Machi 17, 1973 Mbaraka akimvisha pete mkewe Amne. Picha kwa hisani ya Kijiwe cha Kitime.
Kupanda kwa bei
ya mafuta kulimkimbiza Moro Jazz 1973
Na Daniel Mbega
MOROGORO kuna
vipaji vingi – kuanzia soka, ndondi na muziki. Huko ndiko walikotokea akina
Leodgar Tenga, Hashim Kambi, golikipa wa zamani wa Sunderland Mbaraka Salum
Magembe, Hassan Mlapakolo, Adam Sabu na wengineo ni baadhi tu ya wanasoka
waliotoka Morogoro.
Hivi karibuni tu
bondia kutoka Morogoro, Francis ‘Maputo’ Cheka alitwaa ubingwa wa dunia
kuonyesha kwamba vipaji vya ndondi vimekuwepo kwa miaka mingi tangu enzi zile
za klabu za shule za sekondari za Forest Hill na Mzumbe.
Lakini ukizungumzia muziki, hapo nadhani ndipo mahala pake. Walikuwepo akina Salim Abdallah Yazidu ‘Say’ aliyetamba na bendi za Cuban Marimba na Moro Jazz pamoja na ‘Mfalme’ wa gitaa za solo nchini Tanzania, Mbaraka Mwinshehe Mwaruka. Lakini pia tumeshuhudia wanamuziki wengi wa Bongo Fleva wakiinukia huko kama ‘Mfalme wa Rhymes 2004’ Selemani Msindi ‘Afande Sele’ na akina Mdogo Ditto na Belle 9.
Lakini ukizungumzia muziki, hapo nadhani ndipo mahala pake. Walikuwepo akina Salim Abdallah Yazidu ‘Say’ aliyetamba na bendi za Cuban Marimba na Moro Jazz pamoja na ‘Mfalme’ wa gitaa za solo nchini Tanzania, Mbaraka Mwinshehe Mwaruka. Lakini pia tumeshuhudia wanamuziki wengi wa Bongo Fleva wakiinukia huko kama ‘Mfalme wa Rhymes 2004’ Selemani Msindi ‘Afande Sele’ na akina Mdogo Ditto na Belle 9.
Mafaniko mengi
yametokea Morogoro kwenye fani hizo. Tulishuhudia mwaka 1975 wakati Mseto
iliponyakua Ubingwa wa Taifa wa kandanda na kumaliza utawala wa timu za Dar es
Salaam, mafanikio ambayo yalifikiwa pia na Mtibwa Sugar ya Turiani iliyotwaa
ubingwa wa Ligi Kuu miaka ya 1999 na 2000.
Lakini, Morogoro
ulitangazwa zaidi na Mbaraka Mwinshehe, ambaye pia ndiye alikuwa Alama ya Taifa
ya Muziki wa Dansi. Ingawa asili yake ni Mdoe ambaye babu yake Chifu Mwaruka
alilowea Uzaramoni huko Mzenga, Kisarawe, lakini walio wengi bado wanaamini
kwamba jamaa alikuwa Mluguru.
Wakati Mbaraka anazaliwa
Juni 27, 1944 katika Kijiji cha Kingolwira, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro,
bendi ya Morogoro Jazz nayo ilianzishwa rasmi mwaka huo ikiundwa na akina Makala
Kindamile, Joseph Thomas, Seif Ally, Daudi Ally na Shaaban Mwambe.
Mbaraka alikuwa
mtoto wa pili katika familia ya watoto 12 wa Mzee Mwinshehe Mwaruka, aliyekuwa
karani katika mashamba ya mkonge pale Kingolwira. Nduguze ni Said, Kapita,
Halima, Zanda, Zawadi, Matata, Nassibu, Almasi, Mwereka, Kate na Mwazaina.
Mapenzi yake
katika muziki yalimfanya Mbaraka akatishe masomo katika kidato cha tatu kwenye
shule ya sekondari Mzumbe. Tangu utotoni alikuwa napenda kuimba.
Aalianza
kushiriki maonyesho ya bendi ya Moro Jazz akiwa shule, ambapo alipenda kupiga
filimbi. Mwaka 1965 wakati waimbaji wa Moro Jazz wakiwa wanabarizi nje ya klabu
yao, Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa. Kumbe tayari alikuwa ameondoka shule
na alikuwa anaelekea Dar es Salaam ‘kutafuta maisha’. Wanamuziki hao wakamsihi ampumzike
atafakari kwanza.
Hata hivyo, kesho
yake walipoamka wakamkuta Mbaraka anapiga gitaa, ala ambayo hawakuwahi kumuona
akiipiga zaidi ya filimbi yake.
Huo ndio ukawa
mwanzo way eye kujiunga na bendi hiyo kwani alifundishwa kupiga rhythm kwa vile
hawakuwa na mpigaji. Safari ya Dar ikaishia hapo.
