Na
Daniel Mbega
LEO
ni miaka 14 tangu Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Burito Nyerere,
alipofariki dunia katika Hospitali ya St. Thomas jijini London kwa ugonjwa wa
saratani ya damu (leukemia).
Mwalimu Nyerere alifanya mambo mengi makubwa, kitaifa na kimataifa, kiasi kwamba hata Mataifa ya Magharibi yalishindwa kumwelewa alikuwa na kichwa cha aina gani.
Mwalimu Nyerere alifanya mambo mengi makubwa, kitaifa na kimataifa, kiasi kwamba hata Mataifa ya Magharibi yalishindwa kumwelewa alikuwa na kichwa cha aina gani.
Alifikiri
mambo ya walio wengi kabla ya kujifikiria mwenyewe, na aliamini katika kile
alichokiabudu, ndiyo maana hakuwa na mzaha katika maamuzi yake. Alipenda amani
iwepo kila mahali duniani, ndiyo maana hata baada ya Tanganyika kupata uhuru,
akasema asingejivunia hilo hadi pale Afrika nzima itakapokuwa huru.
Kwa
kuanzia, akaamua kuja na wazo la kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar ili uwe
mfano thabiti wa kile alichokuwa anakipigania. Alipenda usawa kwa hali na mali,
ndiyo maana haikushangaza mwaka 1967 alipoanzisha Azimio la Arusha akaamua
kutaifisha uchumi uliokuwa mikononi mwa wachache huku walio wengi wakiwa katika
umaskini mkubwa.
Lakini
kama kuna kitu ambacho Mwalimu Nyerere alikipigania kwa nguvu zote mpaka
anaingia kaburini ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Muungano wa Tanzania)
wenye umri wa miaka 49 tangu nyaraka zake ziliposainiwa mwaka 1964.
Katika
miaka ya mwisho ya uhai wake hili lilionekana dhahiri ambapo alilifanya kwa
vitendo, si maneno peke yake. Hatua ya kwanza ilikuwa ile ya mwaka 1994
alipozima hoja ya Mbunge wa Chunya, Njelu Kasaka, ya kudai serikali ya
Tanganyika ndani ya Muungano.
Hakuishia
hapo, akatoa kitabu cha “Uongozi wetu na hatma ya Tanzania” kilichochapishwa
nchini Zimbabwe mwaka 1994 ambapo pamoja na maneno makali aliyotumia, pia
alitumia tenzi kuwananga wale waliokuwa wakiupinga ama kuubeza Muungano na
kutishia mustakabali wake.
Mwaka
uliofuata wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi alifikia mahali
akasimama kidete, akisaidiana na wanachama wengine wa CCM (pengine waliopata
nguvu kuona Nyerere yupo nyuma yao), wakazima jaribio la rais wa Zanzibar wa
wakati ule Dk. Salmin Amour Juma aliyetaka kuifanyia marekebisho Katiba ya
Serikali ya Mapinduzi ili apate nafasi nyingine ya kugombea urais kwa mara ya
tatu ifikapo mwaka 2000.
Wakati
wa uchaguzi mkuu wa CCM wa mwaka 1997 Mwalimu alilazimika kwenda mwenyewe
Chimwaga, Dodoma ingawa hakuwa amealikwa, na kwenda kuzima majaribio kadhaa
yaliyokuwa yameandaliwa na “vijana” wa chama hicho kutaka kumng’oa Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara, John Samuel Malecela, na badala yake wakapanga
wamchague Waziri Mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye. Akafanikiwa.
Mambo
haya yote yalimuudhi na kumkera sana Mwalimu kwa sababu aliamini, japokuwa
hakuwa kwenye wadhifa wowote - si wa chama au serikali - kwamba kama
asingesimama kidete ustawi wa Muungano, ambao ulikuwa umeanza kutishiwa tena
kama ilivyokuwa miaka ile ya 1980, basi ungetetereka.
Ndiyo.
Kisa cha kujiuzulu kwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi katika nyadhifa za Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Muungano, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
mwaka 1984, kilitokana na hoja za Muungano.
Binafsi
naona hoja za Jumbe zilikuwa sahihi kabisa kama ilivyokuwa kwa hoja ya Njelu
Kasaka na wafuasi wake wa G55, ingawa nao baadaye walibadilika kama kinyonga
hasa baada ya kupewa vyeo mbalimbali serikalini. Mpaka leo hii si mtoa hoja au
mtu yeyote wa kundi hilo aliye tayari kuitaja tena hoja ya serikali ya
Tanganyika ndani ya Muungano, ambayo safari hii imeibuliwa kwenye Rasimu ya
Katiba Mpya.
Lakini
pamoja na kujiuzulu kwa Jumbe, hoja zile bado ziko fikrani mwa Wazanzibari
mpaka kesho, kwani itakumbukwa wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka
1990 uliomweka madarakani Dk. Salmin Amour Juma, Wazanzibari walikuwa wamepanga
kuitisha maandamano na kugomea uchaguzi huo kwa maelezo kwamba Zanzibar
inakandamizwa na Bara na wananchi wa visiwa hivyo hawapati baadhi ya haki zao
za msingi zilizomezwa ndani ya Muungano.
Ingawa
tatizo hili limekuwa likitajwa kwamba linatokana na historia ya visiwa hivyo;
Unguja na Pemba, lakini bado linagonganisha vichwa vya wengi, hata wale
Wazanzibari wa Unguja “wenye nafasi”. Unguja ndiko kwenye maendeleo zaidi
kuliko Pemba, ambako ndiko karafuu inakozalishwa kwa wingi. Wananchi wa Pemba
ni maskini sana kiasi kwamba huwezi kuamini kama ni sehemu ya Tanzania
ukiwalinganisha na wenzao wa Unguja.
Waunguja
hawazungumzii kasoro za Muungano kwa kisingizio cha kulinda maslahi ya Chama
cha Mapinduzi kwa sababu wengi wao ni wafuasi wa CCM na kule Pemba asilimia 99
ni wafuasi wa chama pinzani cha CUF. Kwa hiyo wanadhani kwamba wakiupinga
Muungano na kasoro zake watawapa nguvu wapinzani, fikra ambazo kwa namna moja
ama nyingine ni potofu.
Zanzibar,
tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, hakuko shwari kwa sababu
Dk. Salmin anaelezwa kwamba hakushinda kwa haki na CUF walikwenda mpaka kwenye
jumuiya za kimataifa kupiga kelele kwamba waliibiwa kura zao. Hata uchaguzi wa
mwaka 2000 na ule wa mwaka 2005, bado kilio cha CUF kimeendelea kuwa kile kile.
Katika
uchaguzi wa mwaka 1995, kwa mfano, uchaguzi ulirudiwa Zanzibar, na inasemekana
kwamba viongozi kadhaa wa CCM na wanasiasa wakongwe walikwenda usiku Unguja na
kurejea alfajiri Dar es Salaam katika kile kilichoelezwa na wachunguzi wa mambo
ya siasa kwamba “kuunusuru Muungano”.
Baadhi
wanasema ikiwa CUF itaruhusiwa na wananchi kutawala Visiwani, basi utakuwa ndio
mwisho wa Muungano, ambao Mwalimu alipiga kelele na kusema asingekubali kuona
Muungano unakufa wakati yeye akiwa hai.
Alikuwa
sahihi kabisa. Kwa sababu kitendo cha kushuhudia “mtoto wake mpendwa” Azimio la
Arusha aliyezaa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea “anauawa” rasmi mwaka 1991 kwa
Azimio la Zanzibar, hakika asingekuwa tayari kuona “mwanawe wa pekee” ambaye ni
Muungano anakufa yeye akitazama.
Siri
ya Muungano huu wanaoijua ni Nyerere na Karume tu, wote wanaosema wanaijua
wanajaribu “kukonyeza gizani”. Yaani wanakisia na si kile kitokacho moyoni.
Leo
hii CCM imeendelea kusimama kidete kuhakikisha kwamba “mwana pekee” wa Mwalimu
hakati roho kama baadhi wanavyoombea.
CCM
yenyewe inajitetea kwamba hoja ya Muungano wa Tanzania inasimama juu ya msingi
wa sera ya chama hicho, ambayo inaelezwa kwamba ina ncha mbili; yaani kuulinda
na kuudumisha Muungano wenyewe kwa upande mmoja na muundo wa Muungano huo kuwa
wa Serikali mbili kwa upande wa pili.
CCM
inaushabikia Muungano na kupania kuulinda na kuudumisha kwa sababu kwanza
inaamini kuwa Muungano huo ni wa watu wenyewe na pili, uliasisiwa na vyama
wazazi wake, yaani TANU na ASP.
Binafsi
sijui kama Muungano ulikuwa wa watu wenyewe, kwa sababu hakuna mtu aliyepata
nafasi ya kuuridhia wakati huo kabla ya kufikia hatua ya kusaini nyaraka za
Muungano, ambazo mpaka leo hii hazipo na hazijulikani zilipo.
Ni
kweli kwamba CCM yenyewe ni matokeo ya Muungano huo na chachu ya kuziimarisha
kwani tendo la kuviunganisha vyama vya TANU na ASP kuunda CCM lilitokana na
utashi wa kukamilisha hatua za kuunda Muungano. Daima CCM inaunga mkono muundo
wa Muungano wa Serikali mbili kwa sababu kwanza ndio ulioamuliwa na waasisi wa
Muungano, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Japokuwa
CCM inajinasibu kwamba muundo wa serikali mbili umeridhiwa na Watanzania wengi,
binafsi nasema siyo sahihi hata kidogo. Kwa kuchukua vigezo vya mwaka 1994
walivyofanya kukusanya maoni kwa wanachama, lazima mtu yeyote anaweza kuhisi
kwamba matokeo yaliyotangazwa yalikuwa ni kwa maslahi ya chama na wale
wanaoushabikia Muungano na si maslahi ya Watanzania walio wengi.
Lakini
kama kweli Muungano huu unapaswa kuwa na mtazamo halisi wa utashi wa wananchi
wote, kuna mambo mengi ya kufanya ili kufikia hatua hiyo ambayo haiwezi kuwa
kero tena; iwe Muungano unakuwepo au unavunjika.
Kwanza; Watanzania wengi wangependa kuziona nyaraka za kwanza kabisa za Muungano ambazo zilisainiwa bila kuwepo kwa ridhaa ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Kwanza; Watanzania wengi wangependa kuziona nyaraka za kwanza kabisa za Muungano ambazo zilisainiwa bila kuwepo kwa ridhaa ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Pili;
serikali ya CCM inapaswa kutambua kwamba suala la Muungano siyo la chama peke
yake, bali ni la Katiba ya Nchi na wananchi kwa ujumla. Chama kinaweza kutawala
kwa kipindi fulani, na kama hoja za kuundwa kwake zinainufaisha zaidi CCM,
lazima itambue kwamba ipo siku hata yenyewe itakuwa pembeni kama ilivyotokea
kwa ZAPU, KANU na vinginevyo.
Tatu;
wananchi wa pande zote wanapaswa kutoa maoni yao katika harakati za kuifanyia
marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili watoe mapendekezo
yao na muundo bora wanaodhani unafaa kama serikali moja, mbili au tatu badala
ya kuegemea kwenye kura za kichama ambazo waliopiga ni wana-CCM, waliohesabu ni
wana-CCM wenyewe na CCM ndio waliokuwa wakipinga serikali moja na tatu.
Nne;
kero za Muungano zinatakiwa kutatuliwa kiutendaji badala ya kisiasa kwa sababu
hali hiyo ndiyo inayosababisha hali ya kisiasa iwe tete Visiwani mpaka sasa.
Kwa
kuyafanyia kazi haya, ambayo ndani yake yamebeba hoja nyingi za msingi, kuna
uwezekano wa kuona mwelekezo sahihi wa Muungano huu, na hapo ndipo tutakapoweza
kusimama madhabahuni na kusema tunamuenzi Mwalimu Nyerere, kwa vitendo.
Tofauti
na hapo, CCM itakuwa haitendi haki kumlinda “mwana pekee” wa Mwalimu Nyerere
hata kama habebeki. Itafikia mahali juhudi zao zitakuwa kama kuitundikia dripu
maiti, hatua ambayo itawafanya wachekwe na mataifa mengine.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA!
No comments:
Post a Comment