Padri Dennis Wigira wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, akihubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman
Dar/Dodoma/Morogoro. Wakristo kote nchini jana waliungana na wengine duniani kuadhimisha Ijumaa Kuu ikiwa ni kumbukumbu ya mateso na kifo cha Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita, huku viongozi wa dini wakieleza kusikitikia mwenendo wa mchakato wa Katiba Mpya.
Askofu Msaidizi wa Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Samwel Mshana akizungumza katika ibada ya Ijumaa Kuu, alisema haoni nuru ya kupatikana kwa katiba bora nchini.
Mshana alisema kuwa ana mashaka huko mbeleni Taifa litaletewa katiba itakayowagawa Watanzania katika matabaka, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
“Mimi kama kiongozi wa dini sina matumaini kabisa ya kupata katiba ambayo itatufanya tuwe kitu kimoja, naona ni katiba itakayowalinda wachache kwa misingi ya matabaka,”alisema.
Alisema katiba ndiyo mkombozi wa wanyonge, lakini kwa jinsi mchakato unavyoendelea ni hofu na mashaka makubwa na inaonekana kuna siri nzito ndani ya vyama vya siasa.
“Ndiyo maana wanavutana ili kuhakikisha itikadi na masilahi ya vyama vyao yanaingizwa katika Katiba Mpya, hatukutegemea wajumbe wawe na itikadi na misimamo ya vyama vyao vya siasa bila kujali maslahi mapana ya Watanzania”.
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa aliwaasa viongozi waliopo madarakani kutowaonea watu wanaoonekana kuwa tishio kwa tawala zao.
“Wapo viongozi ambao wanaishi kama watawala wa Kiyahudi waliomuua Yesu Kristo kwa sababu tu walimwona ni tishio kwao,” alisema Nzigilwa na kuongeza kuwa wanyonge wanabambikiziwa kesi wakati ndiyo wanaohitaji msaada wa kisheria.
Mchungaji Charles Mzinga wa Kanisa la KKKT, Azania Front jijini Dar es Salaam alisisitiza kuwa upendo ndiyo kinga kwa jaribu linalomkuta Mkristo popote alipo katika maisha ya hapa duniani.
Kwa upande wake, Padri Dennis Wigira wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam alilaani tabia ya baadhi ya viongozi waadilifu katika Serikali kukosa uadilifu katika serikali kuonekana hawafai kwa kuwa hawajaiba mali ya umma na kuishi maisha ya kawaida.
Alisema wizi umekithiri kwa watendaji wa umma hivi sasa kiasi kwamba ambaye hafanyi anaonekana mjinga.
Imeandikwa na Pamela Chilongola, Joseph Zablon, Daniel Mjema, Esther Mwimbula, Andrew Msechu, Hilda Sigala, Julius Mathias na Goodluck Eliona.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment