Edward Lowassa
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amesema ataendelea kuzipigania shule za sekondari za kata kwa kuwa shule hizo zimekuwa mkombozi kielimu katika familia za watu walio na kipato cha chini.
Lowassa aliyasema hayo jana wakati alipoendesha harambee iliyoandaliwa kwa pamoja na shule za sekondari 12 za Tarafa ya Mbagala, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam ambapo zilipatikana sh milioni 233 huku lengo likiwa sh milioni 400.
Alisema kuzipigania na kuwa mkereketwa mkubwa wa shule hizo, bado hilo halimfanyi kuwa mmiliki wa shule hizo, bali amefanya hivyo kwa ajili ya kutaka kuleta usawa wa kielimu katika jamii ya Kitanzania.
Lowassa alisema kuna ulazima kwa watoto wote nchini kupatiwa elimu bora bila ya ubaguzi na inayokwenda sambamba na maisha ya sasa.
Alisema elimu bora inayohitajika ni ile itakayomsaidia mtoto kupata ajira pindi anapomaliza masomo ya ngazi husika.
“Endapo shule hizi za serikali za kata zitaendelea kubaki nyuma basi itakuwa lengo la sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM) hazina maana,” alisema Lowassa.
Kuhusu ajira kwa vijana, Lowassa alisema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ni mgogoro unaozikumba nchi za Afrika ikiwamo Tunisia, ambayo imeingia katika mgogoro wa vijana kukosa ajira.
Alisema kuwa ni muhimu tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana likapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza.
Aidha, katika harambee hiyo Lowassa alichangia sh milioni 10, walimu wa shule hizo walichangia sh milioni 1.5, huku wadau wengine mbalimbali walijitolea kwa hali na mali kuchangia na kuweka ahadi.
Lowassa alisema fedha hizo zinatarajiwa kutatua changamoto zinazozikabili shule hizo kama vile upungufu wa madawati, maabara, maji, uzio na vyumba vya madarasa.
Mwanafunzi, Kijoy Selemani, aliwataka wazazi na wadau wengine kujitokeza katika kuchangia elimu hususan kuwajengea maktaba kubwa ya tarafa, ambayo itasaidia wanafunzi hao kujisomea na kuweza kufaulu mitihani yao.
Mbunge wa Kigamboni (CCM), Faustine Ndugulile, alisema pamoja na changamoto za ubora wa elimu ya shule hizo za kata bado elimu inayopatikana imewanufaisha vijana wengi kutoka familia za watu wa kipato cha chini.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment