Mwenyekiti wa IPC Frank Leonard akizungumza na wahabari hivi karibuni ,kushoto ni Katibu Mtendaji wa IPC Francis Godwin
.........................................................................................
Ndugu wanahabari awali ya yote tunapenda kuwapongeza kwa kuitikia wito huu wa ghafla zaidi.
Lengo la kukutana hapa asubuhi ya leo ni kutaka kujitathimini mwenendo wa utendaji kazi wetu na wadau wanaotuzunguka ikiwemo jamii nzima .
Ndugu wanahabari kwa muda sasa wanahabari mkoa wa Iringa tumekuwa na mahusiano mazuri na wadau wetu na jamii nzima inayotuzunguka kwa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa jambo ambalo ni la kujipongeza .
Leo mbali ya kuitana kwa ajili ya kujitathimini mwenendo wetu bado tuna haja ya kuendelea kuikumbusha jamii na wadau wote kuwa chombo cha habari na mwanahabari si mali ya mtu mmoja kwani mwanahabari yupo kwa ajili nzima
Ninasema hivyo kutokana na kauli na matukio mbali mbali yanayoanza kujitokeza hasa kutoka kwa wana siasa wa vyama vya siasa dhidi ya wanahabari mkoani kwetu.
Wapo baadhi ya wana siasa ambao wameendelea kujenga chuki binafsi dhidi ya chombo fulani ama mwanahabari fulani kutokana na sababu wanazozijua wao jambo ambalo si jema kuendelea kulifumbia macho .
Chuki hizi ambazo zilikuwa zikifanyika chini chini bado zilikuwa zikiwafikia wanahabari hao kutoka kwa vyanzo vyao ama mwanahabari mwingine ambae labda mwanasiasa ama chama cha siasa kimekuwa kikimwona anafaa.
Ifahamike kuwa wana siasa hukuona bora mwanahabari ama chombo cha habari pale ambapo wanahitaji kukutumia na baada ya kumaliza kufanya hivyo wanasiasa hao hawakuoni bora tena ,hivyo napenda ifahamike kuwa wanahabari tunapofanya kazi na wana siasa ni lazima kulitambua hilo huku tukijivunia taaluma yetu na ni vema kwa kila kazi tunayoifanya ni lazima kuzingatia maadili ya tasnia hii ya habari .
Mwaka 2010 wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM baadhi ya wanahabari walinyanyasika zaidi katika mikutano wa CCM na miongoni mwa waliopatwa na misuko suko hiyo ni pamoja na mwandishi wa Habari leo Frank Leonard ambae aliondolewa katika mkutano na vijana wa ulinzi wa CCM.
Pia mwandishi wa gazeti la Tanzania daima mkoani hapa Gustav Chahe pia alikutwa na tukio kama hilo akiwa katika mkutano wa serikali serikali ya mtaa huko Kihesa alifukuzwa na hata kunusurika kipigo na viongozi wa eneo hilo ambao walikuwa hawapendi mambo yao kufikishwa katika vyombo vya habari.
Pia wapo wanahabari ambao wamevunjia kamera zao ama kupigwa pindi wanapotimiza wajibu wao.
Mbali ya matukio haya kutulia na wanahabari kuendelea kutimiza majukumu yao bila ya kuingiliwa tukio kama hilo limeweza kujitokeza tena katika mkutano wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) mkutano uliokuwa ukifanyika katika uwanja wa Mwembetoka tarehe 4/6/2014 mgeni rasmi mwenyekiti wa kamati ya hamasa kanda John Mwambigija alitumia mkutano huo kuvishambulia vyombo vya habari na hata kuhamasisha wananchi kuchukia chombo kimoja wapo cha utangazaji mkoani Iringa jambo ambalo si sahihi.
Kwani kitendo cha kiongozi huyo kufanya hivyo ni kupandikiza chuki kati ya watenda kazi wa chombo hicho ,chombo chenyewe na wadau wanaotegemea kupata habari kupitia chombo hicho na wanahabari hao.
Hivyo kama chama cha wanahabari mkoa wa Iringa ambao tunapenda kuona suala la uhuru wa vyombo vya habari linaendelea kukua na si kufinywangwa na mtu ama watu fulani hatujapendezwa na kauli kama hizo za kichochezi ambazo zinafifisha uhuru wa vyombo vya habari na kupandikiza chuki zimekoma mara moja kwa vyama vyote vya siasa na wanasiasa.
Rai yetu kwa vyama vyote vya siasa na wana siasa ni vema watambue kuwa chombo cha habari ama mwanahabari si tawi la chama chochote wala mali ya mwanasiasa ,japo vipo vyombo ambavyo ni mali ya chama fulani mfano gazeti la Uhuru na Mzalendo ,hivyo basi tunapenda kuwakumbusha kuwa ni vema vyama na wanasiasa kutimiza wajibu wao bila ya kugombanisha wanahabari na vyombo vyao na tusingependa kuona uchochezi kama huo unaendelea kwani iwapo uchochezi kama huo utafumbiwa macho leo yawezekana kwa chombo hicho kesho ikawa kwa chombo kingine na ama mwanahabari mwingine .
Mwisho ningependa kuwakumbusha wanahabari wenzangu kuendelea kutimiza wajibu wetu kwa uhuru zaidi bila kukiuka maadili ya tasnia hii pili kuepuka kupandikiza chuki kwa chombo ama mwanahabari mwenzetu kwani iwapo tutafanya hivi ni sawa na kuivua nguo taaluma yetu wenyewe .
Mungu ibariki Tanzania ,Mungu ibariki tasnia hii ya habari nchini
Amina
MWISHO
Imetolewa na Francis Godwin
Katibu Mtendaji Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC)
Tarehe 5/6/2014
No comments:
Post a Comment