ILIKUWA siku
ya Alhamisi, Machi 23, 1995, wakati umma wa Watanzania ulipopata pigo kubwa kufuatia kifo cha
'Jabali la Muziki nchini Tanzania', Marijani Rajabu, au 'Bulldozzer' kama
alivyokuwa akiitwa na wanamuziki wenzake kwenye bendi ya Dar International
'wana-Super Bomboka'.
Halikuwa pigo la Watanzania tu, bali hata Wafrika kwani alitunga nyimbo nyingi, ukiwemo wa 'Kumekucha' ambao ulikuwa ukiwahimiza watu kuacha shuka na kwenda kazi, pamoja na nyingine nyingi.
Halikuwa pigo la Watanzania tu, bali hata Wafrika kwani alitunga nyimbo nyingi, ukiwemo wa 'Kumekucha' ambao ulikuwa ukiwahimiza watu kuacha shuka na kwenda kazi, pamoja na nyingine nyingi.
Marijani na mapenzi, ndoa:
Kwa
ujumla Marijani alikuwa akijua nini alichokuwa anakifanya. Alipozungumzia
mapenzi au ndoa alikuwa kama anajielezea mwenyewe yanayomsibu, na kwa kweli
nyimbo hizo zilisikitisha, kuhuzunisha na pia kufurahisha.
Nyimbo
kama Mama Watoto na Ndoa ya Mateso zilimuonyesha Marijani
kama mtu wa familia aliyekuwa akikabiliwa na matatizo mbalimbali, na kwa kiasi
kikubwa akaweza kuiteka jamii na baadhi ya wanajamii waliokuwa na matatizo kama
hayo kwenye ndoa zao walifanikiwa kujirekebisha.
Alipokuwa
akiimba nyimbo zenye mchanganyiko wa mapenzi na huzuni, Marijani angeweza
kukufanya ulie bila kutaka. Nyimbo kama Salama
na Zuwena, alioupiga mara tu baada ya
kujiunga na Dar International akiwa na akina Abdallah Mensah, ni mfano
mmojawapo wa tungo za aina hiyo.
Katika
wimbo wa Salama, sauti ya Marijani
inayoonyesha masikitiko ya kukosa 'kitu moyo unapenda' inasikika zaidi hasa
pale anaposema:
"Nikilala naota sura yako,
Nikitembea nasikia waniita,
Nageuka sikuoni Salama mama.
Wapi Salama,
Salama nakuomba, Salama nakuita...."
Na hata
wanamuziki wenzake wanapojaribu kumsihi anyamaze kwa kuahidi kwamba apoe tu
Salama atakuja, bado Marijani, akiwa katika hali ya kukata tamaa, anasikika
zaidi katika wimbo huo akilalama:
"...Poa, siwezi poa,
Mpaka nimuone Salama,
Na kula, siwezi kula,
Mpaka nimuone Salama!!..."
Katika
nyimbo za Zuwena na Sikitiko, Marijani alidhihirisha wazi
kuwa ni mwanamuziki aliyejua kuziteka nyoyo za hadhira yake na uwezo mkubwa wa
kufikisha ujumbe kwa namna inayostahili.
Kama
alivyosikika katika wimbo wa Zuwena,
Marijani anasema kuwa, alipokuwa nyumbani kwake asubuhi wakati jua ndio kwanza
linachomoza, alisikia taarifa za ajali ya kutisha iliyokuwa imetokea kwenye
daraja la Sealander jijini Dar es Salaam. Je, alifanyaje?
"...Nilitoka bila kujitambua,
Mikono kichwani huku ninalia...
Mbio kwenda hospitali,
Kwenda kumuona, mpenzi Zuwena,
Sijui kama yuko hai,
Ama Zuwena amekwisha kufa,
Maringo na mikogo yangu
Siku hiyo vyote vilikwisha...".
Marijani
ambaye alilenga zaidi kufikisha ujumbe wake jinsi alivyokuwa anampenda Zuwena
kwa njia inayotia simanzi zaidi, anazidi kueleza zaidi sababu zilizokuwa
zikimfanya kumpenda kimwana huyo.
"...Zuwena, ningempata wapi,
Zuwena mwingine sawa na yeye,
Mtoto aliyeumbika, mwenye tabia za kupendeza,
Zuwena, Zuwena kweli nampenda x2
...Moyo ulianza kutulia
Kukuta Zuwena angali mzima,
Ingawa ana majeraha mengi
Haidhuru kuwa namuona,
Zuwena, Zuwena, Zuwena mama,
Zuwena bibi ee, kweli nampenda.
...Sijui ningefanya nini
Kama Zuwena angenitoweka,
Tumeishi kwa muda mrefu
Wote wawili tumezoeana,
Zuwena, Zuwena, Zuwena bibi kweli
nampenda..."
Mbali na
sauti nzito yenye simanzi na inayomfanya kila ausikiaye wimbo huo kuvutiwa nao,
upigaji wa ala katika wimbo huo na hasa kinanda vinazidi kuufanya muziki huo
upendwe zaidi.
Marijani
pamoja na kuonekana 'fundi' mzuri katika uimbaji wa nyimbo za mapenzi, alikuwa
hodari wa kuwasakama akina mama waliokuwa wakishindwa kujitunza na kujijua kuwa
walikuwa wanawake waliotakiwa kuonyesha kila aina ya adabu na heshima. Wimbo wa
Mayasa ingawa ulitungwa zaidi ya
miaka 20 iliyopita lakini ni dhahiri unaonekana zaidi kuwafaa kwa wakati huu
akina dada wengi ambao wameonakana kujikwatua kupita kiasi!
Marijani na jamii:
Mwanamuziki
huyo alifahamu fika kuikosoa jamii kwa staili ambayo ilimfanya kila mwanajamii
kujijua yuko kwenye kundi gani. Aliweza kuwasema wale wenye tabia ya kutaka
kuvunja ndoa za watu, hususan wanawake, ambao utakuwa wanawapenda waume za watu
kwa lengo la ama kuwakomoa wanawake wenzao au kuwakomoa wanaume wenyewe.
Hayo
aliyaeleza bayana katika wimbo wa Mwanameka,
kibao kinachoendelea kutamba mpaka sasa kikiwa kimeingizwa kwenye mashule ya
sekondari na Wizara ya Elimu kikitumika katika fasihi simulizi, ambapo
wanafunzi wamekuwa wakikumbana na maswali kwenye mitihani ya taifa hasa ya
kidato cha nne tangu mwaka 1992.
Baadhi ya
maneno yaliyoko kwenye kibao hicho ni haya: "Mwanameka
eeeh, Mwanameka jirani yangu...uliposikia eeeh, kwamba Mussa ameoa, kaoa mke wa
ndoa...ukabadilisha njia eeeh, ukienda sokoni kwa Mussa, naye Mussa macho
yakaona, kakutamkia neno la mapenzi...penzi nalo eeeh, penzi nalo halina siri,
na siri si ya watu wawili, mkewe Mussa agundua eeeh, hakupikiki wala hakuliki,
akaanza kudai talaka, Mussa naye akatoa talaka..."
Yapo
maneno mengi sana aliyoyasema katika wimbo huu ambayo yana maana kubwa kwa
jamii nzima, hali ambayo inawafanya hata wale wanawake wenye tabia kama hiyo,
pamoja na wanaume wenye kupenda kuwadanganya wake za watu, waache tabia hizo na
kushika mwenendo mpya wa maisha katika jamii.
Aidha,
nyimbo zake nyingi zilikuwa zikihusu matukio ya kweli kabisa; kwa mfano wimbo
wa 'Masudi amekuwa jambazi'. Wimbo
huu uliopendwa sana katika miaka ya 1980 ulikuwa ni tukio la kweli lililomkuta
kijana mmoja Masudi aliyekuwa akiishi Kigogo Luhanga, ambaye alikuwa hatari
kweli kweli kwa kukwapua vitambaa vya akina, kofia na fedha...
Inasemekana
baada ya kuimbwa na Marijani, Masudi aliacha ukwapukwapu na kuamua kutumia
nguvu zake kusukuma mkokoteni, kwani mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe!
