Tshimanga Kalala Asosa 'Mtoto Mzuri'. Picha kwa hisani ya kajunason.blogspot.com.
Na Daniel Mbega
AHLANI Wasaalani ndugu zangu wapenzi wa kona hii ya
kuzikumbuka na kukumbushana mikito ile ya zamani. Ni matumaini yangu kwamba
nyote mu wazima na mnaendelea vyema na majukumu ya ujenzi wa taifa.
Karibuni tena tuendelee kupashana vile vigongo vya enzi
zetu, enzi zile ambazo muziki wa dansi ulikuwa una hadhi kubwa sana baada ya soka na ndondi. Siyo siku hizi
ambapo unaweza kukuta mwanamuziki anatunga nyimbo tatu ambazo tune inakuwa ile
ile na hata maana nayo inakuwa ile ile.
Enzi zile bwana, jamaa walijua kutunga. Walikuwa wakisugua vichwa kweli kweli kuhakikisha kwamba wanatoa vigongo ambavyo vingewakuna vilivyo mashabiki wao. Na zaidi, nyimbo ambazo zingeweza kuwa lulu na keki hata kwa miongo au karne kadhaa.
Enzi zile bwana, jamaa walijua kutunga. Walikuwa wakisugua vichwa kweli kweli kuhakikisha kwamba wanatoa vigongo ambavyo vingewakuna vilivyo mashabiki wao. Na zaidi, nyimbo ambazo zingeweza kuwa lulu na keki hata kwa miongo au karne kadhaa.
Leo namzungumzia Kaiba, kama anavyoimbwa na wale vijana
wa ‘Kizairwaa’ Marquis du Zaire waliokuwa wakitesa pale White House enzi zile
za ushindani wa bendi za muziki wa dansi kama ilivyokuwa katika ushabiki wa
kandanda wa Simba na Yanga.
Kibao hiki ni utunzi wake Tshimanga
Kalala Assosa 'Mtoto Mzuri', aliyeimba akishirikiana na waimbaji kama akina Mutombo
Lufungula ‘Audax’, Zimwema Mujanga ‘Adios’, Kassongo Mpinda 'Clayton', Bobo Sukari, Fredito Butamu na
wengineo, huku Nguza Viking akicharaza gitaa la solo akishirikiana na Mbwana
Kuwasa ‘Cox’. Walikuwepo pia akina Mbombo wa Mbomboka, Ilunga Banza Muchafu aliyekuwa akikung'uta bass, Ilunga Lubaba na wengineo.
Huyu Kaiba anamsuta mumewe wa zamani anayemkodolea mimacho kwa
kumuona amependeza sasa wakati yeye mwenyewe alimwacha.
Kaiba huyu, ambaye sasa amenawiri na kupendeza ambapo
anamwambia mumewe wa zamani kwamba hajabadilika, ni yule yule Kaiba wa zamani
ambaye mume huyo alikuwa akimtelekeza na kumfukuza kwa kashfa nyingi usiku wa
manane, tena mvua ikiwa inanyesha.
Kaiba huyo anasema; “Unachoshangaa sasa ni nini wee Babu,
Au unafikiri sio mimi kunitamani tena, Basi mimi ni yuleyule Kaiba, Uliyekua
unanitelekeza na kunifukuza, Kwa kashfa usiku mwingi mvua ikininyeshea, Bila
huruma Mama mama.”
Tena Kaiba anaendelea; “Usishangae Babu mimi leo
nimependeza eee, Hii ni kazi nzuri ya mwenzio Babu kanithamini, Basi mimi ni
yuleyule Kaiba, Uliyekuwa unanitelekeza na kunifukuza, Kwa kashfa usiku mwingi
mvua ikininyeshea, Bila huruma Mama Mama.”
Hapa labda niseme hivi, wapo wanaume wengi, na sote ni
mashuhuda ndani ya jamii, ambao wana tabia ya kuwanyanyasa wake zao kwa
kutowapatia mahitaji yao
muhimu, wakiona kwamba hayo hayawastahili huku wakisahau kuwa ni haki yao.
Tena basi, wanaume hawa hujidanganya kwamba kwa kuwa
wakati ule mwanamke huyu ambaye sasa ni mkewe, alikuwa akipendeza kabla ya
kuolewa, sasa hakuna haja ya kupata yale mahitaji kwani kama
ni ndoa tayari anayo. Apendeze anataka nani amuone?! Ndivyo hujidanganya hivyo.
Zaidi, mapenzi kwa wake zao hupungua baada ya kuwaona kama wamechujuka hivi, tena kutokana na wao wenyewe
kutowapendezesha, hivyo kuwaona wanawake wa nje kama
ndio bora zaidi.
Wengine huwatesa mno wake zao na kuwasimanga kwamba kwao
wana nini, maskini wa kutupwa, tena wakiwabeza kwamba hata kama
wataondoka hakuna atakayewatamani. Wanasahau msemo wa Kiswahili usemamo;
‘Haramu kwako, halali kwa mwenzio!’
Jamani si juzi tu tumeisikia huko Tarime jamaa alivyomkata mguu mkewe ambaye mpaka sasa bado yupo wadini? Maskini binti wa watu amepata kilema cha maisha kwa sababu ya ukatili wa mwanamume! Pole sana dada.
Nitumie nafasi hii, kabla ya kukiachia kibao hicho cha
Kaiba, kuwaasa wanajamii kwamba, si tabia njema kukashfiana. Kama
mmependana wakati huo, na sasa mnaona kama
mapenzi yamepungua, ketini chini mtafakari tatizo liko wapi ili muweze kuyaboresha
mapenzi yenu.
Tabia ya dharau na manyanyaso haifai katika jamii kwa
sababu inawabomoa hata watoto na inawajengea taswira mbovu ndani ya jamii
inayowazunguka.
Zaidi, kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake katika
ndoa. Kudharau majukumu yako ni tabia mbovu ambayo haifai. Hakuna haki kama
mtu hatimizi wajibu wake, kwani haki na wajibu ni vitu viwili vinavyokwenda
pamoja.
Tazameni mashairi ya wimbo huu;
Unachoshangaa sasa ni nini wee Babu
Au unafikiri sio mimi kunitamani tena
Basi mimi ni yuleyule Kaiba
Uliyekua unanitelekeza na kunifukuza
Kwa kashfa usiku mwingi mvua ikininyeshea
Bila huruma Mama mama
Usishangae Babu mimi leo nimependeza
Hii ni kazi nzuri ya mwenzzio Babu kanithamini
Basi mimi ni yuleyule Kaiba
Uliyekua unanitelekeza na kunifukuza
Kwa kashfa usiku mwingi mvua ikininyeshea
Bila huruma Mama Mama
Chorus
Hata hivyo Mama ngoya
Kwa kweli dunia kabla hujafa haujaumbika
Namshukuru Mungu umeniacha salama
Mama ngoya ngoya mi Kaiba nimetulia x2
(Halafu anakuja Mbwana Cox na solo moto kabisa )
Rudi mwanzo
Mwenye hoja na maoni asisite kunikandamizia: +255 715 – 070
109, barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment