Kipa wa Simba, Athumani Mambosasa, akiunyaka mpira huku akitazamwa na Kitwana Manara 'Popat' wa Yanga (kushoto).
Kikosi cha Yanga cha mwaka 1973 kabla Dk. Victor Stanculescu (wa pili kushoto) hajaondoka. Anayeongea na wachezaji na meneja wa timu, Shiraz Sharrif. Wengine ni Hassan Gobbos, Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Sunday Manara, Elias Michael, Boi Idd 'Wickens', Selemani Said, Gibson Sembuli, Omar Kapera, Ally Yussuf, Abdulrahman Juma (nahodha).
Na Daniel Mbega
KWA wenye kumbukumbu nzuri
bila shaka kipigo cha Nigeria cha magoli 2-1 toka kwa Italia katika raundi ya
pili ya Kombe la Dunia huko Marekani mwaka 1994 kiliwarudisha mapema miaka ya
1970 pale Yanga ilipoichapa Simba magoli 2-1 kwenye fainali ya Ligi ya Taifa ya
Soka kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Nasema huenda kumbukumbu hiyo ikawa imejitokeza kufuatia kufanana kwa kiasi kikubwa kwa matokeo hayo, hasa muda, yaani ‘timing’, magoli hayo yalipopatikana.
Nasema huenda kumbukumbu hiyo ikawa imejitokeza kufuatia kufanana kwa kiasi kikubwa kwa matokeo hayo, hasa muda, yaani ‘timing’, magoli hayo yalipopatikana.
Katika mchezo wa Nigeria
na Italia Alhamisi ya Julai 14, 1994, Nigeria ilikuwa ikiongoza kwa goli moja
ililolipata mapema kunako dakika ya 26 hadi dakika ya 87 Roberto Baggio
alipoisawazishia Italia na kuufanya mchezo huo uingie kwenye muda wa nyongeza.
Kisha kwenye dakika ya 11 ya muda wa nyongeza, Baggio tena alifunga goli la
penati na kuiondoa Nigeria mashindanoni. Ndivyo ilivyokuwa kwenye mchezo wa
Simba na Yanga wa mwaka 1974.
Pengine watu watajiuliza
kwa nini Simba na Yanga zilipambana kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza badala
ya Karume au Taifa mjini Dar es Salaam zinakotoka timu hizo. Kwa kweli hili
lilikuwa pambano lao la kwanza la Ligi ya Taifa kufanyika nje ya Dar es Salaam.
Mashindano ya kutafuta
klabu bingwa nchini mwaka 1974 yalifanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza
tangu Julai 18 hadi Agosti 10, 1974. Timu maarufu zilikuwepo pamoja na nyingine
ngeni. Timu hizo maarufu zilikuwa Yanga na Simba za Dar es Salaam, Nyota ya
Mtwara, Mwadui ya Shinyanga na Jumuiya ya Arusha. Halafu ikatokea timu mpya
kabisa huko mkoani Dodoma iliyoitwa Ntomoko. Timu nyingine za mwaka huo
zilikuwa ni za kazini. Hakukuwepo na timu kutoka Zanzibar msimu huu.
Hata hivyo, upinzani
mkubwa kwenye ligi hiyo ulikuwa kati ya Simba na Yanga, watani wa jadi wa soka
nchini. Wakati huo Simba walikuwa mabingwa baada ya kuwafunga Lake Stars ya
Kigoma magoli 2-0 mwaka 1973 kama tulivyoona huko nyuma. Watu walikuwa
wanajiuliza nani angeibuka bingwa mwaka 1974 hasa ikizingatiwa kwamba, Yanga
ilifungwa na Simba goli 1-0 kwenye nusu fainali mwaka 1973.
Kwa matayarisho kabla ya
mashindano hayo, Simba walikwenda kuzuru Poland nao Yanga walikwenda Brazil,
ambako walikutana na Mfalme wa Soka Duniani, Edson Arantes do Nascimento
‘Pele’. Katika timu zote zilizokuwemo kwenye mashindano hayo hakuna hata moja
iliyokuwa na matayarisho makubwa kama Yanga na Simba.
Simba na Yanga
zilifanikiwa kuingia fainali baada ya kuzichabanga timu nyingine kwenye
michuano ya awali ya mtoano. Pambano hilo la mwisho na la kihistoria
lilifanyika Nyamagana Jumamosi Agosti 10, 1974.
Siku hiyo Uwanja wa
Nyamagana ulifurika watu isivyo kawaida. Mashabiki walitoka sehemu mbalimbali
za nchi - Arusha, Moshi, Tanga, Dodoma, Dar es Salaam, Tabora, Shinyanga,
Kigoma, Morogoro, Mara na Kagera. Hao ni licha ya wale waliotoka kwenye
vitongoji vya Mwanza. Ilipofika saa 10.30 jioni hapakuwa na nafasi ya kukaa mtu
hapo uwanjani, ingawa wengine walikuwa wanaendelea kumiminika.
Mchezo ulianza kwa nguvu
ingawa Yanga walianza pole pole kidogo wakijaribu kuusoma mchezo wa Simba.
Baada ya dakika tano tu matokeo ya nguvu hizo yalionekana. Saad Ally wa Simba
aliumia baada ya kugongana na Gibson Sembuli wa Yanga na akatolewa nje. Adamu
Sabu aliyeingia badala yake, aliwafurahisha wapenzi wa Simba, kwani aliifungia
goli timu yake katika dakika ya 16.
Yanga walijaribu sana
kukomboa goli hilo lakini walipata taabu kwani ukuta wa Simba ulikuwa imara
sana. Kadiri mchezo ulivyoendelea watu walidhani Yanga isingepata hata goli
moja na kwamba, siku hiyo ingefungwa tena, kwani hadi mapumziko matokeo
yalikuwa ni yale yale ya goli moja kwa Simba na Yanga wakiwa na gurudumu.
Katika dakika ya 87 ya
mchezo, yaani dakika tatu kabla ya mchezo kumalizika, mambo yalibadilika.
Ilikuwa ni golikiki, ambapo mlinzi wa Yanga, Ally Yussuf, alipiga mpira kuelekea
golini kwa Simba. Mpira huo ulipita juu ya vichwa vya wachezaji kadhaa wakiwemo
Abdallah Kibadeni wa Simba na Gibson Sembuli na Sunday Manara.
Mpira huo uliambaa ambaa
kuelekea goli la Simba ambako Kitwana Manara, aliyekuwa amebanwa mno na beki wa
Simba ambaye hakutaka mchezo, Omari Chogo ‘Chemba’, licha ya kuwa ameupa mgongo
mpira huo aliruka na kupiga kichwa kushoto kwake.
Moja kwa moja mpira huo
uliingia kwenye ‘anga’ za nambari nane wa Yanga, Gibson Sembuli, aliyeujaza
wavuni kwa shuti kali la ugoko, lililoingilia kwenye kona ya kushoto na
kumuacha kipa Athumani Mambosasa, aliyekuwa ametoka kumkabili mchezaji huyo,
akiwa hana la kufanya zaidi ya kuutumbulia macho mpira huo ukitinga wavuni
kuandika goli la kusawazisha kwa Yanga. Hivyo, hadi mwisho wa dakika 90 za
kawaida za mchezo matokeo yalikuwa 1-1.
Goli hilo likabadilisha
kabisa sura ya mchezo. Watazamaji ambao walianza kuondoka uwanjani wakidhani
Yanga wameshindwa walikimbilia uwanjani kuangalia mchezo tena. Dakika 90
zilipokwisha ubao wa matokeo ukasomeka Yanga 1 Simba 1 na ndipo dakika 30
zilipoongezwa ili kupata mshindi.
Katika dakika ya saba ya
muda wa nyongeza, mlinzi Ally Yussuf wa Yanga aliipangua ngome ya Simba na
kutoa pasi ya juu kwa mchezaji wa kiungo wa Yanga, Sunday Ramadhan Manara, aliyefunga
goli la pili kwa kichwa. Goli hilo likawa la ushindi kwa Yanga baada ya Simba
kushindwa kusawazisha kwa dakika 23 zilizokuwa zimesalia.
Hili ni pambano lao la
kwanza la ligi kumalizika baada ya muda wa kawaida, yaani ndilo pambano pekee
kwa wakati huo lililokuwa limechezwa kwa dakika 120. Mapambano mengine manne
huko nyuma yalikuwa yamevunjika kabla ya muda wake na siyo zaidi ya muda wake.
Ikawa Yanga wamechukua
ubingwa wa Tanzania kwa ushindi wa magoli 2-1 na kuinyang’anya Simba iliyoutwaa
mwaka 1973 kutoka kwao. Kombe hilo lilikabidhiwa kwa nahodha wa Yanga wa wakati
huo, Abdulrahman Juma na aliyekuwa mgeni rasmi Meja Jenerali Mrisho S.H.
Sarakikya mbele ya mashabiki takriban 50,000 waliohudhuria.
Ilielezwa kuwa, sababu
kubwa iliyoifanya Simba isalimu amri ni ukweli kwamba, haikuwa na stamina ya
kumudu kucheza dakika 120 wakati ambapo watani wao, Yanga, walikuwa na uwezo
huo na kufanikiwa kufunga magoli safi yaliyotinga wavuni katika staili ambayo
ingemshinda golikipa yoyote kuzuia, ingawa baadhi ya wachezaji wa Simba
walikaririwa baadaye wakimlaumu kipa wao Mambosasa kwamba, aliwafungisha kwa
uzembe.
Kadiri mchezo ulivyokuwa
ukisonga mbele ilijidhihirisha kuwa Yanga walistahili ushindi huo ukitilia
maanani jinsi mashambulizi yalivyoielemea Simba. Mtu aliyeivunja nguvu kabisa
ngome ya Simba alikuwa mshambuliaji hodari nambari tisa, Kitwana Manara,
aliyekuwa na mazoea ya kutegea mbele anakobaki na beki mmoja tu, na ambaye
kwenye mechi hiyo alikuwa Chogo. Haikuwa ajabu pale beki huyo alipotolewa nje baada
ya mambo kumzidia uwanjani.
Katika pambano hilo,
golikipa wa Yanga, Elias Michael aligongana na Willy Mwaijibe wa Simba katika
dakika ya 70 na wote wawili wakakimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Nafasi zao zilichukuliwa na Muhidin Fadhil kwa upande wa Yanga na Kessy Manangu
kwa upande wa Simba.
Simba walifanya faulo 17
dhidi ya wachezaji wa Yanga, nane zikiwa katika kipindi cha kwanza, wakati
ambapo Yanga ilicheza faulo 18, 10 zikiwa katika kipindi cha kwanza, ambacho
kwacho Simba ilitawala zaidi kiasi cha Yanga kulazimika kutumia, japo kwa kiasi
kidogo, uamuzi wa ‘Aende mtu mpira ubaki, au uende mpira mtu abaki’.
Aidha, katika mchezo huo,
Yanga ilitumia zaidi mchezo wa kuotea (offside trick) na kuwafanya wachezaji wa
Simba waotee mara 15 wakati wale wa Yanga, kwa kutowekewa mtego kama huo,
walijikuta wakiotea takribani mara mbili tu.
Udhaifu wa Simba kwenye
kufunga magoli ulionekana kwenye upigaji mipira ya kona, ambapo ilipata kona
sita bila hata moja kutinga wavuni. Yanga ilipata kona mbili zote katika
kipindi cha kwanza, na kwa jinsi zilivyolikosakosa goli la Simba, huenda magoli
zaidi yangetinga kama ingepata kona zaidi.
Shabiki mmoja wa Simba
huko Nzega aliamua kujitumbukiza kwenye pipa la kirusu cha pombe kilichokuwa
jikoni na kufa wakati Yanga iliposawazisha bao. Kiingilio cha juu siku hiyo
kilikuwa shilingi 30.
Timu zilipangwa hivi:-
YANGA: Elias Michael/Muhidin Fadhil. Ally
Yussuf, Selemani Saidi, Hassan Gobbos/Boi Iddi ‘Wickens’, Omari Kapera,
Abdulrahman Juma (nahodha), Bona Max Mwangi, Sunday Manara, Kitwana Manara,
Gibson Sembuli na Maulid Dilunga. Kocha: Tambwe Leya (Zaire)
SIMBA: Athumani Mambosasa, Shaaban Baraza,
Mohammed Kajole, Athumani Juma, Omari Chogo, Omari Gumbo, Willy Mwaijibe/Kessy
Manangu, Haidari Abeid ‘Muchacho’ (nahodha), Saad Ally/Adamu Sabu, Abdallah
Kibadeni, Abbas Dilunga. Kocha: Paul West Gwivaha.
Mgeni rasmi, alikuwa Meja
Jenerali Mrisho S.H. Sarakikya.
NB:
Makala haya ni kutoka kwenye muswada wa kitabu cha 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA
YANGA' cha mwandishi Daniel Mbega, ambacho kiko katika hatua za mwisho
kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au
brotherdanny5@gmail.com
No comments:
Post a Comment