Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Dar es
Salaam. Hatimaye mkutano wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), uliokuwa umezuiwa kupisha sherehe za Muungano utafanyika leo
katika Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja baada ya kupata baraka za polisi.
Mkutano huo awali ulikuwa ufanyike
Aprili 19, mwaka huu lakini ukazuiwa na polisi kwa maelezo kuwa intelijensia
yao ilionyesha kuwa kungekuwa na tishio la maisha ya watu. Hivyo walishauriwa
wapange tarehe nyingine baada ya Sikukuu ya Pasaka.
Hata Aprili 23 ambayo ilikuwa imepangwa
kufanyika kwa mkutano huo, ilikataliwa na polisi kwa madai kwamba askari na
maofisa wa jeshi hilo walikuwa Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 50 ya
Muungano yaliyofanyika Aprili 26, mwaka huu.
Msemaji wa Polisi Zanzibar, Mohamed
Mhina amethibitisha kuruhusiwa kwa mkutano huo na kuwataka wananchi
watakaohudhuria kuwa watulivu kabla na baada ya mkutano.
“Tumewaruhusu kufanya mkutano huo lakini
maandamano hayataruhusiwa kufanyika,” alisema Mhina.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius
Mtatiro alisema mkutano huo utakaoanza saa 8 mchana hadi saa 12 jioni,
utahudhuriwa na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, Freeman Mbowe na Dk Willibrod
Slaa wa Chadema, Mchungaji Christopher Mtikila wa DP na Dk Emmanuel Makaidi wa
NLD.
Wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia,
wawakilishi 10 kutoka kundi la 201 na wanachama mbalimbali kutoka umoja huo.
“Tunakwenda kuwaelimisha wananchi nini
maana ya Katiba, jinsi ya kulinda maoni yao waliyoyatoa yasichakachuliwe na
kuwaeleza kwa nini tuliamua kutoka bungeni,” alisema Mtatiro na kuongeza:
“Kesho (leo) tunafanya mkutano Unguja na
keshokutwa (kesho) Pemba na tutatoa ratiba ya mikutano mbalimbali
itakayofanyika Tanzania Bara kwa makundi tofauti.” Aprili 16 mwaka huu, Ukawa
wakiongozwa na Profesa Lipumba walisusia Bunge la Katiba na kutoka nje kwa
madai ya kutokuridhishwa na mienendo ya mjadala ya Bunge hilo.
Baada ya kutoka bungeni, walitangaza
kufanya mikutano nchi nzima wakianzia Zanzibar.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment