Mkuu wa
Kitengo cha Mbinu za Ujenzi toka Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na
Vifaa vya Ujenzi(UNHBRA) Mhandisi Amri Juma akieleza kwa waandishi wa
habari(hawapo pichani) namna wakala hao unavyosaidia kutoa elimu ya ujenzi wa
nyumba bora,wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya
Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Habari na Masoko toka Wakala hao Bw. Frimin Lyakurwa. Picha na Fatma
Salum-MAELEZO
1.0 UTANGULIZI
NHBRA ni Wakala wa Taifa wa
Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (National Housing and Building
Research Agency – NHBRA) ambao ulianzishwa kwa Sheria ya Wakala za Serikali
Namba 30 ya Mwaka 1997 na kuanza shughuli zake rasmi 01 Septemba mwaka 2001. Wakala huu uko chini ya Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
NHBRU ilikuwa ni Kituo cha
Utafiti wa Vifaa vya Ujenzi (Building Research Unit) ndani ya (Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi).
NHBRA inafanya kazi za utafiti pamoja na ushauri na ukandarasi katika
kuwapatia wananchi wa Tanzania wenye kipato cha chini nyumba na makazi bora kwa
gharama nafuu na ya kudumu ili kutimiza malengo ya MKUKUTA pamoja na malengo ya
Maendeleo ya Mlenia (MDGs) Ambayo yanasimamiwa na UNHABITAT.
1.1 Dira
Kuwa kituo cha ufanisi uliotukuka katika nyumba za gharama nafuu na
teknolojia ya uboreshaji makazi ya binadamu ifikapo Mwaka 2025.
1.2 Dhima
Kuwapatia watanzania huduma bora za vifaa na teknolojia ya ujenzi wa
Nyumba Bora za Gharama nafuu kwa kutumia ubunifu ili kukidhi mahitaji ya wateja
hivyo kuinua hali ya maisha kwa kila mtanzania.
2.0
JUKUMU KUU LA NHBRA
Kutafiti, Kukuza, Kushauri na Kushawishi Ujenzi wa NYUMBA BORA za Kudumu
na za GHARAMA nafuu ili kuinua na kuboresha viwango vya nyumba pamoja na kuongeza
ubora wa maisha ya wananchi vijijini na mijini. Mabadiliko hayo yamefanyika ili
kuongeza ufanisi katika kuhudumia wateja.
3.0 MAJUKUMU YA WAKALA
Majukumu ya NHBRA kama Wakala wa
serikali ni haya yafuatayo:
·
Kutafiti, kukuza, kushauri na kushawishi juu ya
ujenzi wa nyumba za kudumu na za gharama nafuu ili kuinua na kuboresha viwango
vya nyumba ili kuongeza ubora wa maisha ya wananchi vijijini na mijini kwa
ujumla.
·
Kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zake pamoja
na habari za kitaalam kuhusu makazi vinapatikana kwa wananchi kwa wakati.
·
Kukuza na kuendeleza matumizi ya vifaa vya
ujenzi vipatikanavyo katika maeneo ya ujenzi pamoja na teknolojia ya nyenzo za
ujenzi wa nyumba bora zinazolinda mazingira.
·
Kuongeza mbinu za utaalam wa ujenzi wa nyumba
bora za gharama nafuu.
·
Kutoa huduma bora za ushauri kuhusu ujenzi wa
nyumba.
4.0 MAANA YA NYUMBA
BORA
Tafsiri kuhusu nyumba bora ni
nyingi na wakati mwingine hutatanisha. Hata hivyo wataalamu wengi wanakubaliana
kuwa ufafanuzi sahihi wa nyumba bora sharti ujumuishe sifa zifuatazo:
- Imara na ya kudumu
Nyumba bora haina budi kuwa imara
na ya kudumu kutegemeana na uwezo wa kifedha. Uimara wa nyumba hutegemea sana vifaa vilivyotumika
kujengea na pia uelewa wa ufundi uliotumika.