Wimbo wa 'Kumekucha' ulikuwa unatumika Redio
Tanzania kuwahamasisha watu asubuhi kuacha shuka zao na kwenda kazini.
Aliwaasa
watoto wa shule, kama alivyofanya katika wimbo wa 'Roza nenda shule' na
'Unakwenda wapi mwana', akina mama kama alivyofanya katika nyimbo zilizotajwa
hapo juu na hata wanaume walevi kama alivyofanya katika wimbo wa 'Pombe siyo
chai'.
Aliimba
kuhusu wanadamu walivyogeuka kuwa wadanganyifu na kukosekana kwa imani duniani,
hakuna uaminifu, watu wanadhulumiana, ndugu wanagombea urithi wakati yatima
wanahangaika, na mengine mengi. Ni katika kibao cha 'Dunia Imani Imekwisha.' Anasema:
"Aeeh aeeh walimwengu x2
Walimwengu fungueni masikio msikie,
Mazingira ya dunia yanatuhusu wenyewe,
Tujihadhari na wanadamu tunaoishi nao hatari
eeeh.
Mwanadamu hana wema usimwamini,
Hana hizo fadhila wala shukrani,
Tenda wema kwake fadhila yake punda mateke..
Usimpe siri yako rafiki hata nduguyo,
Kwani kikulacho ki nguoni mwako,
Utajikuta pabaya halafu ushangae eeeh eeeh.
Kiitikio:
Dunia sasa imani imekwisha,
Nyoyo za watu zimebadilika,
Wala hakuna uaminifu tena,
Si wanawake, si wanaume,
Si kwa wazee, wala si vijana,
Wote tunakwenda mzabwa mzabwa,
Kwenye watu kumi binadamu mmoja.
Hata walaghai ndio mmezidi,
Watu wamezidi kudhulumiana,
Kila mahali unafiki na dhuluma,
Utu umekwisha umebakia unyama.
Bwana fulani amefariki,
Kafa lakini kaacha watoto,
Ndugu waliobaki akili zimewaruka,
Mawazo yote ni kwenye mali,
Wanataka uana sababu ya nyumba,
Wanasahau hata watoto,
Watoto wenyewe bado wadogo,
Wanadhulumu hata watoto yatima.
Fundi cherehani kaletewa vitambaa,
Mwenyewe kataka suruali tatu,
Fundi kajibu hewala vimefika,
Kumbe mfukoni fundi kachacha,
Vitambaa kauza na pesa katia ndani,
Wiki iliyofuata mwenyewe kafika,
Anauliza wapi suruali zangu,
Fundi alia yoo yoo,
Anauliza fundi walia nini,
Ati anajibu leo nimeibiwa.
Ndugu kauzeni kaachiwa duka,
Mwenyewe kaenda Kilwa Kivinje,
Kauzeni kasema, "Sasa watanijua!!
Hasa yule Kabuta atanitambua,"
Kapita Kabuta akamhonga unga,
Karudi jioni kapewa sukari,
Wiki mbili duka limefilisika,
Anajiuliza nitajibu nini,
Kila akiwaza hakuna la kufanya,
Akaiba mapesa na vitu vyote akapotea."
Lakini
kama alivyowahi kuimba yeye mwenyewe katika wimbo wake wa 'Rufaa ya Kifo', Mwenyezi Mungu akaamua kumuita akiwa bado mbichi.
Marijani anasema katika wimbo huo: "...Lakini
Mola eeeh, kazi yake haina makosa, tena hairekebishwi na binadamu
yoyote..."
Achukuliwa na Simba:
Pengine
linaweza likawa jambo la kushangaza. Lakini ndio ukweli wenyewe. Kwamba, mbali
ya kutunga, kupiga na kuimba muziki, lakini pia Marijani alikuwa mwanasoka
mzuri sana enzi zake akichezea nafasi ya golikipa.
Alikuwa
akiutumia muda wake wa ziada kwenda kufanya mazoezi pale kwenye uwanja wa
Karume, zamani ukijulikana kama Uwanja wa Ilala, si mbali sana kutoka pale mtaa
wa Somali alikokuwa akiishi.
