Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 16 April 2014

AIBU TUPU BUNGENI

Mjumbe kutoka Zanzibar, Asha Bakari Makame

UFUNDI wa matusi, vijembe na mipasho ndivyo vilivyotawala jana bungeni wakati wajumbe wa Bunge Maalumu wakijadili sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba zinazozungumzia muundo wa Muungano, jina, alama, tunu za taifa na lugha.
Wajumbe wa Zanzibar ndio waliokuwa vinara wa kutukanana, huku wengine wakizungumzia masuala binafsi ambayo Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, licha ya kuwaonya wasifanye hivyo, walikaidi.
Matusi, malumbano na vijembe hivyo yalianza juzi jioni ambapo mjumbe kutoka Zanzibar, Asha Bakari Makame, alisema wajumbe wenzake kutoka Chama cha Wananchi (CUF) hawana uhalali wa kuwazungumzia Wazanzibar kwakuwa si watawala.
Bakari alitumia muda mwingi kumshambulia Ismail Jussa Ladhu, ambaye aliwasilisha maoni ya watu wachache waliokuwapo kwenye kamati namba sita ambao wanataka muundo wa serikali tatu.
Alisema Serikali ya Zanzibar ni ya kimapinduzi na haikupatikana kwa karatasi bali ilipinduliwa, hivyo wale wote wanaojifanya wana uchungu nayo ni wanafiki.
“Namwambia Jussa si kweli anaionea uchungu nchi hii, kwa sababu kuna Kiswahili kinasema ‘wafadhilaka si wasaidaka ni wapundaka’, namwambia Jussa hamtutoi labda mtupindue, serikali ya kimapinduzi haichukuliwi kwa karatasi, hilo nawatabanaisha.
“Marehemu Karume aliuawa wakati akipigania Zanzibar. Namsikitikia Jussa aliponiita mama japokuwa kweli Jussa ni mwanangu, lakini ingelikuwa amezungumza maneno mazuri, lakini katuambia tumeufyata.
“Namuuliza neno kuufyata anamwambia mama yake? Anajua neno kuufyata ni kitu gani? Mimi sijaufyata, nimeshaufyatua, nimezaa watoto watatu… tafsiri ya kuufyata kule Pemba ni kwamba mtu ana busha analikunjia kwa nyuma, Jussa ameufyata yeye.
“Namsikitikia sana mwanangu Jussa kwa sababu mimi nimeufyatua, lakini yeye hajaoa wala kuzaa watoto, hivyo hana watoto wa kurithi mali,” alisema.
Hija Hassan Hija, alisema baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wakiwa Zanzibar wamekuwa wakitetea serikali tatu, lakini wamefika mkoani Dodoma wamebadilika na kutetea serikali mbili.
Alisema wanaofanya kigeugeu hicho wanafanya hivyo kwa kuwa ni ‘wasaka tonge’ wakati wakijua kuwa muundo wa serikali mbili umeshindwa kuwakomboa wananchi na kumaliza kero zilizodumu kwa takribani miaka 50.
Alimtaja Waziri wa Elimu na Amali, Alli Juma Shamhuna kuwa ni miongoni mwa watu wa kuwa mstari wa mbele kutaka serikali tatu, lakini hivi sasa kwa kuwa amepewa cheo, amenyamaza kimya.
“Wanaotetea serikali mbili kutoka Zanzibar ni wasaka tonge ambao wameweka mbele masilahi binafsi badala ya umma, hawa tusiwaamini hata kidogo,” alisema.
Salehe Nassor Juma, alisema Wazanzibar wanaotetea serikali mbili ni mavuvuzela waliozoea kuzomea bila kujua nini chenye manufaa kwa taifa lao, ambalo kwa muda wa miaka 50 limekuwa likinyonywa kwa Tanzania Bara kuvaa koti la Muungano.
Haji Omari Kheri, aliwapiga kijembe wajumbe wenzake kutoka CUF, kuwa wao ndio wameufyata kwa kuwa walipokuwa Zanzibar walitoa maoni ya kutaka Serikali ya Mkataba, lakini wamefika bungeni wanataka serikali tatu.
“Hawa wanataka kupandikiza chuki baina yetu, wanataka watugawe ili watutawale, huwezi kuwa na uhalali ndani ya Bunge ukakosa nje ya Bunge… wanatikisa kibiriti sasa sisi tunawaambia kibiriti chetu kimejaa,” alisema.
Panya Alli Abdala, alisema CUF wanataka serikali tatu ili wauvunje Muungano na kuukaribisha utawala wa kisultani uliopinduliwa.
“Hawa CUF wanatafuta mbinu za kumrejesha mkoloni, sisi hatutakubali hata kidogo, wamezoea utumwa, hawajisikii raha wakiwa huru,” alisema.
CHANZO: TANZANIADAIMA

No comments:

Post a Comment