Ufundi duni unaweza kuifanya
nyumba iliyojengwa kwa vifaa madhubuti na ghali isiwe imara. Ni vizuri
kuhakikisha vinatumika vifaa bora vya ujenzi kwa kujenga nyumba bora.
Nyumba imara hudumu kwa muda
mrefu zaidi. Faida za nyumba bora, imara na ya kudumu ni:
i)
Huokoa fedha na muda kwa kutoifanyia matengenezo na
ukarabati wa mara kwa mara, (Nyumba yoyote ikichakaa kupita kiasi ni lazima
kujenga nyingine).
ii)
Huhimili misukosuko mingi na kuwafanya wakazi wake wawe
na usalama zaidi.
- Gharama nafuu
Nyumba bora na ya gharama nafuu
ni ile mtu anayoweza kuijenga au kununua kulingana na kipato chake. Iwapo
gharama zitakuwa kubwa mno ni wazi kuwa dhana ya nyumba za gharama nafuu
haitakuwepo. Ni vyema basi jitihada zifanyike ili kupunguza gharama zote zisizo
za lazima kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika sehemu ya ujenzi pamoja na
teknolojia yake.
- Kukidhi mahitaji
Nyumba bora lazima iwe na uwezo
wa kukidhi mahitaji na shughuli za kila siku katika maisha ya binadamu. Nyumba
ni mahala pa kulala, kupikia, kula chakula, kupumzika, kustarehe na shughuli
nyingine kama kusoma, kucheza, kuabudu, kuzaa, na kulea watoto. Nyumba hutumika
kwa kuhifadhi vitu, kulinda siri na kutoa faragha inayotakiwa. Kutokana na
hayo, ni muhimu kuwa na picha kamili ya nyumba unayotaka kujenga kabla ya kuanza ujenzi kwa kuzingatia
shughuli mbali mbali zitakazofanyika ndani yake.
- Masharti ya kanuni za afya
Afya bora ni sharti muhimu kwa
maisha ya binadamu. Nyumba mbovu au ujenzi mbovu wa nyumba unaweza kuathiri
maisha na afya ya watu wanaoitumia. Kwa mfano nyumba ambazo sakafu, kuta, na
paa zake zinakuwa na unyevunyevu kila wakati zinaweza kuhatarisha afya ya
watumiaji. Ni vizuri nyumba iwe na madirisha ya kuingiza na kutoa hewa pamoja
na mwanga wa kutosha. Nyumba ambazo hali ya hewa ya ndani aidha ni baridi au
joto sana nazo
pia huweza kuathiri afya za watumiaji.
Pamoja na hayo yote nyumba bora
haina budi iwe na choo safi.
Mara nyingi watu husahau kuwa choo ni sehemu ya nyumba. Nyumba kama haina choo
inakuwa haijakamilika na hivyo kutostahili kuitwa nyumba bora. Ni muhimu sana
kuwepo choo ndani au nje ya nyumba kutegemeana na mchoro wa nyumba na uwezo wa
mtu. Hili linatakiwa lizingatiwe tangu awali ili kukidhi masharti muhimu ya
afya.
- Kuheshimu mila na desturi
Nyumba bora lazima itilie maanani
mfumo wa maisha ya watu, yaani ikidhi mila na desturi za watumiaji. Kwa mfano
nyumba za watu wa maeneo ya pwani hazina budi ziwe na baraza ya mbele kwa ajili
ya wanaume kupumzika na kuongea, na sehemu ya uani kwa ajili ya akina mama
kufanyia shughuli zao. Pia kuna makabila mengine hayashirikiani vyoo na wakwe
au watoto n.k, Hayo lazima yazingatiwe katika usanifu na ujenzi wa nyumba.
- Hali ya kuvutia, kupendeza na kumpa raha mtumiaji
Nyumba bora lazima iwe ya
kupendeza kwa mtumiaji, na hata watu wengine wanaoiona. Hii itatokana na
kusanifiwa, kujengwa vizuri na kutunzwa vizuri. Ni vema kutumia ushauri wa
wataalam wa usanifu majengo, wahandisi na hata wakadiriaji gharama za ujenzi.
