Maulid Dilunga (kushoto) enzi ya uhai wake akiwa kamisaa wa mchezo wa soka. Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry.
Na Daniel Mbega
ILIKUWA
jioni yenye majonzi na simanzi kupindukia kwa wachezaji, viongozi na wapenzi wa
Sunderland Jumamosi ya Juni Mosi, 1968, kwani siyo tu siku hiyo walipata kipigo
kisichovumilika cha magoli matano kwa gurudumu toka kwa Yanga, bali pia kipigo
hicho kilitia saini Yanga kuchukua ubingwa wa soka nchini.
Kipigo hicho kilikuwa kikiuma zaidi ikikumbukwa kuwa, katika mechi ya kwanza ya ligi hiyo mwaka huo baina yao, mchezo ulivunjika baada ya fujo kuibuka kufuatia Yanga kujipatia goli la kwanza kwenye dakika ya 28 kupitia kwa Kitwana ‘Popat’ Manara. Hii sasa ilikuwa ni mechi ya marudiano ili kumpata bingwa.
Kipigo hicho kilikuwa kikiuma zaidi ikikumbukwa kuwa, katika mechi ya kwanza ya ligi hiyo mwaka huo baina yao, mchezo ulivunjika baada ya fujo kuibuka kufuatia Yanga kujipatia goli la kwanza kwenye dakika ya 28 kupitia kwa Kitwana ‘Popat’ Manara. Hii sasa ilikuwa ni mechi ya marudiano ili kumpata bingwa.
Vinara wa
Yanga katika mechi ya marudiano walikuwa washambuliaji hatari wa timu hiyo, Maulid
Dilunga na Salehe Zimbwe waliofunga magoli mawili kila mmoja, na Kitwana Manara
alifunga goli moja lililokamilisha kifo cha Sunderland siku hiyo.
Katika
mchezo huo wa Ligi ya Taifa uliofanyika kwenye Uwanja wa Ilala (sasa Kumbukumbu
ya Karume), Yanga iliinyanyasa zaidi Sunderland ikielekea kuumudu mchezo katika
kila idara kuliko wapinzani wao na kuwadhibiti ipasavyo, ikiwa ni pamoja na
kucheza watakavyo.
Awali
Sunderland walikuwa wamelalamika kutaka mchezaji wao Emmanuel Mbele,
aliyefungiwa kutocheza mpira kwa kipindi cha miezi 6 kwa kusababisha mchezo wa
kwanza kuvunjika, afunguliwe. FAT ikakataa kwa kufuata sheria, lakini Yanga,
wakiwa wanajiamini, wakaiomba FAT imwachilie huru mchezaji huyo aliyekuwa
tegemeo kubwa la ushambuliaji kwa timu yake. Hivyo, akaachiliwa, lakini bado
maji yakawa mazito kwa Sunderland.
Ukiondoa
rafu za hapa na pale zilizojitokeza mara kwa mara, mchezo ulikuwa wa kuvutia
ambapo timu zote zilipigana kiume ingawa hatma ya yote Yanga walitoka kifua
mbele wakiwa na ushindi mkubwa uliowachukua Sunderland (baadaye Simba) karibu
miaka 10 hadi mwaka 1977 walipokuja kulipa kisasi kwa kushinda kwa magoli 6-0,
kipigo ambacho kinaelezewa kuwa kilitokana na Yanga kuwa ndio kwanza imetoka
kwenye mgogoro mkubwa uliopelekea kufukuzwa kwa wachezaji wake wazoefu wote,
hivyo kuingia uwanjani ikiwa haijatengemaa sawa sawa kwa mikiki mikiki ya ligi.
Katika
dakika ya 10 ya mchezo huo, Omari Kimimbi wa Sunderland aliumia baada ya
kugongana na golikipa wa Yanga, Elias Michael, katika harakati za kuwania
mpira. Kama utakumbuka vyema, mwaka 1974 kwenye mchezo mwingine wa ligi kati ya
timu hizo mbili, golikipa Elias Michael wa Yanga na marehemu Willy Mwaijibe wa
Sunderland waligongana kiasi cha kulazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando mjini Mwanza kwa matibabu ya haraka. Pambano hilo lilifanyika kwenye
Uwanja wa Nyamagana.
Karamu ya
magoli ya Yanga katika mchezo wa Juni Mosi, 1968 ilianza kwenye dakika ya 18
pale Durban wa Sunderland alipounawa mpira kwenye mstari wa goli alipokuwa
akijaribu kuokoa huku golikipa wao, Mbaraka Salum akiwa ‘amekwenda marikiti’.
Kufuatia kitendo hicho cha kuunawa mpira, Yanga ilipewa penati ambayo Maulid
Dilunga hakufanya makosa kuzitikisa nyavu za Sunderland kuandika goli la
kwanza.
Jitihada
zote za Sunderland kusawazisha goli hilo hazikuzaa matunda, kwani ukuta wa
Yanga ulisimama imara. Alikuwa ni Dilunga tena, ambaye siku hiyo ‘control’ yake
ya mpira haikuwa na mpinzani, aliyeandika goli la pili kufanya timu ziende
mapumziko huku Yanga ikiongoza kwa magoli 2-0.
Kwenye
kipindi cha pili, Salehe Zimbwe alifungua kitabu cha magoli kwa kupachika goli
la tatu kwa Yanga kwa mpira wa kichwa baada ya kumvisha kanzu golikipa wa
Sunderland, Mbaraka Salum. Sunderland walicharuka baada ya goli hilo, lakini
Emmanuel Mbele ‘Dubwi’, Saidi Abdallah ‘Walala’, Adamu Athumani na Hamisi
Kilomoni walikosa nafasi za wazi kabisa katika kile kilichoonekana kama ‘Sikio
la kufa halisikii dawa’.
Vibao vya
magoli viliendelea kusomeka 3-0 hadi zikiwa zimesaliwa dakika nne tu Sunderland
waliporuhusu magoli mawili ya haraka haraka. Kwenye dakika ya 87 Dilunga
alimmegea krosi nzuri Kitwana Ramadhani Manara aliyeachia kombora safi na
kufunga goli la nne kwa Yanga kabla Salehe Zimbwe naye hajaipangua ngome ya
Sunderland na kuweka mpira kimiani kufanya kitabu kifungwe huku Yanga ikijidai
na ushindi wa magoli 5-0, ambao hawajaukaribia tena hadi hii leo katika mechi
dhidi ya watani wao wa jadi.
Kwa kuwa
dakika zilikuwa chache, Yanga walianza mchezo wa mzaha na maonyesho (show-game)
ili kuvuta muda. Wachezaji wa Sunderland walikatishwa tamaa na kuudhika sana.
Katika mzaha wao, Yanga walikuwa wanakokota mpira kutoka golini kwa wapinzani
wao hadi golini kwao na kumpasia mlinda mlango wao Elias Michael. Naye
aliurudisha mpira kwa wachezaji wa ndani, ambao walifanya dhihaka kwa wachezaji
wa Sunderland huku wakicheka na kufunga soksi au kufanya kama wanavua jezi au
kaptura zao.
Wakati
ambapo Emmanuel Mbele na Adamu Athumani wa Simba walionywa kwa mchezo mbaya,
Juma Bomba wa Yanga aliumia kwenye kipindi cha pili na kupelekwa hospitali kwa
matibabu huku Twaha Masimenti akiingia kuchukua nafasi yake. Mechi
ilisimamishwa kwa dakika tano wakati mashabiki walipovamia uwanja lakini FFU
walizima vurugu hizo na mchezo kuendelea.
YANGA: Elias Michael, Kitenge Said, Hamisi Mnubi,
Athumani Kilambo, Omari Kapera, Gilbert Mahinya, Awadh Gessan/Leonard Chitete,
Juma Bomba/Twaha Masimenti ‘Bryson’, Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Salehe
Zimbwe.
SIMBA: Mbaraka Salum, Yusuf Salum, Ally Durban, Hamisi
Kilomoni, Adam Athumani, Mussa Libabu, Omari Kimimbi, Emmanuel Mbele, Arthur
Mambetta, Saidi Abdallah ‘Walala’, Ally Wage ‘Kajo’.
Mwamuzi
alikuwa Bwana Banda kutoka Zambia, na alisaidiwa na washika vibendera Marijani
Shaaban Marijani na Ramadhan Kahabuka wa Dar es Salaam.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye muswada wa kitabu cha 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA
YANGA' cha mwandishi Daniel Mbega, ambacho kiko katika hatua za mwisho
kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com
No comments:
Post a Comment