Chancellor wa Ujerumani Angela Merkel akifurahia jambo na Rais Barack Obama wa Marekani
TAARIFA mpya katika vyombo vya habari vya Ujerumani zikiegemea nyaraka zilizovuja za ujasusi za Marekani zimeendelea kubomoa na kuzua maswali mengi kuhusu harakati za ujasusi za Marekani.
Gazeti la Der Spiegel linaeleza kwamba Marekani imekuwa ikipeleleza simu ya kiganjani ya Chancellor Angela Merkel tangu mwaka 2002.
Ripoti nyingine inasema Rais Barack Obama alielezwa mwaka 2010 kuhusiana na uchunguzi huo lakini hakuwahi kuuzuia.
Kashfa ya ujasusi imeongeza mpasuko na mgongano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Nyaraka zilizovuja zinaeleza kwamba chombo cha kunasa mawasiliano kilikuwa kimetegwa kwenye Ubalozi wa Marekani jijini Berlin - na operesheni ya aina hiyo ilikuwa imetegwa katika maeneo 80 tofauti duniani.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani amekaririwa akisema operesheni kama hiyo, ikiwa itathibitika, itakuwa ni haramu.
Ijumaa iliyopita, Ujerumani na Ufaransa zilisema zinataka Marekani isaini mkataba wa kutochunguzana mwishoni mwa mwaka huu.
Mbali ya kufuatilia mawasiliano ya simu ya Bibi Merkel, kuna madai kwamba NSA imekuwa ikichunguza mamilioni ya simu za raia wa Ujerumani na Ufaransa.
No comments:
Post a Comment