Wataalam hawa na wengineo wapo NHBRA, taasisi za ujenzi na makampuni mengine.
- Rasirimali na kitega uchumi
Nyumba bora ni kitu cha thamani
kwa kuwa inaweza kuwa kitega uchumi. Hii ni pale ambapo mmiliki anaweza
kupangisha na kupata pesa kutokana na kodi inayolipwa na mpangaji, au mwenye
nyumba kuishi kwenye nyumba yake na kuepuka gharama za kulipa kodi kama
angekuwa amepanga nyumba kwa mtu mwingine. Pia nyumba inaweza kutumika kama rehani
unapotaka kuchukua mkopo kutoka katika benki, hata kuuzwa kwa ajili ya mahitaji
ya haraka.
5.0 VIFAA VYA UJENZI VYENYE GHARAMA NAFUU
Katika ujenzi wa nyumba, gharama ya vifaa huchukua takribani asilimia 70
ya gharama za nyumba. Hii ni pamoja na kuwa vifaa vya ujenzi ni vizito na
usafirishaji wake mpaka sehemu za ujenzi ni ghali. Tafiti zilizopo zimeonyesha
kuwa katika baadhi ya maeneo tunayojenga tunaweza kutumia malighafi zilizopo
eneo la ujenzi pamoja na utaalamu wa malighafi na hivyo kupunguza gharama za
usafiri wa vifaa na hatimaye kupunguza gharama za ujenzi.
Vifaa bora na vya kudumu ambavyo vinapatikana katika maeneo tunamoishi
ambavyo vyanzo vyake vimeshafanyiwa uchunguzi ili kuweza kuwa na utaratibu
mzuri wa ununuaji, usafirishaji, uhifadhi na utumiaji na pia utumiaji wa
teknolojia rahisi na sahihi kwa mpangilio mzuri wa utekelezaji wa shughuli zote
za ujenzi hupunguza gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa.
6.0 VIFAA BORA VYENYE GHARAMA NAFUU VILIVYOTAFITIWA NA NHBRA
Matofali ya kufungamana ya udongo-saruji:
Ni matofali yanayotengenezwa kwa kutumia udongo ambao huchanganywa na saruji
kwa kiasi kidogo ili kuuimarisha udongo, kisha kuyafyatua kwa kutumia mashine
maalum ili kupata umbo la kufungamana. Ni vizuri kutambua udongo wako na vipimo
vya saruji inayohitajika.
Vigae vya kuezekea: Vigae hivi hutengenezwa kwa kutumia
mchanganyiko wa mchanga, saruji na nyuzi za katani ambazo hukatwa kwa urefu wa
sentimita 2-3 kisha mchanganyiko huu huwekwa katika mashine ya kutengenezea
vigae ambayo huendeshwa kwa betri ya gari. Kwahiyo mashine hii inaweza kutumika
hata katika maeneo yasiyo na umeme hususani vijijini.
7.0 KAZI ZILIZOFANYIKA NHBRA
(i)
Kuvielekeza vituo vya uzalishaji na urekebishaji wa
mashine zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa vya Ujenzi vipatikanavyo hapa
nchini.
·
Mashine 81 za
kufungamana zilitengenezwa katika Kituo cha NHBRA kwa kushirikiana na MM
Foundry kwa kipindi husika.
(ii)
Kuendesha semina za uhamasishaji wa ujenzi wa nyumba
bora za gharama nafuu katika wilaya tatu.
·
Semina za uhamasishaji
wa ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu zilifanyika kwa viongozi wa Wilaya ya
Arusha Vijijini na kwa vijiji vya Engorora watu 23 na Likamba watu 27
·
Semina za
uhamasishaji zilifanyika mkoani Tabora, katika kata kumi (10) ambazo ni Isevya,
Ipuli, Mtendeni, Ng`ambo, Kanyenye, Chemchem, Cheyo, Kariakoo, Kiloleni na
Tambukareli
·
Pia Biharamulo
Mkoani Kagera kuzunguka mgodi wa Tulawaka.
·
Mafunzo kwa
vitendo yalifanyika Mkoa wa Tabora, wilaya ya Tabora Mjini
(iii)
Kuendesha mafunzo kwa vitendo kuhusu teknolojia rahisi
ya ujenzi wa nyumba katika wilaya tatu (3) moja kila wilaya.
·
Mafunzo kwa
vitendo yalifanyika kwa Mafundi Sanifu wanne (4) kutoka Mamlaka ya Uendelezaji
Mji (CDA) Dodoma.
- Mafunzo kwa vitendo yalifanyika Mkoa wa Lindi katika Wilaya ya Kilwa kwa wanakijiji 72 katika jumla ya vijiji sita (6) navyo ni Somangandumbo, Somangasimu, Mtyambuko, Miumbu, Pungutini na Kinjunbi.
- Kuzalisha matofali, vigae pamoja na mashine zake kwa wingi ofisini NHBRA ili wananchi waweze kupata huduma hizi toka NHBRA na hivyo kutengeneza ajira kwa vijana.
- Ujenzi wa nyumba za mfano hutumika vijana wa maeneo husika ili waendeleze teknolojia hii.
8. UBORA WA VIFAA VYA UJENZI
NHBRA inajitahidi kutoa elimu kwa
wananchi ili waweze kujua vifaa bora vipatikanavyo katika maeneo yao, pia
ambavyo vinaweza kuzalishwa katika maeneo wanamoishi wananchi kwa ubora
unaofaa. Hii itasaidia kupunguza matumizi ya vifaa visivyo na ubora au vyenye
ubora duni, pamoja na kuwezesha vikundi kujipatia ajira. Mojawapo ya kazi za
NHBRA ni kutoa mafunzo ya uzalishaji na matumizi bora ya vifaa vya ujenzi
vinavyopatikana karibu na maeneo ya ujenzi na bila kuathiri mazingira.
9. MIKAKATI YA KUJITANGAZA
Mikakati ya kujitangaza
inaendelea kufanyika kwa kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari kama
vile magazeti, redio, televisheni pamoja na kushiriki maonesho mbalimbali
yanayofanyika hapa nchini kwa nyakati tofauti.
Mpaka sasa kuna mikakati ya
kuunda na kuimarisha vikundi vya vijana wa kujitegemea watakaojishughulisha na
uzalishaji wa vifaa, mashine pamoja na ujenzi kuanzia ngazi ya kata. Hawa
watakuwa wawakilishi wa NHBRA katika maeneo yao. Mifano halisi ni vikundi vya
uzalishaji na ujenzi huko Pwani, Namtumbo-Songea, Somanga-Lindi, Manispaa ya
Tabora na Tulawaka-Biharamulo. Vikundi hivi vitaweza kutumiwa na yeyote katika
miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
10. MAFANIKIO YA NHBRA
- Ubunifu na utengenezaji wa matofali ya kufungamana ya udongo – saruji (Tanzanian type) na mashine zake.
- Vigae vya kuezekea nyumba vya mchanga – saruji na mashine zake.
- Tumejenga nyumba za mfano katika sehemu mbalimbali za Mkoa wa Dar es salaam.
- Ujenzi wa vyumba 72 vya biashara huko Ipogolo – Iringa.
- Ujenzi wa nyumba za kuishi wafanyakazi wa halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi, nyumba za kuishi polisi huko Singida, Songea na Ukonga – Dar es salaam.
- Ujenzi wa nyumba za watu binafsi katika sehemu mbalimbali.
- Kutoa semina za uhamasishaji na mafunzo kwa vitendo karibu mikoa yote ya Tanzania bara.
- Ujenzi wa nyumba za kuishi wafanyakazi wa halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
- Majarida mbalimbali ya kitaalam kuhusu tafiti zilizokwisha kamilika.
- Uanzishaji na ulezi wa vikundi vya vijana wajasiriamali vya kuzalisha vifaa vya ujenzi vilivyotafitiwa, na wa kujenga kwa kutumia vifaa hivyo huko Namtumbo-Songea, Tabora Manispaa, Tulawaka-Biharamulo, NHBRA –Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment