Naibu Waziri
wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki akisisitiza umuhimu wa kutoa adhabu
mbadala kwa watuhumiwa baada ya hukumu zao kukamilika alipokuwa anaongea na
watumishi wa Mahakama ya Mwanzo ya Kerege (hawapo pichani) iliyopo Wilayani
Bagamoyo mkoa wa Pwani kwenye ziara yake ya siku moja wilayani humo. Wa kwanza
kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa PwaniBahati Ndeserua, wa kwanza
kushoto ni Msajili Mahakama kuu, kanda ya Dar es salaam Projestus Mhagama.
Hakimu
Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo Liadi Mohamed Chamshama akimwonesha Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki (mwenye gauni kitenge) na ujumbe
wake eneo la mahakama ya Mwanzo ya Kiwangwa alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya
siku moja wilayani mkoa wa Pwani. (Picha zote na Eleuteri
Mangi- Maelezo).
Na Eleuteri Mangi
-MAELEZO
Serikali imewataka
watumishi wa Mahakama nchini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia weledi, sheria,
kanuni, taratibu, misingi ya kazi na maadili ya utumishi wa umma ili waweze
kufikia malengo yao ya kazi katika kutenda haki kwa wateja wao.
Wito huo ulitolewa hivi
karibuni na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki alipokuwa katika ziara
ya kikazi ya siku moja wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Naibu Waziri Kairuki
aliwataka watumishi hao wafikie malengo yao ya kazi kwa kuzingatia ushirikiano
baina yao na wadau wengine wa mahakama, lengo ni kufanikisha utendaji wao wa
kazi.
“Mnapimwa kwa kupunguza
mrundikano wa mashauri mliyonayo, ni
vema muwe na mkakati wa kuyapunguza au kuyamaliza kwa wakati mashauri hayo na
kutenda haki kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, misingi ya kazi na
maadili ya utumishi wa umma” alisema Kairuki.
Aidha, Naibu Waziri Kairuki aliwaasa watumishi
wa mahakama kutojihusisha na rushwa wakati wote wanapokuwa wakitekeleza
majukumu yao ili wananchi waendelee kuwaamini.
“Kila mmoja wenu awe ni
mwangalizi mzuri na balozi wa mwenzake, mfanye kazi kwa kushirikiana ili haki
itendeke”, alisema Kairuki
Naibu Waziri huyo aliendelea
kusisitiza “kwa yeyote mwenye tabia ya kujihusisha na rushwa aache mara moja na
atambue kuwa yeye ni mtumishi wa umma”
Watumishi
wanapojiingiza kwenye rushwa mara zote hawazitendei haki familia zao, taaluma zao
na wateja wao ambao ndio wanaotegemea kupata haki kupitia watumishi wa mahakama
mahalia.
Kwa upande wake Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo Liadi Chamshama alimwahidi
Naibu Waziri Kairuki kwa niaba ya watumishi wa mahakama zilizo chini yake kuwa
watatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu, misingi ya kazi
na maadili ya utumishi wa umma.
Pia Hakimu Chamshama
aliwaasa watumishi wa mahakama hizo waelewe kuwa watapata heshima na kuaminiwa
na wananchi pale ambapo mahakama haitakuwa na upendeleo na kuzingatia sheria na
maadili ya kazi na taaluma.
Idara ya Mahakama
nchini inakabiliwa na changamoto ya kuwa na miundo mbinu na majengo ya mahakama
machakavu yaliyoanzishwa muda mrefu uliopita pamoja na uhaba wa watumishi wa
kada mbalimbali wakiwemo wapiga chapa.
Kwa sasa Serikali ipo
kwenye mpango na utaratibu wa maboresho ya Mahakama zote nchini ambapo mwaka
huu wa fedha 2013/14 zinatarajiwa kujengwa Mahakama za Wilaya sita (06) na
Mahakama za Mwanzo 12.
Katika ziara hiyo ya
kikazi ya siku moja Naibu Waziri Kairuki alitembelea Mahakama ya Wilaya ya
Bagamoyo na Mahakama za Mwanzo sita ambazo ni Kerege, Mwambao, Kiwangwa, Msata,
Msoga-Lugoba na Chalinze.
No comments:
Post a Comment