Inaelezwa kwamba kuna siku walialikwa Dar es
Salaam ili kushinda na Kilwa Jazz ya Ahmad Kipande. Kabla ya kuondoka Mbaraka
aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi. Wakati huo waliokuwa wanalipwa kwa
mwezi ni wapiga ala hasa gitaa la solo, saxophone na trumpet, wengine wote
walikuwa wanapewa posho kila walipopiga dansi.
Baada ya kugoma wazee wa bendi wakakubali
kumlipa Shs. 120 kwa mwezi, uamuzi ambao ulimkasirisha mpiga solo aliyekuwa akilipwa
Shs. 150 ambaye aligoma kwenda Dar kwa kutetea kuwa mpiga rhythm hastahili
malipo.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Mbaraka
akasema angepiga pia solo. Viongozi wa bendi walistaajabu kwa sababu Mbaraka
hakuwahi kupiga solo kabla na kwa vile Kilwa Jazz wakati huo ilikuwa tisho,
walihisi kwamba wangeumbuka. Walipokwenda huko Mbaraka alidhihirisha kwamba
alikuwa ‘mchawi wa gitaa’ baada ya kulikung’uta solo vili na bendi yao ikapata
ushindi. Badala ya kulipwa Shs. 120, sasa wakampandishia mshahara hadi Shs. 250
kwa mwezi, ambazo zilikuwa nyingi mno wakati huo na tangu hapo akawa mpiga solo
hadi alipoondoka mwaka 1973 kuanzia bendi yake ya Super Volcano.
KUHAMA…
Tofauti na sasa,
zamani lilikuwa ni jambo geni kwa wanamuziki kuhama bendi moja bila mpangilio. Oktoba
1973 Tanzania ilishuhudia kupanda kwa bei ya mafuta kwa mara ya kwanza. Hali hiyo
ikafanya shughuli nyingi za uchumi kuyumba.
Bendi za dansi
ambazo zilitegemea kufanya maonyesho ili kujipatia fedha zikashuhudia
kuporomoka kwa uchumi baada ya kuwa zikipiga kwenye kumbi zilizo tupu kwa
sababu watu hawakuwa na fedha, hata zile kidogo walizokuwa nazo, hawakuwa
tayari kuzitumia ovyo.
Ni katika kipindi
hiki ambapo Mbaraka aliona ni vyema akatafuta malisho bora, lakini angekwenda
wapi? Akaamua kuanzisha bendi yake ya Super Volcano. Hatimaye akaelekea Kenya,
akiwa na baadhi ya wanamuziki, japokuwa siyo katika kundi zima kwa sababu
mabadiliko ya uchumi yalikuwa yametokea pia Kenya.
Mbaraka akaanza
kuutangaza muziki wa Tanzania huko wakati akisaidia kuubadili muziki wa Kenya.
MAPENZI NA MWANAJAMII…
Hakuna shaka yoyote
kwamba Mbaraka Mwinshehe ataendelea kuwa utambulisho wa muziki wa dansi Tanzania
na nje ya mipaka yake, ndiyo maana wengi walimwita ‘Franco wa Afrika Mashariki’
(Franco of the East Africa) na wengine wakamwita ‘Mchawi wa Solo’.
Jamaa alijua
kutunga na jamii inathibitisha hili kila nyimbo zake zinapopigwa. Alijua namna
ya kutafuta visa na kuvipangilia, vingi vikiwa ni vya kweli.
Nyimbo kama Mtaa
wa Saba, Shida, Jogoo la Shamba, Choyo Uache, Dk. Klerruu, Masimango, Mapenzi
Shuleni, Urafiki Mwisho wa Mwezi, Kazi Ndio Msingi, zinazungumzia masuala ya
jamii.
Katika nyimbo za Hallo
Betty, Dawa Ya Mapenzi, Niliota Ndoto, Amina Mpenzi, Yameshanichosha, Talaka,
Nashangaa, Mapenzi Yanitesa, Tutakuja Gombana, Esta Wangu, Pole Dada, Daktari
Ni Mimi, Wanisikitisha Mpenzi, Nikupendeje, Nirudie Mama, Roho Ndiyo Mwamuzi, Kasema
Hakutaki, Dina Uliapa, Tina Turudiane, Dawa Ya Mapenzi, Penzi Lako Hatari, Mashemeji
Wangapi, Tunachogombea Nini, na nyingizo zinazungumzia mapenzi na nyingi kati
ya hizo ni visa vya kweli vilivyomtokea ama yeye au wanajamii wengine.
Wimbo wa ‘Mshenga’
unatajwa kuwa ni kisa cha kweli alichotunga kumuelezea mchumba wake ambaye
alikuja kuwa mkewe. Pia aliwahi kumtungia mchumba wake huyo nyimbo za ‘Tunachogombea
Nini’ na ‘Walisema’ kufuatia maneno ya ‘umbeya’ waliyoyasikia.
‘Jogoo la Shamba’
ni kisa cha kweli baada ya Mbaraka, mkewe na shemeji yake kufanyiwa fujo na
fundi cherehani mmoja mjini Morogoro, ambapo mdogo wake Mbaraka aliyeitwa Zanda
alimtwanga fundi huyo mwenyeji wa Ulanga, ambako ni ‘shamba’.
MWANAHARAKATI…
Mbaraka hakuwa
mwanasiasa, bali mwanaharakati. Alihimiza shughuli nyingi za maendeleo kupitia
nyimbo zake kama vile Furaha Ya Saba Saba, Vijana wa Afrika, Mapenzi Shuleni, Mama
Chakula Bora, Makao Makuu Dodoma, Matamko Ya Viongozi Wetu, Expo 70 Pt 1 &
2, Watalii, Twawapongeza Wanasoka, Kazi Ndiyo Msingi, Heko U.W.T., Mwongoza Wa
Tanu, Ukombozi Wa Afrika, Ujamaa Na Kujitegemea na Poleni Rufiji.
Mwanamuziki huyo
aliing’arisha Tanzania kwenye Maonyesho ya Kimataifa nchini Japan mwaka 1970 (Japan
Expo 70) kutokana na nyimbo zake, wakati huo akiwa na Moro Jazz.
NDOA…
Machi 17, 1972
Mbaraka alifunga ndoa na Amne Kadribaksh Shahdad, ambaye walibahatika kuzaa
naye watoto wawili Masiku anayeishi Afrika Kusini na dada yake Muhitaji ‘Taji’,
ambaye anaongoza bendi ya Orchestre Super Volcano akiwa mtunzi, mwimbaji na
mpiga gitaa la bass.
MAUTI YAMFIKA…
Bendi nyingi za
Tanzania zilikuwa na kawaida ya kurekodi nyimbo zao Kenya ambako walikuwa
wamepiga hatua tofauti na Tanzania, ambako walitegemea zaidi Studio za Radio
Tanzania pekee.
Mwaka 1978
mwishoni Mbaraka alikuwa Mombasa akiwa na kundi lake la Super Volcano, lengo
likiwa kurekodi nyimbo zao. Mbaraka alikuwa amekwenda na familia yake, huku
binti yake Muhitaji akiwa na miaka miwili kasoro.
Januari 12, 1979
Mbaraka, akiwa kwenye gari la rafiki yake Omari Abdi wa Moshi aliyekuwa
akiendesha, pamoja na mtu mwingine, waliondoka kwenye hoteli waliyokuwepo na
kwenda kwenye shughuli zao.
Ni katika
mizunguko hiyo ndipo wakakutana na ajali mbaya ambapo gari lao liligonga lori
la mchanga kwa nyuma, ajali ambayo ilitokea katika njiapanda ya Kisauni,
Mombasa. Mwenzao alikufa pale pale, lakini Mbaraka na Omar walifia hospitali.
Mbaraka alifariki
saa 1.55 usiku baada ya kuwa amepoteza damu nyingi na hakukuwepo na mtu wa
kumuongezea damu. Safari yake ikawa imeishia hapo.
Afrika Mashariki
yote ilizizima kwa msiba huo. Hata hivyo, mwili wake ulisafirishwa na kwenda
kuzikwa kijijini kwao Mzenga, Kisarawe.
Hizi ni baadhi ya
albamu alizoshiriki marehemu Mbaraka tangu akiwa na Morogoro Jazz hadi Super
Volcano:
Morogoro Jazz Band
Albamu ya ‘Hallo Betty” akiwa na bendi ya Moro
Jazz ilirekodiwa katia studio za Chandarana huko Kericho, Kenya mwaka 1968 na
1969. Nyimbo zilizokuwemo ni Jirani
Nisaidie, Hallo Betty, Dawa Ya Mapenzi, Niliota Ndoto, Amina Mpenzi, Yameshanichosha,
Talaka, Nashangaa, Moro Phata Phata, Furaha Ya Saba Saba na Waloleni Moro.
Masimango ni albamu ambayo ilirekodiwa ikihusisha nyimbo zilizorekodiwa
kati ya mwaka 1969 na 1972, zikiwemo 6 kati ya 8 zilizomo kwenye Vol. 3 na
baadhi kutoka Vol. 1 na 2.
Super Volcano
Ukumbusho Vol. 1 ni albamu iliyokuwa na nyimbo kama Shida, Nisalimie Wanazaire, Mapenzi
Yanitesa, Choyo Uache, Tutakuja Gombana, Dk. Klerruu na Esta Wangu.
