Kigoma. Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inakusudia kufuta mpango wa ruzuku ya mbolea ya pembejeo kwa wakulima nchini kutokana na madai ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi alipokuwa katika ziara ya wilaya za Kasulu na Uvinza mkoani Kigoma.
Akizungumza na vikundi vya wakulima (AMCOS), Zambi alisema ruzuku hiyo itafutwa kutokana na vitendo vya rushwa ambavyo hujitokeza wakati wa kuigawa katika misimu husika.
Aidha, alisema mpango wa kuanzisha benki ya wakulima kwa ajili ya mikopo uko palepale ili kuwawezesha wakulima kukopa na kuwajengea uwezo wa kumudu uendeshaji wa shughuli hiyo.
Alisema zaidi ya Sh74bilioni zimebainika kutumiwa vibaya na watendaji wa serikali pamoja na mawakala wa pembejeo hizo tangu kuanza kwa mfumo huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Khadija Nyembo alisema licha ya mpango huo kuwa na lengo la kuwanufaisha wakulima ulikabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni rushwa na kwamba baadhi ya watendaji wa serikali wanatumikia vifungo gerezani.
Alisema wakulima wa Mkoa wa Kigoma wamekuwa miongoni mwa waliokuwa wakilalamikia mpango huo kutokana na kuwanufaisha wachache hivyo kutokuwa na tija katika kuboresha kilimo na uzalishaji.
Mkulima wa tumbaku huko Mwamila, Wilaya ya Uvinza, Daniel Mkuyu alisema kuwa tatizo la rushwa katika ugawaji wa ruzuku ya mbolea ya pembejeo limekuwa likijitokeza kila msimu wa kilimo na kwamba dawa yake ni kuanzishwa kwa benki ya wakulima.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment