KLABU ya Villarreal imempiga marufuku ya kudumu ya kutoingia katika uwanja wake wa El Madrigal shabiki aliyemrushia ndizi beki wa kulia wa FC Barcelona, Dani Alves kwenye mchezo wa La Liga jana jumapili.
Beki huyo wa kibrazil baada ya kurushiwa ndizi hiyo aliiokota na kuila wakati akiwa katika harakati za kupiga kona, na kitendo hicho kilionesha shukurani za kejeli kwa shabiki aliyefanya jambo hilo la kibaguzi.
Katika mechi hiyo Barca walitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
Villarreal wamethibitisha kumpa kifungo cha kidumu shabiki huyo na kusitisha tiketi zake za msimu huu, huku wakitarajia kumchukulia hatua kali zaidi juu ya ishara ya ubaguzi wa rangi aliyoionesha jana.
“Villarreal inaitangazia dunia kuwa imekerwa sana na kuchukizwa na kitendo kilichotokea jana kwenye mechi dhidi ya FC Barcelona ambapo shabiki alirusha ndizi katika uwanja El Madrigal”. Taarifa ya klabu imesomeka.
“Shukurani kwa maafisa usalama na mashabiki wote. Klabu imefanikiwa kumbaini shabiki huyo na kuamua kufuta tiketi zake za msimu huu na kumfungia kifungo cha kudumu kutoingia katika uwanja wa El Madrigal”
“Kwa mara nyingine tena, klabu inapenda kueleza msimamo wake juu ya heshima, usawa, undugu na mchezo wa kiungwana ndani na nje ya uwanja na haitavumilia uvunjifu wa kanuni hizi kama vile kuleta fujo na ubaguzi wa rangi”.
Kitendo alichofanyiwa Alves jana kimemkera Mbrazil mwenzake aliyeweka picha katika mitandao ya kijamii akila ndizi kama ishara ya kumuunga mkono kaka yake huyo mweye miaka 30 na kuandika maneno chini ya picha yaliyosema: “Sisi wote ni nyani”.
Mabao mawili ya kujifunga na lile la Lionel Messi yaliwafanya Barca kwa mbali waanze kufufua matumaini ya kutwaa ubingwa katika wiki hii ngumu ambayo wamempoteza kocha wao wa zamani, Tito Vilanova.
CHANZO MPENJA BLOG
No comments:
Post a Comment