Kikosi cha Yanga cha mwaka 1987.
Ndugu zangu,
Najitahidi kuwaletea vidokezo vya historia ya soka nchini. Nimewaletea kuhusu matukio katika timu ya taifa, Taifa Stars, matukio ya mechi za Simba na Yanga na hata mgogoro mkubwa wa Yanga wa mwaka 1975 uliozaa Pan Africans.
Leo hii nawaletea vidokezo vingine - vyote hivi kutoka katika miswada yangu ninayoiandalia vitabu ya 'MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANI' na 'SIMBA NA YANGA: VUTA-NIKUVUTE'.
Hapa ninauzungumzia mgogoro mwingine ulioibuka kuanzia mwaka 1986 ndani ya Yanga, ambao hatimaye ukazaa makundi mawili kwenye klabu hiyo kongwe nchini. Hali hii ikaifanya Yanga kuanza msimu wa 1987 kwa migogoro ambapo kulikuwa na pande mbili zilizokuwa zinapingana. Upande wa uongozi ulikuwa unajiita Yanga-Ukuta na upande wa wanachama waliokuwa wakiupinga uongozi walijiita Yanga-Katiba. Mgogoro huo ulisababisha Yanga ipeleke orodha mbili za usajili FAT.
Mwenyekiti wa Yanga wakati huo, William 'Billy' Bandawe alikuwa analalamikiwa kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na ufujaji wa fedha. Hali hiyo ilisababisha wafadhili wanne wa Yanga wakati huo, Salehe Sultan Hamad, Ali Mohamed, Felician Ferdnand na Juma Said kumsusa Bandawe na kutangaza kwamba wasingetoa misaada tena kama angeendelea kuwepo madarakani.
Kwa upande mwingine wanachama wa Yanga waliokuwa wanapinga uongozi walimlalamikia mwenyekiti wa FAT wakati huo, Said Hamad El-Maamry kwamba alikuwa anausaidia upande wa uongozi ili aendelee kubaki madarakani.
Mgogoro huo ulipelekwa Mahakama Kuu na baadaye pande zote mbili zilizokuwa zinapingana kukutana na Rais wa Awamu ya Pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi, pamoja na mawaziri wote Ikulu kuangalia uwezekano wa kusuluhisha mgogoro huo.
Wanachama waliokuwa wanapinga uongozi waliunda kamati ya watu 13 ambayo ilikuwa na Abdallah Mwamba (Mwenyekiti), Cleophas Kanwa (Katibu), na wajumbe walikuwa S. Sarumanya, S. Omary, Salum Mohamed, Valisanga Mkonjera, D. Othuman, B. Ntila, J. Kayombo, R. Gwao, S. Makule, H. Onyango na Salehe Sultan.
Katika mkutano wao na Rais iliamuliwa zipigwe kura za kuukubali ama kuukataa uongozi, zoezi ambalo lilifanyika Februari Mosi na kuhudhuriwa na Mawaziri pamoja na Wabunge.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Vijana na Michezo, Fatma Said Ally, Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Damian Lubuva, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Nyamka, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Wabunge na Wakuu wa Wilaya za mkoa wote wa Dar es Salaam, pamoja na viongozi wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wote walihudhiria.
Baada ya hapo ilikubaliwa kwamba uchaguzi ufanyike baada ya mwenyekiti wa klabu hiyo Billy Bandawe, kushindwa kwa kura 635-94. Uchaguzi huo ulifanyika Jumapili ya Februari 8 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, ambapo nafasi ya uenyekiti iliwaniwa na watu watatu; William Bocco, Ally Bakari na Mzee Kheri.
Waliowania nafasi ya makamu mwenyekiti ni Robert Mzeru na wenzake wawili, nafasi ya ukatibu mkuu iliwaniwa na Nicholaus Mathias na Joseph Mbele. Ukatibu mkuu msaidizi uliwaniwa na Salum Mohamed na Charles Mgombelo.
Nafasi ya mweka hazina iliwaniwa na Mohamed Rupembecho peke yake, wakati Juma Kambi na Mwilenza E. Mwilenza walikuwa wanagombea nafasi ya mweka hazina msaidizi. Peter Hassan na Charles Newa walikuwa wanawania nafasi ya katibu mipango wakati Salehe Omary na Ramadhani Karababa walikuwa wanachuana katika nafasi ya katibu mwenezi.
Hata hivyo, waliofanikiwa kuchukua nafasi ya uongozi wa klabu hiyo ni William Bocco (Mwenyekiti), Robert Mzeru (Makamu Mwenyekiti), Nicholus Mathias (Katibu Mkuu), Salum Mohammed (Katibu Mkuu Msaidizi), Mohammed Rupembecho (Mweka Hazina), Salehe Omari (Mweka Hazina Msaidizi) na Peter Hassan (Katibu Mipango).
Baadaye FAT iliupitisha usajili uliofanywa na wanachama.
Kikosi cha Yanga kilikuwa chini ya mchezaji wa zamani wa klabu hiyo Mwinda Ramadhani 'Maajabu' na kiliundwa wachezaji wafuatao; Juma Pondamali (Pan Africans), Athumani Juma 'Chama' na Celestine 'Sikinde' Mbunga (wote kutoka Maji Maji), Abubakar Salumu (Sigara), Athumani Abdallah China (Tumaini), Issa Athumani Mgaya (RTC Kagera), Said Mwaibambe 'Zimbwe' (Safari Contractors), Yusuph Ismail Bana (nahodha), Freddy Felix Minziro, Isihaka Hassan 'Chukwu', Rashid Idd Chama, Said Mrisho, Edgar Fongo, Hamisi Kinye, Joseph Fungo, Lawrence Mwalusako, Allan Shomari, Dotto Lutta Mokili, Mohammed Yahaya 'Tostao', Gregory Luanda, Charles Boniface Mkwasa, Muhidini Mohammed 'Cheupe', Hussein Idd, Juma Rashid Kampala, Lucius Mwanga, Ali Mchumila, Abeid Mziba 'Tekero', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji', 'Field Marshal' Juma Mkambi.
Daniel Mbega
brotherdanny5@gmail.com; +255 715 070 109
No comments:
Post a Comment