni ya
kujadili masuala ya Mpango wa Ikolojia katika Hifadhi ya Serengeti.
Katika mkutano huo ilielezwa
kwamba, wanyama wengi walikuwa wanatoweka kwa sababu ya uwindaji haramu ambapo
ilibainishwa kwamba Nyati walikuwa wamepungua kutoka 70,000 hadi 40,000 katika
hifadhi hiyo.
“Tembo walikuwa wamepungua
kutoka 2,500 hadi 500 wakati Faru walipungua kutoka 1,000 hadi 20 tu,” anasema
na kuongeza kwamba hali hiyo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ujangili
uliofanywa na wananchi wa maeneo yanayozunguka hifadhi kwa matumizi ya nyumbani
na biashara.
Anaongeza kwamba, malengo ya
program hiyo ni kuongeza uhusiano mwema kati ya hifadhi na jamii na kuhakikisha
maslahi ya TANAPA yanahubiriwa katika ngazi zote kwa kutoa taarifa katika
vijiji husika.
Mpaka sasa TANAPA inasimamia
hifadhi 15 ambazo ni Arusha, Gombe, Katavi, Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Lake
Manyara, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Rubondo, Saadani, Serengeti, Tarangire, na
Udzungwa.
Hifadhi zote hizo zinazungukwa
na jumla ya mikoa 28, wilaya 52 na vijiji 536 huku hifadhi za Kilimanjaro na
Serengeti zikizungukwa na vijiji 88 kila moja.
Makala haya yamehaririwa, lakini yalichapishwa kwa
mara ya kwanza katika magazeti ya TANZANIA DAIMA na DARAJA LETU.
No comments:
Post a Comment