Kutokana
na uhodari wake aliouonyesha akiwa na timu za mitaani, Marijani alijikuta
akichukuliwa na viongozi wa Simba ili akaidakie timu hiyo. Hiyo ilikuwa katika
miaka ya 1970.
"Kwa
kweli fani yetu ilipata pigo kubwa kipindi hicho na tulidhani kwamba
tungempoteza mwanamuziki muhimu sana hasa kama angeamua kukubali kuichezea
Simba, ambayo alikuwa na mapenzi nayo makubwa. Hata hivyo, aliamua kuachana na
wazo la kuichezea timu hiyo na kurejea kwenye jukwaa la muziki," alipata
unisimulia, Abdallah Mensah (sasa marehemu), rafikiye wa karibu enzi hizo.
Mensah alisema
kuwa, mbali ya kusoma na marehemu Marijani katika shule ya msingi Kisarawe na
baadaye shule ya sekondari Tambaza, lakini pia aliimba naye kwenye bendi ya
Safari Trippers na baadaye wakaenda kuanzisha Dar International.
Kuzaliwa:
Marijani
alizaliwa mwaka 1954 jijini Dar es Salaam na kulelewa katika mazingira ya
kidini ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kusomeshwa Qur'an kwenye Madrasa, ambako
pia alikuwa mwimbaji wa kaswida na mpiga dufu.
Alipofikisha
umri wa miaka 18 tu akajitokeza kuwa gumzo katika midomo mingi ya Watanzania
katika uimbaji. Tangu alipokuwa na bendi ya STC, Marijani, ambaye kwa wakati
huo pia alikuwa bado mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Tambaza, alionyesha
wazi kuwa alizaliwa kwa ajili ya kuburudisha, kufundisha na kukemea yale yote
ambayo yalikuwa hayampendezi Mwenyezi Mungu na wateule wake.
Wimbo wa Ewe ndugu yangu na Shida alizotunga na kuimba wakati akiwa na bendi ya STC mwaka 1971
ni ushahidi tosha wa kuonyesha kuwa Marijani tangu awali aliamua kutumia kipaji
chake kwa ajili ya kuonya dhid ya matendo mabaya.
Kipaji
cha Marijani kilichanua zaidi wakati alipochukuliwa na Saleh Amour aliyekuwa
Mkurugenzi wa Bendi ya Safari Trippers pia ya jijini Dar es Salaam mwaka 1973,
ambako aliibuka na nyimbo za Matilda,
Hanifa, Salama, na Mwana mpotevu.
Mwaka
1978 alihama bendi hiyo pamoja na wanamuziki kadhaa na wakaanzisha bendi ya Dar
International na kibao chake cha kwanza kilikuwa Zuwena kilichofuatiwa na nyinginezo nyingi.
Bendi
hiyo 'ilisinzia' na kupotea katika miaka ya 1980, lakini mwaka 1990 Jabali la
Muziki liliibuka likiwa na vyombo vya kisasa na kuja na bendi nyingine
iliyoitwa Afri Culture ikiwa na mtindo wa 'Mahepe ngoma ya wajanja'. Bendi hiyo
ilikaa miaka takribani mitatu halafu ikapotea kabisa.
Mkewe
Amina binti Ibrahim alifariki mwaka 1992 na kumwachia watoto watatu; Aisha,
Wahida na Rajabu. Mtoto wake mwingine Hanifa alifariki.
Kama
alivyowahi kuimba mwenyewe katika wimbo wake wa Rufaa ya Kifo, Mwenyezi Mungu aliitwaa roho yake Alhamisi, Machi
23,1995 baada ya kuugua kwa zaidi ya mwezi mmoja. Alikuwa amelazwa kwenye
Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
Siku hizi
bendi nyingi zimekuwa zikipiga baadhi ya nyimbo zake katika maonyesho yao na
wale wanaotumia mitindo ya 'Chuna Buzi', yaani wenye vinanda wanaopiga kwenye
sherehe. Hii ni kuonyesha kwamba, nyimbo hizo bado ni 'peremende' kwa
mashabiki.
'Mwenyezi
Mungu ailaze roho yake mahali pema. AMINA'.
No comments:
Post a Comment