Ukumbusho Vol. 2 ilikuwa na nyimbo za Mtaa wa Saba, Pole Dada, Urafiki Mwisho wa Mwezi, Vijana wa Afrika,
Kizena, Jasinta, na Sululu ya Moro.
Ukumbusho Vol. 3 ilikuwa na nyimbo kama Mapenzi Shuleni, Daktari Ni Mimi, Wanisikitisha Mpenzi, Nikupendeje,
Nirudie Mama, Ushamba Umekutoka, Masimango, Ewe Mwana.
Ukumbusho Vol. 4 ilikuwa na nyimbo za Utanikondesha Maria, Uaminifu Nimeutambua, Mama Chakula Bora, Roho
Ndiyo Mwamuzi, Masika Mtindo Mpya, Kasema Hakutaki, Dina Uliapa, Bibi Wa Watu.
Ukumbusho Vol. 5 ilikuwa na nyimbo za Unanitafuta Nini, Nitamtuma Mshenga, Makao Makuu Dodoma, Akula Mwembe
Songo, Fadhili Ya Punda, Matamko Ya Viongozi Wetu, Tina Turudiane, Sina Pesa.
Ukumbusho Vol. 6 ilikuwa na nyimbo za Masika Zole Zole, Harusi No.2, Dawa Ya Mapenzi, Afadhali Umerudi, Ugeni
Tabu, Kifo Cha Pesa, Mshenga No.2, na Unaulizwa.
Ukumbusho Vol. 7 ilirekodiwa mwaka 1970 mara baada ya bendi
hiyo kufanya maajabu katika maonyesho makubwa nchini Japan. Albamu hii ilikuwa
na nyimbo kama Regina, Expo 70 Pt 1 &
2, Masikitiko Yetu, Nipeleke Nikashuhudie, Picnic Ya Volcano, Penzi Lako
Hatari, Watalii.
Ukumbusho Vol 8 ilikuwa na nyimbo za Mashetani, Safari Siyo Kifo, Baba Mdogo, Mashemeji Wangapi, Matrida
Huna Siri na Talaka Kampa Nani.
Ukumbusho Vol. 9 ilikuwa na nyimbo kama Twawapongeza Wanasoka, Kazi Ndiyo Msingi, Regina, Heko U.W.T.,
Mrudishe, Tunachogombea Nini, Mwongoza Wa Tanu na Ukombozi Wa Afrika.
Ukumbusho Vol. 11 ilikuwa na vibao vya Penzi La Mashaka, The Beat is Mahoka, Pole Dada, Ujamaa Na Kujitegemea,
Nasikia Mwaniteta, The Beat is Mahoka II, Esta Wangu, Wana Moro, Nimechoka
Kusemwa, Mandhi, Nalilia Raha, Penzi La Mashaka II.
Ukumbusho Vol. 12 ilikuwa na nyimbo za Usiingilie Ugomvi Wao, Poleni Rufiji, Happy Christmas, Huyu Ni Shemeji
Yako, Harusi No. 2, Sitakata Tamaa, Headquarters Ya Volcano, Vipi Posa (Mshenga
No. 2).
Tazama mashairi
ya wimbo wa Mtaa wa Saba:
Sasa nimehamia mtaa wa saba,
Toka pale nilipokuwa nikikaa zamani
Ile nyumba sio nyumba ilikuwa [na mikosi
ooh]x2
Nimehama nimehama kuona balaa imezidi
Na kama hauishi ndani ya nyumba iyooo jama
Ndoto ndoto za ajabu haziishi [Tulalapo] x2
Darini hakusemeki mapaka hayeshi kulialia
Usiiu kucha usingizi hauji kabisa
Watoto haweshi kuumwa umwa [eeeeh jamaaa eeh]
x2
[Jamaaa]
Kibwagizo:
Maneno; maneno; hakuna
Tunaishi kwa raha sana
Wapangaji hawana zogo nami
Baba mwenye nyumba sina masile naye [Nashukuru
MUNGU eeeh]
Hata mwezi sijamaliza oooh
Kazini wakanipandisha na cheo
Watoto na mama yao sasa kuumwa umwa [kote
kumekwisha eeeh eeeh eeeh]
[Wote tungekwisha]
Oooooh oooh mama x2 OOOH Lusana oyeeee mamah
Maneno; maneno; hakuna
Tunaishi kwa raha sana
Wapangaji hawana zogo nami
Baba mwenye nyumba sina maneno naye
Nashukuru MUNGU
NB: Unaweza kuwasiliana nami kwa simu +255 715 070109 au
brotherdanny5@gmail.com.
Makala nzuri sana ya Historia nzuri sana ya Mbaraka Mwinshehe. Mie nayependa nyimbo zake nimepata kujua zaidi juu ya historia yake.
ReplyDeleteJe waweza tengeneza makala juu ya historia ya wanamuziki wengine? Mfano Marijani Rajabu