Marehemu Freddie Ndala Kasheba enzi za uhai wake
NDUGU zangu, napenda kuwakaribisha
katika makala za aina hii zihusuzo muziki. Hapa tutakuwa tukizisawiri nyimbo
mbalimbali zenye ujumbe maridhawa kwa maisha yetu. Leo hii niemamua kuanza na
kibao hiki cha al-marhum Supreme Freddie Ndala Kasheba kisemacho ‘Dunia
Msongamano’, ambacho alikiimba na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS)
mwanzoni mwa miaka ya 1980 (mwaka 1982).
Hakuna shaka kwamba pamoja na kuimbwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini mashairi yake yamebeba ujumbe murua unaohusu maisha yetu ya sasa na hata yajayo. Siyo ajabu kinapopigwa – aua hata ninapowakumbusha hapa – baadhi yenu mnalinganisha na mambo yaliyowatokea ninyi wenyewe ama ndugu na jamaa zenu.
Hakuna shaka kwamba pamoja na kuimbwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini mashairi yake yamebeba ujumbe murua unaohusu maisha yetu ya sasa na hata yajayo. Siyo ajabu kinapopigwa – aua hata ninapowakumbusha hapa – baadhi yenu mnalinganisha na mambo yaliyowatokea ninyi wenyewe ama ndugu na jamaa zenu.
Ndugu zangu, maradhi humpata mtu
yeyote yule, na kwa hakika kuugua siyo kufa! Kama ambavyo mti humea wakati wa
masika na kupukutika wakati wa kiangazi, ndivyo ilivyo miili ya binadamu. Wakati
mwingine kupata maradhi ndiko kuukomaza mwili.
Lakini inashangaza baadhi ya
walimwengu, tena wakati mwingine wale ambao ni watu wa karibu yetu kabisa,
hutokea kuombea kwamba fulani afe. Wengi hugeuka watabiri kila wanaposikia
fulani anaumwa, na moja kwa moja mawazo yao huwapelekea kuamini kwamba watu hao
hawatapona, bali watakufa!
Walimwengu ni watu wa ajabu kabisa
ndugu zangu. Pindi wanapomuona fulani anasumbuliwa na maradhi, wao tayari
huanza kupiga hesabu ya lini atakufa na wapi atazikwa!
Watu wa aina hii ni wengi sana ndani
ya jamii yetu na inaonekana wamepitiwa hata na maneno ya wimbo wa Salamu kwa
wagonjwa ulioimbwa na Omar Kungubaya miaka ile ya 1970 yasemayo; “…Ajuaye Bwana
Mungu kwa mzima kuwa mfu, mgonjwa kuwa salama…”
Binafsi naamini kwamba kila nafsi itaonja
mauti, kwa sababu sisi sote ni mavumbi na mavumbini hatuna budi kurejea. Hivyo,
suala la kufa huwa silihofii kabisa, ninachokihofia ni kwamba nitakuwa katika
kundi gani baada ya kufa. Daima wenye hekima humuomba Mungu awaongoze katika
haki na kuwaombea wengine washike mwenendo mwema, si ndivyo jamani?
Kasheba hakukosea alipokitunga kibao
hiki na kukiimba akiwa na Orchestra Safari Sound ‘wana-Dukuduku’ kisemacho Kwamba
kilikuwa ni kisa cha kweli kilichomtokea mwenyewe hilo haliwezi kuondoa ukweli
kwamba mambo haya yanatokea ndani ya jamii zetu. “…Mawazo yamenijia leo, Ya
Mzee wangu alokuwa akisema, Dunia ni msongamano wa watu wenye akili tofauti,
Ukitaka kuishi vema lazima uwe na utulivu, Ukitaka kuishi vema fikiri kabla ya
kujibu, Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako, Dunia ni kuona
mambo, Na halafu kuyasahau…”
Ni kweli kabisa, dunia ni msongamano
kwa sababu imejaa watu wengi wenye mawazo tofauti, ambao wanadhani kwamba mtu
akiugua basi atakufa tu, tena yawezekana kabisa wakawa wamempangia siku, saa na
namna kifo chake kitakavyokuwa.
Watu wa aina hii tunawashuhudia
jamani, hawaendi kuwaona wagonjwa mpaka kwanza waulizie; “Anaumwa nini?” “Vipi
amekonda?” “Sijui kama atapona, hivi umeomuona alivyo?” Basi hukumu hizi na
nyingine nyingi ndizo hutawala mawazo ya watu hawa, na hata pale wanapokuwa
wanakwenda kuwatazama wagonjwa huwa ni kama maigizo fulani tu kwao, yaani kana
kwamba wamekwenda kuthibitisha hisia zao kwamba watu hao hawatapona! Utadhani
wao ni maswahiba wa Mungu na wanajua mipango yake!
Kweli naamini maneno ya Kasheba;
“…Dunia msongamano, Kasema baba, Nimeyaona leo nakubali mie, Wengine hupendelea
kufurahia, Wanaposikia fulani kafa…” Lakini wanasahau kwamba; “… Kufa kwa
binadamu hupangwa na Mungu, Namuomba Mwenye Enzi anipe maisha eeh.”
Ndiyo, wanasahau kwamba maradhi
yawapatayo wanadamu wakati mwingi si ya mauti, bali hutokea ili Mungu aweze
kutukuzwa kwayo. Lakini bila kupatwa na masahibu pengine huwezi kamwe kuitambua
tabia ya upande wa pili ya ndugu na jamaa zetu.
Ninachoweza kusema ni kwamba, tuwaombee
kwa Mungu awasamehe wale wote wenye tabia ya kupenda kuwatabiria wenzi wao
kwamba watakufa. Wale wenye tabia ya kujifanya madaktari bingwa wa kupima watu
kwa macho! Wale wenye kawaida ya kujifanya miungu wa dunia kwa kuweza kutoa
hukumu wakati wakijua kwamba hakimu pekee ni Mungu!
Hebu burudikeni na kibao hiki,
lakini kusema kweli nahitaji sana mchango wenu katika mada hii.
AAhhhh DUNIA
MSONGAMANO
Mawazo yamenijia leo,
Ya Mzee wangu alokuwa
akisema,
Dunia ni msongamano wa
watu wenye akili tofauti,
Ukitaka kuishi vema
lazima uwe na utulivu,
Ukitaka kuishi vema
fikiri kabla ya kujibu,
Jifunze kwa
walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako,
Dunia ni kuona mambo,
Na halafu kuyasahau
Kibwagizo:
Dunia msongamano,
Kasema baba,
Nimeyaona leo nakubali
mie,
Wengine hupendelea
kufurahia,
Wanaposiikia fulani
kafa,
Kufa kwa binadamu hupangwa
na Mungu,
Namuomba Mwenye Enzi
anipe maisha eeh
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Mnaweza kunitumia mchango wenu kwa
sms ama kunipigia kupitia kilongalonga – 0715 – 070 109, au barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment