Kikosi cha Simba cha mwaka 1977 kilichopeleka maafa Jangwani.
Na Daniel Mbega
KATIKA
mchezo wa soka kushinda ama kushindwa ni mambo ya kawaida, lakini vipo vipigo
ambavyo timu hupata kiasi cha kujiuliza mara kumi kumi, kulikoni? Kama kuna
kipigo ambacho kitabaki katika kumbukumbu za Yanga milele na milele ni kile cha
mwaka 1977 cha magoli 6-0 kutoka kwa watani wake wa jadi, Simba, kwenye mchezo
wa Ligi ya Taifa.
Kwa
waliokuwepo na waliopata simulizi baadaye, Jumanne ya Julai 19, 1977 ilikuwa
siku yenye majonzi makubwa kwa mashabiki wa Yanga na furaha kubwa kwa wale wa
Simba, ambayo kwa ushindi huo, mbali na kujihakikishia ubingwa wa Ligi ya Taifa
kwa kuwa ilibakiza mechi moja tu dhidi ya Navy (sasa KMKM) ya Zanzibar
iliyokuwa ya kukamilisha ratiba, pia ilikuwa imefanikiwa baada ya miaka tisa
kulipa kisasi cha kufungwa magoli 5-0 na Yanga mwaka 1968.
Kati ya watu waliojihisi wenye furaha kupindukia walikuwa kocha wa Simba, Dimitier Samsarov wa Bulgaria ambaye alikuwa na muda mchache tu tokea akabidhiwe timu na nahodha Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ ambaye siku hiyo ‘alicheka’ na nyavu mara tatu.
Kati ya watu waliojihisi wenye furaha kupindukia walikuwa kocha wa Simba, Dimitier Samsarov wa Bulgaria ambaye alikuwa na muda mchache tu tokea akabidhiwe timu na nahodha Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ ambaye siku hiyo ‘alicheka’ na nyavu mara tatu.
Ilikuwa
hadithi ya kifo cha nyani miti yote huteleza, kwani pamoja na kukuru kakara
zote za Yanga, ikiwemo kubadilisha wachezaji wawili dhidi ya mmoja wa Simba,
ambaye alibadilishwa kufuatia mwenzake kuumia (Martin Kikwa ndiye aliyeumia na
kumpisha Abbas Dilunga), mambo yalichacha na kuvunda kwa vijana wa Jangwani
waliokuwa wakipokea mashambulizi mfululizo na kubaki wakitumia ujanja wa mtego
wa kuotea (offside-trick), ambao hata
hivyo, haukusaidia kitu.
Mwaka huo
Yanga ilikuwa haijatulia baada ya mgogoro mkubwa wa mwaka 1976 uliopelekea
karibu wachezaji 20 nyota kufukuzwa kwa madai ya kutokuwa wazalendo na
kusababisha Yanga kupoteza taji lake la ubingwa wa soka Afrika Mashariki na
Kati mjini Mombasa, Kenya mwaka huo. Wachezaji hao ni Gibson Sembuli, Leodgar
Tenga, Sunday Manara, Boi Idd ‘Wickens’, Ally Yusuf, na wengineo ambao
walikwenda kuunda timu ya Nyota Afrika ya Morogoro kabla ya kuanzisha Pan
African ya Dar es Salaam.
Katika
mchezo huo, Simba walifanikiwa kujipatia magoli matatu katika kipindi cha
kwanza licha ya kucheza huku wakipingana na upepo katika kipindi hicho.
Sentahafu wa Yanga, Selemani Jongo, ndiye aliyeonekana kuwa kikwazo pekee kwa
Simba na hata yeye alilazimika ‘kukubali yaishe’ baada ya washambuliaji wajanja
wa Simba kumshitukia, hivyo kumuandama kama nyuki.
Katika
dakika ya pili tu mashabiki, ambao walianza kuingia uwanjani tangu saa 6.00
mchana, walishuhudia Martin Kikwa wa Simba akitolewa nje baada ya kugongana na
Boniface Makomole aliyekuwa beki wa kulia wa Yanga na nafasi yake kuchukuliwa
na Abbas Dilunga.
Baada ya
kosa kosa nyingi kwenye goli la Yanga na takribani moja tu kwenye goli la Simba
pale juhudi za mshambuliaji wa Yanga, Yanga Fadhil Bwanga zilipozimwa na
golikipa wa Simba Omari Mahadhi bin Jabir, hatimaye karamu ya magoli ilianza
kwa Simba kwenye dakika ya 10. Goli hilo la kwanza lilianzia katikati ya uwanja
ambapo Aluu Ally wa Simba aliwakata chenga beki Charles Mwanga na kiungo Sam
Kampambe na kumpasia winga wa kulia, Willy Mwaijibe, ambaye naye alitoa pasi
safi kwa Jumanne Hassan ‘Masimenti’. Beki Selemani Jongo wa Yanga alitoka
kuucheza mpira huo lakini Jumanne alimuwahi na kumuunganishia Abdallah Kibadeni
aliyekimbia na mpira hatua chache kabla ya kuujaza wavuni huku kipa Bernard
Madale akiwa hana la kufanya.
Yanga
ilikukuruka baada ya goli hilo na kukaribia kusawazisha kwenye dakika ya 18
lakini shuti la nambari 8 wao, Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, lililokuwa
limeshawanyamazisha mashabiki wa Simba, lilipaa juu ya goli.
Hata hivyo,
Yanga ilikuwa kama imejichongea, kwani golikiki iliyopigwa kunako dakika ya 20
kufuatia kosa kosa hiyo ndiyo iliyozaa goli la pili la Simba baada ya gonga za
hapa na pale kumfikia Willy Mwaijibe aliyefumua shuti la chini chini ambalo
katika juhudi za kuokoa, Selemani Saidi Sanga wa Yanga alijikuta akiusindikiza
mpira wavuni. Zikiwa zimesalia dakika chache kuwa mapumziko, kona ya Willy
Mwaijibe ilimkuta Kibadeni katika nafasi nzuri na akaujaza mpira wavuni na
kuifanya Simba imalize kipindi cha kwanza ikiongoza kwa magoli 3-0. Hiyo
ilikuwa dakika ya 42.
Katika
kipindi cha pili, Yanga ilijitahidi kutafuta magoli ya kusawazisha lakini baada
ya dakika 15 kupita wakiwa bado hawajafanikiwa kuingia kwenye eneo la goli la
Simba wakiishia tu nje ya eneo la penati, kibao kiliwageukia kwa Aluu
kumtangulizia pasi Jumanne aliyemzidi maarifa Jongo na kusalimiana na kipa
Madale na kupachika goli la nne, na dakika 13 baadaye Aluu Ally alimpasia tena
Jumanne ambaye kwa mara nyingine alimpita Jongo na kufunga goli la tano.
Yanga
ilikosa kona kadhaa ilizopata. Katika dakika ya 89 Abbas Dilunga alichomoka
kwenye wingi ya kushoto na kumtolea ‘chumba’ Kibadeni aliyekamilisha karamu ya
magoli na kuwaacha mashabiki wa Simba wakilia kwa furaha huku wale wa Yanga
wakitokwa na machozi ya simanzi. Kwa kweli kilikuwa kipigo cha kihistoria.
Mechi
hiyo iliingiza jumla ya shilingi 293,664 ambazo kwa wakati huo ndiyo yalikuwa
mapato makubwa zaidi kupatikana katika mechi ya ligi. Kabla ya hapo, pambano la
timu hizo mwaka 1974 kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ndilo lilikuwa
likiongoza kwa mapato ambapo lilikuwa limeingiza shilingi 150,000.
Katika
mechi hiyo, timu zilipangwa hivi:
SIMBA: Omari Mahadhi bin Jabir, Shaaban Baraza,
Mohammed Kajole, Aloo Mwitu, Mohammed Bakari ‘Tall’, Athumani Juma, Willy
Mwaijibe, Aluu Ally, Jumanne Hassan ‘Masimenti’, Abdallah Kibadeni (nahodha) na
Martin Kikwa/Abbas Dilunga. Kocha: Dimiter Samsarov (Bulgaria)
YANGA: Bernard Madale, Boniface Makomole, Selemani
Saidi Sanga, Charles Mwanga/Fidelis, Selemani Jongo, Sam Kampambe, Ayub
Shaban/Mrisho Caraby, Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, Mwinda Ramadhani ‘Maajabu’
(nahodha), Yanga Fadhil Bwanga na Shaaban Katwila.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye muswada wa kitabu cha 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' cha mwandishi Daniel Mbega, ambacho kiko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com
No comments:
Post a Comment