Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume wakibadilishana hati za Muungano mwaka 1964.
Na DANIEL MBEGA
Salaam Mwalimu Nyerere,
Sina shaka kwamba huko uliko umepumzika kwa amani, kwa uwezo
wa Mungu. Yawezekana umekuwa mwenyeji huko na kazi yako njema uliyoifanya
katika kuhakikisha Tanganyika inajitawala, na hatimaye inaungana na Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar kuzaa Tanzania, bado ni kitambulisho tosha ndiyo maana leo
hii, miaka 14 baada ya kifo chako, bado Watanzania tunakukumbuka huku duniani.
Lakini nina uhakika hujui yanayotokea huku Tanzania. Kwa kifupi, mambo yameharibika. Natamani waraka wangu ungekufikia mwenyewe mkononi ili nikukumbushe ama nikupashe yanayoendelea huku.
Lakini nina uhakika hujui yanayotokea huku Tanzania. Kwa kifupi, mambo yameharibika. Natamani waraka wangu ungekufikia mwenyewe mkononi ili nikukumbushe ama nikupashe yanayoendelea huku.
Wale wote uliowanadi mwaka 1995 ili waienzi Ikulu yetu,
walikugeuka miezi michache tu baada ya wewe kulala na babu zako. Wakaigeuza Ikulu
kuwa sehemu ya biashara – ingawa wapo wengine uliwauliza “…Mnakimbilia Ikulu
kufanya biashara gani!” Viwanda vyote ulivyopigania kuanzishwa waauziana
wenyewe. Ikulu ikawa sehemu ya kusaini mikataba mibovu ambayo immeshuhudia
madini yetu yalikuvunwa na kupelekwa nje huku sisi tukibaki na mashimo tu.
Kwa kifupi, uliona wanafaa walikusailiti. Maadili ya uongozi
uliyoyasisitiza yakatoweka. Vita ya rushwa imeshindikana kwani wenye dhamana ya
kupambana nayo ndio vinara wa kutoa na kupokea rushwa. Natamani hata Chifu
Fundikira angekuwepo naye aone wenzake wanavyofaidi – pengine angesikitika kwa
nini yeye aliondolewa kwenye Baraza lako la Mawaziri miaka michache tu baada ya
uhuru.
Ufisadi umetamalaki kila kona, chaguzi zimegubikwa na rushwa
mbaya. Chama chako cha Mapinduzi kimekuwa ‘Chama cha Matajiri’. Bora hili ni neon
zuri, lakini wengine wanakiita ‘Chama cha Mafisadi’, au ‘Chama cha Majangili’
na wengine wanathubutu kusema ni ‘Chama cha Majambazi’, ilimradi kila mmoja
anatamka neno analoona linafaa. Maskini hawana nafasi, wachache tu ndio wana
sauti kwa sababu ya fedha zao.
Wale uliowapinga ndani ya Chama wakati ule, uliowahoji
kuhusu walikopata utajiri wao, leo hii ndio wanaoabudiwa. Mbaya zaidi wanapita
mpaka misikitini na makanisani kutoa misaada, halafu wanapigiwa makofi na kuimbiwa
mapambio. Ungewaona, nina imani ungemwaga machozi. Naamini mama yetu Maria
anaugulia moyoni kwa yanayotokea.
Mwalimu, sikuwepo wakati huo, lakini nakumbuka ilikuwa Jumapili,
Aprili 26, 1964, saa 4.00 asubuhi wakati wewe – ukiwa Mwenyekiti wa TANU –
ulipokutana na Mwenyekiti wa Afro-Shiraz Party (ASP) Sheikh Abeid Amani Karume mjini
Dar es Salaam na kusaini hati ya makubaliano ya kuziunganisha nchi zenu. Muungano
huu ulifikiriwa kwa takribani miezi mitatu na siku 24 tu tangu yalipofanyika
mapinduzi ya kuung'oa utawala dhalimu wa Kisultani visiwani Zanzibar Januari 12,
1964. Kabla ya kutiwa saini, nyote wawili mlikuwa mmefanya mazungumzo mara
kadhaa mjini Dar es Salaam na Unguja na ndipo mkafikia mwafaka wa kuziunganisha
nchi hizo.
Wapo walioupinga wakati huo (na wanaendelea kuupinga) kwamba
haukufuata misingi inayotakiwa katika muungano halisi, lakini pia wapo
walioufurahia na wanaendelea kuufurahia kwa kuwa umeleta udugu na kujenga umoja
na mshikamano.
Mwalimu, imebaki miezi michache tu ili Muungano huu utimize
miaka 50, lakini nina mashaka kama hautakufa kabla ya miaka hiyo kutimia. Umoja,
amani, upendo na mshikamano uliojengwa na muungano huo umetoweka kabisa.
Ndiyo, si unaelewa kwamba hivi sasa Watanzania wako kwenye
mchakato wa Katiba Mpya? Ile ambayo wewe uliikataa kipindi kile na kushauri
kasoro ndogo ndogo ziwe zinarekebishwa (yaani itiwe viraka), sasa inaelekea
kupatikana, maana mabilioni ya fedha za walipa kodi yamekwishatumika.
Halafu nikwambie kitu kimoja, ile serikali iliyowaponza John
Malecela na Horace Kolimba mpaka ukawatungia kitabu – serikali ya Tanganyika –
sasa inazaliwa rasmi. Ndiyo, na Wanzibari uliokuwa ukiwatetea kwa kuulinda
Muungano, safari hii ndio vinara wa kuupinga Muungano. Tena basi kuna vikundi
tayari huko Visiwani vinavyohamasisha kuupinga na kutaka Serikali ya Tanganyika
iwemo ndani ya Katiba.
Mwalimu, nafahamu kwamba unatambua jinsi Muungano ulivyopitia
katika vipindi vigumu mno na kuna nyakati ambapo umetiwa msukosuko kiasi cha
kutishia hatma yake. Hilo, kwa kiasi kikubwa, limetokana na baadhi ya watu
kutoa mapendekezo anuai yanayoashiria muungano huo ama unaweza kuendelea kudumu
au kuvunjika kabisa.
Wananchi wa Tanzania wanazijua faida na hasara za muungano
huo kwa kipindi chote hicho na ni wazi kwamba ndiyo maana wengi wao
wamejitokeza kuchangia mawazo yao katika Rasimu ya Katiba wakitaka Serikali ya
Tanganyika ndani ya Muungano.
Wazanzibari wanasema wanataka kuona nchi ambayo waliungana
nayo ikitajwa kwenye Katiba, lakini Wabara nao wanasema wanataka Tanganyika ili
wawe na sauti. Ni changamoto kweli Mwalimu. Wakati Wazanzibari wanasema
Muungano umeumeza utaifa wao, baadhi ya Watanganyika nao wamekuwa wakisema
rasilimali nyingi za Tanzania Bara zimekuwa zikitoweka kuwanufaisha Wazanzibari
katika kile kinachoonekana kama kujipendekeza kwa serikali ya CCM kulinda kwa
nguvu zote ili usivunjike.
Wazanzibari, kwa upande wao wanaendelea kusema kwamba kwa
kipindi chote hicho wameshindwa kufanya jambo lolote kwa maendeleo yao kutokana
na kivuli cha muungano na kwamba kila wanalotaka kulifanya lazima serikali ya
Muungano ihoji.
SUALA LA UTAIFA...
Mwalimu, nadhani unatambua kuwa yapo mambo mengi ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitaka kufanya bila kupitia kwenye Muungano na mojawapo ni uamuzi wake wa kutaka kujiunga na Shirikisho la Nchi za Kiislamu Duniani (Organisation of Islamic Conference - OIC) mwaka 1992. Hapo ndipo hasa 'chunusi' wa Muungano alipoingia.
Mwalimu, nadhani unatambua kuwa yapo mambo mengi ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitaka kufanya bila kupitia kwenye Muungano na mojawapo ni uamuzi wake wa kutaka kujiunga na Shirikisho la Nchi za Kiislamu Duniani (Organisation of Islamic Conference - OIC) mwaka 1992. Hapo ndipo hasa 'chunusi' wa Muungano alipoingia.
Lengo kubwa la SMZ kwa wakati ule, chini ya Dk. Salmin Amour
Juma, lilikuwa kuifanya Zanzibar kuwa nchi au taifa la Kiislamu, wakati
inafahamu fika suala kama hilo lilipaswa kujadiliwa kabla ya kuchukua maamuzi
mazito kama aliyokuwa amechukua Dk. Salmin.
Utakumbuka vyema jinsi uamuzi huo ulivyozua mjadala mrefu ndani
ya CCM (wakati huo serikali ilikuwa bado ya chama kimoja) na hata bungeni,
ambako wabunge na wana-CCM wa Bara waliona wamesalitiwa na kiongozi huyo wa
Zanzibar ambaye pia kikatiba, ndiye Makamu Mwenyekiti wa CCM upande wa Zanzibar
na pia wakati huo alikuwa ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano!
Lakini Mwalimu, Zanzibar haikujiondoa OIC kama tulivyoelezwa
na viongozi wetu, bali kilichotokea ni kwamba, OIC ilichunguza na kukuta
Zanzibar siyo Taifa linalojitegemea, yaani Sovereignty State, na kwa mujibu wa
masharti yao, haikustahili kuwa mwanachama, hivyo wakaiondoa, siyo kwamba
yenyewe ilijitoa baada ya shinikizo.
Pamoja na kuondolewa huko, Zanzibar iliendelea kulalamika
kwa kuingiliwa katika mambo yake ya ndani kwa kisingizio cha muungano, ambao
kwa kizazi cha sasa wanaiona hali hiyo kana kwamba imewadumaza.
Kujiunga kwa Zanzibar katika OIC kuliwazindua wabunge wa Tanzania Bara, ambao waliona kuwepo kwa serikali mbili ndani ya Muungano kulikuwa ni kama kuwapa kiburi Wazanzibari, kiasi cha kufanya lolote wanalotaka bila kusubiri baraka za upande mwingine.
Kujiunga kwa Zanzibar katika OIC kuliwazindua wabunge wa Tanzania Bara, ambao waliona kuwepo kwa serikali mbili ndani ya Muungano kulikuwa ni kama kuwapa kiburi Wazanzibari, kiasi cha kufanya lolote wanalotaka bila kusubiri baraka za upande mwingine.
Ndipo katika kikao cha Bunge la Bajeti cha mwaka 1993,
aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Mheshimiwa Njelu Edward Mulugale Kasaka akawasilisha
hoja binafsi bungeni na kudai Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano ili
kutoa uwiano sawa. Hoja hiyo ilipata baraka za Waziri Mkuu wa wakati huo, John
Samwel Malecela 'Cigwiyemisi' na kupitishwa na Spika wa Bunge wa wakati huo,
marehemu Chifu Adam Sapi Mkwawa ili ijadiliwe ingawa alizuia mjadala usiwe
mrefu sana. Hata katika Bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba iliyokuwa chini ya
Spika wa sasa Samuel Sitta, waliainisha kwamba kulikuwa na ‘Waraka wa Kutaka
Maoni ya Wananchi kuhusu Hoja ya Tanganyika (White Paper)’.
Mwalimu, ni katika mjadala huo ambapo kulionekana kuna
mchanganyiko; wengine wakiunga mkono na wengine wakipinga mabadiliko ya Katiba
ya Muungano kufanya ziwepo serikali tatu.
Wabunge 55 waliofahamika kama G55, wakiongozwa na mtoa hoja,
Njelu Kasaka, waliiunga mkono hoja hiyo. Baadaye wakaongezeka wengine kumi na
kuifanya idadi yao kuwa 65 hadi kufikia Julai 22, 1994. Wabunge waliounga mkono
na majimbo yao ya wakati huo yakiwa kwenye mabano ni; Mateo Tluway Qaresi
(Babati), Jenerali Twaha Khalfani Ulimwengu (Taifa/Jumuiya ya Vijana), Mbwete
Polile Hombee (Mbeya Vijijini), John Byeitima (Karagwe), Chediel Yohane Mgonja
(same), Japhet Sichona (Mbozi), Benedict Losurutia (Kiteto), Dk. Mganga Kipuyo
(Arumeru Magharibi), Stanley Kinuno (Nyang'hwale), Dk. Aaron Chiduo (Gairo),
Edward Oyombe Ayila (Rorya) na Shashu Lugeye (Solwa).
Wengine walikuwa John Mwanga (Moshi Mjini), Dk. Deogratius
Mwita (Serengeti), Abel Mwanga (Musoma Mjini), Juma Jamaldin Akukweti
(Tunduru), Patrick Silvanus Qorro (Karatu), Steven Mwaduma (Iringa Mashariki),
Dk. Ndembwela Ngunangwa (Njombe Kusini), Richard Koillah (Ngorongoro), Ahmed A.
Mpakani (Iringa Magharibi), Paschal K. Mabiti (Mwanza), Luteni Lepilal Ole
Moloimet (Monduli), Lumuli Alipipi Kasyupa (Kyela), Profesa Aaron Masawe (Hai)
na Arcado Ntagazwa (Kibondo).
Mwalimu, inakumbukwa pia walikuwemo Phineas Nnko (Arumeru
Mashariki), Paschal Degera (Kondoa Kusini), Mussa Nkhangaa (Singida Mjini),
Halimenshi Kahema Mayonga (Kigoma Kaskazini), Said Abdallah Nakuwa (Lindi
Mjini), na Mosi Tambwe (Taifa/Wanawake).
Wengine ni Luteni Kanali John Mhina (Muheza), Charles
Kagonji (Mlalo), Kisyeri Werema Chambiri (Tarime), Tobi Tajiri Mweri (Pangani),
William H. Mpiluka (Mufindi), Aidan Livigha (Ruangwa), Philip Sanka Marmo
(Mbulu), Erasto K. Lossioki (Simanjiro), Shamim Khan (Morogoro Mjini), Raphael
Shempemba (Lushoto), Phares Kabuye (Biharamulo), Evarist Mwanansao (Nkasi),
Mussa Masomo (Handeni), Jared Ghachocha (Ngara), na Mariam Kamm
(Taifa/Wanawake).
MAMBO WALIYOYATAKA...
Mwalimu, wote hawa walitaka Muungano wa Tanzania, uliozaliwa bila kupata baraka za wananchi wengine na hivyo kuwa na mapungufu, utazamwe upya. Walifikiria kwamba kwa wakati huo ulizaliwa kwa makubaliano tu kati ya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP), lakini bila ridhaa ya wananchi.
Mwalimu, wote hawa walitaka Muungano wa Tanzania, uliozaliwa bila kupata baraka za wananchi wengine na hivyo kuwa na mapungufu, utazamwe upya. Walifikiria kwamba kwa wakati huo ulizaliwa kwa makubaliano tu kati ya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP), lakini bila ridhaa ya wananchi.
Wakaeleza kwamba kwa wakati huo ilikuwa lazima Muungano huo
ufanywe haraka ili kulinda mapinduzi ya kumwaga damu ya ndugu zatu wa Zanzibar;
Unguja na Pemba, ambavyo ni visiwa vidogo sana, kwa hiyo Sultan Jamshid
angeweza kurejea tena kwa msaada kutoka kokote kule duniani na inasemekana
tayari alikuwa ameandaa majeshi ili arudi kuivamia Zanzibar.
Lakini baada ya kusikia Zanzibar na Tanganyika zimeungana
hata yeye kule alikokimbilia na wafadhili wake walikata tamaa kurejesha tena
utawala wa kibwanyenye (Usultani) visiwani humo.
Kwa maana nyingine, tunaweza kusema nchi hizo ziliungana kwa
sababu za ki-ulinzi au kiudugu zaidi na kwa uzalendo wa Kiafrika, Muungano
ambao haukupata baraka za wananchi kama walivyokuwa wakipigania uhuru wao.
Lakini sasa baada ya miaka 49 hakuna tena tishio kama hilo (dhidi ya ndugu zetu
wa Visiwani).
Kwanza, hata wale ambao wangefanya hivyo, sasa nao wamekata
tamaa kabisa. Pili, kikubwa zaidi ni kwamba hata serikali yenyewe ya Mapinduzi
Zanzibar sasa ina uhusiano mzuri tu hata na watawala wake wa zamani.
Ni suala la u-taifa tu kwa sababu chini ya mwavuli wa
Muungano, Mtanganyika amepoteza kabisa utaifa wake (National Identity). Hakuna
popote katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano panapotaja kitu kinachoitwa
'Tanganyika' au u-Tanganyika. Badala yake sehemu kama hiyo imemezwa na neno
Tanzania. Lakini Zanzibar ina serikali yake yenyewe, SMZ.
Ndiyo maana hata serikali ya CCM ilipoagiza hoja hiyo
iondolewe Bungeni mwaka 1994 na kuamua kuendelea na mfumo wa serikali mbili
ndani ya Muungano huku ikifanya mikakati kuunda serikali moja, Wazanzibari
waligoma kabisa kuafiki muundo huo wa serikali moja.
Mwalimu, unakumbuka jinsi Wazanzibari, wakiongozwa na Rais
wao wa wakati ule Dk. Salmin Amour Juma, walivyosema katu SMZ haiwezi kufa na
kwamba hawaafiki serikali moja. Wengine wakaendelea kusema kwamba Muungano
haujainufaisha Zanzibar kwa lolote, hivyo kumaanisha kwamba hawana haja nao.
CCM iliamua kuendesha kura za maoni kwa wanachama wake na
wananchi kwa ujumla ili kuona walikuwa na mtazamo gani kuhusu suala la
Muungano. Waliokuwa wakitetea Muungano ilionekana waliutetea kwa lugha kali ya
hasira, ghadhabu na hata vitisho vya kuwafukuza wenzao kwenye Chama. Waliodai
Utanganyika nao walidai kwa lugha hiyo hiyo ya ukali, wakijibu mapigo.
Kitu kilichopaswa ama kinachopaswa kutazamwa hapa ni mambo
machache kama yafuatayo; Kwanza kabisa, kudai Utanganyika siyo kosa la uhaini
wala la jinai. Pili, Chama cha Mapinduzi siyo wananchi kwa sababu wananchi wako
milioni 35, lakini wanachama wa CCM hadi kufikia mwaka 1994 walikuwa 3,506,355
tu. Pengine kutokana na kuwepo kwa vyama vingi vya siasa idadi hiyo imepungua
kwa sasa.
Tatu, walioulizwa maoni hayo kuhusu Muungano mwaka 1994 ni
wanachama wa CCM peke yao, tena wapatao 1,349,501. Hesabu hiyo ilikuwa sawa na
asilimia 33.49 tu ya wanachama wote nchi nzima. Asilimia 61.75 ya asilimia
33.49 walipendekea serikali mbili, asilimia 29.21 walipendekeza serikali moja,
na asilimia 8.27 walitaka serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Kura za
maoni zilizoharibika zilikuwa asilimia 0.67.
Mwalimu, Wtanzania wanajiuliza, kura hizo zilihesabiwa na
nani? Waliopiga kura ni wana-CCM na waliozihesabu ni hao hao wanachama wa CCM
pamoja na viongozi wao, ambao walikuwa wakipinga hoja hiyo. Unategemea wangetoa
majibu gani? Walichosahau ni kwamba, suala hilo ni nyeti na linawagusa wote,
wananchi wa Tanzania kwa ujumla wao, bila kujali itikadi zao za siasa.
Nakumbuka Mkuu wa Mkoa wa Mara wa wakati huo, Bwana Joseph
Butiku, alitoa kauli kali kwamba msimamo uliokuwa umefikiwa na CCM ni kuwa na
serikali mbili katika Muungano kuelekea serikali moja na kwamba kama Rais wa
Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, alikuwa anapinga shauri yake. Butiku aliyasema
hayo Jumanne, Agosti 23, 1994 kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam wakati
akishiriki mjadala wa hoja ya serikali ya kufuta Azimio la Bunge la mwaka 1993
la kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Nanukuu maneno
yake: "Wananiuliza, umemsikia Rais
wa Zanzibar? Aah mimi nasema Rais wa Zanzibar ni kiongozi wetu... tunamheshimu
... lakini kakosea ... Huu ndio msimamo wa Chama; serikali mbili kuelekea
serikali moja na kama Waziri Mkuu hataki, shauri yake, kama Rais wa Zanzibar
hataki, shauri yake, maana Chama cha Mapinduzi kina utaratibu wa kuliongoza
taifa hili..." mwisho wa kunukuu.
Mwalimu, nakumbuka hapa ndipo ulipoamua kuingilia kati hoja
ya Tanganyika na kusema kwamba, kuundwa kwa serikali hiyo kungemaanisha kifo
cha Muungano. Hivyo, ukasema usingekuwa tayari kuona Muungano unakufa hali wewe
ukiwa hai!
