“Karume alimtaka Mwalimu waunde serikali moja; yeye awe Makamu wa Rais na Nyerere awe Rais. Lakini Mwalimu hakutaka wazo hilo akihofia maadui wangesema ameimeza Zanzibar na pia alizingatia udogo wa nchi hiyo pamoja na hofu ya kuwa mkoloni mamboleo,” Pius Msekwa.
Dar es Salaam. Wiki mbili kabla ya Tanzania kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa ametoboa siriya Muungano huo akisema “mchakato wa kuundwa kwake ulifanywa kwa siri na haraka sana,” kutokana na upepo wa kisiasa na usalama wa kipindi hicho.
Akizungumza katika moja ya mfululizo wa vipindi vya miaka 50 ya Muungano vinavyorushwa na Redio ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Taifa), Msekwa alisema woga wa hayati Abeid Amani Karume kupinduliwa na maadui, ulikuwa ni miongoni mwa sababu za kuharakisha Muungano huo.
Msekwa aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati Muungano unaasisiwa, alisema pia yeye na wenzake walichelewa kujua kwamba Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa Kwanza wa Tanganyika) na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Karume walikuwa na majadiliano ya kuunganisha nchi hizo.
“Kikubwa cha kusema ni kwamba mazungumzo ya Muungano huo yalifanywa kwa siri.... kwa siri sana baina ya waasisi wa nchi hizo. Kwa nini yalifanywa kwa siri? Siyo kwa sababu walikuwa wababe, la hasha, balikwa mazingira ya wakati ule, kulikuwa na maadui ambao wasingependa nchi hizi kuungana,” alisema Msekwa na kuongeza:
“Kwa woga huohuo, ndipo Mwalimu alipokubaliana na mwenzake wafanye mazungumzo ya siri mpaka waliposaini yale makubaliano na kunijulisha.”
Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Spika wa Bunge la Muungano, alisema baada ya makubaliano ya Muungano, Nyerere alimwita na kumjulisha kuwa walishakubaliana (na Karume) kuungana, hivyo walihitaji baraka za Bunge kuridhia Muungano huo.
“Mwalimu akaniambia, ‘wewe Katibu wa Bunge unaweza ukawaita wabunge wakaja kwa harakaharaka kuridhia makubaliano?’
“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa Jumanne na Mwalimu alipendekeza wabunge wafike Ijumaa ya juma hilohilo, nao wabunge wakaja wakaridhia.”
Simulizi hii ya Msekwa kuhusu Muungano imekuja wakati kukiwa na vuguvugu la muundo wa Muungano katika Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba kupendekeza serikali tatu badala ya Serikali mbili za sasa.
Bunge kuridhia
Aliongeza kuwa, baada ya Bunge la Tanganyika kuridhia Mwalimu Nyerere aliutaka muswada huo “kwa haraka sana” ili aufanye kuwa sheria na alitaka kupelekewa kwa mkono.
“Baada ya wabunge kuridhia pale Karimjee, nikauchukua muswada na kuupeleka Ikulu, sio mbali pale.
“Mwalimu alifurahi sana, alishajua kuwa ulikuwa umesharidhiwa kwa sababu alikuwa anafuatilia mkutano wa Bunge kupitia redio, ukumbuke zamani hakukuwa na televisheni,” Msekwa anasimulia.
Sababu za kuharakisha
Msekwa alisema kulikuwa na sababu kuu mbili za kuharakisha Muungano; moja ni Mwalimu Nyerere kutaka nguvu ya Afrika itokane na miungano ya nchi, wakati Karume alitaka kuimarisha usalama wa Zanzibar miezi miwili baada ya kuuondoa utawala wa Sultani Januari 12, 1964.
Aliongeza kuwa Nyerere alikuwa amejifunza kutokana na makosa ya awali ambapo maadui waliharibu mpango wa kuziunganisha nchi za Afrika ya Mashariki na kuwa shirikisho.
Hata hivyo, Msekwa aliongeza kuwa, Mwalimu alimwambia Karume wangoje kwa muda, lakini kiongozi huyo wa Zanzibar hakuafikiana na wazo hilo kutokana na masuala yake ya kiusalama.
Alisema hata wakati Bunge la Tanganyika likiridhia muswada wa kuanzisha Muungano, tayari wenzao wa Zanzibar walikuwa wamekwishauridhia.
Muundo wa Muungano
Msekwa alisema suala la kubuni muundo wa Muungano ambalo linasumbua vichwa wajumbe wa Bunge la Katiba sasa, halikuwa tatizo kubwa wakati huo, japo Karume alimwomba Nyerere watengeneze Serikali moja.
“Karume alimtaka Mwalimu waunde serikali moja; yeye awe Makamu wa Rais na Nyerere awe Rais. Lakini Mwalimu hakutaka wazo hilo akihofia maadui wangesema ameimeza Zanzibar na pia alizingatia udogo wa nchi hiyo pamoja na hofu ya kuwa mkoloni mamboleo,” alisimulia Msekwa.
Msekwa alisema mara tu baada ya Nyerere kusaini muswada wa Muungano kuwa sheria, alianza kuunda Serikali ya Jamhuri ya Muungano na aliwachukua wajumbe 20 kutoka Zanzibar kuingia katika Bunge la Muungano.
Alisema baada ya Muungano huo hakukuwa na chokochoko zozote na hata maadui waliotaka kuipindua Serikali ya Zanzibar walikata tamaa.
“Hakukuwa na kitu kinachoitwa kero za Muungano mpaka pale Aboud Jumbe alipoingia madarakani baada ya kifo cha Karume 1972. Jumbe na wenzake walikuwa wanahoji Tanganyika tuliyoungana nayo ipo wapi?” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya miaka kadhaa ya uongozi wake, Jumbe alianza harakati za kuandaa Katiba ya Serikali tatu kimyakimya.
“Jumbe alimwomba Mwalimu apatiwe mwanasheria mzoefu ili awe Mwanasheria Mkuu Zanzibar licha ya kuwa tayari alikuwapo mwanasheria mkuu.
Nyerere alimpatia Jaji Damian Lubuva, ambaye alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa upande wa Muungano, huku Joseph Warioba akiwa Mwanasheria Mkuu.
Alisema baada ya miaka takriban sita, Jumbe alimrudisha Jaji Lubuva Tanzania bara akidai ameshampata mwanasheria mwingine na haposiri za kuunda Katiba mpya zilianza kugundulika mwanzoni mwa mwaka 1984.
“Jumbe alikuwa na mpango wa kumtafuta mwanasheria mkuu kutoka Ghana. Mwanasheria huyo walimuozesha binti wa Kizanzibari kabisa na baadaye walianza mchakato wao wa kutengeneza Katiba ya Serikali tatu kwa siri,” alisema Msekwa.
Hata hivyo, usiri wa Jumbe ulivuja na kumfikia Mwalimu, ndipo katika Mkutano Mkuu wa CCM, chama kilimwadhibu kwa kumtaka ajiuzulu na rais huyo alifanya hivyo bila hiyana.
Hata baada ya Jumbe kujiuzulu, Msekwa alisema bado madai ya Serikali tatu yaliendelea kuibuka katika tume mbalimbali ikiwamo ile ya Jaji Francis Nyalali, Kundi la Wabunge (G55) na hata sasa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba.
Utashi wa kisiasa
Mwanasiasa huyo mkongwe anasema hatima ya Muungano ipo mikononi mwa wajumbe wa Bunge la Katiba ambao jana walianza kujadili mapendekezo ya kamati kuhusu Ibara za Kwanza na Sita za Rasimu ya Katiba, zinazozungumzia Muungano.
“Muungano wowote unahitaji utashi wa kisiasa. Kuna watu wanasema kero za Muungano zitaondolewa na Serikali tatu na huku wengine, kikiwamo CCM, wanasema watahakikisha wanatatua kero hizo kwa kutumia Serikali mbili.
Hivyo, mimi naona iwapo uamuzi wa Bunge la Katiba utaondoa kero za Muungano, sawa na wananchi wakiridhia uamuzi huo sawa, hakuna tatizo kwa sababu hapo awali, uamuzi ulitoka kwa Serikali pekee,” alisema Msekwa.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment