Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Profesa Sifuni Mchome akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu
ya upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi
na ufaulu leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Elimu Profesa
Eustella Bhalasesa.
Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome (hayupo
pichani).
Waandishi wa habari na maafisa wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome(hayupo pichani). Picha zote na Eliphace Marwa (MAELEZO)
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA
UFUNDI
UPANGAJI
WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU
UTANGULIZI
Wizara imekusanya
maoni ya Wadau wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges)
katika Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya
Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha
ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu
sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika
mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja
na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala
mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti
ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa
kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.
Muundo wa Kwanza
ni upangaji wa viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade
Ranges) zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41
– 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na
umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.
Muundo wa Pili ni
wa viwango vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya
mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible
grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika
badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini
kuanzia mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando
(Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama mgando ambapo: A
= 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa upande wa
Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 –
74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza
haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu ya malalamiko katika sekta
ya elimu na mafunzo.
Vilevile, Sera ya
Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha
ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho
utachangia asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na
mtihani wa mwisho asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi
kuutumia mifumo hii tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na
mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa
watahiniwa wa kujitegemea (private
candidates). Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa
yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu
ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini
anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.
Kwa mantiki hii,
Wizara imedhamiria kufanya harmonization
ya masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita ili
kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya sekondari. Lakini
pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi katika ngazi
mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo
inahuishwa mara kwa mara ili iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika
ngazi mbalimbali.
VIWANGO
NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA
MWAKA 2014 KIDATO CHA SITA
Baada ya
kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa
katika maamuzi kuhusu makundi ya alama na muachano wake:
a)
Alama zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana, isipokuwa
tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na muachano
tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.
b)
Makundi ya alama hayatakuwa na clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta
tija katika kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa
mantiki hii
(i) makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters mbili.
Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka 59 na
litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50 hadi 59 na
kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).
(ii) Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 kama jedwali
linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka
mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado
wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna haja ya
kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili
kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika
kundi hili.
(iii) Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama 20 kama jedwali
linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni mwanafunzi aliyepata
alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa chini kabisa au hafifu kwa
kiwango cha alama D na ingawa
ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha. Alama F ilikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia alama 20 hadi 29 na D – 30 -39.
Lengo la muundo huu ni kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache,
zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea badala ya kuanzia kwenye
moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo
unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo
za elimu msingi na sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.
c)
Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato
cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0 hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu
limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya
mwanafunzi kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo
zitakatumika
(i) Alama A itakuwa na
maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion
or outstanding performance),
(ii) Alama B+ itakuwa na
maana ya ufaulu bora sana (excellent
performance),
(iii) Alama B itakuwa na
maana ya ufaulu mzuri sana ( very good
perfomance),
(iv) Alama C itakuwa na
maana ya ufaulu mzuri (good performance);
(v) Alama D itakuwa na
maana ya ufaulu wa wastani (low
performance),
(vi) Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii) Alama F itakuwa na
maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory
performance).
Wataalamu
katika maeneo mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na
Wizara, watatoa maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana
pia na mahitaji yao.
d)
Alama C iwe ndiyo
alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na E ni alama za ufaulu unaohitaji
urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na masomo ili kuthibitisha
kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya eneo husika (targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi
huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia
katika ulimwengu wa kazi.
e)
Makundi ya alama yatajumuisha CA kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia
isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private candidates). Hii ni kwa
kuzingatia kwamba CA siyo vizuri
izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.
f)
CA kwa upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili
(alama 15), matokeo ya Kidato cha Tatu
(alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama
10) na kazi mradi au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato
cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo
unaotumika sasa.
g)
CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa
kujitegmea ambao wanarudia Mitihani, CA zao zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake
ya mitihani ya awali. Kwa watahiniwa wa
kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya QT yatumike
kama CA na mtihani wa mwisho uchangie
alama 60.
h)
Kwa vile alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi
wa Kidato cha Nne tayari zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40
katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013.
i)
Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA)
utaandaliwa na kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa
kuhusu muundo huo ili wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya
sekondari.
j)
Muundo huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa
miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya
changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii ya muda
itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya
sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza
ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo
la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.
Kwa mantiki
hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa
chini:
Jedwali Na 1
MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU
ALAMA
|
UWIGO WA ALAMA
|
IDADI YA ALAMA
|
TAFSIRI
|
A
|
75 - 100
|
26
|
Ufauli Uliojipambanua
|
B+
|
60 - 74
|
15
|
Ufaulu bora sana
|
B
|
50- 59
|
10
|
Ufaulu mzuri sana
|
C
|
40 - 49
|
10
|
Ufaulu mzuri
|
D
|
30 - 39
|
10
|
Ufaulu Hafifu
|
E
|
20 - 29
|
10
|
Ufaulu hafifu sana
|
F
|
0 - 19
|
20
|
Ufaulu usioridhisha
|
Kwa aina hii
ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau
kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika kipindi hiki mpaka wakati huo,
muundo wa madaraja utakuwa kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 2 hapa chini.
Jedwali Na 2
MUUNDO WA MADARAJA
MUUNDO WA ZAMANI
|
MUUNDO MPYA
|
MAELEZO
|
||
POINTI
|
DARAJA
|
POINTI
|
DARAJA
|
|
7-17
|
1
|
7-17
|
I
|
Kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana
|
18-21
|
II
|
18-24
|
II
|
Kundi la ufaulu mzuri sana
|
22-25
|
III
|
25-31
|
III
|
Kundi la ufaulu mzuri na wa wastani
|
26-33
|
IV
|
32-47
|
IV
|
Kundi
ufaulu hafifu
|
34-35
|
0
|
48-49
|
V
|
Kundi
la ufaulu usioridhisha
|
Wataalamu
wa mifumo ya mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili
liweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri
linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo
litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika ufaulu.
HITIMISHO
Mabadiliko
haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi
taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako mambo mengi
mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala,
walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa
vingine muhimu katika elimu. Masuala haya yanaendelea kuangaliwa kupitia
mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN). Ushirikiano wa
wadau wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara
itaendelea kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia
wanaombwa wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo lolote
ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata mafanikio katika
sekta ya elimu.
Imetolewa,
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA
UFUNDI
No comments:
Post a Comment