Mzee Hamisi Ally Kilomoni, mchezaji wa zamani wa Sunderland anayekumbukwa na Yanga kwa jinsi alivyokuwa anapachika mabao dhidi yao. Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry.
SUNDERLAND, ambayo wakati huo ilikuwa ikishikilia ubingwa wa kandanda wa Afrika Mashariki ‘Allsopps Cup’ pamoja na ubingwa wa Taifa, Jumapili ya Mei Mosi, 1966 iliinyoa Yanga bila maji kwa kuifunga magoli 4-0 katika Uwanja wa Ilala, mbele ya waheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa, Mawaziri, Mabalozi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Selemani Kitundu na maelfu ya watazamaji waliojazana hapo.
Mara baada ya mchezo mashabiki wa Sunderland walilipuka kwa mayowe ya furaha huku wakiitania Yanga kuwa ni ‘Four-Four’ kwa kufungwa magoli manne bila majibu. Wakati huo gari za Peugeot 404 kutoka Ufaransa ndiyo kwanza zilikuwa zinaingia nchini.
Hii ilikuwa ni fainali ya kugombea Kombe la NUTA lililotolewa kushindaniwa maalum kwa sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, yaani May Day.
Mpira ulianza huku mvua ikinyesha na upepo mwingi ukivuma. Yanga ndio walioanza kuingia uwanjani wakipitia mlango usiostahili kupitiwa, lakini yote hiyo haikufaa kitu, kwani goli nne kwa yai ziliamua nani bingwa wa soka. Kipigo hicho kilikuwa kama cha kulipa kisasi baada ya Sunderland kufungwa 5-4 na Yanga hapo Machi Mosi katika fainali ya Kombe la Nyota.
Timu zote zilitambulishwa kwa mgeni wa heshima, Makamu wa Pili wa Rais, Rashid Kawawa. Baada ya hapo mpira ukaanza huku Sunderland, Sanda au Abidjan, kama walivyokuwa wakiitwa, wakicheza mchezo wa haraka haraka (quick game) ili kuwachosha mabeki wa Yanga.
Zilipotimu dakika tatu tu mpira ukawa miguuni mwa Asmat, winga wa kushoto wa Sunderland, na hapo ikatumika ‘one touch’, akamlamba chenga Abuu Mapyopyo wa Yanga na kumpasia Hamisi Kilomoni, ambaye alimzungusha Athumani Kilambo wa Yanga na kisha akampasia Mustafa Choteka, naye bila kuchelewa akammegea Haji Lesso, ambaye alifumua shuti kali la ‘mwana-ukome’ huku akiwa kafumba macho. Alipofumbua akapashwa habari kwamba mpira umetikisa nyavu za Yanga.
Haukupita muda mrefu Mustafa aliutupa mpira hadi kwa Haji, ambaye kwa mara nyingine tena bila kufanya makosa akafunga goli la pili kwa Sunderland. Mpira uliendelea huwa wa vuta-nikuvute hadi kilipomalizika kipindi cha kwanza.
Wakati wote huu Sunderland walikuwa wakitumia staili zao mpya za ‘Abidjan’. Watu wengi walikuwa hawajui jinsi staili za Abidjan zinavyochezwa, lakini siku hiyo walijionea wenyewe, yaani mfungaji magoli huwa mmoja tu naye ni ‘Insaidi’ au ‘sentafowadi’. Ndivyo ilivyokuwa siku hiyo, kwani Haji ndiye aliyefunga magoli mengine mawili katika kipindi cha pili na kuipatia timu yake ushindi mnono dhidi ya mahasimu wao wakubwa, Yanga.
Siku hiyo timu zilipangwa hivi:
YANGA: Saad Mohammed Songambele, Abuu Mapyopyo, Omari Kapera, Athumani Kilambo, Juma Washokera, Awadh Gessani, Kassim Lengwe, Mfamau, Peter Mandawa, Mtumwa Mgeni, Mwinyiamiri Mwinyimadi.
SUNDERLAND: Mbaraka Salum Magembe, Tayari Mussa, Mussa Libabu, Yussuf Omari Kimimbi, Gilbert Mahinya, Adam Athmani, Abdu Rashid Kibunzi, Hamisi Kilomoni, Haji Lesso, Astmati, Mustafa Choteka, Arthur Mambetta.
Mwamuzi alikuwa Marijani Shabani Marijani aliyesaidiwa na Gration Matovu kutoka Tanga. Kamisaa alikuwa Balozi B.J. Maggid, aliyekuwa Rais wa FAT, wakati mgeni rasmi alikuwa Rashid Mfaume Kawawa, Makamu wa Pili wa Rais.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye muswada wa kitabu cha 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' cha mwandishi Daniel Mbega, ambacho kiko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com
No comments:
Post a Comment