Furaha ya ubingwa kwa Simba 2012 huku wakisherehekea ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya mahasimu wao, Yanga.
Na Daniel Mbega
HUKU utasikia: “Simba! Simba! Simba!” halafu kule
nako kutasikika: “CCM! CCM! CCM!” Naam, hivi ni vibwagizo vinavyosikika kila
wakati Simba na Yanga zinapokutana, iwe kwenye mechi za Ligi, mashindano
mbalimbali na hata zile za kirafiki.
Mashabiki wa Simba wanaweza kusikika pia wakisema:
“Amesimama kidedea, eeee kidedea!” halafu upande mwingine utawasikia
wakichombea: “Kitimtimu, mtakiona leo, nyumba ya shetani mwendawazimu
kaingiaje!”
Hapo hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama buradani nyingine ndani ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye jezi za kijani na manjano.
Hapo hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama buradani nyingine ndani ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye jezi za kijani na manjano.
Mandhari haya ndiyo yanayotazamiwa kuwepo Jumapili hii Oktoba 20, 2013 kwenye Uwanja Mkuu wa
Taifa, wakati Simba na Yanga zitakapoumana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014, huku ukiwa na msisimko wa aina yake.
Wakati Yanga, ambayo inatetea ubingwa wake huku ikiwa
katika nafasi mbaya kwenye msimamo, itakuwa inatafuta ushindi ili kukwea kileleni lakini pia kulipa kisasi cha mabao 5-0
ilichokipata mwaka 2012 katika mchezo wa mwisho, jambo ambalo linaonekana kuwa
ndoto.
Simba wao wanaingia uwanjani wakiwa na mambo
mawili: Kwanza, wanataka kulipa kisasi cha kufungwa katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Mei 17, 2013, lakini pili,
wanatafuta ushindi ili kujiweka sawa zaidi na kutwaa ubingwa baada ya
mwaka huu kukosa nafasi hata ya pili.
Mechi zao
Hii ni mechi ya 76
kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa
Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan Celebic.
Katika kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekeza
mechi hizi umekuwa mkubwa, bila kujali nani anawania kitu gani.
Hata hivyo, katika mechi 75
zilizopita, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala zaidi kwa kushinda mara 29,
wakati Simba imeshinda mara 22. Timu hizo
zimetoka sare mara 24 huku mabao 156
yakifungwa. Kati ya mabao hayo, Yanga imefunga 83
na Simba imefunga 72. Ikumbukwe kwamba, mechi hizi hazihusishi mechi za Ligi
ya Muungano.
Idd Pazi, Kaseja kiboko
Makipa wa Simba, Idd Pazi
‘Father’ na Juma Kaseja wana rekodi ya
pekee kwenye mechi za Simba na Yanga kutokana na ukweli kwamba ndio
makipa pekee baina ya timu hizo kufunga
bao. Pazi alifunga bao la kuongoza kwa penalti Jumamosi Machi 10, 1984 katika
dakika ya 20 na akajitahidi kulinda lango la Simba hadi dakika ya 72 wakati
Omar Hussein alipomzidi ujanja na kusawazisha. Matokeo yakawa 1-1.
Kaseja naye aliingia kwenye rekodi hiyo katika mechi
ya Mei 6, 2012 ambayo Simba ilishinda 5-0 baada ya kufunga kwa penalty katika
dakika ya 67, likiwa ni la nne kwa timu yake.
Mlinzi Suleiman Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’,
ndiye pekee aliyewahi kujifunga wakati timu hizo mbili zilipomenyana kwenye
Ligi. Sanga alijifunga katika harakati za kuokoa katika mechi ya Julai 19, 1977
wakati Yanga ilipokubali kipigo cha mabao 6-0, huku Abdallah Athumani ‘King
Kibadeni’ akifunga hat trick (mabao matatu) peke yake na mengine mawili
yakifungwa na Jumanne Hassan Masimenti.
Wafungaji wa
mabao
Katika mechi 72 zilizopita na kuzaa mabao hayo
147, Omar Hussein ‘Keegan’ wa Yanga ndiye anayeongoza kwa ufungaji, akiwa
amezifumania nyavu mara sita akifuatiwa na Abeid Mziba ‘Tekero’, Idd Moshi na
Jerry Tegete wa Yanga pia, pamoja na Edward Cyril Chumila na Musa Hassan
'Mgosi' ambao wamefunga mabao manne kila mmoja.
Waliofunga mabao matatu kila mmoja ni Kitwana
Manara ‘Popat’, Maulid Dilunga, Said Mwamba ‘Kizota’ na Mohammed Hussein
‘Mmachinga’ wa Yanga, pamoja na Abdallah Athumani ‘Kibadeni’.
Orodha hiyo inaonyesha waliofunga mabao mawili kwa
upande wa Yanga ni Salehe Zimbwe, Juma Mkambi, Rashid Hanzuruni, Said Sued
'Scud', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji’, Issa Athumani, Idelfonce Amlima, Sekolojo
Chambua, Ben Mwalala na Sunday Manara.
Kwa upande wa Simba ni Jumanne Hassan ‘Masimenti’,
John Makelele 'Zig Zag’, Malota Soma ‘Ball Jugler’, Nicodemus Njohole, Dua Said,
Steven Mapunda, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe,
Athumani Machupa, Emmanuel Okwi.
Wachezaji waliopachika bao moja kwenye mechi hizo kwa
upande wa Yanga ni Mawazo Shomvi, Abdulrahman Lukongo, Andrews
Tematema, Emmanuel, Leonard Chitete, Gibson Sembuli, Charles Boniface, Edgar
Fongo, Justin Mtekere, Thomas Kipese, Sanifu Lazaro, Ken Mkapa, James
Tungaraza, Akida Makunda, Constantine Kimanda, Salvatory Edward, Kally Ongala,
Pitchou Mwango Kongo, Aaron Nyanda, Said
Maulid, Athumani Idd, Stephano Mwasika, Davies Mwape, Said
Bahanuzi, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza.
Nyota
wa Simba waliofunga bao moja kila mmoja ni Mustafa Choteka, Haji Lesso, Willy
Mwaijibe, Haidari Abeid 'Mchacho', Adam Sabu, Mohammed Bakari ‘Tall’, Abbas
Dilunga, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwein Ally, Kihwelu Musa, Zamoyoni Mogella,
Mohammed Bob Chopa, Sunday Juma, Mavumbi Omar, George Masatu, Athumani China,
Mchunga Bakari, Abdallah Msamba, Athumani Machepe, Abuu Juma, Juma Amir, Joseph
Kaniki, Athumani Machupa, Nurdin Msigwa, Emmanuel
Gabriel, Moses Odhiambo, Ramadhan Chombo, Haruna Moshi, Uhuru Suleiman, Hilary
Echesa, Idi Pazi, Patrick Mafisango, Juma Kaseja, Felix Sunzu, Amri Kiemba.
Kukimbiana
Mechi za Simba na Yanga hazikosi kuwa na vituko,
lakini vinavyojulikana zaidi ni kule ‘kukimbiana’ uwanjani ama kwa kutopeleka
kabisa timu uwanjani, au kwa kugomea mchezo.
Zifuatazo ni rekodi za timu hizo kukimbiana kwenye
Ligi Kuu:
05/11/1966: Mchezo ulivunjika katika dakika ya 75
baada ya Yanga kugoma kumtoa mchezaji wao Awadh Gessani aliyeamriwa atoke nje
baada ya kumchezea vibaya yule wa Sunderland. Sunderland wakapewa ushindi na
baadaye kuwa bingwa wa taifa kwa mara ya pili. Kabla ya mchezo kuvunjika Yanga
ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0. Nahodha wa Yanga, Mohammed Hussein Hassan
‘Msomali’, alifungiwa na FAT kutocheza mpira kwa miezi 12 na kwamba asipewe
cheo cha unahodha, na Awadh Gessani akafungiwa kutocheza mechi tatu. Yanga
ikatishia kujitoa kwenye ligi pamoja na African Sports, lakini baadaye timu
hizo zikashauriwa kuendelea na ligi.
30/03/1968: Mchezo ulivunjika baada ya mchezaji wa
Sunderland, Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’, kumpiga mwamuzi Jumanne Salum katika
dakika ya 20. Wakati huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na
Kitwana Manara. Mchezo huo ukapangwa kurudiwa Juni Mosi, 1968 ambapo Yanga
ilishinda kwa mabao 5-0.
03/03/1969: Sunderland iligoma kabisa kutia mguu
uwanjani, hivyo, FAT ikaipa Yanga ubingwa na kuitoza Sunderland faini ya
shilingi 500, ambazo hata hivyo, hazikulipwa baada ya kulisuluhisha suala hilo.
18/06/1972: Sunderland iligoma kuingia uwanjani
kwa kipindi cha pili kupambana na Yanga huku Yanga ikiwa inaongoza kwa bao 1-0
lililofungwa na Leonard Chitete. Huu ulikuwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya
Taifa, ambapo Yanga ilipewa ushindi.
10/08/1985: Simba iligomea penati iliyotolewa na
mwamuzi Bakari Bendera wa Tanga katika dakika ya 84 baada ya sentahafu wake
Twalib Hilal kuunawa mpira katika eneo la hatari. FAT ikaipa Yanga ushindi na kuwa
bingwa wa Tanzania Bara.
26/08/1992: Yanga ilikataa kutia timu uwanjani
kucheza na Simba katika mchezo wa marudiano wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania
Bara kwa kuwa tayari ilikwishatwaa ubingwa. Simba ikapewa ushindi na kisha FAT
ikaipiga Yanga faini ya shilingi 250,000 ambazo zililipwa na Murtazar Dewji
aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Pan African.
25/02/1996: Simba iligoma kupeleka timu uwanjani
baada ya FAT kukataa ombi lao la kuahirisha mchezo huo kwa kuwa ilikuwa
inajiandaa na mechi ya Kombe la Washindi dhidi ya Chapungu FC ya Zambia, ambayo
hata hivyo, haikuja kabisa. Yanga ikapewa ushindi.
Msimamo kamili
Yanga 75 29
24 22 83
– 72
Simba 75 22
24 29 72 - 83
No comments:
Post a Comment