Pengine kwa vile tayari umekwishatangulia mbele ya haki
ndiyo maana waliobaki wameamua kuua Muungano – mwanao pekee aliyesalia – kama walivyoua
Ujamaa na Kujitegemea, tena kule kule Zanzibar.
SERIKALI ILIKUWEPO...
Wazanzibari wanaendelea kupinga muundo wa muungano wa serikali moja, na sasa hawazitaki hata hizo mbili. Sababu kubwa inayowafanya wakatae muundo huo ni kwamba wanadai Zanzibar ilikuwa na serikali yake kamili wakati Muungano ulipofanyika Aprili 26, 1964!
Wazanzibari wanaendelea kupinga muundo wa muungano wa serikali moja, na sasa hawazitaki hata hizo mbili. Sababu kubwa inayowafanya wakatae muundo huo ni kwamba wanadai Zanzibar ilikuwa na serikali yake kamili wakati Muungano ulipofanyika Aprili 26, 1964!
Mwalimu, hapa Wazanzibari hawajadanganya. Ni kweli kabisa,
tangu Januari hadi Aprili 1964 Zanzibar ilikuwa nchi huru (Sovereign State)
ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Mnamo Aprili 6, 1964 Zanzibar ilikuwa
imefungua Balozi tatu; London, Uingereza alikuwepo Othman Shariff; Cairo, Misri
alikuwepo Salim Ahmed Salim, na New York, Marekani alikuwepo Hasnu Makame.
Waziri wa Mambo ya Nje alikuwa Profesa Abdulrahman Mohammed Babu.
Pia nchi 17 zilikwishaitambua Zanzibar hadi kufikia Aprili
26, 1964. Nchi hizo ni Ghana (28/1/1964), Cameroon (30/1/1964), German
Democratic Republic - GDR (30/1/1964), Poland (30/1/1964), Israel (1/2/1964),
Misri (4/2/1964), Urusi (4/2/1964), China (6/2/1964), Czechoslovakia
(18/2/1964), Algeria (18/2/1964), India (22/2/1964), Uingereza (24/2/1964), Marekani
(24/2/1964), Mali (26/2/1964), Congo-Brazzaville (26/2/1964), Ceylon
(26/2/1964) na Liberia (29/2/1964).
Aidha, nchi tisa zilikwishafungua Balozi zao huko Zanzibar
kabla ya Muungano. Nchi hizo ni Ghana, GDR, Israel, Urusi, China, Uingereza,
Vietnam, Marekani na Ufaransa.
Zanzibar pia tayari ilikuwa mjumbe katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN), mnamo Aprili 6, 1964, na ilikuwa inashirikishwa UNESCO, ADB na mashirika mengine ya kimataifa.
Zanzibar pia tayari ilikuwa mjumbe katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN), mnamo Aprili 6, 1964, na ilikuwa inashirikishwa UNESCO, ADB na mashirika mengine ya kimataifa.
Mwalimu, lakini kilicho wazi ni kwamba, Wazanzibari
wamesahau kuwa hata Tanganyika ilikuwa na serikali yake kamili kabla ya
Muungano. Pengine kwa kutambua hilo ndiyo maana safari hii wenyewe wamesimama
kidete kuitaka Serikali ya Tanganyika.
Na kwa vile Katiba siyo Msahafu, hata Watanganyika nao
wameamua kuwa na serikali yao. Hata hivyo, ninavyoona – ukiacha wananchi wa
kawaida – wale wote wanaoipigia kelele ambao wako kwenye nyadhifa mbalimbali,
wanakililia siyo serikali, bali madaraka.
Yaani Mwalimu, ukiwaona wanavyozungumza huku mishipa ya
shingo imewatoka na mate yanawadondoka ungecheka badala ya kusikitika. Wanataka
kwenda Ikulu ya Tanganyika na wengine wanataka kwenda Magogoni. Lakini sijui
hiyo Ikulu ya Tanganyika itakuwa wapi? Sijui wataidai na Ikulu yao halafu
Serikali ya Muungano itafute Ikulu nyingine?
Samahani Mwalimu, usingizi umenibana, wacha nisinzie kidogo.
Keso asubuhi nitakutumia salamu nyingine. Alamsiki. <MWISHO>.
No comments:
Post a Comment