Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday, 17 October 2013

KING ENOCH ALIYETAMBA DAR JAZZ HADI SIKINDE

King Michael Enoch (wa pili kutoka kushoto mwenye gitaa) akiwa na kikosi cha Dar Jazz mwaka 1968. Picha kwa hisani ya Kijiwe cha Kitime.

Na Daniel Mbega
WENGI walimwita Teacher, yaani ‘Mwalimu’, na wengine wakamwita King, yaani ‘Mfalme’. Inawezekana kabisa alikuwa mwalimu kweli kutokana na kuusomea muziki tangu akiwa shule ya msingi, lakini Michael Enoch Chinkumba hakuwa mfalme, na kama ni mfalme basi hakuwa na Dola.
Ndiyo, mwanamuziki huyo mkongwe kabisa katika historia ya muziki wa Tanzania, hakuweza kujivunia matunda ya kazi yake tangu alipoanza muziki mwaka 1958, lakini pia aliweza kujivunia wanamuziki wengi waliopitia mikononi mwake hasa katika kipindi cha miaka ya 1960 wakati upinzani wa bendi za Dar es Salaam Jazz na Western Jazz ulipokuwa umechukua chati ya juu.
Nilizungumza naye katika mahojiano maalum enzi ya uhai wake mwaka 2000 nyumbani kwake Mwenge jijini Dar es Salaam ambapo King Enock alieleza bayana kwamba, si yeye tu, bali wanamuziki wengi wa enzi zake wamekufa na wengine wanaendelea kuwa maskini wa kutupwa kutokana na kushindwa kunufaika na jasho lao hasa katika kipindi hicho ambapo walitunga nyimbo na kuzirekodi Shirika la Utangazaji la Tanganyika (TBC baadaye Redio Tanzania Dar es Salaam, au RTD na sasa TBC Taifa).
Mwanamuziki huyo alisema kwamba, kutokana na kutorekodi kanda nyingi kwa ajili ya mauzo, wanamuziki wengi wa enzi hizo wameshindwa kunufaika na jasho lao, kauli ambayo ilijidhihirisha kutokana na mazingira aliyokuwa anaishi huku akiwa amepooza, hali aliyokuwa nayo ilisikitisha ukilinganisha na yale mema aliyoyafanya katika maendeleo ya fani hiyo na kwa hakika alikufa maskini.
Ingawa wakati huo King Enoch alisema hali yake haikuwa mbaya sana, lakini kwa kweli ungemhurumia mzee huyo, ambaye Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC) lililokuwa linamiliki bendi ya Mlimani Park Orchestra lilikuwa likimhudumia kwa kadiri ya uwezo wake. Kwa ujumla lilikuwa linauthamini na kuujali mchango wake.
Yeye mwenyewe alikiri kwamba, miaka 44 aliyokaa kwenye muziki hajanufaika na chochote zaidi ya kufa maskini, na hasa baada ya kupata maradhi ya kiharusi mwaka 1989.
"Sikutegemea kuwa hivi, lakini ukweli ni kwamba, jasho letu limepotea kweli katika miaka ya nyuma kwa kuwa hakukuwa na kitu chochote kilichotulinda. Kazi zetu nyingi ziliwanufaisha wengine na sisi tulikuwa tukiimba kwa kujiburudisha tu.
"Sasa wenzetu wanaoinukia ndio wanaoweza kunufaika na matunda ya jasho lao...wanarekodi na kuuza kanda zao, lakini sisi tulitunga nyimbo na kuzipeleka Radio Tanzania Dar es Salaam, ambako hazikurekodiwa kwa kusambazwa kibiashara, bali zilikuwa zikitumika kuburudisha katika vipindi mbalimbali," alisema katika mahojiano hayo.
Mwanamuziki huyo mzaliwa wa Luansha, Zambia mnamo Oktoba, 1942 kutoka kabila la Wawemba, alikufa akijivunia mambo mengi aliyoyafanya katika muziki tangu alipokuja nchini Tanzania mwaka 1960.
Mkongwe huyo ndiye aliyeiongoza vyema Dar es Salaam Jazz na baadaye Dar es Salaam International kabla ya kuanzisha Mlimani Park Orchestra mwaka 1978.
King aliuzungumzia muziki wa zamani na wa sasa, akisema tungo za sasa zinalipuliwa, hazipangiliwi na hata midundo inakolezwa na madoido mengi ya nje, hali ambayo inaweza ikawa na mwisho mbaya kwa nyimbo, bendi zenyewe na hata watunzi wenyewe.
Alisema, ingawa yeye alisomea muziki tangu miaka ya 1950, lakini wakati walipotaka kwenda kurekodi RTD mashairi yao yalipitiwa upya na wakati mwingine kurejeshwa kwenye bendi kwa ajili ya marekebisho, hali ambayo, ingawa ilikuwa ya ukiritimba, lakini iliboresha tungo nyingi.

TANGU SHULE YA MSINGI...
King Enoch alikuwa na kipaji cha muziki tangu utoto wake, kwani nyakati za mapumziko nyumbani alikuwa akijishughulisha kutengeneza gitaa la makopo na kufunga nyuzi nyembamba kisha kuanza kupiga.
Kwa bahati nzuri kaka yake Steven alikuwa amenunua gitaa la Galatone, na rafiki yake mwingine Boston Masatunya naye kaka yake alimnunulia gitaa aina ya Gibson, ambalo lilikuwa la bass.
Kutokana na mapenzi yao ya muziki, wakati wakiwa shule ya msingi Luansha walikomaliza mwaka 1958, wakaanza kupiga muziki wa maonyesho nyakati za usiku hasa mwisho wa wiki, ambapo kikundi chao kilichojulikana kama Music Brothers Concert Group kilikuwa na akina dada watatu Adesi, Rhoda na Pani, na rafiki yao mwingine Godwin alikuwa akipiga drums.
Aliendelea na kikundi hicho, lakini mwaka uliofuata akina dada hao wakaanza kuchumbiwa na kuolewa, naye Enoch, akiwa kiongozi, akaamua kujiunga na bendi kubwa iliyojulikana kama Luansha Band.
Mnamo mwaka 1960 aliyekuwa mdhamini wa TANU, marehemu John Mwakangale, alikwenda Zambia na baada ya kuona uwezo wa kijana Enock akawaambia wadogo zake Godfrey na Elias, aliyekuwa DC wa Mbeya, wanunue vyombo na kumchukua mwanamuziki huyo.
Bendi hiyo ikaundwa kwa jina la Three Brothers Band kwa lengo la kutoa upinzani dhidi ya Mbeya Jazz, ambapo ilikuwa na wanamuziki wageni tupu; Wazambia Michael Enoch, Boston Masantunya, Saizi na Godwin, Wamalawi John na Felix na Wazimbabwe John Tagoma, Mwasibanda na Thomas.
Lakini mwaka huo huo baada ya kufanya maonyesho Mbeya, Chunya, Tabora na Mwanza, bendi hiyo ikafa, tena kifo kibaya sana.
"Tuliibiwa vyombo vyote vya muziki mjini Mwanza wakati tukijiandaa kwenda kupiga mjini Musoma… tulipakia vyombo kwenye Canter moja, dereva akasema kwamba, nisubirini nikajaze dizeli kwenye gari, lakini kumbe alikuwa mwizi, akatokomea na vyombo," alikumbuka kwa masikitiko.
Hata hivyo, bahati bado ilikuwa upande wake, kwani aliazimwa na bendi ya Cuban Tabora kwa ajili ya maonyesho kadhaa huko Nzega, na wakati huo huo mwanamuziki mmoja wa Dar es Salaam Jazz, Bilimi Ally, alikuwa amefika Nzega akiwa njiani kwenda Ukerewe, Mwanza kumfuata mpiga solo wao Ausi.
Baada ya kumuona akipiga solo vizuri, aliamua kurudia hapo, akafanya mazungumzo naye, na baada ya King Enoch kuruhusiwa na wenyeji wake akina Godfrey Mwakangale, akapanda treni kuja Dar es Salaam pamoja na Mzambia mwenzake Saizi aliyekuwa akipiga saxophone.
Dar Jazz ilikuwa ikimilikiwa na Mzee Muba (Mndengereko), ambapo waimbaji walikuwa Hamisi Nguru, Bilimi Ally, Ally 'Chongo', Shaaban Mangano (solo), King Enoch (solo), Nassoro (tumba), Edward Salvi (sax), Gray Sindo (sax) na Saizi (sax). Baadaye Juma Akida akaongeza nguvu katika uimbaji.
Mwaka 1968 ulishuhudia kujiunga kwa wanamuziki wengine kama waimbaji Issa Ntini na Omar Seya, Makwaya Sudi (bass), Meckline Ibrahim (rhythm), Ramadhan (solo namba 2), Kulwa Thomas (drum), Zimataa (tumba), Majengo Selemani (sax), Albino (sax) na Abdallah Kimeza (sax).
Wakati huo bendi ilikuwa ikitamba na nyimbo kama Dada twende tukalime, Mbuzi, Kama kisu utajichoma mwenyewe, Dada karibu kwetu, Heko Mwalimu Nyerere, Haifai kusimama juu ya milima, Haya yote ni ya dunia, Nitawaachia wenzangu na Mary Kamata zilizokuwa katika mtindo wa Mundo ambazo zilitungwa na Michael Enoch, na Juma Akida naye aliibuka na nyimbo za Mtoto acha kupiga mayowe na Michael Hapendi Ugomvi, ambazo zilirekodiwa RTD.
Mwaka 1972 wakaenda kurekodi nchini Kenya nyimbo za Kama Kisu Utajichoma Mwenyewe, Mbuzi, Lydia Umenitoroka na Mary Kamata katika studio za Chandarana, lakini mwaka huo bendi hiyo ikapata pigo baada ya mmiliki wake Mzee Muba kufariki dunia.
Hussein Kawambwa (Mzaramo) akaanza kuiongoza bendi hiyo, ambayo sasa ikaongezewa nguvu na ndugu wawili Saulo Ndumbaro (bass) na Duncan Ndumbaro (rhythm), mwimbaji Hamisi Abdallah, wapiga saxophone Mathias, Komsoni na Abeid na mpiga tumba Ramadhan Shomvi, na ilikuwa ikitumia mtindo wa Pachanga.
Mambo hayakuwa mazuri kutokana na uchakavu wa vyomo, na mwaka 1978 akatoka na kuanzisha bendi ya Dar International iliyokuwa ikimilikiwa na Zakaria Ndabamei, Mrundi aliyekuwa akiishi Tanga, ikiwa na mtindo wa Super Slow.
Miongoni mwa wanamuziki waanzilishi walikuwa Marijani Rajabu Marijani, Cosmas Thobias Chidumule, Ally Rajabu, Salehe ‘Belesa’ Kakere, Mzambia mwenzake Joseph Mulenga ‘String Master’ (bass), Abel Baltazar kutoka NUTA Jazz (solo), Michael Enoch (sax), Abdallah Gama (rhythm), Haruna Lwari (tumba), Saidi (drum), Joseph Bernard (sax), Machaku Salum (trumpet), Ibrahim Mwinchande (trumpet) na Betto Julius (trumpet).
Bendi hiyo ikaibuka na vibao vitano; Rufaa ya Kifo kilichotungwa na Cosmas Chidumule na kuimbwa na Marijani Rajabu, Nyerere Baba Mlezi (Joseph Mulenga), Margreth msikilize shangazi (Kakere Belesa), Sikitiko (Marijani) na Mwana rudi wee (Joseph Mulenga).
Bendi hiyo, hata hivyo, ilidumu kwa miezi miwili tu kisha ikafa baada ya kutoelewana na mmiliki wake. Wanamuziki wote (isipokuwa Marijani Rajabu) wakaondoka kuanzisha Mlimani Park Orchestra iliyokuwa inamilikiwa na Tanzania Transport & Taxes Services - TTTS.
Wanamuziki wengine waliokuja kuanzisha Mlimani Park ni Muhidini Maalim Gurumo, Hassan Rehani Bitchuka, Juma Hassan 'Town', Selemani Mwanyiro na Abdallah Omar 'Dullah' wote kutoka Msondo Ngoma.
Wakaibuka na nyimbo tatu za kwanza ambazo zilikuwa Celina (Joseph Mulenga), Barua kutoka kwa mama (Chidumule) na Kassim Kafilisika (Gurumo).
King Enoch alidumu na bendi hiyo kwa miaka yote mpaka mauti yalipomfika mwaka 2004, na ingawa katika siku za mwisho hakuwa na uwezo wa kupanda jukwaani kuimba, lakini alikuwa akihudhuria mazoezi pale DDC Mwenge na kupangilia muziki. Bendi ilikuwa inamthamini na kumpatia matibabu na mshahara wake kama kawaida.
Hakubahatika kuoa, lakini alipata kuzaa watoto wawili, mmoja bahati mbaya alifariki, na wa pili Iddi Enoch (ambaye kwa sasa atakuwa na miaka 31) alikuwa akiishi Manzese na mama yake.
"Ndugu zangu hapa Tanzania ni Watanzania wote, kwa kuwa nimeondoka kwetu Zambia miaka 42 iliyopita na sijakwenda tena mpaka leo. Wazazi wangu kule walikufa wakati nikiwa shule ya msingi na ndugu zangu kila mmoja yuko kivyake... naishukuru sana Sikinde kwa kunithamini mpaka leo hii," alipata kunieleza.
Huyo ndiye King Enoch, mwalimu aliyewatengeneza wanamuziki wengi Tanzania.

No comments:

Post a Comment