Rais wa Sudan, Jenerali Gaafar Mohamed el-Nimeiry akisalimiana na wachezaji wa Taifa Stars. Hapa anasalimiana na Hassan Gobbos 'Wa Morocco' na kushoto kabisa ni beki mstaarabu Mohammed Chuma. Anayemtambulisha kwa wenzake ni nahodha wa Stars Abdulrahman Juma. Mwingine pichani ni Kitwana Manara na anayeonekana uso wake ni Abdallah Kibadeni.
Na Daniel Mbega
KATIKA historia ya soka Tanzania kuna mambo ya
kufurahisha kutokana na matoeo ya timu zetu uwanjani kama kufuzu kwa fainali za
Mataifa ya Afrika 1980 na kuna mambo ya kusitikisha kama Simba kushindwa kutwaa
Kombe la CAF mwaka 1993.
Hata hivyo, kuna mambo ya kufedhehesha ambayo
hayasimuliki. Mambo haya, ni afadhali yatokee kwetu wenyewe, lakini yanapotokea
mbele ya wageni aibu yake haifutiki kirahisi.
Tukio la Taifa Stars kucheza vifua wazi mbele ya marais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Jenerali Gaafar Mohamed el-Nimeiry wa Sudan mwaka 1972 lilikuwa na fedheha kubwa.
Tukio la Taifa Stars kucheza vifua wazi mbele ya marais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Jenerali Gaafar Mohamed el-Nimeiry wa Sudan mwaka 1972 lilikuwa na fedheha kubwa.
Ndiyo maana, waliokuwa kwenye jukwaa kuu
waliwahi kunidokeza kilichotokea katika mzungumzo baina ya Mwalimu Nyerere na
Nimeiry. Inaelezwa kwamba, baada ya timu kujipanga uwanjani huku wachezaji wa Taifa
Stars wakiwa vifua wazi, Nimeiry alimtania Mwalimu na kusema: “Ndugu yangu,
yaani umefilisika kiasi kwamba hata wachezaji wako hawana jezi?” Mwalimu naye
akamjibu: “Wewe subiri, tutawafunga tu…” Ulikuwa ni mzaha, lakini naamini
Mwalimu Nyerere na Watanzania kwa ujumla – japo hawakusikia mazungumzo hayo –
walifedheheka mno.
Mechi hiyo iliyochezwa Julai 4, 1972 kwenye
Uwanja wa Taifa (sasa Shamba la Bibi) ulikuwa wa kuadhimisha sherehe za Saba
Saba ambapo timu kadhaa, ikiwemo Nigeria, zilikuwa zimealikwa.
Zamani ulikuwa ni utamaduni wa kawaida kwa timu
za soka za taifa kualikwa kwenye sherehe mbalimbali za kitaifa kwa mataifa ya Afrika.
Kilichotokea siku hiyo, kwa mujibu wa
waliokuwepo, ni kwamba mtu aliyekuwa amepewa dhamana ya kukaa na jezi
alichelewa kufika uwanjani. Unajua zamani jezi za timu – iwe klabu au timu ya
taifa – zilikuwa ni pea moja na alikabidhiwa mtu maalum kwa ajili ya kuzitunza.
Mtu huyo alifika uwanjani wakati tayari mchezo ukiwa unaendelea, hivyo ikabidi
abaki na furushi lake mpaka kipindi cha kwanza kilipomalizika. Stars waliingia
uwanjani kipindi cha pili wakiwa wametinga jezi hizo.
Hata
hivyo, katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Gration Matovu, Stars
waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 ambayo yalipatikana kipindi cha pili kupitia
kwa Gibson
Sembuli (dakika za 65 na 68) na Abdallah Kibadeni 79.
Stars, ambayo ilikuwa inanolewa na Pak Jung
Yang wa Korea aliyesaidiwa na Marijani Shaabani Marijani (kaka yake Marijani
Rajabu Marijani kwa baba mkubwa na mdogo), siku hiyo iliwakilishwa na Omar Mahadhi, Juma Mzee, Mohammed Chuma, Hassan Gobbos, Omar Kapera (nahodha),
Nassoro Mashoto, Abdallah Kibadeni, Abdulrahman Juma, Kitwana Manara, Willy
Mwaijibe/Gibson Sembuli, Isihaka Marande/Muhaji Mwabuda, Kassim Manga.
Sudan yenye
ilikuwa na wachezaji mahiri wakati huo kama Zughbeir, Kaunda, Gadaura, Najru,
James, Mohsin, Bushara, Bushra, Isaid, Hasab, Dehiesh, Kamar.
Hii
ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuifunga Sudan kati ya mechi tatu
walizopata kucheza. Mara ya kwanza walikutana kwenye Kombe la Saba saba Julai
5, 1964 mjini Dar es Salaam na Tanzania ikafungwa 3-1, bao la Tanzania
lilifungwa na Abdulrahman Lukongo katika dakika ya 43 wakati yale ya Sudan
yalifungwa na Abo Eskandar (dakika ya 15 na 78 kwa penati) na Tigani dakika ya
22. Siku hiyo Tanzania iliwakilishwa na Maganga, Mathias Samuel Kissa (nahodha), Hamisi
Fikirini Nkwabi ‘Liston’, Mbwana Abushiri, Abdulrahman Lukongo, Chaki, Mtumwa
Mgeni, Hamis Kilomoni, Abdullah Aziz.
Mara
ya pili ilikuwa kwenye nusu fainali ya Kombe la Gossage Februari 21, 1967
ambapo Tanzania ililala kwa bao 1-0.
Kikosi
cha Taifa Stars wakati huo kilikuwa imara kwani kiliweza kutoka suluhu na
Nigeria Julai 6, 1972 katika mchezo mwingine wa Kombe la Saba Saba. Nigeria ilikuwa
inafundishwa na Dan Anyim na ilikuwa na wachezaji hatari kama nahodha Godwin
Achebe, Otarekhua, Olayambo na Mathias Obianika.
Huko nyuma Stars ilikuwa imezifunga Lesotho na
Mauritius mabao 4-1 kila moja katika michuano ya awali ya Michezo ya Afrika
(All African Games).
Fedheha kama hiyo ilijirudia tena Oktoba 9,
2010 wakati wa mechi kati ya Taifa Stars na Morocco kuwania kufuzu kwa fainali
za Kombe la Mataifa Afrika. Safari hii halikuwa suala la jezi, bali Rais Jakaya
Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi alishikwa na fedheha pamoja na Watanzania wote baada
ya nyimbo za taifa kushindwa kupigwa kwa maelezo kwamba CD za nyimbo hizo ‘ziligoma’.
Wakati watu
wote wamesimama na timu zimejipanga kusubiri nyimbo za taifa kabla ya kuanza
mchezo huo ambao Morocco ilishinda 1-0, hakuna kilichosikika, ghafla mashabiki
wa Yanga wakaanza kuimba: “…Mungu Ibariki Yanga…”.
Hali hiyo
ilifanya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumsimamisha
kazi msemaji wake, rafiki yangu Florian Kaijage, kwamba ndiye aliyepaswa
kuhakikisha kila kitu kipo sawa. Akawajibishwa kwa makosa ya wengine.
No comments:
Post a Comment