INNOCENT A. NDAYANSE
(ZAGALLO)
0755 040 520 / 0653 593
546
UTANGILIZI
Judith ameondoka
mpakani na kuingia Tanzania baada ya kukutana na Baraki. Makella naye
anahangaika kumtafuta kila kona na anafika mpakani baada ya kuelekezwa na
dereva wa teksi kwamba amekwenda huko. Anapofika hapo anabuni uongo kwamba
Judith ndiye aliyehusika na tukio la kutungua ndege iliyomuua Rais, uongo ambao
ofisa wa mpakani anaupinga. Je, nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako …
SIKU iliyofuata, wakati jua linakaribia kuzama, lori aina ya Fuso lilikuwa likiingia katika mji wa
Biharamulo, mkoani Kagera, nchini Tanzania.
“Itabidi tulale hapa,” Baraki aliwaambia
Livingstone na Judith. Kisha akamgeukia Judith: “Unaionaje Tanzania?
Kuna vurugu kama kule kwenu?”
Badala ya kujibu, Judith alitabasamu kidogo na kuyaepuka macho ya Baraki
ambayo yalikuwa yamemganda, akisubiri jibu.
“Naamini utaipenda Tanzania,” Baraki aliendelea. “Kama nilivyokwambia
jana, huku hakuna mauaji ya kikabila kama kule kwenu. Tuna makabila zaidi ya mia moja na ishirini,
na makabila kati ya matano au sita ni makubwa
sana kama ilivyo huko kwenu kwa
makabila ya Kihutu na Kitutsi. Lakini huku Tanzania ukabila hauna nguvu. Mtu wa
kabila moja anaweza kuoa au kuolewa na wa kabila jingine. Kule kwenu
inawezekena hiyo?”
Judith alikataa kwa kutikisa kichwa.
“Inasikitisha,” Baraki alisema kwa sauti ya chini.
Yalikuwa ni maneno yaliyomwingia vizuri Judith. Alielewa na akashangaa.
Kwake, haikumwingia akilini kuwa anaweza kumchojolea nguo Mhutu, iweje aolewe
naye?! Eti Watanzania wao hawana utamaduni wa kujali ukabila. Mmakonde anaweza
kuolewa na Msukuma, Muha akamwoa Mchaga, na kadhalika na kadhalika.
Hata hivyo, mawazo hayo yalipeperuka haraka kichwani mwake pale Makella
alipomjia tena akilini. Hakuhofia kuwa huenda akavuka mpaka na kuingia Tanzania katika harakati zake za kumsaka,
bali alizidi kuumia moyoni pale kumbukumbu ya jinsi Makella na wenzake
walivyodiriki kunyanyua bunduki na kuwamiminia risasi baba, mama na wadogo zake
watatu usiku wa siku iliyopita.
Kwa mbali alihisi machozi yakilenga machoni. Akaharakisha kuyafuta kwa
namna ambayo Baraki hakutambua. Kwa ujumla hakuiona haja ya kila mtu kuyajua
masaibu yaliyompata. Kila mtu, hata huyu Baraki! Ajue ili iweje? Na kwani akijua atamsaidiaje?
Akiwa ni msichana mwenye umri wa miaka 22, tayari alikuwa na uwezo wa
kupambanua baya na zuri. Alikuwa na uwezo kuamua chochote kwa hiari yake, mradi
aijue faida au madhara yake.
Alihitaji kumtoroka Makella, na kwa hilo amefanikiwa. Suala kuwa hawa
wasamaria wema walistahili kujua yaliyomsibu, hakuona kuwa lilistahili. Dola 2,000
zilizokuwa ndani ya bukta aliyoivaa ndani ya sketi zilimtia matumaini ya
kutotetereka kimaisha japo yuko ugenini.
Saa 2 usiku Baraki alikuwa akiegesha gari kando ya nyumba ya wageni
ambayo walikuwa na mazoea ya kufikia kila walipofika mjini humo. Ni Kyaka Guest
House.
Usiku huo ukawa ni mtihani mwingine kwa Judith, mtihani ambao hakujua
kama ataushinda ilhali yuko ugenini na yuko na watu ambao kwake ni wageni
kabisa. Kilichomtorosha kule Kiyovu Hotel ni kutokubali kufanya mapenzi na
Makella. Lakini huyu mfadhili wake, Baraki ameonyesha bayana tangu kule mpakani
kuwa anamhitaji kwa ajili ya kustarehe naye kimwili.
Akatae? Na akikataa Baraki atachukua hatua gani? Kwa vyovyote uhusiano
utavunjika. Na matokeo ya kuvunjika kwa uhusiano huenda pia kukamfanya Baraki
atoe taarifa katika Idara ya Uhamiaji kuwa kuna Mnyarwanda mmoja aliyeingia
nchini kinyume cha sheria.
Hadi wakati Baraki alipokuwa akifunga mlango wa gari na kumshika mkono
Judith wakielekea ndani ya gesti hiyo, bado Judith hakuwa akijua uamuzi
aliostahli kuchukua kama ataombwa penzi na Baraki.
Baraki alichukua vyumba viwili; kimoja kwa ajili ya Livingstone, na
kingine kwa ajili yake na Judith.
Moyo wa Judith ulikuwa mzito pale alipokaribishwa chumbani na Baraki.
“Tutakuwa pamoja, mpenzi,” Baraki alimwambia huku akimtazama kwa macho
yaliyozungumza bayana uchu dhidi yake. Akaongeza, “Naamini utakuwa usiku mzuri
kwako na kwangu, usiku utakaoiliwaza mioyo yetu kwa kiwango kikubwa, eti?”
Yaleyale! Judith aliwaza kwa uchungu. Afanye nini? Akahisi kitu kikimshawishi
kutoleta ukaidi wowote kama Baraki atataka penzi. Jambo moja tu lilimtia
faraja; kufanikiwa kumtoroka Makella. Kufanya mapenzi leo na Baraki haitakuwa
mara ya kwanza kwake maishani. Tayari alishafanya tendo hilo na kijana mmoja
huko Gisenyi, kijana ambaye alimwondolea usichana wake na wakaendelea kufanya
hivyo mara kadhaa kabla kijana huyo hajakumbwa na mauti ya ghafla katika
sekeseke lilelile la ukabila miezi takriban sita iliyopita.
Lakini kwa kijana yule, Judith alifanya mapenzi kwa kuridhia. Na ni kwa
itikadi hiyo ya kufanya mapenzi na mtu ampendaye, ndiyo maana aliamua kumtoroka
Makella. Pamoja na hayo, kumtoroka Makella akiepuka kumvulia nguo, na
kumkatalia Baraki, ni mambo mawili tofauti.
Makella alikuwa ni muuaji; aliwaua baba, mama na wadogo zake na pia
alikuwa ni wa kabila la Wahutu. Huyu
Baraki siyo Mhutu, ni Mtanzania. Isitoshe, Baraki amemfadhili kwa kiwango
kikubwa, ufadhili ambao hata yeye mwenyewe haujui uzito wake. Kumvulia nguo
Baraki hakuona kuwa ni kosa, zaidi atakuwa naye amelipa fadhila. Kwa ujumla
bado aliuhitaji ufadhili wa Baraki, na aliuhitaji ufadhili wa Watanzania. Dola
2000 alizokuwanazo, hakuona kuwa ni kinga madhubuti katika nchi hii ngeni. Bado aliihitaji roho yake!
Itaendelea kesho…
No comments:
Post a Comment