Mwalimu Nyerere akiwa na Waziri Mkuu wake, Edward Moringe Sokoine
Na Daniel Mbega
KAMA kuna kitu
ambacho Mwalimu Nyerere alikiabudu – mbali ya Mungu kupitia katika imani yake
ya Kikatoliki – ni Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyozaliwa ndani ya Azimio
la Arusha, ambayo aliendelea kuihubiri na kuitetea kwa nguvu zake zote hadi
kikomo cha uhai wake.
Kila alikokwenda daima alitembea na Biblia pamoja na Azimio la Arusha, akiamini kwamba misingi ambayo TANU iliiweka kwenye azimio hilo Februari 5, 1965 pale Arusha ilikuwa mizuri na ingeendelea kuwa mizuri ikiwa tu Watanzania wangemwelewa dhamira yake.
Kila alikokwenda daima alitembea na Biblia pamoja na Azimio la Arusha, akiamini kwamba misingi ambayo TANU iliiweka kwenye azimio hilo Februari 5, 1965 pale Arusha ilikuwa mizuri na ingeendelea kuwa mizuri ikiwa tu Watanzania wangemwelewa dhamira yake.
Azimio la
Arusha lililohimiza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea bado liko katika maandiko,
ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa kwa sasa ni nadharia
tu na si vitendo.
Hii inatokana
na azimio hilo ‘kuuawa’ na Azimio la Zanzibar la mwaka 1991, ambalo lilileta
‘Soko Huria’ enzi za Awamu ya Pili ya uongozi chini ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi,
ambaye alitoa ruksa kwa kila kitu, zikiwemo nguo za mitumba (maarufu wakati huo
kama ‘kafa Ulaya mazishi Bongo’).
Soko huria hili
likatafsiriwa vibaya na watu wengi, wakiwemo watumishi wa umma ambao enzi zile
za Mwalimu na siasa yake ya ujamaa na kujitegemea walijiona wameminywa, sasa
wakaachana hata na misingi ya utawala bora na maadili ya uongozi wa umma,
pamoja na miiko ya viongozi, na kuamua kujilimbikizia mali kadiri walivyotaka
kwa kutumia nyadhifa zao, jambo ambalo TANU, na baadaye CCM, ililikemea kwa
nguvu zote.
Kwa zaidi ya
miaka 24 chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, Tanzania iliishi chini ya mfumo
wa Ujamaa, siasa ambayo iliweka njia zote kuu za uchumi chini ya umiliki wa
umma, ambapo wengi wanasema hali hiyo ndiyo ilichelewesha maendeleo kwa
Tanzania.
Rais mstaafu wa
Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, alikaririwa Julai 2008 akisema kwamba
ujamaa ulikuwa hautekelezeki.
Ujamaa ni siasa
nzuri lakini unapingana na uasili wa binadamu. Watu, wakati wote wanapenda kuwa
matajiri. Hawataki kuwa maskini kwa maisha yao yote. Msingi mmoja wa ujamaa ni
kwamba kusiwepo na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini, pengo ambalo sasa
tunalishuhudia huku wachache wakiwa wamejilimbikizia mali kinyume cha utaratibu
na wakitamani kuendelea kuchota mali za umma na hata kununua uongozi au
madaraka ili waendelee kuifaidi keki ya fursa za kiuchumi huko walio wengi
wakiendelea kuogelea katika ufukara wa kutisha.
Alhaji Mwinyi,
au maarufu kama ‘Mzee Ruksa’, alisema wakati anashika uongozi wa juu katika
miaka ya 1980 bidhaa mbalimbali muhimu zikiwemo sukari, dawa za meno na hata
sabuni zilikuwa adimu.
“Tungeweza
kuendelea na sera ile au kufanya mabadiliko? Ujamaa kweli ulikuwa unafanya kazi
1980? Lakini ukiniuliza kama ujamaa ulikuwa mbaya? Nitakwambia, ni siasa nzuri
duniani. Tatizo lake ni kama ndoto,” alikaririwa akisema siku hiyo ya uzinduzi
wa kitabu chenye maoni ya wakuu 13 wa nchi za Afrika akiwemo yeye mwenyewe na
Rais aliyemfuata Benjamin Mkapa ambapo wanaeleza uzoefu wao.
Ndani ya kitabu
hicho, Mwinyi anasema alikuwa mkuu wa nchi ambaye alitaka kufanya mabadiliko
lakini wakati huo makamu mwenyekiti wa CCM ambacho wakati huo mwenyekiti wake
alikuwa ndiye muasisi wa Azimio la Arusha, Mwlaimu Nyerere.
Itakumbukwa kwamba,
sera na mipango aliyoianzisha Mwinyi ikafuatiwa kwa kasi kubwa na Rais Mkapa
asliyemfuatia, hali ambayo ilidhihirisha kuuzika kabisa ujamaa.
Ingawa hili
lilikuwa dhahiri, lakini hakuna aliyewahi kuthubutu kutoa kauli kwamba ujamaa
umeshindikana wakati Mwalimu Nyerere akiwa hai, hadi baada ya kifo chake mwaka
1999 ndipo tunazisikia kauli hizi kwa uwazi zaidi. Wengi enzi hizo walipenda
kusema chini chini.
Lakini
nakumbuka vyema Mwlimu Nyerere aliwahi kukaririwa na jarida la New
Internationalist, toleo namba 309 la Januari-Februari 1999 (wakati huo akiwa
msuluhishi mkuu wa mgogoro wa Burundi) akisema kwamba ujamaa haukushindwa
duniani, bali haukuwahi kujaribiwa!
Ndiyo! Alikuwa
na kila sababu ya kusema hivyo, kwa sababu hadi wakati huo mataifa makubwa yaliyoasisi
ujamaa yalikuwa yamegeukia ubepari. Sera za ujamaa katika Poland zilikuwa
zimeshindikana, Cuba iliendelea kukabiliwa na upinzani mkubwa na vikwazo vingi
kutoka Mataifa ya Magharibi, Urusi (USSR) ilikuwa imesambaratishwa mwaka 1991
chini ya Rais Mikhail Gorbachev, Ujerumani Mashariki nayo ilikuwa imeungana na
Magharibi mwaka 1990 na ‘kuuvunja ukuta wa Berlin’ uliodumu kwa miaka mingi,
huku Czechoslovakia ikigawanyika na kuzaliwa kwa mataifa mawili – Jamhuri ya
Czech na Slovakia, kama ilivyokuwa kwa Yugoslavia ya zamani iliyozaa Yugoslavia
na Serbia!
Mwalimu Nyerere
alikuwa na lengo zuri tu (kwa maoni yangu) katika kuanzisha Azimio la Arusha,
kama alivyokaririwa akisema; “Bado naendelea kulibeba (azimio) kila niendako.
Kila wakati nasoma tena na tena kuona nini ambacho naweza kukibadili. Labda
nitaboresha katika Kiswahili kilichotumiwa lakini Azimio hili bado linafaa:
Siwezi kubadili chochote. Tanzania ilikuwa imepata uhuru muda mfupi tu lakini
tayari tulikuwa tumeshuhudia pengo kubwa kati ya wenye-nacho na wasio-nacho.
Matajiri walikuwa wameibuka kutoka katika kundi la wanasiasa na maofisa ambao
walikuwa maskini wakati ule wa utawala wa wakoloni, lakini sasa walikuwa
wanatumia madaraka yao ndani ya chama na serikali kujinufaisha. Maendeleo ya
aina hii yangewanyang’anya wananchi madaraka (kama ilivyo sasa). Kwa hiyo
tukaanzisha chombo kipya: tukasema maendeleo ni kwa watu wote na si kikundi
kidogo cha watu,” alisema.
“Azimio la
Arusha ndicho kitu kilichoifanya leo Tanzania iwe Tanzania. Tulisema kile tulichokisimamia,
tukaweka miiko ya uongozi kwa viongozi wetu na tukafanya juhudi kufikia malengo
yetu. Hili lilikuwa dhahiri kwa kila mmoja, hata kama tulifanya makosa – na mtu
anapojaribu kitu fulani kipya na kigeni lazima kuwepo na makosa.
“Azimio la
Arusha na mfumo wetu wa demokrasia ya chama kimoja, pamoja na lugha yetu ya
taifa, Kiswahili, na jeshi la taifa lililonolewa kisiasa na lenye nidhamu,
liliweza kuyaunganisha makabila zaidi ya 126 katika taifa imara.
“Hata hivyo,
pamoja na mafanikio yote haya, bado wanasema tulishindwa katika Tanzania,
kwamba ‘tulichemka’. Lakini ni kweli tulishindwa? Lazima tuseme hapana.
Hatuwezi kukanusha kila jambo tulilofanikiwa. Kuna rafiki zangu ambao
hatukuwaruhusu wawe matajiri; sasa wametajirika na wanasema “Unaona, tunatajirika
sasa, kwa hiyo hukuwa sahihi’. Lakini hilo ni jibu la aina gani? Kusuasua kwa
ujamaa kumekuwa ni kwa dunia nzima. Hili ndilo linalopaswa kutolewa maelezo,
siyo tu upande wa Tanzania. George Bernard Shaw, ambaye alikuwa anapinga kuwepo
kwa Mungu, alipata kusema: “Huwezi kusema Ukristo umeshindikana kwa sababu
haujajaribiwa.’ Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa ujamaa: huwezi kusema ujamaa
umeshindwa eti kwa sababu haukujaribiwa,” alifafanua.
Lakini leo hii
tunapokumbuka miaka 10 ya kifo chake tunapaswa kujiuliza: Hivi ni kweli ujamaa
ulishindwa au haukujaribiwa? Inavyoonekana ni kwamba viongozi wetu ndio
wanaotufanya tuamini kwamba ujamaa kweli ulishindwa, wakati wananchi wa kawaida
wanaelewa tofauti.
Itakumbukwa
kwamba, enzi zile wakati siasa ya ujamaa na kujitegemea ikiimbwa kila kona,
hata wanafunzi walijifunza kujitegemea, kwa kuzingatia Azimio la Musoma
lililopitishwa Halmashauri Kuu ya TANU Novemba 1974 mjini Musoma likisisitiza
kwamba ‘Elimu ni Kazi’.
Enzi zile kila
shule, hasa za vijijini, zilikuwa na mashamba zikijishughulisha na kilimo,
ikiwa ni elimu mojawapo ya kumwandaa mtoto aje ajitegemee baada ya kumaliza
elimu yake ya msingi. Kilimo bora kilionekana hata katika Mashamba ya Ujamaa ya
Vijiji ambapo kila kaya ilitakiwa kuwa na walau ekari moja na mazao yaliyovunwa
humo yaliwekwa katika akiba ya kijiji ili kupambana na baa la njaa endapo
lingetokea.
Wananchi
walikuwa tayari kushiriki, lakini ukweli ni kwamba, viongozi wetu – wengi wao –
hawakuwa tayari kuijaribu siasa ya ujamaa na kujitegemea kwa sababu iliwanyima
fursa za kuchuma mali na kujilimbikizia.
Leo hii watoto
hawajui hata mche wa mhindi ukoje, hawajui hata jembe linashikwaje, wakimaliza
elimu ya msingi wanaambiwa ni wadogo, watafanya kazi gani. Lakini watu
hawajiulizi kuhusu wale watoto waliokosa fursa za elimu ambao wengi ni wadogo
kuliko hata hawa wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari, ambao wanachunga na
kulima. Hawasemi kama ni wadogo, badala yake wanapiga kelele kwamba serikali
imeshindwa kazi. Hivi ni kweli?
Tutafakari
katika kipindi hiki na tuone tunawezaje kuinusuru nchi yetu na kongwa hili. <Mwisho>.
No comments:
Post a Comment