Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 13 April 2014

BURIANI GURUMO MUASISI WA MITINDO YA MSONDO, SIKINDE NA NDEKULE

Muhidin Maalim Mohammed Gurumo enzi ya uhai wake akisalimiana na Rais Jakaya Kikwete.

Na Daniel Mbega

HABARI za kifo cha gwiji wa muziki nchini, Muhidini Maalim Mohammed Gurumo, zimeutikisa ulimwengu wa muziki. Tunaambiwa amefariki leo Jumapili Aprili 13 saa 9.00 alasiri katika hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na kusumbuliwa na tatizo la mapafu kwa muda mrefu.
Miaka takriban minne iliyopita aliwahi kuzidiwa na kulazwa katika Hospitali ya taifa Muhimbili, na walilazwa pamoja na nguli mwingine wa muziki, Ramazan Mtoro Ongalla, maarufu Dk. Remmy Ongalla, ambaye jitihada za kupigania uhai hazikuweza kuishinda nia na mipango ya Mwenyezi Mungu. Akatangulia mbele ya haki.
Kifo ni wajibu wetu, kwa maana ndiyo maagizo ya Mungu baada ya baba yetu Adam na mkewe Hawa kutenda dhambi kule bustanini Aden.
Sote, ama wengi wetu, tunautambua mchango mkubwa kabisa wa Gurumo katika maendeleo ya muziki wa Tanzania. Kama Wazaire walivyokuwa wakimuenzi Verkys Kiamwangana Mateta, ndivyo ambavyo nasi tunastahili kuuenzi mchango wa Mjomba Gurumo.
Wapo wanamuziki wengi waliotangulia, wakatamba na bendi mbalimbali kama akina Salim Abdallah Yazidu na Ahmed Kipande, au akina Mbaraka Mwinshehe Mwaruka, Marijani Rajabu Marijani, Hemedi Maneti Ulaya, na wengineo wengi, lakini kwa uhalisia, mchango wao hauwezi kufananishwa na huu wa Mjomba Gurumo.
Ndiyo. Wengine watamtaja ‘Teacher’ King Michael Enock Chinkumba aliyeziongoza Dar Jazz, Dar International na Sikinde, lakini bado tunaweza kusema mchango wa Gurumo ni kipekee katika maendeleo ya muziki wa dansi Tanzania. Amefanya makubwa sana kwa miaka 53 aliyodumu kwenye muziki.
Katika umri wake wa miaka 74, hakuna kazi nyingine yoyote aliyoifanya kwa mapenzi makubwa kama muziki. Sidhani na sina uhakika kama alikuwa mfanyabiashara ama mkulima.
Katika bendi zote tatu maarufu alizopitia, NUTA Jazz (zamani ikijulikana kama Kilimanjaro Chacha Band), Mlimani Park Orchestra na International Orchestra Safari Sound ya Hugo Kisima, alikuwa kiongozi, mwalimu, mtunzi na mwimbaji mahiri sana.
Mitindo aliyoibuni kwenye bendi hizo Msondo wa NUTA Jazz (baadaye ikaitwa JUWATA na OTTU), Sikinde wa DDC Mlimani Park na ule wa Ndekule katika IOSS ambayo haipo kwenye ramani ya muziki, ilishika hatamu nab ado inaendelea kutumika mpaka sasa huku Msondo ukibeba jina la bendi. Mitindo yote hiyo mitatu ni ngoma za Kabila la Wazaramo wanaopatikana mkoani Pwani.
Alizaliwa mwaka 1940 katika Kijiji cha Masaki wilayani Kisarawe katika Mkoa wa Pwani. Kutoka Masaki hadi Mzenga alikotokea Mbaraka Mwinshehe siyo umbali mrefu wa kutisha, hiyo ikimaanisha kwamba Pwani inajivunia historia ya wanamuziki wengi kuwahi kutokea huko wakiwemo Francis Lubua (Nassir Lubua) aliyekuwa anatokea Chalinze na Athumani Momba ambaye alikuwa anatokea maeneo ya Msanga wilayani Kisarawe.
Wakati fulani katika mahojiano enzi ya uhai wake aliweka bayana kwamba muziki ulikuwa kwenye damu yake tangu akiwa mdogo. Alirithi kwa mama yake ambaye alikuwa mahiri katika uimbaji wa ngoma ya Ndekule.
Alipopelekwa Dar es Salaam kwa mjomba wake Suleiman Sultan Mikole ikabidi wampeleke madrasa ili kupata elimu ya dini yake ya Kiislamu. Huku ndiko akaanza kujifunza kuimba kaswida.
“Baada ya kumaliza shule ya msingi pale Pugu Kajiungeni mwaka 1956, alikuja mjomba wangu, baba mmoja mama mmoja na mama yangu , kunichukuwa na kunileta hapa jijini ambapo alinisomesha elimu ya dini. Na wakati nipo hapo madrasa ndipo mwaka 1960 nilipoanza kushiriki kwa siri masuala haya ya muziki,” alipata kusema.
Alisema wakati huo kwamba, yeye alianza na mshahara wa shilingi 5 kwa wiki wakati alipojiunga na bendi ya Kilimanjaro Chacha mwaka 1961, bendi ambayo ilikuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara Samuel Machangu na ilikuwa na makao yake makuu sehemu ambayo sasa ni Amana Club, yalipo makao makuu ya Msongo Music Band. Bendi hii ndiyo ambayo Alfred Tandau, wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi cha TFL (Tanzania Federation of Labour) aliamua kuwashawishi viongozi wenzake wainunue mwaka 1964 na ndipo ikazaliwa NUTA Jazz.
Kilimanjaro Chacha ilimchukua baada ya kumuona akiimba vizuri katika bendi ya mtaani kwao iliyokuwa ikiitwa African, ambayo mara nyingi ilikuwa ikifanya maonyesho yake kwenye harusi.
Wakati huo alikuwa akitoroka nyumbani akimdanganya mjomba wake kwamba anakwenda shughulini na ustaadhi wake, huku akiwa amevalia kama vile kweli anaelekea kwenye shughuli. Mjombe wake alikuwa akipenda dini na aliouona muziki kama ni uhuni.
“Haikuchukua muda mrefu kukapatikana taarifa za kuanzishwa kwa bendi kubwa itakayokuwa ikilipa watu mishahara hapa hapa maeneo ya Ilala,” alisimulia Gurumo akimaanisha bendi hiyo kuwa ni Kilimanjaro Chacha.
Kwa kuwa bendi hiyo kwa kiasi kikubwa iliundwa kwa kutegemea wanamuziki kutoka Afrikan Band, mmiliki wa bendi hiyo mpya Machangu alielezwa bayana kuwa kati ya wanamuziki waimbaji Gurumo awe wa kwanza kuorodheshwa.
Hata hivyo, juhudi za kumsajili Gurumo kwenye kundi hilo zikakwaa kisiki baada ya mjomba wake Mikole kutokuwa tayari mwanawe aache kusoma Qur’uan na kwenda kujiunga na muziki.
Mmiliki wa Kilimanjaro Chacha, Samuel Machangu, alielezwa na wapambe wake kuwa afanye kila liwezekanalo hadi Gurumo apatikane, vinginevyo juhudi zake za kuanzisha bendi kwa kipindi hicho zingeonekana ni kazi bure, aliamua kutumia nguvu ya fedha kumlainisha mjomba wa nyota huyo wa muziki.
“Mjomba alipoletewa kitita cha shilingi 300, mwaka huo wa 1961, wakati ambapo yeye alikuwa akifanya kazi na mshahara wake ulikuwa shilingi 80, akaona isingekuwa busara kwake kuendeleza msimamo wa kunizuia mwanawe kwenda kuimba kwenye bendi, japo alinisisitiza sana nisiache kuswali na nisiguse pombe,” alibainisha.
Huo ukawa mwanzo wa safari ndefu ya mwanamuziki huyo ambaye alisema kibao chake cha kwanza kutunga na kushiriki kuimba kilikuwa kikiitwa ‘Mapenzi ya Kung’ang’aniana’ alichopiga mwaka 1963 akiwa na Rufiji Jazz Band ya jijini Dar es Salaam.
Kama ilivyo kawaida ya wanamuziki wengi, suala la kuhamahama ni kitu cha kawaida sana kwao, kama ambavyo Gurumo alivyohama kundi hilo na kujiunga na Kilwa Jazz, bendi iliyokuwa na maskani yake Mtaa wa Kilwa Ilala ambapo alidumu kwa miezi nane tu kabla ya kujiunga na NUTA Jazz mwaka 1964.
“Kilichonipeleka hapo ilikuwa maslahi tu, kwani ingawa nilikuwa nikituzwa pesa jukwaani ambazo wakati mwingine ni zaidi ya mshahara wangu, lakini ilikuwa haijafika shilingi 120, nilizoahidiwa kulipwa nilipojiunga na bendi hiyo iliyokuwa chini ya Jumuiya ya Wafanyakazi,” alieleza Gurumo.
Akiwa na bendi hiyo Gurumo alitunga na kurekodi nyimbo nyingi zilizokuwa zikipendwa sana na mashabiki wa muziki zikiwemo Nidhamu ya Kazi, Mpenzi Zalina, Dada Fatuma, Kilimo cha Kufa na Kupona, Heko Baba Nyerere na nyinginezo nyingi.
Alikaa hapo mpaka mwaka 1978 alipotoka na kwenda kuanzisha bendi ya Mlimani Park Orchestra na kuanzisha mtindo wa Sikinde Ngoma ya ukae unaotumiwa hadi leo na bendi hiyo maarufu hapa nchini.
“Hii ilikuwa ndiyo bendi yangu ya kwanza kuwa kiongozi wa bendi, na mtindo wa sikinde mimi ndio niliuanzisha rasmi kutumika kwenye muziki wa dansi, ukiondoa kwetu uzaramoni unakotumika kama aina mojawapo ya ngoma za asili,” alieleza.
Wakati alipokuwa Sikinde, Gurumo alitunga nyimbo ambazo zilivuma sana, baadhi ya nyimbo hizo ni kama vile Kassim Namba 1 na 2, Barua Kutoka kwa Mama utunzi wake Cosmas Thobias Chidumule na yeye alishiriki kuweka sauti na kuimba.
Mwaka 1985 alihama Mlimani Park akiwa na wanamuziki watano - Hassan Bitchuka, Abel Bartazal, Kassim Rashid Kizunga, Charles John ‘Ngosha’ - mwenyewe wa sita na kwenda OSS kulisuka upya kundi hilo ambalo lilionekana kupoteza umaarufu na kuanzisha mtindo wa Ndekule Ngoma ya Mababu.
Kundi hilo ambalo liliwahi pia kutumia mitindo ya Masantula na Dukudukuku chini ya magwiji Kikumbi Mwanzo Mpango ‘King Kiki na ‘Supreme’ Ndala Kasheba kwa nyakati tofauti, lilikuwa moto wa kuotea mbali mara baada ya kutoka vibao kama Bwana Kinyogoli na Usimchezee Chatu, ambao ulikuwa majibu ya ‘dongo’lililotupwa na Mlimani Park alikokuwa kiongozi wa bendi.
Mwaka 1990 Gurumo alihama Ndekule na kurejea JUWATA Jazz. Amekuwa kiongozi wa bendi hiyo tangu ikiwa chini ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (OTTU, baadaye TFTU na sasa TUCTA) hadi shirikisho hilo lilipojitoa kuihudumia na wanamuziki wenyewe wakaamua kuiongoza. Amekaa nayo hadi mauti.
Huyu ndiye Mjomba Gurumo, nguli wa muziki ambaye leo hii amefariki akiwa mwingi wa umri na busara. MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA, AMINA!


No comments:

Post a Comment